Utajiri wa damu

Utajiri wa damu

UTAJIRI WA DAMU - 14-


Mzee Chambilecho aliingizwa moja kwa moja kwenye ofisi ya Inspekta Ado na aliyemuingiza humo ni yule askari ambaye alikuwa ananihoji mimi.

"Chepriska nisubiri hapa ofisini kwangu. Nampeleka mlinzi wenu Mzee Chambilecho kwa afande."
Sikuitikia kwa kutoa sauti isipokuwa niliitikia kwa kubetua kichwa tu, polisi yule alinielewa.

Baada ya muda mfupi yule askari alirudi kwenye ofisi yake na kuniambia nahitajika kwa Inspekta Ado. Nilijiuliza maswali mengi kwamba kwa nini nami niitwe tena au kuna jambo amelisema yule mzee kuhusu mimi?



Moyo ulinidunda wakati nasindikizwa na askari yule hadi kwenye ofisi ya afande Ado.
"Karibu tena Chepriska. Nilihitaji unisaidie wakati wa kumuuliza maswali huyu mzee. Anajibu lakini baadhi ya maneno siyaelewe anachanganya na lugha ya kwao ambayo wewe nimeambiwa unaijua vyema."
"Ni kweli, sisi ni kabila moja."Nilimjibu huku nikitafakari jambo.

Nilimuona askari yule kuwa siyo makini kabisa. Nilijiuliza kama majibu ya yule mzee nikiyapotosha atajuaje?
Hata hivyo, kati ya maswali yote aliyomuuliza sikuona hata moja la kumpotosha kwa sababu yalikuwa hayahatarishi usalama wangu au wa bosi wangu, Mzee Mitimingi.

Aliulizwa alianza kazi lini na analipwaje pale, akajibu. Alihojiwa pia kama anahafamu biashara nyingine anayofanya Mzee Mitimingi ukiacha ya magari na nyumba za wageni.
Hata hivyo, mzee huyo aliwaeleza kwamba mambo ya kazi za bosi wake hayajui na anachojua yeye ni kuja kazini saa kumi na mbili jioni na kutoka saa kumi na mbili asubuhi.

Aliwachekesha maofisa wa polisi kwa kusema kuwa asubuhi mara nyingi huondoka saa moja na nusu au saa mbili kwa sababu maalum.
Alipoulizwa sababu gani hiyo maalum inayomfanya ashindwe kuondoka kwenda nyumbani kulala japo kwa mchana huo alisema.
"Achubuhi mara nyingi huwa nagoja chai. Nikinywa tu huyoo nachapalika kwendaga nyumbani."
"Ina maana kinachokufanya uchelewe ni chai tu."
"Wewe unaona kitu kidogo hicho? Wenchako bila chai kichwa kinauma."
Baadaye tuliruhusiwa kuondoka kituo cha polisi kurudi nyumbani. Tulipotoka nje Mzee Chambilecho aliniuliza maswali mengi ya haraka haraka.
"Tumeletwa hapa polichi kwani kuna nini?"
"Nikuulize."
"Uniulize mimi wakati nimekukuta wewe polichi?"
"Wamekuuliza habari za Mzee Mitimingi, umesema hujui lolote, labda mzee ana tatizo."
"Najua ana mataticho, si mgonjwa? Chacha ugonjwa na polichi wapi na wapi?"
"Ngoja baada ya siku chache tutajua kwa nini wametuita huku.Wakinijulisha nitakuarifu." Niliyakatisha mazungumzo baada ya kulifikia gari ambalo lilikuwa pembeni ya kituo, mbali kidogo lakini ndani yake alikuwepo mzee Mitimingi.
Alitoa macho kwa wasiwasi alipotuona tukitoka kituo cha polisi. Hakujua kama mlinzi Chambilecho naye alikamatwa.
"Wewe umekuja kufanya nini hapa polisi?" alimhoji kwa ukali yule mlinzi.
"Nzee chi wale polichi walikuja tena na gari lao, wakanichukua, chijui kuna nini kabichaaaa!!!"
"Sawa. Chepriska, wewe una akili sana maana mazungumzo yenu kati yako na polisi nimesikia kila kitu baada ya kunipigia simu, Nilipoipokea nikawa nasikia kama nami nilikuwa ndani ya kituo cha polisi. Wewe ni mbunifu sana."
"Nakushukuru mzee."
Tulitoka pale polisi na kwenda moja kwa moja sokoni kununua mahitaji.Tulinunua mchele, unga wa mahindi na ngano, sukari, nyanya, vitunguu, mchicha na nyama ya kusaga.
Baadaye tulipitia kwenye nyumba zake za wageni mbili, nadhani alikwenda kuchukua fedha kwani hakuishia hapo, tulikwenda pia kwenye mabasi yake, stendi kuu na kukuta manne yamefika isipokuwa moja ambalo madereva walisema limeharibika njiani.
Tulitoka na kufika nyumbani kwa Mzee Mitimingi ajabu ni kwamba tulikuta polisi wamejaa tele nje ya geti. Wote tulianza kutetemeka.

Je, ni nini kitatokea? Watakikuta kiganja ndani na yule mbwa mtu watamuona? Fuatilia wiki ijayo.
 
tabia ya kuning'iniza wenzako kwenye kitanzi cha taharuki sio nzuri mkuu. mi nimesusa hadi ulete episode zote ndo nitarudi, kwikwikwi!
 
UTAJIRI WA DAMU - 15-


Polisi baada ya kuona gari tulilokuwamo walionyesha kana kwamba walikuwa wakitutii kwani waliweka gari lao kando na kutupisha.
Tukiwa ndani ya gari tuliangaliana tusijue la kufanya, haraka haraka nikamtazama mzee Mitimingi, sura yake ilijaa uoga.
“Kwani kile kiganja kimo ndani?” nilijikuta nimemuuliza.
“Kimo ndani, kwani wewe uliwaambia chochote kuhusu hilo?”


“Hata kichaa hawezi kuwaambia kwa sababu kama ningewaambia ina maana ningejiweka matatani mimi na wewe ndiyo maana nakuuliza kama kiganja kipo ndani au ulikitoa.”
“Kiganja kimo ndani, tena sehemu mbaya sana,”
“Tumekwisha.” Nilisema huku nikimuangalia mzee Mitimingi.
“Kuna mtu una ugomvi naye?” nilimuuliza.
“Sisi wafanya biashara tuna maadui wengi, si unajua watu wana wivu?”
“Sasa sijui tutafanya nini kuokoka na haya majanga. Endela kujifanya mgonjwa,” nilimshauri huku nikiwaza jinsi ya kuwafanya polisi wasiwe na wasi wasi na sisi. Nilishuka kwenye gari nikaenda pale walipokuwa.
“Jamani kulikoni tena? Naona mmetufuata huku nyumbani?”
“Tumeambiwa na Inspekta Ado kwamba tuje kupekua nyumba.”
“Lakini mnapekua nyumba kwa sababu gani? Au mnatutuhumu nini?” niliuliza huku moyo wangu ukidunda.
“Sikiliza Cheprisca. Polisi ukiona wanafuatilia jambo ujue kuna ukweli fulani. Sisi tumeambiwa huyu mzee wako Mitimingi ndiye anayehusika na vifo vingi sana vinavyotokea hapa mjini. Ni vigumu sana kuamini au kupata ushahidi kwa sababu ni mambo ya kishirikina.”
Geti lilifunguliwa na Mmakonde mzee Chambilecho.
“Chacha dada Cheprishika, hawa polichi wanataka nini kwetu hapa?” aliuliza yule mzee mlinzi.
Sikumjibu chochote. Polisi waliingia ndani ya ua na gari lao na mimi pamoja na mzee Mitimingi tukatangulizwa mbele. Kulikuwa na polisi wenye silaha wanne na ambao walikuwa wamevaa kiraia watatu akiwemo yule mama aliyekuwa akituhoji, walivalia magwanda ya polisi.
Tulipoingia ndani walituonyesha hati ya upekuzi yaani search warrant na walikuwa na mtu mwingine ambaye raia aliyeishi katika ule mtaa kama shahidi.
“Tumekuja kusachi nyumba hii kwa sababu tumeambiwa kuwa kuna vitu vipo ambavyo hairuhusiwi kisheria wananchi kuvimiliki,” alisema yule mama huku akimuangalia mzee Mitimingi.
“Mzee umenielewa?” aliuliza baada ya kuona hakuna mtu aliyemjibu.Walianza upekuzi wao jikoni kwa kufunua makabati yote lakini hawakukipata hicho walichokuwa wakikitafuta.
Baadaye waliingia chumba cha wageni wakapekenyua vitanda, makapeti, makabati na hata magodoro mawili yaliyokuwa kwenye vitanda viwili chumbani humo, lakini hawakuona kitu walichokuwa wakikitafuta ambacho mimi nilikuwa sikijui.
“Wewe Cheprisca, hiki ni chumba chako?” Yule askari wa kike aliniuliza. Nilikataa kwa kutikisa kichwa.
“Wewe unalala wapi?”
“Mimi nina chumba changu.”
“Kipi kati ya hivi hapa ndani?”
“Niliposema nina chumba changu nina maana siyo humu ndani, nina maana kuwa nimepanga huko mtaani.”
“Kwa nini upange wakati mzee wako ana nyumba kubwa hapa na haina watu wa kuishi?”
“Niliamua tu kukaa kivyanguvyangu, najitegemea.”
Baada ya polisi hao kupekua chumba cha wageni waliingia katika stoo. Humo walikaa muda mfupi sana kwa sababu hakukuwa na makorokoro mengi, kulikuwa na kigunia cha mchele na unga kilo kumi, maharage na njugumawe kama nusu salfeti.
Lakini wakati maofisa makachero hao wa upelelezi wanatoka katika chumba hicho juu ya kabati waliona gunia likiwa limetundika juu ya waya. Walilifungua na kukuta ndani kuna ngozi za chui mbili.
“Mzee una kibali cha kumiliki ngozi hizi?”
“Sina,” alijibu mzee Mitimingi.
“Hujui kuwa na vitu kama hivi ni kosa kisheria? Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Hamisi Kagasheki kila siku anatangaza vita dhidi ya wanaoua wanyama pori, hujasikia vita hivyo?”
“Nimewahi kusikia.”
“Sasa wewe unambishia siyo?”
”Hapana.”
Waliendelea na ukaguzi wao, waliingia hadi vyooni baadaye walihamia chumba cha mzee Mitimingi. Wakati makachero wale wanaingia katika chumba cha mzee, alianza kutetemeka kama vile amemwagiwa maji ya barafu.
Walipoingia na kufungua kabati la nguo walikumbana na kiganja cha mtu kilichokaushwa.Wakapekua sanduku wakakutana na fuvu la mtu na mifupa ya mkono ikiwa imezungushiwa nguo nyeupe.
Ndani ya sanduku hilo walikuta tunguri mbili zilizokuwa zimevishwa mavazi yaliyokuwa yametapakaa mafuta.
“Mzee hivi vitu vya kwako?” aliuliza kiongozi wa wale polisi, Mzee Mitimingi hakujibu kitu badala yake mkojo ukawa unamtoka.

Je, nini kiliendelea? Fuatilia Jumatano ijayo.
 
UTAJIRI WA DAMU - 16-


ILIPOISHIA
Wakati makachero wale wa polisi wanaingia katika chumba cha mzee, alianza kutetemeka kama vile amemwagiwa maji ya barafu. Walipoingia chumbani na kufungua kabati la nguo walikumbana na kiganja cha mtu kilichokaushwa.
Wakapekua sanduku wakakutana na fuvu la mtu na mifupa ya mkono ikiwa imezungushiwa nguo nyeupe.

"Mzee hivi vitu vya kwako?" aliuliza kiongozi wa wale polisi. Mzee Mitimingi hakujibu badala yake mkojo ukawa unamtoka. SONGA NANYO..

Upekuzi wa polisi katika chumba cha mzee Mitimingi ulichukua muda mrefu hasa baada ya kukuta viungo hivyo vya binadamu ambavyo vilionesha dhahiri kwamba vinahusiana na mambo ya kishirikina.
"Cheprisca, unajua vitu hivi ni vya nini?"
Nilikataa kwa kubetua mabega bila kutoa sauti.
Baadaye walifunua kapeti jekundu chumbani mle na kukuta furushi la nywele. Mwili ulinisisimka kwa kuwa nywele zile nilivipeleka mimi kwa mzee Mitimingi.
Niliingiwa na woga kwa kuwaza kwamba kama mzee huyu atasema aliyezileta nywele zile ni mimi ni wazi ataniingiza katika matatizo mazito.
Polisi wanaweza kuamini kuwa hata kile kiganja na fuvu nimemletea mimi. Niliwaza kuwa makachero wataweza kunitesa ili niseme ni kiganja cha nani wakati sijui chochote kuhusu vitu hivyo.
Baadaye yule kiongozi mkuu wa polisi katika upekuzi ule aliviandika vitu alivyovikuta kuwa amevikuta ndani ya chumba cha mzee Mitimingi kisha akamtaka yule raia ambaye alijitambulisha kwa jina la Ben Mtwanga, mjumbe wa nyumba kumi , atie sahihi maelezo kama shuhuda.
"Bwana Ben Mtwanga wewe ni mjumbe wa nyumba kumi katika mtaa huu na nimekuandika na umetia sahihi kama shahidi wa polisi. Nikufahamishe tu kwamba ukihitajika kutoa ushahidi mahakamani, tutakuarifu. Umeelewa?"
"Nimeelewa," alijibu Mtwanga.
Polisi waliingia chooni kwa mzee Mitimingi kusachi lakini hawakupata kitu chochote cha maana na baadaye wakaingia katika chumba chakuhifadhi spea za magari yake.
Ndani ya chumba hicho walitoa meno kadhaa na kucha za simba ambazo zilikuwa zimewekwa kwenye kibuyu. Ajabu ni kwamba kila akiulizwa swali kuhusiana na vitu hivyo, mzee Mitimingi alikuwa hajibu badala yake akawa ananiangalia mimi.
Nilizidi kuingiwa na woga kwa kudhani kwamba anaweza kunisukumia mimi msala huo wa kukutwa na viungo vya binadamu na nyara za serikali, jambo ambalo sasa serikali inalipiga vita sana.
"Koplo John, nenda na Bwana Mtwanga mkakague mabanda nje," aliamuru kiongozi wa polisi. Moyo ulinipasuka ‘paa'. Ulinipasuka kwa sababu nilijua kuwa siri ya mbwa mtu itabumburuka.
Walianza kuingia katika banda la kuku lakini hawakukuta chochote kisha wakaingia katika banda la ng'ombe.
Wakati wakiendela kukagua vyumba hivyo mbwa mtu akawa anabweka kama ishara ya kuwaita polisi.
"Inaelekea mbwa huyo anayebweka ni mkali sana. Tusikaribie banda lile, anaweza kuchomoka akang'ata watu. Muda wa kuchomwa sindano za tetenasi saa hizi hatuna," alisema yule askari kiongozi wa upekuzi.
"Lakini kule kwetu wazee wanasema ukiona mbwa anabweka sana ujue kuna kitu," alidakia askari mwingine na kunifanya nisikie tumbo langu likinguruma kwa woga maana nilijua kuwa wakienda na kumkuta mbwa mtu, mambo yatakuwa mazito zaidi.
"Hizo imani zimepitwa na wakati. Mbwa yule ni mkali na anatamani ararue mtu," alisisitiza yule bosi wa polisi.
Majibu hayo yalinifanya nipate faraja na hata nilipomuangalia mzee Mitimingi alionekana kufurahia uamuzi wa kuachana na wazo la kwenda kupekua kibanda cha mbwa.
‘Wangejua kuwa banda lile lina kiumbe wa ajabu kamwe wasingeacha kwenda kupekua na kujua siri ya mbwa yule kuwa na sura za binadamu,' niliwaza kimoyomoyo.
Mimi pia nilitamani sana kujua ilikuwaje mbwa yule awe na sura ya binadamu. Lakini tamaa yangu ya kujua hayo ilikatizwa na vile vitu hasa nywele kwa sababu nilijua kuwa mzee Mitimingi akibanwa anaweza kunitaja mimi kuwa ndiye mletaji.
"Sasa mzee Mitimingi, hebu tueleze, hivi vitu ni vya nini na umevipata wapi?" alihoji askari mmoja huku akiwa na daftari lake alilokuwa akitumia kuandika vitu vilivyokutwa ndani ya nyumba ya mzee huyo, alikuwa akingoja jibu aandike.

Je, wakipekua kwenye kile kibanda na kumkuta mbwa mtu nini kitatokea? Fuatilia jumatano ijayo..
 
UTAJIRI WA DAMU - 17-


ILIPOISHIA
"Sasa mzee Mitimingi, hebu tueleze, hivi vitu ni vya nini na umevipata wapi?" Alihoji askari mmoja huku akiwa na daftari lake alilokuwa akitumia kuandika vitu vilivyokutwa ndani ya nyumba ya mzee huyo, alikuwa akingoja jibu aandike. SONGA NAYO...


MZEE Mitimingi alishindwa kutoa jibu badala yake alikuwa akitetemeka huku akitokwa na jasho jembamba usoni.
Ilibidi awe anatumia leso kuondoa jasho lililokuwa likivuja usoni mwake.
Baadaye askari walielekea kwenye banda la mbwa na wakati huohuo mbwa huyo akawa anabweka kwa nguvu sana.
"Huyu mbwa ana jambo, haiwezekani awe akibweka namna hii," alisema askari mmoja aliyeonekana kuwa ni kiongozi wa oparesheni hiyo ya upekuzi.
"Tuhamie kwenye banda la mbwa," aliamuru.
Umati wote ulianza kuelekea kwenye lile banda ambalo mbwa alikuwa akibweka.
"Mzee Mitimingi au wewe Cheprisca mtangulie, mumtoe mbwa kibandani ili tukague ndani."
Maneno hayo yalimfanya mzee Mitimingi azidi kuingiwa na wasiwasi na kunyong'onyea. Ilikuwa karibu adondoke kutokana na wasiwasi aliokuwa nao.
Alilisogelea banda la mbwa na kulifungua. Mbwa haraka sana alichomoka bandani na kuanza kugalagala chini kabla ya kuketi na kutukodolea macho.
Watu wote walipigwa na mshangao kuona mbwa huyo ana sura ya binadamu. Mbaya zaidi alikuwa akitokwa na machozi kama afanyavyo mtu ambaye ameteswa sana na sasa anataka huruma ya mtesaji.
"Mzee Mitimingi, huyu ni mbwa au jini?" aliuliza askari mmoja.
"Naam," aliitikia mzee Mitimingi.
"Unaitikia nini? Jibu swali huyu ni mbwa au jini? Mbwa gani ana pua na macho kama ya binadamu, tena analia machozi kama mtoto wako?"
Hakuweza kujibu na badala yake akawa ameinamisha kichwa chini kwa aibu ya kugundulika siri zake.
Yule askari baada ya kuona mzee Mitimingi hajibu lolote aligeuka na kuniangalia mimi. Alipiga hatua kama tatu na kufika karibu kabisa na niliposimama.
"Chepriska, unaweza kutusaidia, huyu ni mbwa au jini?"
"Mimi sijui."
"Hujui wakati mbwa mtu huyu yupo hapa kwenu? Ina maana wewe hujawahi kumuona humu?"
"Niliwahi kumuona, lakini chochote kuhusu mbwa mtu huyo anajua mzee, mimi sina ninalolijua."
"Unataka kutuambia wewe mara baada ya kumuona mbwa huyu wa ajabu ambaye dunia nzima hayupo kama huyu hukumuuliza mzee wako?"
"Nilimuuliza, mimi pia siku ya kwanza kumuona nilishangaa."
"Alikujibu nini mzee wako?"
"Aliniambia kuwa hadithi ya mbwa huyo ni ndefu."
"Hebu tusimulie hadithi yake maana kama ulivyoona mzee Mitimingi ameshindwa kujibu maswali yetu ya awali."
"Hakunisimulia chochote bila shaka alikuwa akitafuta nafasi ya kufanya hivyo."
Askari aliyekuwa akinihoji aliandika mambo fulani kwenye daftari lake kisha akaniangalia usoni.
"Wewe Cheprisca baada ya kumuona mbwa huyu kuwa ni wa ajabu, uliripoti popote?"
"Hapana."
"Kwa nini?"
"Niliogopa."
"Uliogopa kudhurika na jini au ulimuogopa mzee Mitimingi?"
"Niliogopa vyote, kudhurika na hata mzee kwani alishawahi kunionya."
"Aliwahi kukuonya kuhusu nini?"
"Kuhusiana na huyu mbwa."
"Ilikuwaje mpaka akakupa onyo."
"Siku moja nilimuona mbwa huyo akiwa anamchapa, akanionya kuwa nisimuambie mtu na kama nitakiuka basi kilichompata mbwa huyo kitanipata na mimi."
"Alikuambia kuhusu kilichompata huyo mbwa?"
"Hapana hakuwahi kuniambia."
"Kwa nini usimuulize."
"Sikumuona mbwa huyu siku nyingi, nilimuona juzi tu na leo ndiyo tulipanga anielezee historia yake ambayo alisema ni ndefu sana."
Askari yule alitulia kidogo, akachukua daftari lake na kalamu na kuanza kuandika, bila shaka alikuwa akiandika yale niliyomuambia.
"Umesema siku ya kwanza ulimuona akimchapa mbwa huyu, ilikuwaje? Fafanua kidogo."
"Siku hiyo nilifika hapa nyumbani kama saa kumi na mbili jioni. Nikasikia mbwa akilia, nilichungulia kwenye tundu la geti nikamuona mzee huyu akimchapa huyu mbwa huku akitamka maneno."
"Alikuwa anasemaje?"
"Alikuwa anasema, nakupiga kutokana na kutotimiza masharti niliyokupa."
"Wafunge pingu," yule afisa wa polisi aliamuru, tukafungwa.

Je, nini kitaendelea? Fuatilia simulizi hii wiki ijayo siku kama ya leo.....
 
UTAJIRI WA DAMU - 18-


Baada ya kufungwa pingu mimi na mzee Mitimingi, yule askari aliyekuwa akihoji alitulia kidogo, akachukua daftari lake na kalamu na kuanza kuandika, bila shaka alikuwa akiandika yale niliyomuambia.
Askari walikagua ndani ya banda la mbwa lakini hawakuweza kuambulia chochote.
Yule askari aliyekuwa akionekana kama kiongozi wao alimgeukia mlinzi korokoroni wa mzee Mitimingi ambaye ni mzee wa Kimakonde aitwaye Chambilecho, alikuwa haelewi kinachoendelea kutokana na yeye ;kuganda' getini.
"Wewe askari, njoo," aliitwa kwa sauti kama ya amri ya kijeshi na akatimua mbio kwenda kwa bosi wa askari huyo ambaye alikuwa na redio call mkononi.
"Wewe uliitwa polisi ukahojiwa, kweli au si kweli?"
"Kweli."
"Unajua chochote kuhusu mbwa huyu?"
"Chijui kitu."
"Aliletwa lini?"
"Chijui kabichaa, nilishitukia akibweka."
"Lini?"
"Nimechahau chiku."
"Huyu mbwa umewahi kutumwa kumpa chakula kwenye banda lake?"
"Nzee aliniambia ni malufuku kuchogelea banda lile."
"Alikupa sababu?"
"Hakuchema."
"Uliwahi kumuona?"
"Nimuone wapi? Nilikuwa nachikia akibwekabweka tu."
Yule askari hakuona sababu ya kuendelessa kumhoji korokoroni huyo bila shaka kutokana na kutojua kila analoulizwa.
"Sasa mzee Mitimingi funga nyumba yako kwa funguo na mkabidhi lindo mlinzi wako. Tunakwenda Kituo cha Polisi Nyasa, mambo mengine ataenda kuamua Afande Ado,"aliamuru askari yule.
"Koplo Anjela utakaa na Chepriska nyuma na mzee Mitimingi pia atakaa nyuma ya gari na askari wengine," alizidi kufafanua.
Nilisaidiwa kuingia kwenye ‘Defender' na yule askari wa kike, haikuwa kazi kubwa kwangu kuingia nyuma ya gari hilo isipokuwa shughuli pevu ilikuwa kwa mzee Mitimingi.
Kutokana na utu uzima wake na unene alishindwa kupanda mwenyewe na hata askari mmoja alipojitahidi kumpandisha alishindwa.
Ilibidi askari watatu wafanye kazi ya kumpandisha kwenye gari mzee huyo. Mmoja alikuwa ndani na wawili walikuwa nje ya gari wakawa na kazi ya kumpandisha garini.
"Mzee Chambilecho usisahahu kumpa chakula mbwa," alisema mzee Mitimingi huku akimuangalia mlinzi wake.
"Chacha nzee chakula umiweka wapi?"
"Angalia nyuma ya banda kuna chakula maalum cha mbwa cha kwenye makopo. Kuna katoni moja, utakuwa unampa asubuhi na jioni na maji yasikauke kwenye banda lake. Sawa?"
"Chawachawa."
Askari ambaye alikuwa kiongozi wa msafara alimsifu mzee Mitimingi kwa kukumbuka mbwa kulishwa chakula.
"Umefanya vizuri sana kukumbuka hilo maana hii kesi yako inaweza kuwafanya tukawashikilie kwa siku kadhaa."
"Mtanishikilia siku ngapi?"
"Itategemea! Hii kesi imeingilia majanga ya nchi," alisema askari yule.
"Hii kesi ina majanga, mbona sikuelewi?"
"Hunielewi nini? Ndani ya nyumba kuna kiganja cha mtu, hatujui ni cha mtu wa kawaida au ni albino kutokana na kubadilika rangi na kukaushwa na kuwa cheusi."
"Lakini…"
"Lakini nini? Hata kama mtu aliyekatwa siyo albino bado kukutwa na kiganja ni kesi nzito sana kwa sababu ni jinai. Ni majanga kwa sababu kuna kesi mbili."
"Ipi na ipi afande!" alihoji dereva wa askari.
"Kuna kesi ya kiganja na kuna kesi ya kukutwa na ngozi za chui. Kule kukutwa na nywele siyo kitu sana kwa sababu hata mahakamani anaweza kusema ni zake au za nduguye."
"Sawa afande na huyu dada Chepriska je?"
"Huyu anaweza akawa na kesi nyepesi sana kama ataweza kujieleza vizuri."
"Kwa nini?"
"Kwa sababu hata katika mahojiano hapa sikuona kama ana kesi ."
Gari liliwashwa na hatukuchukua muda mrefu, tulifika kituoni na moja kwa moja tukaenda ofisini kwa Inspekta Ado.
"Afande tumekuta kiganja, ngozi ya chui na nywele, pia kuna mbwa mtu nyumbani kwa mzee huyu."
Afande Ado aliviangalia vitu vilivyotajwa na kumuangalia mzee Mitimingi na mimi.
"Mzee kwa usalama wako tuambie ukweli."alisema Inspekta Ado akiwa amekunja sura.


Nini kitafuata? Fuatilia Jumatano ijayo.
 
Mzizi unatuzingua wewe jumatano ndio hii au siku hizi week mbili mbili kama vipi tuambie hivyo mkuu
 
UTAJIRI WA DAMU-19-


"Mzee Mitimingi hapa umeletwa mbele yangu kwa sababu ya vitu viwili, kiganja cha mkono na ngozi za chui, basi. Unaelewa hili?"
"Naelewa." Akajibu.
"Bila kukutwa na vitu hivyo wala usingehojiwa hapa. Je, kile kiganja ni cha nani?" alihoji mtu yule ambaye ni askari wa upelelezi.
Mzee Mitimingi alipata kigugumizi cha kujibu swali akawa anang'aang'aa macho tu.
SASA TIRIRIKA NAYO..


Ndani ya chumba kile cha mahojiano kulikuwa na baridi kali kutokana na kuwa na kiyoyozi, lakini nadhani iliongezeka mwilini mwangu kutokana na woga wa kesi inayotukabili.
Nilikuwa najiuliza kwamba inawezekana kabisa tukaunganishwa na kesi ya mauaji ikiwa kama kuna maiti iliwahi kuokotwa ikiwa haina kiganja.
Naamini kabisa kuwa woga wangu wa kuhojiwa na polisi haukumzidi mzee Mitimingi ambaye alikuwa akitetemeka waziwazi.
Licha ya mwili wake kutetemeka lakini pia meno yake niliyasikia yakigongana na nikahisi kwamba anaweza kuanguka kwa presha.
Yule askari aliyeletwa atuhoji alikuwa akitembeatembea katika chumba kile kana kwamba hakuwa na kazi ya kufanya.
Baadaye alirudia kumuuliza mzee Mitimingi swali lilelile.
"Kile kiganja ni cha nani?"
Mzee Mitimingi hakujibu akawa anazidi kutetemeka. Nilishitukia akizabwa kibao cha shavuni.
"Mzee sema, nitakuumiza na sitaki kabisa kupoteza wakati hapa. Niambie kile kiganja ni cha nani?"
"Mimi nililetewa tu mheshimiwa."
Baada ya jibu hilo alikula konzi ya nguvu kichwani, akawa anamwagika jasho.
"Sitaki majibu nusunusu, sema aliyekuletea."
"Nililetewa na mganga wa kienyeji."
"Mzee nadhani unataka kuleta mchezo. Huyo mganga hana jina siyo?"
"Anaitwa Mwapacha."
"Anaishi wapi au mtaa gani?"
"Anaishi Mtaa wa Kamchape, jirani na grosari."
"Alikuambia kiganja kile ni cha kazi gani?"
"Alisema kitanifanya niwe tajiri sana."
"Je, tangu akuletee kiganja hicho umetajirika."
"Sikutajirika kwa ajili ya kiganja nilikuwa nimeshakuwa tajiri ila alisema utajiri utaongezeka mara dufu."
"Uliongezeka?"
"Ahh wapi!!"
"Alikuambia sababu za wewe kutotajirika zaidi?"
"Alisema angenipa sababu hivi karibuni."
"Kiganja kile ni cha nani?"
"Sijui, kwa sababu aliniambia nimtafutie kiganja nikasema hiyo kazi sitaweza, akasema ataifanya yeye."
"Je, vipi kuhusu ngozi ya chui?"
"Hii nililetewa na mwindaji mmoja anayeishi Mtandi."
"Mtandi?"
"Ndiyo, Kijiji cha Mtandi."
"Nakifahamu."
"Unafanya biashara haramu ya ngozi za chui wewe mzee?"
"Hapana, sifanyi."
"Sasa wewe ngozi ya chui kuwa ndani ya nyumba yako maana yake ni nini""
"Hapana, hii ngozi siyo yangu…"
"Siyo yako wakati imekutwa ndani ya nyumba yako? Au kuna mtu aliiweka, kama yupo, nitajie."
"Mle ndani niliiweka mimi…"
"Ndiyo maana nikasema umekutwa na ngozi ya chui maana hata wahenga walisema anayekutwa na ngozi ndiye mwizi wa ng'ombe, hujawahi kusikia msemo huo mzee Mitimingi?"
"Nimewahi."
"Basi hili ni lako. Au unamjua huyo mtu aliyekuletea anakaa wapi."
"Ni yule yule mganga wa kienyeji aliyeniletea kiganja cha mtu."
"Khaa! Huyu mtu ana matatizo kweli, kakuletea kiganja, akaleta na ngozi ya chui, hii nayo alisema ni ya kazi gani?"
"Alisema zote hizo zinahusiana na uganga wake wa kunizidishia utajiri."
"Jamani duniani kuna mambo, mzee utajiri wote ulionao unakubali kuwa na vitu vya ajabu nyumbani kwako, tena siyo vya ajabu bali ni vya hatari kwa maisha yako."
"Kweli kijana wangu, nimekosea sana. Mnisamehe."
"Hili siyo jambo dogo tena, hukusoma kwenye gazeti la Uwazi?"
"Sijasoma."
Yule askari alitoa gazeti na kumuonesha mzee Mitimingi. Kichwa cha habari kilikuwa kikisomeka kwa wino uliokolea, ‘Tajiri akamatwa na kiganja, ngozi ya chui na nywele za watoto.'
"Mzee habari ikishatoka kwenye gazeti kama hivi ni sawa na moto wa petroli, kuuzima ni kazi nzito,"alisema yule askari aliyekuwa akihoji.
"Sasa niambie zile nywele ambazo tulizikuta ndani ni za nani?"
"Mwenye nywele simjui, nazo nililetewa."
"Uliletewa na yule yule mganga?"
"Hapana, alileta ni Che … Che…"
"Unababaika nini?"
Nilianza kutetemeka kwa kuona kuwa akinitaja basi nitakuwa nimekwisha.
Kwa kuwa nilikuwa nipo jirani na mzee huyo nilisogeza mguu wangu na kumkanyaga, kumkataza asinitaje.
Aliniangalia huku akibubujikwa na machozi.



Je, Mzee Mitimingi atamtaja Chempriska kuwa ndiye aliyemletea nywele hizo? Fuatilia Jumatano ijayo.
 
UTAJIRI WA DAMU -20-


"Alizileta yule mganga."

Baadaye yule askari alichukua redio call yake na kuzungumza:

"Roja, namba kumi na saba hapa, naomba askari wawili afande." Baada ya kusema hayo

alipunguza sauti ya redio yake hivyo sikusikia jibu alilopewa na badala yake nikaona askari wawili

wanaume wakiingia.


"Tumekuja afande."
"Mchukueni huyo mzee Mitimingi akawaoneshe alipo mganga wake. Mkimkuta mkamateni mleteni hapa."
Alitoa amri na dakika ileile mzee Mitimingi alifungwa pingu na kutoka na askari wale.
Mle ndani ya chumba cha mahojiano tulibaki mimi na yule askari tu na hakuwa ananiangalia usoni.
Nilikumbuka usemi wa wahenga kuwa ukitaka kumuua nyani usimuangalia usoni. Nilijikaza nisionekane natetemeka lakini ukweli ni kwamba nilikuwa natetemeka.
"Msichana taja jina lako."Alianza kunihoji huku akiwa ameketi kwenye kiti kilichokuwa mbele yangu tofauti na wakati anamhoji mzee Mitimingi kwani wakati ule alikuwa akirandaranda chumbani kama vile alikuwa akitafuta kitu.
"Naitwa Cheprisca."
"Uliona nilivyomchapa makofi yule mzee. Sitaki majibu nusunusu, jibu kikamilifu ndiyo tutaelewana," alinionya yule askari.
"Jina langu ni Chepriska Nahatani."
"Kwani wewe baba yako Mchina."
"Hata kidogo baba yangu ni Mmakua."
"Mimi najua Nahatani ni Wajapani na nilivyokuona u mweupe na macho ya Kichina nikadhani baba yako ni Mchina."
"Hapana afande."
"Hebu niambie huyu mzee ni baba yako ki vipi?"
"Mzee Mitimingi siyo baba yangu wa damu ni baba yangu kwa kuwa ana undugu na baba yangu mzazi."
"Undugu wao ukoje?"
"Wamezaliwa kwa mama mkubwa na mdogo lakini mzee Mitimingi ni mdogo kwa baba yangu."
"Ilikuwaje akakuchukua wewe kuishi naye?"
"Alikuja kwa baba na kuniomba akasema anataka niwe mhasibu wa kampuni yake hasa kwa kuwa mimi nilikuwa nimesomea DSA, kule Kurasini."
"Uliwahi kugundua kuwa baba yako anajihusisha na mambo ya kishirikina?"
"Sikujua lolote. Mimi kazi yangu ilikuwa ni kukusanya fedha zinazoletwa na madereva wa malori na mabasi yake kisha kuzipeleka benki."
"Hujawahi kuona kiganja katika nyumba yenu?"
Swali hilo lilifanya moyo huo upige paa, nilijiuliza kwamba labda siku ile nilipokiona kwenye jokofu kuna askari aliniona na ndiyo maana wakaja kutukamata. Hata hivyo, nilijisemea kimoyomoyo kuwa itakuwa ni ujinga kukiri jambo zito kama hilo.
"Kwa kweli sijawahi. Kwanza sikuwa na mazoea ya kuingia chumbani kwake. Ki ukweli sijawahi kuingia chumbani kwa baba."
"Unajua chochote kuhusu mbwa mtu?"
"Ninachokumbuka ni kwamba aliniambia nisilikaribie banda la mbwa kwa sababu alisema ni mkali sana hasa kwa wanawake na mbaya zaidi alinitisha akasema amemchanjia kuuma watu, hivyo anilipiga marufuku hata kwenda kumuona."
"Ina maana wewe hujawahi kumuona huyo mbwa mtu anayesemwa?"
"Siku moja kabla ya polisi hawajatukamata nilimuona mbwa yule, nilimuuliza akasema atanipa mkasa wote kuhusiana na mbwa yule na kuniambia sababu za kuwa na sura kama ya mtu."
"Alikusimulia mkasa huo?"
"Hakuwahi kusimulia kwani tulikamatwa siku ambayo ilikuwa nipate simulizi yake."
"Kuna habari kuwa ulikuwa unashiriki kumletea mzee Mitimingi vitu vya kichawi, niambie kuna ukweli wowote hapo?"
"Hakuna ukweli. Nani kakuambia?"
"Wewe kazi yako ni kujibu maswali yangu na siyo kuniuliza, jibu ndiyo au siyo."
"Hapana."
Baada ya mahojiano hayo niliangalia kwa nyuma kumbe alikuwepo yule askari wa kike ambaye alifanya ukaguzi pale nyumbani kwa mzee Mitimingi aliniambia niinuke, nikatii kisha yule polisi wa kike akanifunga pingu.
"Kamfungie mahabusu." Alitoa amri na yule askari wa kike akawa ananipeleka kwenye mahabusu ya wanawake.
Nilishangaa baada ya kutoka kwenye chumba kile nje nilikuta umati wa watu ulijazana kumuangalia yule mbwa mtu.

Itaendelea wiki ijayo Siku ya Jumatano...
 
Back
Top Bottom