MSD yasambaza vifaa tiba vya zaidi ya Tsh 930m katika Vituo vya Afya 24 vya Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Dar es Salaam imesambaza vifaa tiba vya zaidi ya sh. milioni 930 kwa ajili ya vituo vya afya 24 vya halmshauri ya Wilaya ya Ulanga.

Akizungumza Wilayani humo mkoani Morogoro, Mbunge wa Jimbo la Ulanga Salim Hasham amesema, wamepokea vifaa tiba hivyo na dawa za zaidi ya Tsh. Milioni 900 kwa ajili ya vituo vya afya vya Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga.

adf308ee-3a00-4bf6-89b6-24d2676d581e.jpeg

c7c506d5-e8fb-4a28-8fdc-d82fb08f725f.jpeg


Amesema kishindo cha Serikali ya Rais Dk.Samia Suluhu Hassan sekta ya afya ni kikikubwa hivyo hatua ya kupokea vifaa tiba hivyo vya kisasa ni muendelezo wa maboresho sekta ya afya ambapo Ulanga na mkoa wa Morogoro kwa ujumla ni wanufaika.

“Huu ni utekelezaji wa Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ibara ya 83 sura ya 3 na kwa kiasi kikubwa Mwenyekiti wetu wa Chama ambaye ndie Rais anatutendea haki sisi wanachama kwa kufanya zaidi ya matarajio yetu, sekta ya afya ni sekta muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa hili.

3701a6c5-84df-423d-89f1-bf6f68092762.jpeg

396e77a3-210c-4a7e-882d-356495890c93.jpeg


“Tunaona mabadilika kwa bohari yetu ya dawa ni makubwa sana kwa miaka mitatu ya hivi karibuni, hapa kwetu hospitali ya wilaya ilikuwa na shida ya X Ray mashine kwa zaidi ya miaka minne lakini tumepata na watu waliokuwa wakienda kupata huduma wilaya nyingine sasa hawahangaiki tena,” alisema.

Alisema, mbali na hatua hiyo wamepokea fedha Sh. milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa hospitali ya wilaya ambapo mazungumzo yanaendelea ili waweze kupatiwa eneo lingine litakalokidhi mahitaji ya wilaya hiyo ambayo kwa sasa ni makubwa yakihusisha wawekezaji na wafanyabiashara wa madini ambao watapatiwa huduma.

Salim alisisitiza kuwa, wilaya hiyo ndani ya miaka mitatu imepata vituo vya afya viwili na zahanati 10 na cha kushangaza vipo vituo vya afya ambavyo havijamaliza ujenzi kikiwemo kituo cha afya cha Ruaha lakini MSD imeshafikisha mahitaji yote muhimu vikiwemo vifaa tiba.

“Zamani vituo vya afya vilikuwa vinaisha na tunakaa kusubiri vifaa tiba zaidi ya mwaka, lakini kwa sasa vifaa tiba vinasubiri mmalize wafunge na wananchi wapate huduma kwa wakati mnyonge mnyongeni haki yake mpeni, MSD mabadiliko ni makubwa sana MSD ya mama yetu Rais Samia sio ile tuliyokuwa tunainyooshea vidole kila wakati,”alisisitiza.

Naye Meneja wa MSD Kanda ya Dar es Salaam Betie Kaema alisema, MSD kwa niaba ya serikali wanaahidi kutomuangusha Rais katika utekelezaji wa majukumu yake, hivyo upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba nchini utaendelea kuimarika zaidi, lengo likiwa ni kuboresha huduma za afya.

Alisema, ujio wa dawa na vifaa tiba hivyo vya zaidi ya sh. milioni 900 ni muendelezo wa maboresho hayo.

“Julai hadi Novemba tumehakikisha dawa na vifaa tiba vya sh. milioni 600 vinaletwa hapa na sasa tumekabidhi dawa na vifaa tiba vya zaidi ya sh. milioni 300, hivyo vituo vya afya 23 vya Ulanga watapata bidhaa za sh. milioni 900 ambazo zote zimekamilika na sasa vinasambazwa vituoni.

“Tunaahidi chini ya serikali yetu na wizara ya afya tutarajie mambo makubwa zaidi kwetu MSD Mkurugenzi wetu Mkuu Mavere Tukai ametuagiza wote tunaosimamia hii mikoa kuwa mawakala wazuri katika kuokoa maisha ya wananchi na maisha ya wananchi yanaokolewa kwa upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba zikiwemo mashine hizi za kisasa za maabara ambazo tumezishusha hapa leo (jana),

Alitaja baadhi ya vifaa tiba ambavyo wamepatiwa wananchi wa Ulanga kuwa ni kiti cha huduma ya meno, vitanda vya huduma ya uchunguzi, vitanda vya wodini vya wagonjwa, vifaa vya joto kwa ajili ya watoto njiti, vifaa vya kusaidia upumuaji, vifaa vya oxygen, vitanda vya upasuaji na Ultrasound mashine.

Vingine ni viti vya kubebea wagonja, vifaa vya kutundikia maji tiba, pasi ya hospitali, stendi ya pazia za kuzibia wagonja, mikebe ya vifaa vya kujifungulia, matoroli ya kutolea dawa, vitanda vya kujingulia na vinginevyo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Alli Ramadhan, alisema kwa sasa hali ya huduma za afya wilayani humo imekuwa na maboresho makubwa kuanzia watumishi, dawa na vifaa tiba.

“Hali ya upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ni asilimia 95 hadi 97 tofauti na awali ilikuwa ni asilimia 70 hadi 80, hali hii imepunguza sana malalamiko ya wananchi na kuwa na imani na watumishi wetu naomba niipongeze sana MSD maboresho ni makubwa kuanzia huduma kwa sisi wateja wao na kupata zile dawa na vifaa ambavyo tulikuwa tunachukua kwa mshitiri na uletaji wa dawa na vifaa kwa wakati mkiagiza hakuna longolongo mnaletewa hii inatuma ari hata sisi katika utendaji wetu,”alisema.
 
Back
Top Bottom