Ada mpya Mlimani itakwamisha maendeleo ya kitaalumaCHUO Kikuu cha Dar es Salaam kinatarajia kupandisha ada kwa kozi zote zinazotolewa chuoni hapo kuanzia muhula wa masomo wa kuanzia Septemba, mwaka huu kwa wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo.
Kwa mujibu wa mapendekezo ya Tume ya Uchunguzi juu ya Uendeshaji wa Vyuo Vikuu na Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa serikali, kwa wastani ada hiyo inatarajiwa kupanda kwa zaidi ya asilimia 40 ya viwango vya sasa kwa kozi zote zinazotolewa kwenye chuo hicho.
Kwa mfano mapendekezo hayo yanaonyesha kuwa kozi za Sayansi ya Jamii isipokuwa Uchumi na Elimu karo itapanda kutoka Sh722,000 kwa mwaka hadi zaidi ya Sh1 milioni kwa mwaka na kozi za sayansi, udaktari na uandishi wa habari kuwa Sh1,122,000 badala ya Sh922,000 huku wanaosoma sheria wakitakiwa kulipa Sh2.5 milioni.
Mchanganuo huo pia unaonyesha kuwa wanaoendelea na masomo watatakiwa kulipa kati ya Sh1.3 hadi 2.5 milioni kwa mwaka kutegemeana na kozi wanazosoma na kwamba ongezeko hilo ni kwa ajili ya ada ya masomo (tuition fee), bila gharama nyingine kama malazi, chakula, vitabu na mahitaji mengine muhimu ya kitaaluma.
Licha ya uongozi wa chuo kusema kuwa haya ni mapendekezo yanayowezakuidhinishwa au kukataliwa na serikali, ni dhahiri kwamba chuo kimepania kuongeza ada kwa kiwango hicho ambacho tunadhani kwamba utakuwa mzigo mkubwa kwa wanafunzi na wazazi.
Kuna fununu kwamba ongezeko hilo ni kama maandalizi kwa chuo hicho kujitegemea kutokana na maelekezo ya serikali kwamba vyuo vyote vinavyojiweza vianze kujiendesha bila kutegemea ruzuku.
Ni dhahiri kwamba ongezeko hilo likipitishwa litakuwa na madhara makubwa kwa wanafunzi na wazazi, kutokana na ukweli kwamba, gharama zitakuwa zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Inawezekana uongozi wa chuo umeliangalia jambo hilo kwa mtazamo kwamba, itakuwa rahisi kupata fedha kutoka kwenye Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ambayo hutolewa na serikali kwa wanafunzi wanaotimiza masharti.
Hata hivyo, bado mzigo huo unawaelekea wanafunzi na wazazi kwa kuwa ndiyo watakaolipa mkopo huo baada ya kumaliza masomo na zaidi ya hapo, wanatakiwa kuchangia asilimia 40 ya fedha hizo, ambalo pia ni tatizo kutokana na wengi kutokuwa na uwezo.
Itakumbukwa kwamba, mwaka jana kulitokea mgomo chuoni hapo baada ya kufukuzwa wanafunzi walioshindwa kulipa asilimia 40 ya ada hiyo mpaka serikali ilipoingilia kati na kuwasaidia walioshindwa kabisa.
Si hivyo tu, kuna baadhi ya wanafunzi ambao hawana sifa zinazotakiwa kupata mkopo huo, lakini wana sifa za kusoma Chuo Kikuu, ambao hulipiwa na wazazi wao, kwa hiyo kuongezwa kwa karo unakuwa mzigo mzito unaoweza kusababisha baadhi yao kushindwa kuendelea na masomo na idadai ya wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho kupungua kwa kiasi kikubwa.
Tunashauri kwamba, kama suala hilo halijapelekwa serikalini uongozi wa chuo ufikirie upya juu ya viwango hivyo na kama kuna haja ya kuongeza, ongezeko lisizidi asilimia 20 ili wanafunzi waweze kusoma na taifa letu liendelee kupata idadi kubwa ya wasomi na wataalamu wanaohitajika sana kwa maendeleo ya taifa letu katika karne hii.
Hata kama mapendekezo hayo yamepelekwa, serikali ione umuhimu wa kushusha na badala yake vyuo vishauriwe vitafute njia mbadala ya kupata fedha badala ya kuwatwisha mzigo wanafunzi na wazazi. Tunaamini kwamba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambacho kinaaminika kitaaluma, kina uwezo kwa kupata fedha kutoka kwenye miradi mbalimbali ya utafiti ambazo zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuziba upungufu utakaotokea endapo serikali itapunuguza ruzuku au fedha za uendeshaji wa chuo hicho bila kuongeza ada kwa asilimia kubwa.