Mvutano mkubwa Kamati Kuu CCM
2007-07-31 10:44:42
Na Mary Edward, PST, Dodoma
Mvutano mkubwa umeibuka ndani ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM iliyoanza kukutana mkoani Dodoma tangu Jumamosi iliyopita, hali ambayo imesababisha Kamati hiyo kuongeza siku moja zaidi.
Katika hali ya kawaida kamati hiyo hukutana kwa siku mbili, lakini mvutano huo umesababisha kuendelea kwa muda wa siku tatu.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kamati hiyo zimesema kuwa kumeibuka makundi mawili, moja likitaka vijana wapewe nafasi nyingi zaidi, huku kundi lingine likitaka vigogo ambao wengi ni wazee ndani ya chama hicho wabakishwe.
Chanzo chetu cha habari kilisema jana kuwa mvutano huo umekuja baada ya mtandao unaowatetea vijana kutoa nafasi nyingi kwa kundi hilo na kusababisha vigogo wanaoshikilia nafasi hizo na ambao wanazitetea katika uchaguzi huo kuachwa.
``Hali hiyo imeibua hasira kutoka kwa baadhi ya wazee wa CCM na kusababisha kikao kushindwa kumalizika ndani ya siku mbili na hivyo kuendelea tena leo ambayo ni siku ya tatu,`` kilisema chanzo hicho cha habari.
Chanzo hicho kilisema kwa kuwa mtandao wa vijana ndio unaoonyesha kuwa na nguvu zaidi kwa upande mwingine matokeo yanaweza kuwa tofauti.
Chanzo kulitabiri kuwa mvutano huo unaweza kusababisha mpasuko mkubwa kwa kuwa vijana wengi hawajakomaa kisiasa.
``Kuna usemi unaosema kuwa uzee ni dawa ? Sasa endapo nafasi nyingi za wazee zitaondolewa, kunaweza kutokea mpasuko ndani ya chama,`` kilisema chanzo hicho.
Wakati hayo yakiendelea, Chama cha Mapinduzi kimevionya baadhi ya vyombo vya habari vinavyotoa taarifa juu ya kikao hicho, kwa madai kuwa baadhi ya taarifa si za kweli.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Itikadi na Uenezi, Bw. Aggrey Mwanri, iliwataka waandishi kusubiri taarifa rasmi itakayotolewa na chama hicho.
Wakati huo huo, Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (NEC) inakutana kwa kikao cha siku mbili mjini Dodoma kuanzia leo na kesho.
Mkutano huo utafanyika chini ya Mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete.
Miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na hali ya kisiasa nchini, kupokea taarifa ya ziara ya Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Rais Aman Abeid Karume na kuteua wagombe uongozi wa CCM ngazi za Wilaya, Mikoa na Taifa.
Hata hivyo, hadi mwandishi wetu alipokuwa anaondoka nje ya viwanja vya mkutano jana saa mbili kasorobo usiku, mvutano katika mkutano huo ulikuwa haujamalizika.
SOURCE: Nipashe