TWAWEZA yawasilisha Matokeo ya Mpango wa 'KiuFunza' ambao umesaidia Wanafunzi 26,000

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,811
11,981


Baada ya majaribio ya miaka mitatu, Twaweza, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, wameonesha kuwa malipo ya fedha kwa walimu kulingana na utendaji (au malipo ya ufaulu) yanaweza kuchangia kuboresha stadi za msingi za kusoma na kuhesabu kwa wanafunzi wote wa elimu ya msingi.

Matokeo ya mbinu hii ya motisha ijulikanayo kama KiuFunza, ambayo ni ya kipekee Afrika Mashariki, yatawasilishwa kwenye hafla ya kuwatunuku baadhi ya walimu malipo ya bakshishi yao Jijini Dodoma tarehe 7 Mei 2022. Wabunge na Maafisa kutoka Wizara za Elimu na Halmashauri husika watahudhuria hafla hiyo.

KiuFunza ni mpango unaotoa bakshishi kwa walimu kulingana na matokeo ya ujifunzaji wa wanafunzi wao. Mpango huu umefanyiwa majaribio makini tangu mwaka 2013 ili kuzitaarifu sera za serikali. KiuFunza imepitia awamu tatu hadi sasa, kila awamu imekuwa ikibuni vipengele vipya ili kuboresha utekelezaji wake na matokeo yanayopatikana.

Katika awamu hii, Maafisa wa Uthibiti Ubora wa Shule walikuwa sehemu ya timu ya utekelezaji wa KiuFunza. Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ilitoa ushirikiano mzuri, ukiwepo ushauri wa kuandaa upimaji, kutoa takwimu na kibali cha kuzifikia shule za mpango wa KiuFunza. Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) lilipitia na kutoa ushauri kuhusu majaribio ya wanafunzi.

Matokeo muhimu:

Matokeo ya awali yanaonesha kuwa KiuFunza inachangia maboresho kwenye viwango vya ufaulu sawa na theluthi moja ya ziada ya mwaka wa masomo. Hivyo, theluthi moja ya mwaka wa masomo huongezwa kwenye kile ambacho kwa kawaida mwanafunzi hujifunza. Utafiti unaonesha zaidi kuwa wanafunzi wasiofanya vizuri wananufaika zaidi na programu ya KiuFunza.

Zaidi ya hayo, utafiti unaonesha kuwa wanafunzi wenye uwezo mdogo au matokeo duni wananufaika zaidi

Mwezi Aprili 2022, Twaweza iliwazawadia fedha za motisha walimu wa masomo wa darasa la kwanza, la pili na la tatu na walimu wakuu kutokana na utendaji kazi wao ulioboresha ufaulu mwaka 2021. Walimu 547 wamenufaika na mpango huu

Shule tisa zilizofanya vizuri zaidi kwa ujumla katika kila mkoa zimepokea bonasi ya miundombinu kwa ajili ya miradi watakayoichagua wenyewe.

Thamani ya jumla ya fedha zote zinazotolewa kama bakshishi kwa kila mwaka ni Tsh 204,000,000, ambazo hulipa walimu wa masomo na walimu wakuu kutoka shule 100 za mikoa sita. Wastani wa bakshishi kwa kila mwalimu ni 3.5% ya wastani wa mshahara wa mwalimu wa mwaka mzima.

Karibu walimu wote wanaunga mkono wazo la kuwapatia bakshishi walimu wanaofanya vizuri zaidi kwa kuangalia ujifunzaji wa wanafunzi. Asilimia 77 ya walimu wanaona ni jambo zuri sana, na wachache kati yao wanaona si jambo zuri sana (asilimia 19).


Mwaka 2021
Shule 100 katika wilaya 21 zilishiriki kwenye upimaji wa majaribio; Shule 100 zilikuwa kundi linganishi.
Wanafunzi 26,751 wa madarasa ya mwanzo waliandikishwa na kunufaika na programu hii.

Matokeo haya yanatoka awamu ya tatu ya KiuFunza. Awamu ya kwanza ilifanya majaribio ya kupeleka moja kwa moja shuleni ruzuku wa wanafunzi (ambayo ilipitishwa na serikali kama sera mwezi Januari 2016) na kulipa fedha kwa walimu kulingana na utendaji - tofauti na kwa pamoja. Awamu hii ilipata mafanikio makubwa kwenye matokeo ya kujifunza kutokana na mchanganyiko wa motisha ya walimu na utoaji wa moja kwa moja wa fedha za ruzuku ya wanafunzi. Awamu ya pili ilitumia uzoefu wa awamu ya kwanza na kufanyia majaribio mifumo tofauti ya motisha kwakuwa utaratibu wa kupeleka ruzuku ya wanafunzi moja kwa moja shuleni ulikuwa umepitishwa na serikali. Katika awamu hii ya tatu, Twaweza imekuwa ikifanya majaribio ya mfumo mmoja wa motisha ambao kwa sehemu umeunganishwa na mifumo ya serikali.

Twaweza ilichagua kujikita kwenye mbinu ya kutoa motisha kwa walimu kupitia KiuFunza, kwasababu ushahidi kutoka mahali kote duniani unaonesha kuwa jitihada za walimu zina mchango mkubwa kwenye kuboresha matokeo ya kujifunza. Aidha, KiuFunza (na tafiti nyingine) zinaonesha wazi kuwa motisha ya walimu, uwajibikaji na jitihada za kusaidia wanafunzi wafanye vizuri zaidi ni nadra sana.

Ni asilimia 17 tu ya walimu ndio wanaopenda kufundisha madarasa ya mwanzo ya shule za msingi (darasa la IIII), hii ina maanisha kuwa walimu hawana ari ya kufundisha madarasa haya muhimu.

Mazingira ya kufundishia na kujifunzia ni magumu zaidi kwa madarasa ya mwanzo. Walimu wa madarasa haya (darasa la I-IV) wanalazimika kufundisha wanafunzi hadi 100 au zaidi ikilinganishwa na wastani wa wanafunzi 65 kwa darasa la V-VII.

Walimu wana makadirio makubwa yasiyo na uhalisia kuhusu uwezo wa wanafunzi wao: walimu wa darasa la I-III walikadiria kuwa wanafunzi wao asilimia 70 wangeweza kusoma hadithi ya Kiswahili na kuielewa vizuri, lakini walipopewa majaribio, ni asilimia 27 tu ndio waliweza kufanya hivyo. Vile vile walimu hawa walikadiria kuwa wanafunzi wao asilimia 78 wangeweza kufanya hesabu rahisi za kujumlisha namba kati ya 1 na 20, matokeo ya majaribio yalionesha asilimia 32 tu ya wanafunzi ndio waliweza kufanya hivyo.

Asilimia 41 ya wanasema usimamizi haujawahi kufanyika kabisa, wakati asilimia 36 wanasema huwa unafanyika angalau mara moja kwa mwezi.

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, alisema “KiuFunza inaendelea kuboresha ujifunzaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka la tatu. Kwa sababu ya matokeo haya mazuri , Twaweza imepata ufadhili mpya utakaotuwezesha, kwa kushirikiana na serikali, kupanua jitihada ya KiuFunza”.

Aliendelea kusema kuwa "Pia tunaona mfano mzuri wa KiuFunza umeigwa na wadau mbalimbali wa elimu. Mfano mmoja ni wa Mbunge wa Ubungo, Dar es Salaam aliyetoa motisha kwa walimu wa hisabati kwa kutumia mbinu ya KiuFunza, na jimbo hilo limeboresha ufaulu wa somo la hisabati kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma. Sote tuna jukumu la kufanya kuhakikisha watoto wanajifunza na walimu wanahamasishwa na kuwajibika kufundisha watoto kwa mafanikio.

Twaweza inafanya kazi ya kuwawezesha wananchi kuchukua hatua za kuleta mabadiliko na serikali kuwa wazi na sikivu zaidi nchini Tanzania, Kenya na Uganda.

KiuFunza ni mfumo wa motisha unaounganisha malipo ya bonasi ya walimu na ujuzi wa KKK (kusoma, kuandika na kuhesabu) unaofanywa na wanafunzi wao. KiuFunza imetekelezwa na kujaribiwa shuleni kote nchini Tanzania tangu 2013. Mfumo wa bonasi wa KiuFunza unalenga walimu wa Darasa la 1-3, kwasababu walimu hawa wanawajibika kufundisha stadi za muhimu za KKK na wana madarasa makubwa zaidi. Walimu hulipwa kulingana na kiasi ambacho wanafunzi wamejifunza: kadiri watoto wanavyozidi kupata ujuzi wa msingi darasani (unaopimwa na tathmini huru), ndivyo bonasi ya ufaulu inavyoongezeka.

Muundo wa jitihada ya KiuFunza: mwanzoni mwa mwaka wa masomo, wafanyakazi wa programu ya Kiufunza hutembelea shule, kuwaeleza walimu kuhusu ofa ya bonasi na kuandikisha walimu watakaoshiriki; mwishoni mwa mwaka wa masomo wanafunzi wanapimwa kuona viwango vya ujuzi waliopata; kwa kuangalia alama za majaribio walizopata wanafunzi, malipo yanakokotolewa na motisha hutolewa kwa mwalimu husika mwanzoni mwa mwaka ujao. Muhimu zaidi, shule na wasimamizi hupokea ripoti ya ufaulu wa wanafunzi kulingana na somo na darasa husika ili kuwasaidia kutambua mapungufu na kuboresha utendaji wao.

Takwimu za walimu na shule zilitolewa katika muhtasari huu zimetokana na utafiti wa awali na uchambuzi wake uliofanywa Shirika la RISE nchini Tanzania mwaka 2019. RISE Tanzania ni sehemu ya jitihada ya RISE (Utafiti wa Kuboresha Mifumo ya Elimu), ambao ni program ya kimataifa ya utafiti. Takwimu zilikusanywa kati ya tarehe 18 Februari na 10 Mei, 2019 kwenye shule za msingi zipatazo 397, Maafisa Elimu Wilaya 22, na Maafisa Elimu Kata wapatao 397 kutoka mikoa sita ya Tanzania: Simiyu, Pwani, Singida, Tanga, Songwe na Kigoma, walishiriki.
 
Huku nilipo daraja A” mwalimu analipwa 20000 ... daraja B “ 10000 ukipata F” unakatwa 5000 ... yani ni Do or Die.
 
Back
Top Bottom