JF Summary
Senior Member
- Jul 3, 2015
- 163
- 108
Utangulizi
Oktoba 29, 2025 Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu katika mazingira yanayoelezwa kuwa yenye hali wasiwasi mkubwa na taharuki. Uchaguzi huu unakuja takriban mwaka mmoja baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, uliosababisha mijadala mikubwa kutokana na matukio ya ukiukwaji wa haki za wagombea, uonevu, mauaji na vitendo vya kuzuia baadhi ya watu kushiriki katika uchaguzi huo. Tukio hilo lilichukuliwa na wengi kama ishara mbaya, na wachambuzi kadhaa walitabiri kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu ungekuwa mbaya zaidi, huku wengine wakihofia huenda vifo na vurugu vikaongezeka kutokana na ongezeko la misuguano ya kisiasa na uminywaji wa haki.
Kumbukumbu ya Uchaguzi wa 2020 bado ina uzito mkubwa katika mjadala wa sasa. Uchaguzi huo ulilalamikiwa kwa kuwa na kiwango kikubwa cha uonevu, ukandamizaji wa wapinzani, na mazingira yaliyokuwa hayatoi nafasi sawa ya ushindani baada ya wagombea wa vyama vya upinzani kuenguliwa na wagombea wa CCM kupita bila kupigwa. Wakati tukikaribia kwenye uchaguzi mkuu 2025 viongozi wengi wa kisiasa na wasio wa kisiasa walijitokeza kukosoa uchaguzi mkuu waa 2020 wengi wakisema ulikuwa "Uchafuzi". Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) pia hawakuwa na maoni tofauti kwenye hilo, miongoni mwa waliotoa kauli hiyo ni Abdulrahman Kinana, ambaye alikiri kuwa chaguzi za 2019 na 2020 zilikuwa za uonevu na zilileta hofu akiahidi kuwa yale ya 2019 na 2020 yasingejirudia na kwamba chini ya Rais Samia uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025 utakuwa wa Huru na wa Haki. Kauli hiyo ilionekana kama ahadi ya mwanzo wa mageuzi kuelekea siasa za ushindani wa haki, japokuwa baadhi walikuwa na mashaka kama hayo kweli yangetekelezeka, 2024 na 2025 zikasubiriwa kwa hamu.
Hata hivyo, kuelekea uchaguzi wa mwaka huu 2025 hali imeonyesha tofauti, ahadi ile ilikuwa ni maneno matupu! Wadau wa siasa na wanaharakati wamekuwa wakisisitiza kwamba uchaguzi huu haupaswi kufanyika bila kwanza kufanyika mabadiliko ya msingi kwenye sheria za uchaguzi ili kuweka uwanja sawa wa ushindani. CHADEMA ilitangaza wazi kutoshiriki uchaguzi huu hadi mabadiliko hayo yafanyike, ikitoa wito kwa Watanzania kuwaunga mkono katika kuhakikisha serikali ya Chama Cha Mapinduzi inatekeleza takwa hilo.
Kilichowashangaza wengi ni baadhi ya wanachama wa CCM wenyewe kama Humphrey Polepole na Askofu Josephat Gwajima kujitokeza hadharani kupitia mitandao ya kijamii kupinga uchaguzi huu kufanyika bila mabadiliko ya msingi, wakilaani pia vitendo vya utekaji na ukandamizaji vinavyowakumba wale wanaokosoa serikali, uchaguzi, au wanaopanga kuandamana na kwa nyakati tofauti kuitaka Serikali kumwachia Tundu Lissu - Mwenyekiti wa CHADEMA ambaye anaonekana kuwa mpinzani mkubwa wa Samia na CCM na kesi yake ya uhaini kufutwa ili wote washiriki kwenye uchaguzi kukiwa na uwanja sawa wa ushindani. Hali ilizidi kuwa ya taharuki baada ya Gwajima kujificha mafichoni kwa hofu ya usalama wake Polepole kuripotiwa kutekwa na watu wasiyojulikana huku Mafwele akitajwa kuhusika na tukio hilo.
Oktoba 27, audio iliyovuja mtandaoni ambapo Afande Muliro na Mafwele walisikika wakiwa kwenye mkutano wa ndani na askari wakitoa takwimu za watumishi wa umma waliokamatwa kutokana na kuunga mkono maandamano huku wakitishia askari kutojihusisha na maandamano hayo kwani wanaweza kufa. Pia waliwapa askari maagizo ya kufuatilia mazungumzo ya magrupu ya Whatsapp ili kuhakikisha wanazuia wale wote wanaopanga kuandamana. Audio hiyo ilichukuliwa na wengi kama uthibitisho mpango wa polisi kukamata wote wanaopanga kushiriki maandamano yanayotarajiwa kufanyika siku ya uchaguzi, Oktoba 29 pamoja polisi na kuhusika kwenye vitendo vya utekaji vinavyotokea nchini ambapo polisi wamekuwa wanatajwa mara kwa mara kama wahusika wakuu. Tukio hilo limechochea hasira kubwa kwa wananchi na kuongeza mwito wa kushiriki maandamano, hatua iliyoongeza mvutano na hofu kuelekea siku ya uchaguzi.
Kwa hali ilivyo sasa, uchaguzi wa kesho Oktoba 29 unaonekana kuwa wa aina yake — ukiwa si tu kinyang’anyiro cha kisiasa, bali pia jaribio la wananchi kudai haki, mageuzi, na uwajibikaji wa viongozi kupitia njia ya amani. Je, uchaguzi utafanyika kama ilivyokuwa miaka iliyopita au maandamano yatafanikiwa na kuwa mwanzo wa mageuzi kwenye siasa za Tanzania? Oktoba 29 inasubiriwa kutegua kitendawili hiko!
======================
Muhtasari wa Matukio – Oktoba 27, 2025
- Polisi wamethibitisha kumkamata mfanyabiashara ‘Niffer’ leo Oktoba 27, 2025, maeneo ya Sinza Kumekucha, kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu na kuharibu miundombinu kuelekea Uchaguzi Mkuu. Awali taarifa zilidai alitekwa na ‘watu wasiojulikana’, jambo lililozua taharuki mtandaoni. Wananchi mitandaoni wameonyesha hasira na mashaka kuhusu utaratibu wa kihuni uliotumika kumkamata ikiwemo kumpiga.
- RC Chalamila amewatoa hofu wakazi wa Dar kuhusu hali ya usalama na kuwataka washiriki kupiga kura siku ya uchaguzi akisema vyombo vya ulinzi viko imara. Wengi mitandaoni wameonyesha kuunga mkono maandamano na kuahidi kutokwenda kupiga kura.
- Kenani Kihongosi (Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM) ameongelea press ya Askofu Gwajima, akisema kauli za askofu huyo ni za uchochezi na zilizojaa upotoshaji mwingi kwani nchi ipo salama. Wananchi wengi wameonesha kuumunga mkono Gwajima kwa ujasiri wa kuikosoa CCM na kuongelea kuhusu utekaji, huku wengi wakifurahi kuona yuko mzima kwani ulipita muda mrefu bila kuonekana mtandaoni kama alivyoahidi; wengi walidhani huenda naye ametekwa kama ilivyokuwa kwa Polepole.
- Prof. Issa Shivji ameeleza kwamba utekaji ni aina ya utesaji wa hali ya juu unaodhalilisha utu wa binadamu, na kwamba kiongozi yeyote anayevumilia au kususia matukio ya utekaji si muumini wa usawa wa binadamu. Amesisitiza umuhimu wa kushughulikia matukio hayo kwa haraka, kufuata taratibu za kisheria, na kukomesha desturi ya kutumia mabavu. Wananchi mitandaoni wameunga mkono kauli yake, wakisema matukio ya utekaji yanapaswa kulaaniwa, huku wakikosoa matumizi mabaya ya nguvu na madaraka ya kisiasa dhidi ya raia.
- Prof. Anna Tibaijuka (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi enzi za Rais Kikwete) ameonya kwamba utekaji usipokomeshwa utaleta ugaidi na kutaka mtu akikosea, taratibu zifuatwe kwa kufikishwa mahakamani ili haki ipatikane la sivyo wote tutaumia kutokana na matokeo ya vitendo hivyo kutokomeshwa. Wananchi mitandaoni wamekuwa na maoni mbalimbali wengi wamempongeza kwa onyo alilotoa huku Polisi wakiendelea kulaumiwa kwa kuruhusu utekaji uendelee nchini na baadhi kushutumiwa kuhusika kwenye matukio hayo.
- Mafwele na Murilo wamesikika kwenye audio iliyovuja wakisikika wanawaonya askari kuhusu kujihusisha na utekaji; huku wakiwaambia wachunguze makundi ya WhatsApp na waripoti wanaohusishwa na maandamano, pia wametoa takwimu za Polisi, Wanajeshi na watumishi wengine wa umma waliokamatwa (na wanaoendelea kushikiliwa nchini) kutokana na kujihusisha na maandamano na huku wakitoa vitisho ikiwemo kifo ikiwa askari yeyote atakaidi na kujihusisha na maandamano hayo. Wananchi wengi wameonesha kukasirishwa na tukio hilo huku wakichukulia hilo kama sababu nyingind ya wao kujitokeza kuandamana ili kukomesha uonevu wa Polisi ambao wanatumika na CCM (chama tawala) kuumiza wananchi. Wengine wamechukua maneno hayo kama onyo la kuwa makini zaidi ili waweze kufika siku ya kuandamana wakiwa salama.
- Mabasi mengi mikoani na huduma za usafiri majini (kama Azam Marine na Zan Fast Ferries) yametangaza kusitisha safari zao kuanzia Oktoba 28 hadi 30, hasa Oktoba 29, siku ya Uchaguzi Mkuu, ‘ili kurahisisha upigaji kura’. Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kimeeleza sababu za kusitisha safari, lakini Chama cha Kutetea Abiria kimekosoa hoja hizo kikisema hazina mashiko kwani kila mtu ana mahitaji yake ya kijamii na kifamilia. Wananchi wamekuwa na maoni tofauti juu ya hilo, wengi wameonesha kushangazwa na jambo hilo huku wakionesha wasiwasi wa upatikanaji wa huduma muhimu siku hiyo, mfano matibu huku wachache wakiona kwa kufanya hivyo itarahisha watu kushiriki vizuri zoezi la kupika kura.
====
Muhtasari wa Matukio – Oktoba 28, 2025
Wenje asema CHADEMA hawataki kukosolewa, ukihama chama wanasema hauna akili
Aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje, ambaye sasa ni mwanachama wa CCM, amezua mjadala mtandaoni baada ya kuilalamikia CHADEMA kuwa haipendi kukosolewa wala kuambiwa ukweli. Akizungumza katika kipindi cha Dakika 45 cha ITV, Wenje alisema kuwa unapokuwa kwenye chama hicho unaonekana mtu wa maana, lakini ukihama wanasema huna akili. Kauli yake imezua hisia mseto mtandaoni, baadhi wakimtuhumu kuwa ameuzwa kisiasa na sasa anatumia majukwaa kuishambulia CHADEMA badala ya kuelezea sera za chama chake kipya, huku wengine wakimtaka aache kulalamika na kuonyesha tofauti za kweli alizoona ndani ya CCM.
Jeshi la Polisi lasema litawachukulia hatua wanaohamasisha vurugu hata kama ‘wakitiki’
Jeshi la Polisi limewaonya wahamasishaji wa maandamano kuwa watachukuliwa hatua hata kama watakuwa ‘wametiki’ (ikimaanisha kupiga kura), huku likieleza kuwa hakuna tishio lolote la kiusalama kuelekea Uchaguzi kesho Oktoba 29 na kwamba kuna kikundi cha watu ambacho baada ya kushindwa kuvuruga amani wameunda kundi la vijana wanaotengeneza video na taarifa za matukio ya zamani ili kuleta taharuki. Suala hili limeibua mjadala mtandaoni, baadhi wakishangaa kama kuhamasisha maandamano au kuhoji uvunjifu wa sheria ni kosa, huku wengine wakiona wanayofanya polisi ni utekelezaji wa maagizo kutokna huenda wamelipwa kufanya hivyo.
Waziri Bashungwa aonya vijana kufanya maandamani, asema watakutana na visiki
Akizungumza katika mkutano wa kufunga kampeni za CCM Oktoba 28, 2025, Waziri wa Mambo ya Ndani na mgombea ubunge wa Karagwe, Innocent Bashungwa, amewaasa vijana wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuwaonya kuepuka vurugu au uchochezi siku ya uchaguzi, huku akiahidi ulinzi imara ili wananchi wapige kura kwa amani. Kauli yake imepokelewa kwa namna tofauti mtandaoni, wengi wakimkosoa kwa kutozungumzia uhalifu unaokithiri nchini hasa kutokana na matukio ya utekaji unaofanywa na ‘watu wasiojulikana’, na wengine wakijiapiza kujitokeza siku ya uchaguzi kwaajili ya kuandamana
Makonda asema wasiolitakia mema taifa waliumia kuona hakuna vifo ajali ya SGR Oktoba 23
Mgombea ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia CCM, Paul Makonda, amezungumzia ajali ya treni ya SGR iliyotokea Oktoba 23, 2025 mkoani Pwani, akisema kuwa wale wasiolitakia mema taifa waliumia kuona hakukuwa na vifo katika ajali hiyo na kwamba huduma zilirejeshwa ndani ya saa mbili pekee, ameyasema hayo katika mkutano wa kufunga kampeni za mgombea Urais wa CCM uliofanyika katika viwanja vya CCM Kirumba jijini Mwanza. Wananchi wengi wamekosoa kauli ya Paul Makonda wakisema alizungumza maneno yasiyofaa mbele ya Rais, kwani hakuna mtu anayefurahia wengine wakifa na ndio maana wanataka kuandamana ili matukio ya uteji na wananchi kuuliwa yakomeshwe, na wengine wakisema hayo ni matokeo ya uchawa uliopitiliza kiasi kwamba mtu anasema kitu chochote bila kufikiria ili mradi wamfurahishe Samia ili waweze kupata teuzi.
Manara asema hakuna mtu mwenye ubavu wa kutoka kuandamana kwa jinsi Jeshi la Polisi lilivyojidhatiti
Mgombea wa Udiwani wa Kata ya Kariakoo kupitia CCM, Haji Manara, amesema kuwa hakuna mtu atakayetoka kuandamana kama baadhi wanavyodai kwenye mitandao ya kijamii. Amesema ameshuhudia majaribio ya Jeshi la Polisi likiwa limejipanga kwa nguvu kubwa, likitumia farasi wapatao 3,000 ambao walitembea kutoka Leaders Club hadi Bibi Titi, pamoja na mbwa elfu kumi akisisitiza kuwa hakuna mtu atatoka kwenda kuandamana. Kauli ya Manara imewakasirisha wananchi wengi, wakisema propaganda hizo hazitawazuia kujitokeza kuandamana Oktoba 29, huku wengine wakimkosoa kutumia kivuli cha dini kueneza chuki za kisiasa.
Hitimisho kampeni za Urais CCM na chapuo kwa mgombea huyo vyatawala kwenye magazeti, upinzani wachomoza kiduchu
Vyombo vya habari hasa magazeti vimeipa uzito mkubwa tukio la CCM kuhitimisha kampeni zao za mgombea wa Urais jijini Mwanza pamoja na kuweka tangazo linaloelezea jinsi ya kumpigia kura Samia na mgombea mwenza wake, Nchimbi huku habari za vyama vingine zikiachwa au kuwekwa kwa uchache. Baadhi ya wananchi wameonesha kutofurahishwa na hali hiyo wakikosoa vinavyochapisha taarifa hizo kuwa vimenunuliwa na CCM na kwamba hawana ushawishi tena, huku wengine wakisema muda si mrefu habari hizo zitabadilika kwani wananchi watakuwa wamerudisha nchi mikononi mwao hivyo habari za CCM hazitatawala tena kwenye vichwa vya habari.
TLP, AAFP wajiondoa mbio za Ubunge na Udiwani Arumeru Mashariki na Magharibi wakidai kuchezewa rafu
Chama cha TLP, AAFP watangaza kujiondoa katika mbio za ubunge na udiwani katika majimbo ya Arumeru Mashariki na Magharibi, kikidai kuhujumiwa na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC). Katibu wa AAFP, Mgina Ibrahim, amesema wasimamizi wa uchaguzi wameshindwa kuwapatia orodha ya vituo vya kupigia kura na wamewanyima haki ya kuwa na mawakala, akiongeza kuwa tayari wamewasilisha malalamiko kwa INEC lakini hawajapatiwa majibu hadi sasa. Wananchi wengi wamesema hayo ndio matokeo ya kuisaliti kampeni ya “No Reforms, No Elections” hivyo waache kuzua taharuki na kulalamika.
Kura ya mapema Zanzibar; ACT walalamika kufanyiwa rafu
Wakati upigaji kura wa mapema kwa makundi maalum ukianza Zanzibar Oktoba 28, mgombea wa ACT-Wazalendo Jimbo la Pangawe, Omar Said Shaaban, ameeleza wasiwasi kuhusu dosari alizoshuhudia kituoni, ikiwemo uwepo wa watu wengi wanaodaiwa kuwa wanajeshi wa JWTZ waliowasili kwa magari ya kijeshi bila vitambulisho, akisema ni aina ya hujuma kwani hawafahamiki eneo hilo. Pia alitaja ukosefu wa vifaa na wapiga kura kuruhusiwa kutumbukiza sehemu ndogo ya kidole kwenye wino. Mgombea wa Mji Mkongwe, Ali Saleh, naye alikosoa ZEC kwa kupoteza udhibiti wa idadi ya wapiga kura na kudai baadhi wanapiga kura zaidi ya mara moja, huku wengine wakiingia kama wafanyakazi wa tume bila vitambulisho halali. Mwenyekiti wa ZEC, George Kazi, alikiri changamoto hizo lakini akasema zimeshughulikiwa, akisisitiza kuwa wote waliopiga kura ni raia halali waliosajiliwa. Wananchi wahoji kwamba ACT walisema njia ya kuiondoa CCM ni kushiriki uchaguzi na kuhakikisha wanalinda kura, sasa inakuaje wanalalamike wakati walionywa na wakapuuza?
BAVICHA waunga mkono maandamano Oktoba 29
Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) limetoa tamko la kuunga mkono maandamano ya amani yatakayofanyika Oktoba 29, 2025, yenye lengo la kudai uchaguzi huru, haki na kupinga ufujaji wa rasilimali za Taifa. BAVICHA imesema hatua hiyo ni sehemu ya kuunga mkono msimamo wa chama wa “No Reforms, No Election” na kuungana na vijana wa kizazi kipya (Gen Z) wanaopaza sauti dhidi ya changamoto za ukosefu wa ajira, matukio ya utekaji na mauaji. Baadhi ya wananchi wamewapongeza BAVICHA na kuona tamko hilo kama sehemu ya kuongeza hamasa kwa wananchi kujitokeza kudai haki huku wengine wakihofia kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha chama kufutiwa usajili wake.
===
Muhtasari wa Matukio – Oktoba 29, 2025
October 29, 2025 | 5:00 am
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametoa wito kwa wananchi kulinda amani katika siku ya uchaguzi, akionya kuwa vurugu za kisiasa zinaweza kuathiri uchumi. Akizungumza Sinza, alisema vijana waliokuwa nje usiku walikuwa wakihangaikia shughuli halali, na polisi wapo kudumisha utulivu. Aliongeza kuwa machafuko yanaweza kusimamisha biashara na kudhoofisha ustawi wa wananchi na taifa, huku akibainisha kuwa wanaochochea vurugu wengi wapo nje ya nchi.
October 29, 2025 | 5:15 am
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, amewahakikishia wakazi wa jiji hilo kuwa usalama umeimarishwa kikamilifu kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Akizungumza Sinza, alisema polisi wapo kila eneo kuhakikisha wananchi wanapiga kura kwa amani na kuwataka kurejea nyumbani au kuendelea na shughuli zao baada ya kupiga kura.
October 29, 2025 | 07:00 am
Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa rasmi kote Tanzania kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, ambapo wananchi wanachagua Rais, Wabunge na Madiwani. Kura zilianza kupigwa saa 1:00 asubuhi na zinatarajiwa kumalizika saa 10:00 jioni, huku vituo vya magereza na taasisi za mafunzo vikiendelea hadi saa 3:00 usiku ili kutoa fursa kwa wanafunzi na wafungwa waliostahili kupiga kura ya urais.
October 29, 2025 | 07:15 am
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla, amepiga kura katika kituo cha Hospitali ya AICC na kupongeza maandalizi mazuri ya uchaguzi. Amesema kuwa utaratibu wa upigaji kura ni mzuri na usalama umeimarishwa katika vituo vyote, huku akihimiza wananchi kutumia likizo ya siku hiyo kushiriki zoezi hilo muhimu kwa utulivu.
October 29, 2025 | 07:30 am
Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, amethibitisha kuwa hali ya usalama nchini ni tulivu na hakuna tishio lolote lililoripotiwa. Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura bila woga, akibainisha kuwa polisi wapo vituoni kote nchini kwa ufanisi na haki ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani.
October 29, 2025 | 08:00 am
Mgombea urais wa Tanzania kupitia chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Paul Kyara, amepiga kura katika kituo cha Mbuyuni Changanyikeni jijini Dar es Salaam akiwa na mke wake. Baada ya kupiga kura, aliahidi kupambana na msongamano wa magari Dodoma, kurejesha uwajibikaji serikalini, na kuwekeza katika sekta za kilimo, viwanda na teknolojia kwa lengo la kuunda ajira milioni 10.
October 29, 2025 | 08:10 am
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia CCM, Dkt. Hussein Mwinyi, amepiga kura katika kituo cha Kariakoo, Jimbo la Kwahani, akiwa na familia yake. Baada ya kupiga kura, alisifu maandalizi ya Tume ya Uchaguzi na mwitikio mkubwa wa wananchi, akiwahimiza wote ambao hawajapiga kura kujitokeza. Aidha, alitaja hali ya amani iliyopo tangu kampeni hadi siku ya kupiga kura kuwa ya kutia moyo.
October 29, 2025 | 08:30 am
Spika wa Bunge na mgombea ubunge wa Uyole, Dkt. Tulia Ackson, amewahimiza wakazi wa jimbo lake kujitokeza kwa wingi kupiga kura. Akiwa amepiga kura katika kituo cha Tambukaleli, Dkt. Tulia alisifu mwamko mkubwa wa wapiga kura na hali ya utulivu, akisisitiza kuwa polisi wapo kulinda usalama, si kuwatisha wapiga kura, na kuwataka wananchi kuendelea kushiriki kwa amani na uwajibikaji.
October 29, 2025 | 09:30 am
Maandamano yamezuka eneo la Ubungo–Kimara wakati Watanzania wakielekea kupiga kura, huku polisi wakilazimika kuingilia kati kuwatawanya waandamanaji. Tukio hilo, lililorekodiwa kwenye picha na video zilizosambaa mitandaoni, linadaiwa kusababishwa na madai ya dosari katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Oktoba 29 2025 saa nne asubuhi
Wananchi wamezidi kujitokeza eneo la kimara na kuanza kusogea kuelea Shekilango, huku shekilango tayari kukiwa na watu waliojitokeza wakiwa tayari kujiunga na wengine kwenye maandamano hayo. Polisi wametoka na kuanza kupiga risasi juu ili kutawanya waandamanaji. Maeneo ya Kariakoo napo wananchi wameanza kuongezeka barabarani kufanya maandamnao.
Oktoba 29, 2025 Saa tano asubuhi
Vituo vya mwendokasi Ubungo, Kimara vimechomwa moto. Zimamoto wamejaribu kuzuia moto lakini wameshindwa nguvu na waandamanaji na hivyo kukimbia na kuacha vituo vikiendelea kuwaka moto.
Saa sita mchana
Msuguano kati ya wananchi na polisi unaendelea, huku mabomu ya machozi yakirushwa wakati waandamanaji wakiendelea kuongezeka kwenye eneo hilo.
Saa saba mchana
Wananchi wanaendelea na maandamano katika maeneo mbalimbali Dar, huku polisi wakiendelea kujaribu kuwatuliza raia na mabomu ya machozi.
Muhtasari wa Matukio - Novemba 4, 2025
Heche atuhumiwa kujihusisha na Vitendo vya Kigaidi
Taarifa iliyotolewa na Wakili Hekima Mwasipu imeeleza kuwa Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, amesafirishwa leo Novemba 4 kutoka Dodoma hadi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tuhuma mbili za kujihusisha na vitendo vya kigaidi—katika maeneo ya Kimara hadi Magomeni, na Msewe hadi External. Kwa mujibu wa wakili wake, Heche ametumia haki yake ya kisheria kukataa kuandika maelezo ya onyo, akieleza kuwa atayatoa mahakamani huku taarifa zisizo rasmi zikieleza kuwa anaweza kufikishwa mahakamani muda wowote. Wananchi wanahusisha tuhuma hizi na maandamano yaliyofanywa Dar es Salaam kupinga uchaguzi, huku wengi wakionesha mshangao, wakisema Heche alikuwa gerezani Dodoma hata kipindi cha uchaguzi na kuhoji inawezekanaje atuhumiwe kuhusika na matukio yaliyotokea wakati akiwa kizuizini? Huku wengine wakisema matukio yanayofanywa sasa yanawazishia hasira wananchi wambao wanaomboleza kupoteza wapendwa wao jambo linaloweza kusababisha maandamano mengine yafanywe ndani ya muda mfupi ujao.
Huduma ya Mwendokasi Dar yasitishwa kuanzia November ili kufanya tamthmini ya uharibifu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kusitishwa kwa huduma ya usafiri wa Mwendokasi kuanzia Novemba 04, 2025, baada ya vituo vingi kuharibiwa na kuchomwa moto wakati wa maandamano Oktoba 29. Amesema usafiri huo umesitishwa katika njia za Morogoro na Mbagala (BRT 2) ili kufanyika tathmini ya uharibifu. Aidha, ameiagiza LATRA kutoa vibali kwa wamiliki wa Daladala kutoa huduma ya dharura katika maeneo hayo. Baadhi ya wananchi wameitaka serikali kurekebisha uharibifu badala ya kusitisha huduma, huku wengine wakipendekeza barabara za BRT zifunguliwe pia kwa magari binafsi ili kupunguza msongamano. Wapo waliouona uamuzi huo kama hatua ya kisasi kufuatia maandamano yaliyofanywa kupinga uchaguzi, na wakasisitiza haja ya serikali kushughulikia chanzo cha hasira za wananchi badala ya kuchukua hatua za kulipiza
Zuio la kutotoka ndani kuanzia saa 12 jioni kwa wakazi wa Dar laondolewa
Jeshi la Polisi nchini limetangaza kuondolewa rasmi kwa amri iliyowataka wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kubaki majumbani kuanzia saa 12 jioni. Taarifa hiyo iliyotolewa Novemba 04 imeeleza hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maelekezo ya Rais Samia yaliyotolewa Novemba 3 baada ya uapisho wake, alipoagiza kuwa shughuli za wananchi zirejee katika hali ya kawaida. Wananchi wengi wameonyesha hasira kubwa dhidi ya Jeshi la Polisi kufuatia mauji yaliyotokea siku ya maandamano wakilitaka jeshi hilo kutoka hadharani na kueleza kwanini waliua raia, huku wananchi wengine wakionesha kutokuwa na imani na jeshi hilo.
Wananchi wakosoa ukimya wa vyombo vya habari wakati na baada ya maandamano, baadhi wajieleza
Wananchi wengi wamelalamikia ukimya wa vyombo vya habari vya ndani kufuatia mauaji na vurugu zilizotokea wakati wa maandamano ya siku ya uchaguzi, Oktoba 29. Wameutafsiri ukimya huo kama ishara ya uoga na kutumika na dola, wakisema vyombo hivyo vimepoteza wajibu wake wa kuhabarisha umma kwa uwazi na uadilifu. Wamepongeza vyombo vya habari vya kimataifa kwa kuripoti matukio hayo kwa ujasiri, huku vya ndani vikitajwa kukaa kimya kana kwamba havioni majonzi na mateso yanayowakumba Watanzania. Hali hii imezua hasira na masikitiko makubwa mtandaoni, huku wengi wakiamini kuwa tasnia ya habari imepoteza uaminifu na imeshindwa kusimama na wananchi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na majeruhi. Kwa utetezi wao, baadhi ya vyombo vya habari vimetoka hadharani wakisema tuzimwa kwa mtandao kumefanya wengi wakose namna ya kutoa taarifa kwa wananchi kwa wakati, ufafanuzi ambao kwa baadhi ya wananchi umechukuliwa kama namna ya kujitetea baada ya wananchi kuvikosoa
Amnesty International yalaani ukandamizaji wa haki za binadamu wakati mtandao ulipozimwa nchini, wananchi waelekezana kufikisha malalamiko ICC
Baada ya taarifa ya Amnesty International kulaani Mauaji na ukandamizaji wa haki za binadamu uliofanyika wakati huduma za Mtandao na Intaneti zilipozimwa nchini kufuatia maandamano yaliyofanyika siku ya uchaguzi mkuu Oktoba 29, wananchi wameelezea hasira na majonzi wakitaka hatua za haraka zichukuliwe dhidi ya waliohusika na mauaji ya waandamanaji. Wengi wametoa maoni kuwa viongozi wa kidikteta hawasikii maneno bali vitendo, wakisisitiza haja ya haki kwa jamaa zao waliouawa au kujeruhiwa wakati wa maandamano. Baadhi ya raia wamehoji takwimu rasmi za vifo, wakisema idadi ni zaidi ya 3000 tofauti na ile 700 iliyotangazwa awali, wakionyesha masikitiko makubwa na kukosa imani na mamlaka za nchi katika kushughulikia matukio hayo ya kikatili, wakati baadhi ya wanaharakati na wananchi wakielekeza umma jinsi ya kufikisha malalamiko yao ya juu kilichotokea pamoja na ushahidi kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ili serikali ya Rais Samia ilipe madhila waliyosababishia Watanzania.
Wanachi wakosoa ukimya wa wasanii juu ya vifo vilivyotokea baada ya maandamano
Wasanii wa Bongo fleva wameendelea kukosolewa vikali na wananchi baada ya kukaa kimya kutokana na vifo vya raia vilivyotokea Oktoba 29 na 30, wakati wa maandamano yaliyokuwa na lengo la kushinikiza Serikali na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kusitisha uchaguzi mkuu wa 2025 kwa madai ya kutokuwa huru na haki. Baada ya muda, baadhi ya wasanii walianza kuonyesha msikitiko juu ya vifo vilivyotokea na kutoa pole kwa wafiwa na familia za waliopoteza maisha huku wakisisitiza Amani, Mshikamano na Umoja. Wananchi wengi wameonyesha hasira na kadhia juu ya kitendo cha wasanii hao kukaa kimya, kwa kutokuzungumzia vifo vilivyotokea mpaka wananchi walipoanza kupika kelele na kukosoa hilo wakisema kitendo cha wasanii kutoa pole ni unafiki na kuwa wamefuata maagizo ya CCM na si matakwa yao, wengine wamejiapiza kutoshiriki tena kwenye matamasha yao wala kuunga mkono kazi zao na kuendesha kampeni (#Unfollow) ambayo inalenga kuhamasisha wananchi kuacha kuwafuatilia mtandaoni.
Makalla awahakikishia wananchi Arusha, wageni na watalii hali ya usalama ni shwari
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amewahakikishia wananchi wa mkoa huo, wageni na watalii wanaofika Arusha kuwa hali ya ulinzi na usalama ni shwari, huku shughuli za kijamii na kiuchumi zikirudi katika hali yake ya kawaida. Makalla amebainisha hayo leo Jumanne Novemba 04, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yake. Wananchi wameonyesha kukosa imani katika usalama unaodaiwa kuwa upo katika jiji hilo hasa baada ya wananchi kushuhudia jinsi polisi walivyokuwa wakiua na kujeruhi ndugu na jamaa zao wakati maandamano ya kupinga uchaguzi yalipokuwa yakiendelea ambapo wananchi wengine walifuatwa majumbani mwao na kumiminiwa risasi. Wengine wamedai kuwa wamefukuzwa na mgambo wa jiji wakiwa bado wanaendelea na shughuli zao leo, huku wengine walisema kuwa hatua ya kutolewa kwa vitambulisho ili kutambua uraia wao imeonekana kuwa kero.
Wananchi wandelea kushea picha na video kama uthibitisho kuwa waliouliwa kwenye maandamano ni Watanzania
Baada ya jeshi la polisi na mamlaka kusema raia wa kigeni ndio waliosababisha vurugu nchini na kwamba walioonekana wamekufa wakati wa maandamano sio Watanzania, wananchi wameendelea kutoa video na picha kuonesha watu mbalimbali wakiwemo maafuru wenye uraia wa Tanzania waliokufa kwa kupigwa risasi wakati wa maandano na kuhoji je, hao ni raia wakigeni. Suala hilo limechukuliwa na wengi kama namna ya serikali na vyombo vya ulinzi kukwepa uwajibikaji juu ya vifo vilivyotokea wakati wa maandamano.
Muhtasari wa Matukio - Novemba 5
Mbatia asisitiza miili ya vijana waliopoteza maisha kwenye maandamano kurejeshwa kwa familia zao
Mwanasiasa mkongwe James Mbatia, akizungumza Novemba 05, 2025, amesema hali ya kisiasa iliyoibuka baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 si suala la kisiasa pekee, bali ni matokeo ya “maumivu ya wengi dhidi ya wachache.” Ametoa wito kwa mamlaka kuruhusu miili ya vijana waliopoteza maisha siku ya maandamano kurejeshwa kwa familia zao kwa heshima, akisisitiza umuhimu wa utu, uungwana na maadili ya kiimani katika kushughulikia tukio hilo. Maoni ya wananchi yanaonyesha kumpongeza Mbatia kwa ujasiri wake wa kuzungumzia hali hiyo iliyoathiri familia nyingi za waathirika.
Musiba aachana na siasa, atoa wito wa kudumisha amani
Mwanasiasa Cyprian Musiba ametangaza rasmi kuachana na siasa na kujiondoa katika vyama vyote vya siasa, akitoa wito kwa Watanzania kutafakari hatima ya taifa lao kwa kudumisha amani, umoja na mshikamano. Kupitia ujumbe wake Novemba 5, Musiba amesema taifa linapaswa kurejea kwenye misingi ya utu, upendo na uvumilivu aliyoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere, akisisitiza kuwa licha ya maumivu na vifo vilivyotokea, visasi havina nafasi. Hata hivyo, maoni ya wananchi yamegawanyika wengine wakimkosoa wakidai amejiondoa kwa sababu mfumo umemjia vibaya, na wengine wakimkosoa kwa kutozungumzia masuala ya haki kwa uwazi.
Jeshi la Polisi Kilimanjaro lasema hakuna ripoti ya vifo au majeruhi kufuatia vurugu za maandamano wakati wa uchaguzi
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, SACP Saimon Maigwa, ameeleza kuwa hakuna ripoti yoyote ya mauaji au majeruhi ya raia au askari mkoani humo kufuatia vurugu za maandamano wakati wa uchaguzi, na badala yake Jeshi hilo limewashikilia watu 11 tu kwa tuhuma za kuchochea vurugu huku wengine 300 wakiwa wameachiliwa baada ya kubainika kuwa hawakuwa na makosa yoyote walipokamatwa. Aidha, amesisitiza kuwa taarifa za vifo katika mamlaka ya Mji mdogo wa Himo kutokana na maandamano si kweli. Wananchi wamepinga kauli hiyo wakidai kuwa sio za kweli, wakieleza kuwa baadhi ya vijana walipoteza maisha siku ya maandamano mkoani hapo, huku wakibainisha kuwa taarifa za polisi kwamba hakuna vifo au majeruhi hazilingani na matukio yaliyotokea.
Chacha Heche asema Viongozi wa CHADEMA wanakamatwa kwa tuhuma za kuratibu na kuchochea Maandamano Oktoba 29
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Mara, Chacha Heche, ameeleza kupitia mahojiano na DW kuwa viongozi wengi wa chama hicho wamekamatwa hasa katika Wilaya ya Bunda na kupewa kesi za kuratibu na kuchochea maandamano yaliyofanyika Oktoba 29, 2025, akisisitiza kuwa maandamano hayo yalifanywa na wananchi bila chama kuhusika. Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa mtandaoni, ambapo baadhi ya wananchi wamehoji maridhiano yaliyokuwa yameahidiwa na Serikali ya Rais Samia ndani ya siku 100 baada ya uchaguzi kugeuka kukandamiza wapinzani, huku kitendo cha wapinzani kukamatwa kuonekana kama namna ya CCM na serikali kukwepa kuwajibika na uvunjifu wa haki za binadamu uliotokea wakati wa maandanamo
Diaspora wa Tanzania waandamana kupinga mauaji ya raia wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, wataka Rais Samia ashtakiwe ICC
Baadhi ya Watanzania waishio Uholanzi, Afrika Kusini, Holland na Ubelgiji wamefanya maandamano Novemba 5, wakipinga mauaji ya raia yaliyotokea nchini Tanzania wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025. Waandamanaji walibeba mabango yenye jumbe mbalimbali ikiwemo kuhamasisha usitishwaji wa mauji Tanzania pamoja na kuhimiza haki ipatikane kwa waathirika wa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu. Waandamanaji hao wametaka Uchaguzi wa Oktoba 29 ufutwe kwa madai ya kutokuwa huru na haki pamoja na Rais Samia kuchunguzwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), na Katiba mpya ipatikane ili kuimarisha misingi ya haki, demokrasia na uwajibikaji. Suala hilo limeonekana kuungwa mkono na wananchi wengi wakiamini kuwa shinikizo la ndani na nje ya nchi linaweza kuchochea kupatikana haki na kuwawajibisha watakaobainika kufanya makosa.
Wabunge Wateule waitwa Bungeni; Uchaguzi wa Spika na uthibitisho wa Waziri Mkuu kufanyika Novemba 11, 2025
Wabunge wateule wametangaziwa kufika kwaajili ya shughuli za usajili na taratibu nyingine za kiutatawala zitakazofanyika Dodoma, Novemba 8 mpaka 10 huku kikao cha kwanza cha Bunge la 13 kikitarajiwa kufanyika Novemba 11 ambapo uchaguzi wa Spika, kiapo cha uaminifu kwa Wabunge, kuthibitisha uteuzi wa Waziri Mkuu, uchaguzi wa Naibu Spika pamoja na ufunguzi rasmi wa Bunge vitafanyika. Wananchi wameendelea kuhoji matokeo ya ubunge pamoja na ya Rais wakisema uchaguzi huu uliofanyika Oktoba 29 umekosa sifa kutokana na hali ilivyokuwa siku hiyo ambapo sehemu nyingi watu hawakushiriki uchaguzi pamoja na udanganyifu unaodaiwa kufanywa na wasimamizi wa uchaguzi walioonekana katika maeneo mbalimbali kupitia video zilizosambaa mtandaoni wakijaza karatasi za uchaguzi zilizokuwa zimebaki siku hiyo.
Mwabukusi alaani kukamatwa kwa Heche, asema tuhuma za ugaidi hazina msingi, aonya Matumizi mabaya ya vyombo vya dola
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Boniface Mwabukusi, amelaani vikali kumhusisha Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Bara, John Heche, na tuhuma za ugaidi, akisema hatua hiyo haina uthibitisho na inaashiria matumizi mabaya ya vyombo vya dola. Kupitia ukurasa wake wa X Novemba 5, Mwabukusi amekosoa Ofisi ya Mashtaka (DPP) na Jeshi la Polisi kwa, kama alivyoeleza, “kumwaga petroli kwenye moto,” akionya kuwa hatua hizo zinachochea hasira zaidi kwa wananchi na kuvuruga amani huku akizitaka mahakama kutojihusisha na ukandamizaji wa demokrasia. Pia amesisitiza kuwa kabla ya mazungumzo ni lazima wale wote waliohusika na mauaji na utekaji wa raia kabla, wakati na baada ya uchaguzi wawajibishwe kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu kupitia Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC), akisema mazungumzo kabla ya uwajibikaji kwa yaliyotokea ni kutukana wote waliouawa bila hatia na kubariki udhalimu uliofanyika. Kauli zake zimeibua mjadala mkubwa mtandaoni, baadhi ya wananchi wakimpongeza kwa ujasiri na kuuita msimamo wake ni wa kizalendo, huku wengine wakimkosoa wakisema angechukua hatua za kisheria zaidi badala ya matamko pekee.
Kenan akosoa wananchi kuharibu mali wakati wa maandamano, ahoji aongelee watu kufa kwenye nini?
Katibu Mwenezi wa CCM, Kenani Kihongosi, akiwa mubashara kupitia mtandao wa Instagram alikosoa vikali wanaharakati waliohamasisha maandamano siku ya uchaguzi Oktoba 29, akieleza kwamba kutokana na wao baadhi ya wananchi walifanya vurugu na uharibifu wa mali na kwamba jambo hilo halikubaliki. Alipouliza kuhusu vifo vilivyotokea aliwajibu wananchi kwa swali, aongelee watu kufa kwenye nini mbona wao (waliouliza swahi hilo) hawajafa? Wananchi wameonyesha kukerwa na kauli ya Kenani, wakihoji kwa nini anakemea maandamano lakini hakuwahi kulaani vitendo vya kukamatwa, kupotea au kutekwa kwa wananchi. Wamesema kauli hiyo imeonyesha kutojali maisha yaliyopotea wakati wa maandamano, huku wengine wakidai ilikuwa ya dharau na iliyokosa utu.
Serikali yadaiwa kuzuia matangazo ya Al Jazeera nchini Tanzania
Baada ya kituo cha kimataifa cha Al Jazeera kurusha taarifa na video zinazoonyesha mauaji yaliyotokea Tanzania wakati wa maandamano katika siku ya uchaguzi Oktoba 29, 2025, watazamaji wamegundua kuwa kituo hicho kimeondolewa kwenye visimbuzi vingi vya ndani, ikiwemo Azam, StarTimes, na Zuku. Aidha, tovuti ya Al Jazeera imeripotiwa kuzuiwa kufunguka bila kutumia VPN. Hatua hii imeibua maswali kutoka kwa wananchi wanaouliza sababu za kuficha taarifa ikiwa serikali inasisitiza kuwa hakuna maandamano wala mauaji yaliyotokea. Wengine wamekosoa hatua hiyo wakisema inalenga kudhibiti taarifa kuhusu hali halisi nchini. Baadhi wamesisitiza kuwa hata bila Al Jazeera, mitandao ya kijamii na mawasiliano ya moja kwa moja yataendelea kufichua ukweli.