Jamani hapa mkuu wa kaya anastaili pongezi, mafisadi watapona kweli?
Baadhi ya pikipiki ambazo Rais Kikwete alikuwa azigawe jana
Zilitolewa na wafanyabiashara kwa CCM Arusha
Mussa Juma, Arusha
RAIS Jakaya Kikwete jana alikwepa kugawa pikipiki 19 zilizonunuliwa na wafanyabiashara na viongozi wa CCM wilaya ya Arusha kwa ajili ya watendaji wa chama hicho huku akiwataka wawe makini na misaada.
Kinyume na matarajio ya viongozi wa CCM Wilaya ya Arusha walioandaa hafla kubwa ya ugawaji wa pikipipiki hizo Kikwete aliwakatalia na kuwataka wazigawe wenyewe.
"Pikipiki ni zenu mnajua mlipozipata mimi nimezishuhudia
gawaneni wenyewe," alisema Rais Kikwete.
Hali hiyo ilijitokeza mara baada ya Rais Kikwete kufika katika ofisi za wilaya hiyo na kuonekana kubadilika sura na kutumia dakika tano tu katika hotuba yake na kuondoka.
Rais Kikwete mara kwa mara alikuwa akizungumza na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mohamed Mbonde na Mwenyekiti wa mkoa, Onesmo ole Nangole ambao kwa mujibu wa ratiba hawakuwa wamepewa nafasi kuzungumza.
Baadaye baada ya majadiliano na meza kuu, ratiba hiyo ilibadilishwa na nafasi ya kumkaribisha Rais Kikwete ambayo awali ilikuwa ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Jubilate Kileo ilihamishiwa kwa Nangole
Katika hafla hiyo, wafanyabiashara mbalimbali wa mkoa wa Arusha walihudhuria akiwamo mmoja wa watuhumiwa wa wizi wa Fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje ya Benki Kuu ya Tanzania (EPA), (jina linahifadhiwa) ambaye alikuwa meza ya mbele, mkuu wa mkoa wa Arusha, Isdori Shirima na madiwani wa CCM.
Katika hotuba yake fupi, Kikwete aliwataka viongozi wa CCM kuwa makini na misaada ambayo wanapata kwa ajili ya chama chao.
"Ni kweli hatuwezi kujenga chama bila ya kuwa na rasilimali bora, lakini pia msitafute rasilimali zitakazowaletea matatizo," alisema Rais Kikwete bila ya kufafanua.
Alisema ameziona pikipiki hizo, lakini hatazigawa kwa kuwa hana muda kutokana na kuwahi uwanja wa ndege na akawaachia jukumu la kuzigawa viongozi wenyewe wa CCM wa Wilaya ya Arusha.
Rais Kikwete pia aliwataka wana CCM Wilaya ya Arusha kuanza kujiandaa na uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mara baada ya maneno hayo, Rais Kikwete aliaga na kuondoka na kuwaacha wana CCM wakiwa wameduwaa.
Hata hivyo, katika hali ya kuonyesha kukerwa na alichokibaini Rais Kikwete, ilidaiwa baadaye kuwa aliwaita uwanja wa ndege Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arusha, Kileo na Katibu wake, Mohamed Nyawenga.
"Wameitwa uwanja wa ndege katibu na mwenyekiti hivyo sasa hatujui nani atagawa tena hizi pikipiki," alisema kiongozi mmoja wa CCM wilaya.
Kabla ya kuitwa uwanja wa ndege, Kileo alikuwa ameomba kukutana na wajumbe wa kamati ya siasa ya wilaya katika ofisi za chama jambo ambalo pia lilikwama.
Hadi saa 17:30 jioni hakuna kiongozi yoyote wa CCM ambaye alikubali kugawa pikipiki hizo na hivyo kuwaacha makatibu kata wa CCM waliotakiwa kuchukua pikipiki hizo wakihangaika kujichagulia kila mtu ya kwake.
Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Arusha, Semmy Kiondo ambaye alikuwa kiongozi pekee wa wilaya aliyebaki katika ofisi hiyo jana, alisema msemaji wa kilichotokea ni katibu wa wilaya.
"Mimi sio msemaji wa hili suala naomba uwasiliane na katibu wa wilaya ambaye kaondoka na mwenyekiti
na hizi pikipiki tutazigawa,"alisema Kiondo.
Awali, akisoma risala kwa Kikwete, Nyawenga alisema pikipiki hizo 19 zina thamani ya shilingi milioni 24.7 na zimetolewa ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utendaji wa viongozi wa kata za CCM katika Wilaya ya Arusha.
Mara baada ya Rais Kikwete kuondoka watu walikusanyika katika makundi katika viwanja wa CCM na wengi walionekana kumpongeza Rais kwa kutojiingiza katika ugawaji wa pikipiki hizo.
"Rais wetu yupo makini hawezi kujiingiza katika hili suala lenye utata,"alisema
kiongozi mmoja.
Hata hivyo, wengi waliitafsiri hali hiyo na makundi ndani ya CCM Mkoa wa Arusha hasa yaliyotokana na uchaguzi mkuu ndani ya chama hicho mwaka jana, huku wengine wakisema ni sehemu ya juhudi za rais kupambana na vitendo vya ufisadi.
Tuma maoni kwa Mhariri
Contact Us DISCLAMER
Email:webmaster@mwananchi.co.tz © Mwananchi Communications Ltd 2006- 2009