Uhaba Kifaa Cha Kuchunguza VVU Kwenye Vituo Vya Afya Zanzibar Unaathiri Vijana Kutambua Afya Zao

G-Mdadisi

Senior Member
Feb 15, 2018
157
99
KUMEKUWA na uhaba wa wa kifaa cha uchunguzi wa Virusi Vya UKIMWI ( HIV Kits) katika vituo vya afya vya serikali Zanzibar jambo ambalo limepelekea huduma ya upimaji wa Virusi Vya UKIMWI kusita.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara iliyofanywa na Chama cha waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) watoa huduma za Afya katika vituo mbalimbali vya Wilaya ya Magharibi "B" na Wilaya ya Kati Unguja, wamesema waathirika wakubwa wa uhaba huo ni Vijana ambao katika siku za hivi karibuni wameonesha mwamko mkubwa wa kutaka kupima VVU na kujua Afya zao hasa kupitia vituo vya huduma rafiki kwa vijana.

Wataalamu hao kutoka kituo cha afya Fuoni, Tunguu, SUZA, Mwera, Magirisi walieleza wananchi hasa vijana wamehamasika kupima VVU na hufika kwa wingi kupata huduma hiyo lakini kutokana na uhaba wa kifaa hicho huduma hiyo haipatikani kwa sasa.

Sultani Shela daktari kiongozi wa kituo cha afya Fuoni, alisema tatizo hilo ni zaidi ya miezi miwili sasa vifaa havipatikani katika vituo vya huduma rafiki kwa vijana pamoja na vituo vya afya hali ambayo wateja hulazimika kwenda katika hospitali binafsi ambapo huduma hiyo hutolewa kwa malipo.

Alisema huduma hiyo hupatikana kwa mama wajawazito pekee kituoni hapo kwa sababu vifaa walivyonavyo ni vichache na mama mjamzito hulazimika kujua afya yake ili kumkinga mtoto na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI.

“Vituo vyote vya Serikali huduma ya upimaji wa VVU ni bure na ndio maana wananchi hufika kwa wingi kwa ajili ya kujua afya zao,” alisema Khadija Ali Khamis wa kituo cha huduma rafiki kwa vijana Mwera.

Waziri wa Afya Nassor Ahmed Mazrui, alikiri uwepo wa uhaba wa kifaa hicho alipohojiwa na Mwanahabari wetu ambapo alibainisha kuwa tatizo hilo limetokana na kuchelewa kufika kontena lenye vifaa hivyo ambavyo hutoka nje ya nchi.

Aidha alisema tayari kontena hiyo imeshafika na kuanzia Septemba 4 vifaa hivyo vitaanza kusambazwa katika vituo vyote vya afya vya serikali ili kuendelea kutoa huduma hiyo ya uchunguzi wa VVU.

Alieleza serikali inapata msaada wa vifaa hivyo kutoka Global fund, na vifaa vilivyofika vitakidhi mahitaji kwa muda wa mwaka mmoja.

Waziri huyo aliwataka wananchi kuendelea kuvitumia vituo vya afya na vituo vya huduma rafiki kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za kiafya ikiwemo uchunguzi wa VVU ambapo maambukizi yake kwa sasa yapo katika makundi maalum ikiwemo vijana wanaotumia dawa za kulevya na wanaofanya biashara ya ngono.

Ziara hiyo ya waandishi wa habari imeandaliwa na Chama cha waandishi wa habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kupitia mradi wa kuendeleza utetezi wa afya ya uzazi kwa wanawake na wasichana mjini na vijijini ambao unaendeshwa na chama hicho Zanzibar katika Wilaya mbili za Unguja ambazo ni Wilaya ya Kati na Magharibi "B" na wilaya ya Chakechake kwa Pemba kwa ufadhili wa Wellspring Philanthropic Fund (WPF) kutoka nchini Marekani.
 
Back
Top Bottom