Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 2,812
- 11,987
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro
Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma, Julius Mtatiro amesema mara baada ya Serikali kutoa muongozo wa bei elekezi ya sukari uongozi wa Wilaya ukafanya vikao kwa ajili ya kutoa mwelekeo.
Amesema “Kwanza ilikuwa kupata orodha ya watu wanaofanya biashara ya sukari ngazi ya Wilaya ili kuwapa maelekezo.
“Baada ya hapo tukatoa maelekezo kwa Wananchi kuhusu muongozo wa bei kuwa ni Tsh. 2,900 hadi Tsh. 3,200 pamoja na kuwapa namba za kutoa taarifa lakini tumewapa maelekezo Wafanyabiashara wote kuwa wanatakiwa kuweka vibao vinavyoonesha bei ya sukari ili kama muuzaji atauza bei tofauti iwe rahisi mteja kubaini hilo.”
Ameongeza “Kama hawataweka vibao ndio itakuwa mwanzo wa kufanya udanganyifu.
“Baada ya kutoa namba za mawasiliano Wananchi wakatoa mrejesho, tulipokea ripoti 17 awali kuhusu wananchi kuuziwa bei tofauti na zilizoelekezwa kesho yake tukapata ripoti nyingine 11 na waliotuhumiwa wote walifikishwa Kituo cha Polisi na kutoa maelezo.
“Wakati wanachukuliwa kwa ajili ya kwenda kutoa maelezo biashara zao hazikufungwa, walitakiwa kuwaachia watu mbadala wa kuuza kisha wao wakawa wanachukuliwa, baada ya hapo wote 17 na wale 11 wamepatiwa dhamana.
“Hawa Wafanyabiashara wetu wa vijijini sio busara kuwapelekea Mahakamani mwanzoni, ndio maana wanachukuliwa maelezo yao, na kutakiwa kurejea Polisi baada ya siku kadhaa.”
Tangazo la Serikali lililotolewa lilisema mtu yeyote anayeuza Sukari kinyume na Bei Elekezi zilizoainishwa atakuwa ametenda Kosa na akitiwa hatiani atawajibika kwa adhabu iliyoainishwa katika masharti ya Sheria ya Tasnia ya Sukari.
Bei Elekezi za Rejareja kwa Kilo 1 Sukari ziko kama ifuatavyo: Dar, Morogoro, Pwani Tsh. 2,700 - 3,000, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe Tsh. 2,700 -3000, Dodoma, Singida, Tabora Tsh. 2,800 - 3,000, Lindi Mtwara, Ruvuma Tsh. 2,900 - 3,200.
Mikoa ya Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara Tsh. 2,800 - 3,000, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara Tsh. 2,700 - 3,000 na Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa Tsh. 2,800 - 3,200.