UTAJIRI WA DAMU-23-
Umati wa watu uliminyana kila mmoja akitaka kuona kitakachotokea kwa mbwa mtu ambaye alikuwa akila mkia wa kondoo huku akilia.
Alikuwa akitiririkwa na machozi kama binadamu hasa ikizingatiwa kuwa macho yake yalifanana kabisa na ya binadaamu.
Kutokana na watu kumzunguka mbwa mtu huyo, polisi iliwabidi wafanye kazi ya ziada kuwatawanya na baadaye sangoma akaamua kumchukua na kumuingiza katika chumba chake cha uganga.
Watu hawakuridhika na uamuzi huo kwani walikimbilia dirishani kuchungulia ili waone kinachoendelea ndani, hata hivyo, waligonga mwamba baada ya sangoma kufunga madirisha yote, ndani nilikuwepo mimi Chepriscar, mzee Mitimingi, mbwa mtu na wasaidizi wa mganga.
Haukupita muda mrefu yalianza kusikika manyanga yakipingwa huku nyimbo zikiimbwa na sangoma pamoja na wasaidizi wake. Polisi na watu wengine walikaa nje na kushuhudia moshi wa ubani ukitoka kupitia kwenye nyufa za madirisha.
Baada ya dakika thelathini mganga huku akiwa amejifunika kitambaa cha rangi nyekundu alitoka nje ya ile nyumba na kuanza kutangaza:
Ndugu zangu, kazi imekamilika, mbwa mtu amegeuka binadamu na baada ya dakika chache nitamtoa nje mumuone,
Mtoe sasa hivi, Mtoeeeee, Mtoeeeeeee, zilikuwa ni kelele za watu waliokuwa wameongezeka baada ya habari hiyo kusambaa mji mzima.
Ndugu zangu, tuache apumzike na anapewa dawa ili akili zake ziwe sawasawa
.. Msiwe na shaka atatoka na mtamuona, alizidi kuwasihi, niliogopa nikawa na hofu kuwa wanaweza kuvamia na kuingia ndani kwa nguvu.
Baadaye aliingia ndani na baada ya nusu saa alitoka mmoja wa wasaidizi wake na kumchukua mkuu wa wale polisi wakaingia ndani, alipoingia aliniangalia kama vile alitaka kusema na dakika kumi baadaye walitoka sangoma, kamanda na mtu anayetajwa kuwa aligeuzwa mbwa.
Umati ulishangaa huku wengine wakipiga kelele ambazo hazikuwa zikieleweka walitaka nini kwani wapo waliokuwa wakisema; Azungumzeeee, wengine wakawa wanasema; Mpeni kipaza sauti.
Hii ni kutokana na mkuu wa polisi kutumia kipaza sauti cha kiganjani mara kwa mara alipotaka kuwaambia jambo.
***
Tulikuwa tukishushwa kituo cha polisi kutoka kwenye gari difenda ambalo lilikuwa na askari wenye silaha, watu walikuwa wengi kituoni kushuhudia tukio hilo japokuwa walikuwa wakisogezwa mbali na askari.
Alianza kushuka sangoma, akafuatia mzee Mitimingi kisha mbwa mtu ambaye sasa alikuwa binadamu na alivikwa kile kitambaa cha rangi nyekundu na shati alilopewa na sangoma, nikamalizia mimi.
Wewe Chepriska, mfuate huyo kamanda wa kike akupeleke mahabusu ya wanawake, alisema yule mkuu wa polisi.
**
Ilikuwa ni Jumatatu, saa mbili asubuhu nilishitukia yule askari wa kike akifungua geti la chuma la chumba cha mahabusu.
Cheprisca jiandae, tunawapeleka mahakamani, alisema.
Kwa kosa gani? nilimuuliza.
Utajua hukohuko, aliniambia huku akitoa pingu kwenye mkanda wake.
Nilifungwa pingu hiyo na kupelekwa nje ambako niliingizwa kwenye difenda. Baada ya dakika chache waliingizwa mzee Mitimingi na yule sangoma, lakini yule mbwa mtu ambaye sasa ni binadamu sikumuona, nadhani aliachiwa.
Baadhi ya ndugu zangu walikuwepo na ndugu wa Sangoma pia walijaa tele pale. Dada yangu mmoja aliniambia nisiwe na wasiwasi kwa sababu wamenitafutia Wakili Mabere Marando ambaye nitamkuta mahakamani.
Nilifarijika sana kusikia hivyo lakini nikajua pia kuwa kwa upande wa mzee Mitimingi alitafutiwa wakili aitwaye Dk. Ngali Maita. Ni sangoma tu ambaye sikusikia ndugu zake wakimfahamisha kuwa atakutana na wakili wake huko kortini.
Itaendelea Jumamosi ijayo