Tunamkumbuka Edward Sokoine - Mtu wa Watu

Mzee ES,
kugis alitoa mchango mkubwa sana wakati wa vita vya kagera. magari yake mengi yalitumika kusafirisha wapiganaji wetu, pamoja na vifaa vyao. wako waliosikitishwa na kukamatwa kwake kwa tuhuma za "kuhujumu" uchumi. infact, alikamatwa kwasababu alikutwa na shehena ya matairi ya malori.

zoezi la kukamata wahujumu uchumi lilikuwa ni kati ya blunders za marehemu sokoine. we would rather remember him for something positive kama kusimamia vita ya kagera.

ni kinyume cha taratibu,demokrasia, na utawala bora, kumuweka mtu rumande, halafu kukimbilia bungeni kuandika sheria kuhalalisha kitendo hicho. hivyo ndivyo nyerere na sokoine walivyoanzisha sheria na mahakama za wahujumu uchumi. katika historia ya tanzania, sidhani kama kuna kitendo kilicholidhalilisha bunge kama kile cha kuanzisha sheria ya wahujumu uchumi.

kwa kweli watu wasio na hatia wameteseka sana kutokana na zoezi lile. wako waliopoteza maisha yao bila sababu zozote za msingi. wengine wamepoteza mali walizozipata kihalali kabisa and have never recovered since then.

Mimi ningependa tumkumbuke Sokoine kwa mambo mengine mazuri aliyoyafanya, siyo usimamizi wake wa kampeni ya kukamata "wahujumu" uchumi.

Kyoma,
kuna version nyingine ya "mechi" kati ya Sokoine na Msuya. Inasemekana Sokoine alituma "vijana" wake kwenda kumpekua Mzee Mberesero[Mzee Ngorika], tajiri wa mabasi ya Ngorika.

Inasemekana kuna safe ambalo Mzee Mberesero alikataa kulifungua akidai funguo anazo "Mzee." Alipoulizwa "Mzee" ni nani, akadai ni Cleopa Msuya. Inasemekana "vijana" walimfuata Msuya na yeye akawaambia hajui chochote kuhusu safe hiyo. "Vijana" waliporudi tena kwa Mzee Ngorika safe ikafunguliwa na hakikupatikana kitu!!

Sina uhakika na ukweli wa habari hizi. somo tunalopaswa kulielewa hapa ni kwamba: Sokoine na Msuya walitofautiana kuhusu mbinu za kutumia kuikwamua nchi kutokana na matatizo ya uchumi yaliyokuwa yakitukabili.

Kitu ambacho umekielezea kama "mechi" kwa kweli kilikuwa ni mjadala mzito ulikuwa ukiendelea kuhusu mustakabali wa kiuchumi wa tanzania. mwalimu, ambaye umemtaja kama mwamuzi, alikuwa akipokea ushauri unaokinzana toka kwa sokoine na msuya kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na matatizo ya uchumi ya wakati ule. inaelekea mwalimu alimwamini zaidi sokoine, na kumtema msuya.

kumbuka kwamba msuya ndiye aliyepewa jukumu la kusimamia industrial master plan ya tanzania baada ya kuvunjika East African Community. mwalimu aliheshimu sana ushauri wa msuya katika masuala ya fedha,uchumi,na mipango, isipokuwa ule wa kukubaliana na masharti ya IMF na WB.

mwalimu alipoondoka madarakani naweza kusema ndiyo ilikuwa mwisho wa "mechi" uliyoitaja. tanzania ilifuata masharti ya IMF na WB, na kuachana na sera za Mwalimu na Sokoine.

Kwa maoni yangu Mwalimu alisuasua mno katika majadiliano yake na IMF na WB. Wakati akisuasua uchumi uliendelea kuharibika, na kufikia mahali nchi zote wafadhili zikatususa. Naamini tungekubali ushauri wa kurekebisha uchumi mapema yasingetufika haya yanayoendelea leo hii Tanzania.
 
Mzee Joka,

Heshima mbele mkuu, anyway maneno ya Mzee Kyoma ni mazito sana na ni authority ya kutosha kwenye hili suala zima la marehemu na kazi yake,

Binafsi kuna elimu nyingi ninaona hapo, maana siku zote nilikuwa ninamchukulia marehemu kama ni kiranja safi wa viongozi wenziwe, nilikuwa nina wasi wasi sana na kama alikuwa na skills za kutosha kuwa msimamizi wa operation za serikali, na hasa za uchumi,

Halafu huwa ninajiuliza kuwa angekuwepo leo ingekuwaje? Lakini ninampa Mzee Kyoma, salute kwa kuyaweka mambo sawa!
 
Article ya mzee Kyoma imenikuna sana na imenipa mwangaza mkubwa kwenye utendaji kazi wa Sokoine(kwa wale ambao ni 80s na 90s babies) nadhani kumfananisha Lowasa na Sokoine ni kumkosea heshima marehemu.

Lowasa by the time uchaguzi wa mwaka 95 unakaribia alikuwa na jumba la kifahari pale masaki amepangisha ubalozi wa South Africa na alikuwa na viwanja lukuki mbezi/kawe/kunduchi, kwao ndio haijulikani.

Pamoja na yote hayo mzee wa pamba naona aliamua kumpa nafasi
 
sasa viongozi wetu ndio hata hawatamani kuwa angalau nusu ya Sokoine alivyokuwa? is that too much to ask?
 
Mzee ES,
every thing is open for discussion. vilevile siamini kama kuunga mkono operesheni vijiji ni njia nzuri ya kumuenzi Baba wa Taifa. Operesheni ile ilikuwa a disastour; uzalishaji wa korosho ulianguka, and we have never recovered since then.

vivyo hivyo, tukitaka kumuenzi marehemu Sokoine ni vizuri tukafanya hivyo kwa kukumbushana mambo mengine na siyo harakati za kukamata "wahujumu" uchumi. ile ilikuwa ni witch hunt tu. watu walikuwa wanaswekwa ndani bila dhamana. nakumbuka Mzee mmoja anaitwa kengere mingi, mzee wa miaka kama 90, naye alikamatwa kwa "uhujumu" uchumi!!

Mzee ES, wananchi walikuwa wakigongewa milango USIKU WA MANANE na kukamatwa kwa kosa ambalo kisheria lilikuwa halipo. wengine walikamatwa kwa kuwa na vitu vidogo kama mafuta ya kimbo, sabuni za lifeboy, au dawa ya mswaki colgate. wengine wakatiwa jela kwa kuwa na saa za mei-mei.
 
Heshima zenu wakuu,

Nadhani inabidi mtu mwenye taarifa kamili kuhusu shule ya marehemu Sokoine atueleze. Inavyosemekana katika kipindi 1981-1983 marehemu Sokoine alichukua na kufuzu digrii ya uzamili (Masters) ya political science. Je taarifa hizi ni kweli?
 
Mzee Kafara,

Heshima mbele mkuu, nafikiri Marehemu alisoma katika nchi moja ya kijamaa kama ninakumbuka vizuri, ila sina uhakika ilikuwa nchi gani!

Mzee Joka Kuu,

Heshima mbele mkuu, katika kuchambua siasa zetu na viongozi wetu, ni muhimu sana kuangalia kwa makini NIA NA MADHUMUNI, ya kiongozi au mfumo mzima wa kisiasa at the time.

Operation Vijiji, Operation Maduka, pamoja na Operation ya Wahujumu Uchumi, ni kweli kabisa kuwa utekelezaji wake haukupewa critical thinking ya kutosha na ni kweli kulikuwa na mafanikio na mapungufu yake,

lakini cha muhimu at the end of the day ni kwamba nini nia na madhumuni ya Mwalimu na marehemu Sokoine? Je walifanya hizo Operations kwa ajili ya kujaza matumbo yao? au Account zao Ulaya? au kusomesha watoto wao Ulaya? au kupeleka wake zao Ulaya for shopping?
 
Mzee Es anassema cha muhimu katika kuangalia mchango wa viongozi ni kuchanganua nia na madhumuni yao. Sasa nia na madhumuni ya Sokoine katika kukamata wananchi waliokuwa na sabuni za kuogea au dawa za miswaki yalikuwa yapi? Ni kwamba wananchi wasiwe na colgate? Mbona viongozi walikuwa na duka lao la kupatia hivyo vitu?

Haitoshi kiongozi awe na nia nzuri na madhummuni mazuri. Lazima awe vile vile na mipango mizuri na utekelezaji mzuri. Nia ya Sokoine ya kuhakikisha hakuna chochote nchini ilikuwa upumbavu. Mtu unayetembelea benzi kwa nini upende kuhakikisha hakuna yeyote anakuwa hata na sabuni ya kuogea? Sisi tunakula sana mahindi. Madhumuni ya Sokoine kuzuia usafirishaji wa hata gunia moja la mahindi kutoka kijiji kimoja kwenda kingine yalikuwa yapi? Sio kuleta njaa kweli?

Mzee ES; ni nini kinakufanya udhani kwamba Sokoine alikuwa na nia nzuri? Hakuna ushahidi wa kuridhisha wa kuonyesha kwamba Sokoine alikuwa na nia nzuri. Ushahidi wa kuonyesha alikuwa na nia mbaya ndio upo. Matendo yake yanamsema.

Si vema kutukuza upumbavu uliotendeka huko nyuma. Au mnataka kuurudia?

Augustine Moshi
 
Mwalimu Moshi,'
Soma tena bandiko la Kyoma. Kuna mengi nimejifunza huko.
 
Kafara,
Sokoine alisoma wakati akipata "matibabu" huko YUGOSLAVIA. Vilevile aliporudi Tanzania na hata alipokuwa Waziri Mkuu alikuwa akisomea masters chuo kikuu cha DSM.

Sidhani kama kipindi alichoacha Uwaziri Mkuu na kwenda "kutibiwa" kinatosha kupata shahada ya kwanza. Nadhani UDSM walimruhusu kuchukua masters degree kwa kuzingatia uzoefu wake ktk uongozi na siasa.

Mzee ES,
Hawa viongozi ni watu kama mimi na wewe. Huyo Sokoine mtu wa watu wanawe wamesoma ngambo pia. Sokoine mtu wa watu alipougua alikwenda YUGOSLAVIA kutibiwa. Kama Sokoine, na Kawawa, walikwenda Yugoslavia, na Uchina kwa matibabu, nini kinachowazuia viongozi wa sasa hivi kutibiwa nje?

Tukiendelea kuwabeba viongozi wenye "nia nzuri" lakini kazi mbaya basi Taifa letu halitaendelea. Watanzania tunapaswa ku-raise standards za kupima utendaji kazi wa viongozi wetu. So far Tanzanians have set the standards so low.
 
ni kweli kuwa viongozi hutuangusha. Je katika kufanya maamuzi yake Sokoine alikuwa na lengo la kujinufaisha yeye au familia yake? Je katika maamuzi hayo alikuwa anataka kulinda maslahi yake fulani? Wakati mwingine kama kiongozi unachukua uamuzi ambao baadaye utaonekana haukuwa wa maana sana. Ukweli ni kuwa wakati wa "kuhujumu uchumi" kama hatua zisingechukuliwa, sijui sisi wengine tungekula wapi.

Mimi nashukuru kuwa niliweza kupata vipande vya Mbuni nikienda pale RTC, na debe la mafuta na unga wa "yanga"~ Watu wachache waliokuwa na uwezo wa kuwa na vitu hivyo walianza kuvichimbia ili kupandisha bei yake na hivyo kujinufaisha kupitia matatizo ya watu wengine. NI kweli kuna watu ambao walihisi kuonewa lakini haiwezekani hata chembe wakati wa shida watu wachache watumie nafasi hiyo kujitajirisha!!

Katika vitendo hivyo vya sokoine wazo kubwa lilikuwa kila mtu apate hicho kidogo tulichonacho! Sasa hivi, viongozi wetu wameamua kuwa kile kidogo tulichonacho wapewe wachache wetu huku wengi wetu tukiendelea kutamani na kugombania kile tunachodhania bado kipo!! Na huko tunakokwenda, kwa hakika tutahitaji mtu kutufunga mikono maana ubepari "hauna macho"!
 
Mzee ES,
Kyoma,
Kitu ambacho umekielezea kama "mechi" kwa kweli kilikuwa ni mjadala mzito ulikuwa ukiendelea kuhusu mustakabali wa kiuchumi wa tanzania. mwalimu, ambaye umemtaja kama mwamuzi, alikuwa akipokea ushauri unaokinzana toka kwa sokoine na msuya kuhusu hatua za kuchukua kukabiliana na matatizo ya uchumi ya wakati ule. inaelekea mwalimu alimwamini zaidi sokoine, na kumtema msuya. kumbuka kwamba msuya ndiye aliyepewa jukumu la kusimamia industrial master plan ya tanzania baada ya kuvunjika East African Community. mwalimu aliheshimu sana ushauri wa msuya katika masuala ya fedha,uchumi,na mipango, isipokuwa ule wa kukubaliana na masharti ya IMF na WB. mwalimu alipoondoka madarakani naweza kusema ndiyo ilikuwa mwisho wa "mechi" uliyoitaja. tanzania ilifuata masharti ya IMF na WB, na kuachana na sera za Mwalimu na Sokoine. .

Mzee JokaKuu, Heshima yako Mzee!

Sokoine akifufuka leo hii, hawezi kuona ajabu ya ufisadi unaofanywa na viongozi wetu. Bahati mbaya, vyombo vya habari kwa wakati ule vilimilikiwa na Serikali, hivyo, hakuna chombo chochote cha habari kingediliki kuweka wazi msuguano uliokuwepo miongoni mwa viongozi. Nasema Sokoine hawezi kuona ajabu ya ufisadi unaofanyika sasa hivi kwasababu alijua viongozi wetu wengi, ambao hawajabadilika, walikuwa wanafanya unafiki kwa Mwalimu.

Mechi kati ya Sokoine na Msuya haikuwa katika sera za kuongoza nchi, bali kwenye maisha ya baadhi ya viongozi ambao yalikuwa hayafanani na sera walizokuwa wanasimamia. Achana na porojo za Msukule, kwa maana kuwa, eti Sokoine alionekana akitembea mjini baada ya kifo chake. Hata hivyo, tetesi kuwa kifo cha Sokoine kilitokana na mkono wa mtu, au kundi fulani la watu, hazipashwi kudhalauliwa.

Hizi tetesi zilitokana na msuguano uliokuwepo baina ya Sokoine na baadhi ya viongozi. Sijasema ni za kweli, bali hazijawahi kufanyiwa uchunguzi, alafu taifa likatangaziwa kuwa ni za uongo.

Nashangaa kitendo cha Mwalimu kulihutubia taifa kukana uzushi wa kivuli cha Sokoine, lakini akakaa kimya kuhusu tetesi za mauaji yake, ambazo zote zilisambaa kwa kasi ileile. Kumbuka Sokoine alikuwa haganganii sera ya Ujamaa na Kujitegemea, bali alikuwa anasisitiza kuwa sisi ni viongozi, na kama tumeamua kufuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, basi maisha ya viongozi wote lazima yafanane na sera tunayoihubiri na sivinginevyo. Hii ndio ilikuwa mechi kati ya Sokoine na baadhi ya viongozi akiwemo Msuya.

Nilitumia maneno kuwa Nyerere na Kawawa walikuwa marefa katika hiyo mechi, lakini ukweli ni kuwa Nyerere alikuwa anamkwamisha Sokoine, alafu Kawawa alikuwa anampoza, yaani alileta mambo ya chondechonde mzee. Ndio maana Nyerere hakusita kuwatangazia watanzania pale Hotel ya Kirimanjaro 1995, kuwa Sokoine hakuwa na sababu ya kutokumwambia mkubwa wake wa kazi kuwa mambo yanakwenda vibaya. Inawezekana Mungu alimchukuwa Sokoine kabla hajakamilisha dhamila yake, lakini mazingira yaliyokuwepo kabla ya kifo chake, ndiyo yalipelekea watu waliokuwa karibu na msuguano huo wazushe kuwa ameuwawa.

Huwezi kuamini kuwa hawa viongozi wote unaowaona sasa hivi, miaka ya sabini mpaka mwalimu anang;atuka madarakani, walikuwa wahubiri wa kinafiki wa siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Nyerere aliwaamini, lakini Sokoine aliwastukia. Ndio maana nasema ni Nyerere peke yake ambaye akifufuka leo hii, hawezi kuamini macho yake kuwa huyu ndiye Ben, Msuya, Kingunge n.k. Kumbuka Mwalimu hakuwa na mbadala katika mambo ya sera. Waziri angevulunda au kuiba sehemu fulani, basi Mwalimu angembadilisha wizara. Hakuna Waziri ambaye angeitilafiana kisera na Mwalimu alafu akabaki madarakani. Labda kama tunamuongelea Nyerere mwingine. Katika suala la sera, Nyerere hakuwa na suluhu.

Tafsiri rasmi ya mwalimu kuhusu jinsi Raisi wa nchi anavyotakiwa kufanya kama kutatokea mkinzano wa sera na mawaziri wake, uko kwenye kitabu chake cha Uongozi wetu na Hatima ya Tanzania. Katika ukurasa wa 41, Mwalimu anatoa taswira kuwa Waziri hawezi kumshauri Raisi jambo fulani linalopingana na sera ya chama, alafu akabaki na wadhifa wake. Alikuwa akimshauri Mzee Mwinyi kuhusu sakata la sera ya CCM ya mambo ya muungano, kwa maana kuwa, Kolimba na Chigwemise walikuwa wanaleta mambo ya kubadili rangi kama vinyonga. Alisema wajiuzuru kwa hiari yao, au Raisi awafukuze kazi. Mwalimu alikuwa hateteleki katika masuala ya misimamo ya sera zinazoendesha nchi.

Kusema kuwa mechi ya Sokoine na Msuya ulihusu sera, tena zile za Majangiri wa IMF na WB, sio saihi, kwani kama Msuya angekuwa anazikubali zile sera, angeutema uwaziri mara moja. Tena Sokoine angekaa pembeni na moja baridi moja moto, wakati Nyerere anamwashia Msuya kimulimuli chekundu. Kama unabisha, mshauri Mheshimiwa Edwin Mtei atoe ushuhuda hapa hapa Jambo Forums. In fact, Mzee Mtei, ndiye alikuwa na tofauti kidogo za kisera na Mwalimu ambazo unaziongelea kuhusu IMF na WB.

Katika mkutano wake wa kwanza kuwahutubia wananchi akiwa kama kiongozi wa chama cha siasa cha upinzani pale Mnazimmoja, ambapo hata mimi binafsi nilihudhulia, Mtei aliweka bayana uvumi uliokuwepo kuwa alikuwa na mitizamo tofauti na Mwalimu kuhusu hawa wababe wa IMF na WB. Mtei alitaka tukubaliane na baadhi ya zile sera.

Binafsi, naona kuna tofauti kubwa kati ya Masharti na Sera. Masharti si Sera, na wala Sera si Masharti. IMF na WB hawana Sera, bali wana Masharti tu ya mikopo, ambayo ukishayakubali, na kuyatekeleza, unakuwa kama vile umeonja Ganja, au Cocaine, kwa maana ya kukufanya uendelee kuwa tegemezi wa ile mikopo, na wao waendelee kukukopesha mpaka siku ya kiama chako. Hiyo si sifa ya Sera. Nikipata nafasi nitaelezea tofauti kati ya Sera na Masharti.

Nyerere alipogundua Mtei anashawishika kukubaliana na hawa waheshimiwa, alimtema palepale. Haya mashirika kuonyesha dharau ya kiburi cha Nyerere, yakamwita Mtei na kumpa ajira. Sera za viwanda za Nyerere unazoziongelea zilikuwa katika msingi wa Ujamaa na Kujitegemea, na si vinginevyo. Hizo ndizo Sera alizokuwa anasimamia Msuya. Kwa upande mwingine, nakiri ukweli usiopingika kuwa, Mwalimu alikuwa na mapenzi ya rohoni juu ya Msuya, Kawawa, Salimu, na Jamal ukilinganisha na viongozi wengine wa kitaifa kwa wakati huo.

Ilishangaza kuona jinsi Nyerere alivyofumbia macho udhaifu wa kibinadamu wa Msuya. Nasisitiza kuwa sio udhaifu wa sera, bali wa kibinadamu, kama ulivyo wa Lowasa na wengineo. Wakati wa kinyanganyiro cha kumchuja mgombea wa uraisi kupitia CCM mwaka 1995, Mwalimu alishiriki kwa karibu zaidi kuzidi kiongozi yeyote wa CCM. Makundi ya mitandao miongoni mwa wagombea wa CCM, yalipenyeza lawama kwa Mwalimu kupitia kwenye vyombo vya habari kuwa, Mwalimu anamchukia Lowasa bure, kwa sababu kama ni tabia ya kupenda kujilimbikizia mali, mbona hata Msuya yuko vilevile lakini Mwalimu anafumba macho? Wengine walidiriki kusema kuwa Msuya hakustahili kuwa kwenye tatu bora ya CCM, yaani Mkapa, Kikwete, na Msuya.

Naitimisha kuwa mechi ya Sokoine na Msuya haikuwa ya Kisera. Pia, Nyerere hakumpenda Sokoine kama alivyowapenda, Msuya, Kawawa, Salimu, na Jamal. Uhusiano wa Mwalimu na Sokoine ulikuwa katika usimamizi wa sera ambazo Nyerere aliziamini. Sokoine hakutaka flexibility, kwa maana ya kuoneana haya. Alitaka sheria zisiwe za kibaguzi, kwa maana kwamba hata viongozi wazitii kama zilivyoandikwa. Pia, alitaka sera zilizoendesha nchi zitekelezwe kama zilivyoandikwa.

Alitaka taasisi za kusimamia sheria zipewe nguvu, na zisiingiliwe na wenye madaraka ya kisiasa. Hapa ndipo Nyerere alikuwa akimuheshimu, lakini kumbuka Nyerere aliwapenda na kuwaamini mawaziri wake. Sokoine alipingana na Mwalimu kuhusu utamaduni wa kuhamisha wabadhilifu wa mali ya Umma kutoka wizara moja hadi nyingine, au kutoka shirika moja hadi lingine. Sokoine alikuwa amedhamilia, na mtu pekee ambaye angemsimamisha kufanya hivyo, alikuwa Nyerere, ambaye hakuwa tayari kumfukuza kwasababu ya kutekeleza sera zinazoongoza nchi. Hivyo Nyerere alizidiwa hoja, ndio maana watu walitaka kuona uhondo wa mechi.

Kumbuka kuna wimbo mmoja ulikuwa unaimbwa katika Redio Tanzania miaka ya tisini ambao ulinukuu maneno ya Sokoine wakati wa vita dhidi wa wahujumu uchumi kuwa ' hawa watu wangefikia mahala pa kuliuza taifa letu la Tanzania" alafu ubeti wa wimbo huo unaendelea ‘hiyooo, tunalia machozi yatililika, wapinga Ujamaa wamejifunga kibwewe...... sikumbuki maneno mengine. Pia rejea hotuba ya Sokoine ya kuhairisha Bunge muda mfupi kabla ya kifo chake, utakubali kuwa ni kifo peke yake ndicho kingemsimamisha kutekeleza dhamila yake.

Sokoine hakuwa kama viongozi wa sasa wanaoropoka kuwa wanachukia rushwa, wakati ni wala rushwa. Viongozi wa zamani walikuwa na mtindo wa kukaa vikao kwanza, kupanga mikakati, kufikia maamuzi, na kuziusisha taasisi ili zianze utekelezaji, alafu ndipo walitoka kulihutubia taifa, kwa kuwafahamisha wananchi utekelezaji wa maamuzi yao. Ndio maana nikisoma maneno ya sokoine, nayaamini kuliko ninavyoamini porojo za hotuba za viongozi wetu wa sasa. Waliozusha kuwa Sokoine ameuwawa kwenye ajali iliyokuwa imepangwa, sio akina Kyoma, bali ni wale waliokuwa kwenye mfumo wa uongozi na kushuhudia hii mikirikiti.
 
Kyoma,
Mimi sipendi mambo ya uvumi uvumi hasa ktk masuala mazito kama KIFO. Pamoja na hayo ni mtu mmoja tu katika siasa za Tanzania aliyekuwa na uwezo wa kumuua Sokoine and getting away with it. Kumtaja mtu huyo hapa itakuwa kumchafua. Vilevile naamini kwamba Sokoine alikufa kwa ajali ya gari.

Nakubaliana na mawazo yako kwamba masharti ya IMF ni kama Cocaine, ni vigumu sana kuacha Cocaine. Lakini madhara yake yanatofauti kubwa kabisa kama mwili na afya yako vitakuwa dhaifu. Hakuna jambo lisilowezekana, kwa hivyo at a certain point and time nchi yoyote ile inaweza kuachana na masharti ya IMF/WB.

Masharti ama "prescription" ya IMF/WB siyo muarubaini wa matatizo ya uchumi Tanzania. Suala hilo halina ubishi. Lakini nadhani utakubaliana na mimi kwamba kampeni ya uhujumu uchumi ya Sokoine ilikuwa haitupeleki popote. Nchi ilifika mahali tukawa hatuna ujanja tena bali kukubaliana na hao wakubwa. Walichokuwa wana-argue Msuya na wenzake ni kwamba tukubali haya masharti kabla mambo hayajawa mabaya kupita kiasi.

I wouldnt dwell much kuhusu "mechi" ya Msuya na wanamtandao. Sidhani kama kuna mtu bado ana hamu nao. Wanamtandao walifikia kueneza uvumi kwamba ile Press Conference ya Mwalimu katika makazi ya Waziri Mkuu ilikuwa na lengo la kumbomoa "CD," Msuya. Ilikuja kubainika kwamba Msuya alikuwa haishi ktk makazi ya Waziri Mkuu, na Mwalimu aliitisha press conference hapo kwasababu nyumba yake ya msasani ilikuwa inakarabatiwa.

Sidhani kama unaamini kwamba ktk vinara wa mtandao yuko mwenye uwezo wa kusimama na kwenda punch-for-punch, hoja-kwa-hoja, na CD katika suala lolote lile. Pamoja na mapungufu yake, Msuya alikuwa mjenga hoja mzuri, anayetetea hoja zake kwa data. Zaidi alikuwa mchapakazi mzuri, mwenye uwezo wa kujifunza mazingira mpya ya kazi kwa haraka sana.When Msuya covered up for Late Stephen Kibona in the bunge session, na kupangua mpaka maswali na hoja za ziada, that was just CD at his best. Hicho ndicho kilichomfanya Mwalimu ampende Msuya.

Labda nihitimishe tu kwamba kampeni ya Sokoine ya kukamata "wahujumu" uchumi ilikuwa ni sawasawa na kutibu dalili na siyo chanzo cha matatizo ya uchumi wetu. It wasnt making any economic sense to me. Zaidi haikuleta unafuu wowote ule, and that proves that Sokoine was wrong.
 
Mzee ES,
Kyoma,
Kwa maoni yangu Mwalimu alisuasua mno katika majadiliano yake na IMF na WB. Wakati akisuasua uchumi uliendelea kuharibika, na kufikia mahali nchi zote wafadhili zikatususa. Naamini tungekubali ushauri wa kurekebisha uchumi mapema yasingetufika haya yanayoendelea leo hii Tanzania.

Mzee JokaKuu, sijuhi hii ulonipiga ni chenga ya mwili, tobo, kanzu, au vyote kwa pamoja. Niko tayari kupata somo kutoka kwako Mzee, kuhusu hawa Majangiri wa IMF na WB. Yaani unasema Mwalimu angewasikiliza hawa Magaidi tusingekuwa hapa tulipo kiuchumi? Binafsi, nadhani tupo hapa tulipo kwasababu tulitelekeza sera za Mwalimu na Sokoine, alafu tukakumbatia za haya Majangiri , ndio maana tupo hapa tulipo. Kabla sijaenda mbali, mosi, binafsi, napendekeza haya mashirika mawili ya IMF na WB yasifanyiwe ukarabati kama wengine wanavyofikiri bali yavunjwe na kufutwa kabisa. Mbili, nadhani tulifanya makosa kama watanzania kutokufanya matembezi kama yale ya Azimio la Arusha, kuunga mkono juhudi za Nyerere na Sokoine za kupinga Masharti ya haya mashirika ya kijambazi duniani. Nitatoa mawzo yangu machache, yale ya ukeleketwa, nitayaweka kiporo, alafu naomba nikimaliza, na wewe utoe yako kuhusu hawa waheshimiwa ili niweze kupata mwanga wa kile nisichokiona.

Katika biashara ya mitaji, kama ilivyo ya mabenki yote, ukijumlisha na magaidi wa Benki ya dunia, utajiri wao mkubwa unatokana na fedha iliyo katika mzunguko, kwa maana ya kukopeshana. Tatizo sio letu, bali ni lao kwa sababu wanafedha kama mitaji. Hawawezi kutengeneza faida mpaka hizo fedha ziende kwenye mzunguko, yaani wawakopeshe watu ambao watalipa hizo fedha walizokopa, fees, na riba. Vilevile, lazima wahakikishe kuwa kuna watu wa kukopa hizo fedha kwa muda wote ili wanedelee kutengeneza faidaama sivyo biashara yao inadoda na kufa kifo cha kawaida. Ndio maana wanakuja na Cocaine, kwa maana ya masharti yatakayowadumaza na kuendelea kuwafanya mafukara wa mawazo, au tegemezi wa fedha, ili muendelee kukopa, na kuamini kuwa bila Ganja, yaani fedha za mikopo, hamuwezi kutatua matatizo mliokuwa nayo.

Ni Wizara chache ndani ya nchi zilizoendelea, amabazo zinaingiza fedha nyingi, tena kwa mkupuo, kama fedha ziingizwazo kutokana na vitengo au Wizara zianzoshughulikia masuala ya nchi zijulikanazo kama masikini duniani. Angalia idadi ya nchi zinazojiita masikini duniani, alafu jumlisha matirioni ya madola ambayo nchi hizo zinadaiwa, ongeza mlundikano wa fees na riba katika miongo kadhaa, alafu gawanya kwa idadi ya nchi tajiri. Ukifanya hesabu vizuri, utaona kwamba, kutokana na fees pamoja riba amabzo nchi zinazoitwa masikini zinalipa nchi tajiri, hawa jamaa, wamevihakikishia vitukuu vyao mlo wa neema usio na jasho kwa karne nyingi zijazo. Mitambo au Mirija inayofanikisha hili zoezi, ni mashirika ya IMF na WB. Eti sisi tunasema kuwa hawa jamaa wanatupenda sana mpaka wanatuwekea wizara au vitengo vinavyoshughulikia masuala ya Afrika. Asthakafululahkii! You are not even a Nigger!

Kabla siajenda mbali, labda tukumbushane chimbuko la hawa Majangiri. Tuwajue ni akina nani, wanatufanyia nini ambacho sisi wenyewe hatuwezi kufanya, alafu baada ya hapo tuone kama Mwalimu na Sokoine wangewasikiliza toka zamani, tungekuwa mbali. Si vibaya pia tukatafuta mifano, ambayo nadhani mzee JokaKuu utakuwanayo tele, ya nchi zilizowasikiliza hawa majangiri mapema kabla yetu, alafu zikafanikiwa, au ziko wapi sasa.

Benki ya Dunia WB na Shirika la Fedha Duniani (IMF), ambao viongozi wetu wa kisasa wanayataja haya mashirika kuwa ni miongoni mwa wahisani wetu, vilianzishwa mwaka 1944 mjini Bretton Woods, New Hampshire, wakati vita kuu ya pili ya dunia inakaribia kuisha. Mataifa wanzilishi, walihepuka mabolongo yaliyowapata baada ya vita kuu ya kwanza ya dunia. Hivyo, walitaka iwepo Benki ambayo wangeweza kupata mikopo ya muda mfupi ya kuwawezesha kuyajenga upya mataifa ya Ulaya baada ya kushinda vita. Kumbuka, wakati huo haikuwepo dunia ya tatu, bali zilikuwepo dola kubwa ambazo zilikuwa zinatawala maeneo makubwa duniani. Haya mashirika mawili hayakuundwa na jumuia ya Kimataifa, hivyo, yaliundwa kwa maslahi ya wale walioyaanzisha.

Mpaka sasa hivi, muundo wa Shirika la Fedha duniani (IMF), bado unayapa nguvu mataifa makubwa yenye nguvu za kiuchumi. Kura ya kila taifa inategemea na ukubwa wa uchumi wake. Marekani inaongoza kwa kuwa na zaidi ya asilimia 17 ya kura zote, ikifuatiwa na nchi kama Japan na Ujerumani. Kuathiri maamuzi ya IMF, unahitaji asilimia 80 ya kura zote. Hata hivyo, Marekani na nchi za Ulaya peke yake wana zaidi ya asilimia 80 ya kura zote. Kwa maana hiyo, mataifa mengine hayawezi kubadilisha kitu chochote mpaka wapate ruhusa yao.

Mikopo ‘misaada” inayotolewa na haya mashirika imekuwa na masharti magumu na yanayofanana kwa nchi zote duniani ambazo hazina nguvu za kiuchumi. Mifano ya mojawapo ya hayo masharti ni kuweka viwango vya ubadirishaji wa fedha za kigeni, matumizi katika bajeti ya nchi, Mzunguko wa fedha katika benki za ndani ya nchi, pamoja na ubinafsishaji wa mashirika ya Umma. Mathalani, tulipewa mkopo na Benki ya Dunia kwa masharti ya kubinafsisha sekta ya maji, na sisi tukajaribu kufanya hivyo, lakini tukapigwa kanyabwoya. Hata hivyo, zile fedha lazima tuzilipe na riba juu yake, hata kama hatukufanikiwa katika hilo. Kwa kifupi, IMF na WB, hawakulazimishi kupunguza mipango katika sekta, kwa mfano Afya na Elimu, bali wanakuwekea makadirio ya kiwango cha fedha unachoweza kutumia katika hizo sekta, hivyo, unaishia kupunguza baadhi ya mipango katika hizo sekta, kama tulivyofanywa katika michezo, masomo ya ufundi, n.k

Masharti mengine ni kwamba, nchi ikitaka kuongeza kiwango cha bidhaa zinazouzwa nje (export), na kupunguza kiwango cha bidhaa inazonunua kutoka nje (import), inabidi fedha ya nje iwe na thamani kuzidi ya ndani ya nchi husika ili kukatisha tamaa manunuzi ya bidhaa kutoka nje. Hivyo, unatakiwa kushusha thamani ya fedha ya nchi husika, mfano kama tulivyofanya kushusha shilingi ya Tanzania, na thamani ya dola inapanda. Hata hivyo, kwasababu tunakwenda kichwakichwa, hatukukumbuka kuwa viwango vya uzalishaji katika jamii zetu ni vya chini sana. Tunategemea malighafi kutoka nje ili tuweze kuzalisha. Mfano wa bidhaa za lazima zitokazo nje ni Mafuta, Vitabu, Madawa, na Mbolea. Bidhaa zote hizi zinanunuliwa kwa fedha za kigeni. Thamani ya fedha ya nchi inaposhuka na fedha za kigeni kupanda, gharama za uzalishaji zinakuwa juu na kusababisha mfumuko wa bei kwa bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi. (hupo hapo Mzee JokaKuu?). Hizi zi Sera, ni Masharti.

Benki ya dunia na Shirika la fedha duniani wakisha tukopesha fedha kwa makubaliano ya hayo masharti, na madhara yakishaanza kuinyemelea nchi husika, mataifa yenye nguvu za uchumi yanaanzia yalipoishia hayo mashirika. Wanaitaka nchi ifungue milango ya biashara bila masharti yoyote, ikiwa ni pamoja na kuondoa vizingiti kwa bidhaa kutoka kutoka nje za nchi. Kuvunja vunja mashirika yetu makubwa ili mashirika ya nje yaweze kushindana vizuri, kama tulivyofanya kwa benki yetu ya NBC.

(unakumbuka Mwalimu alivyolalamika pale Kilimanjaro Hotel 1995, kuwa hawa jamaa wanawaambia viongozi wetu kuwa eti NBC ni kubwa, hivyo ivunjwe katika vibaba ili benki zao ziweze kushindana. Mwalimu aliuliza, can NBC open branch in New York? Aliuliza kuwa NBC ni benki kubwa kuzidi benki gani?), Lakini viongozi wetu walitii amri. Wanasema ni soko huria, utandawazi, ujasirimali, na ujinga mwingine unaofanana na huo. Wanasema biashara inaendeshwa na nguvu ya soko, lakini wanatuwekea masharti kuwa lazima tuwawekee mazingira bora wawekezaji kwa kutokuwatoza kodi kwa muda kadhaa. Tufungue ardhi yetu bila masharti kuruhusu makampuni makubwa kuchimba madini bila masharti.

Masharti mengine ni kwamba, fedha wanazotukopesha, kamwe, haziwezi kutumika kutumika kuwasaidia wakulima au wafugaji wetu ili kupunguza makali ya uzalishaji (subsidize). Hata hivyo, serikali zao, zinawasaidia wakulima wao ili kupunguza makali ya uzalishaji. Wanataka tufungue milango kwa maana kuwa bidhaa za wakulima wao ambazo ziko subsidized, zishindane na bidhaa za wakulima wetu ambazo haziko subsidized katika mfumo wa kitu kinachoitwa soko huria. (Ndio maana Mwalimu aliuliza palepale Kirimanjaro 1995, kuwa bingwa wa ngumi wa uzito wa juu hawezi kuingizwa ulingo mmoja na yule wa uzito wa kati. Alisema Bukina Faso and German haziwezi kuwekwa kwenye ulingo mmoja). Viongozi wetu walisalimu amri katika hayo masharti.

Matokeo ya hizi ghiliba za IMF na WB, bidhaa zinazoingia nchini kwetu kutoka nje zinauzwa kwa bei ndogo kwa sababu mbili, mosi, njia za uzalishaji katika nchi zenye nguvu za kiuchumi ni za kisasa, kwa maana ya kutumia mashine, wakati sisi tunatumia majembe ya mpini. Pili, Uzalishaji wa bidhaa zao unapatamsaada wa fedha kutoka katika serikali zao kwa lengo la kupunguza makali ya uzalishaji, kitu wanachotukataza sisi tusifanye kwa wakulima na wazalishaji wetu.

Mfano halisi katika nchi yetu, tuna idadi ya kutosha ya wananchi wetu ambao ni wafugaji. Hata hivyo, ilitupate mkopo kutoka Benki ya dunia, hata kama ni wa kununua Ndege ya Raisi, na hauna mahusiano yoyote na wafugaji, basi, WB itakwambia kuwa umekuja kwetu kukopa fedha kwasababu huna mipango mizuri ya kuingiza fedha. Hatuingilii Uhuru wako, lakini fedha zetu zina masharti yatakayo kusaidia kurekebisha matumizi yako ya fedha ili uwe na fedha na usije kukopa tena. Masharti yenyewe ni kuwa uondoe vikwazo ili makampuni ya nje yaingize nchini kwako maziwa ya Unga. Of course, maziwa ya Unga yanauzwa kwa bei rahisi ukilinganisha na maziwa ya Ng’ombe. Hii ina maana, wafugaji wetu wanapigwa kaputi kwa sababu maziwa yao yanashindana soko ma maziwa ya Unga. Pia, watu wetu hawapati lishe bora kwasababu maziwa ya Ng'ombe ni bora kuliko ya Unga.

Mfano mwingine ni ule wa Serikali yetu kuwekewa masharti isiwape fedha (subsidize) wakulima wa Pamba, lakini nchi ya Marekani inawasaidia fedha (subsidize) kwa kiasi kikubwa wakulima wake wa Pamba. Wakulima wetu wanatumia majembe ya mkono na wale wa Kimarekani wanatumia Mashine za kisasa. Hata hivyo, Pamba inayotoka Marekani na ile ya Tanzania inauzwa kwa mashindano katika soko la pamoja bila kuangalia upendeleo katika njia za uzalishaji. Haya ndio masharti ya IMF na WB, yaliyojumlishwa katika mfumo wa uchumi wa Soko huria au utandawazi, ambapo njia zote zinazoweza kuinua viwango vya maisha ya wakulima na wazalishaji wa watu wa nchi yetu zinapigwa mweleka na haya majinamizi.

Ndio maana baada ya kifo cha Sokoine na Nyerere, uchumi wa nchi yetu unaendeshwa na mataifa ya nje kwa kutumia mitambo ya ukopeshaji inayoendeshwa na mashirika ya fedha ya kimataifa IMF na WB, hivyo kuondoa dhana nzima ya matumaini na ndoto za kujitegemea. Viongozi wetu wanasema huu ndio uhisani. Binafsi, naamini kuwa Mhisani anapashwa kuwa mtu wema, anayependa kuwasaidia wenzake bila hila, ulaghai, au utapeli (kamusi ya kiswahili sanifu 1981). IMF na WB sio wahisani bali ni Majangiri. Nyerere na Sokoine walikuwa na haki ya kukataa masharti yao.

Azimio Rome Februari 2003, na lile la Paris Machi 2005, yaliyohudhuliwa na wabia pamoja na mataifa yanayojiita masikini duniani, ambapo Tanzania ilitia saihi maazimio yote mawili, yalikuwa na lengo la kupunguza ukali wa masharti ya mikopo na kuziachia nchi masikini uwanja wa kufurukuta na kupanga mipango ya maendeleo. Hata hivyo, waliweka vipengele katika hayo makubaliano kuwa lazima kuwepo na uangalizi wa wabia katika baadhi ya nyanja. Mathalani, Mgogoro uliojitokeza kati ya Denmark na Serikali ya Tanzania, ni matokeo ya mwendelezo wa maazimio ya Paris na Rome. Mswada wa marekebisho ya sheria ya rushwa unaojadiliwa na Jambo Forums sasa hivi, umetokana na msukumo kutoka nje ya nchi na si msukumo wa wananchi wa Tanzania. Tumefikia mahala mabapo sheria za kuendesha nchi yetu, zinatungiwa Paris na Rome, wala sio Kiwaga, Arusha, iringa, au Musoma kama tulivyokuwa tumezoea enzi za Sokoine na Nyerere. Of course, wabunge muda wote wamekuwa ni vikaragosi wa Serikali.

Mkutano wa mataifa yaliyo na maendeleo ya viwanda duniani G8, uliofanyika mjini Gleneagles, Scotland Julai 2005, Ulifuta madeni ya nchi 19 zilizokuwa zimebeba msalaba mkubwa wa madeni ikiwemo Tanzania, kwa masharti kadhaa yaliyowekwa na hizo nchi. Kitu cha maana kilichoongelewa Gleneagles ambacho kinawanufaisha Wakulima na Wazalishaji wengine wa nchi masikini duniani kuliko mikopo na madeni yaliyoishia kwenye mikono ya wajanja wachache, ni mfumo wa biashara ya haki duniani. Kuweka mazingira na kuondoa masharti yanayowakwaza wakulima wa nchi masikini na yanawaneemesha wakulima wa nchi tajiri. Waliliweka hilo jukumu katika mkutano wa Mawaziri wa Jumuia ya Biashara Duniani (WTO) uliofanyika Hong Kong, China Disemba 2005. Hata hivyo, hakuna maamuzi yoyote yaliyofikiwa juu ya suala hilo katika huo mkutano. Hata mkutano wa G8 uliofuatia huko St. Petersburg, Russia, haukuwa na agenda ya kuleta mfumo wa biashara ulio na haki duniani.

Binafsi, sikubaliani na nia ya mataifa yenye nguvu za kiuchumi duniani, ingawa kwa nje wanaonekana kuazima sera za utu za kutufutia madeni. Haya mataifa hayawezi kumpinga shetani upande mmoja kwa kutufutia madeni, alafu wakahalalisha shetani upande wa mwingine kwa kukataa kuondoa mifumo ya uchumi duniani isiyo ya haki. Tumefutiwa madeni, lakini mifumo iliyo ndani na nje ya nchi yetu iliyotuingiza kwenye madeni, bado iko palepale. Tunachokifanya ni kuzunguka duara, na mwishowe tunarudi palepale.

Binafsi, sipingi nchi kukopa, ila napendela zaidi mifumo ya uchumi ambayo inatoa haki sawa kwa wote. Ikibidi kukopa, basi tuhakikishe tunahitaji (needs) hizo fedha, na sio tunazitaka (wants) fedha. Ili niweze kueleweka vizuri, nitatoa mifano ya baadhi ya fedha tulizokopa kutoka Benki ya Dunia na jinsi ambavyo tungehepuka hiyo mikopo. Benki ya dunia ni wasiri sana, hivyo, si rahisi kujua masharti yanayoambatanishwa na hii mikopo ninayoielezea chini. Lakini mikopo yote hii ina masharti magumu ya kutushikisha adabu. Leo nitaanza michache, na mingine naiweka kiporo.

Disemba 16, 2003, Serikali ya Tanzania ilipata mkopo wa dola za kimarekani milioni 40 kutoka katika Benki ya Dunia kwa ajili ya kuboresha Sekta ya Afya (Health Sector Development Project). Lakini kabla ya kukopa hizo fedha, kulikuwa na udhaifu katika Idara ya Afya ambao tungeuondoa kwanza ili fedha ziweze kuwafikia walengwa. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2002/2003, Wizara ya Afya ilitumia shilingi 85, 300, 510 katika manunuzi hewa ya vifaa na madawa. Pia, Wizara hiyo, ilionyesha kuwa imeilipa Bohari Kuu ya Madawa kiasi cha shilingi 651, 235, 602 kwa ajili ya usambazaji wa madawa na vifaa mbalimbali, kumbe kiasi cha fedha kilichotumika kufanya kazi hiyo ni sh 44,625,191.

Mei 9, 2006 Washington , habari namba 2006/400/AFR, Serikali ya Tanzania ilipata mkopo wa dola za kimarekani milioni 40 kutoka katika Benki ya Dunia kwa ajili ya Uwajibikaji, Uwazi, na Uadilifu (Accountability, Transparency and integrity program). Lakini kabla Serikali haijakopa hizo fedha, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2004/2005 inaonyesha kuwa Serikali ilipata hasara ya shilingi bilioni 140 kwa sababu ya kukosa nidhamu katika matumizi ya fedha. Yaani, tunakosa nidhamu ya matumizi ya fedha, hivyo, tunakwenda kukopa fedha ili tupate nidhamu ya matumizi.

Juni 15, 2006 Washington, habari namba 2006/472/AFR, Serikali ya Tanzania ilipata mkopo wa dola za kimarakani milioni 12 kwa ajili ya kufanya mfumo wa utozaji kodi uwe wa kisasa (Tax Modernization Project), kwa kuzifanya huduma ziwe bora kwa wateja, haki pamoja na uadilifu. Binafsi, nafikiri tungekuwa tunakusanya kodi kwa haki na uadilifu tusingehitaji kukopa hizi fedha. Februari 2006, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Lawrence Masha, aliliambia Bunge kwamba Serikali imekusanya jumla ya dola za kimarekani 54, 765, 462 kama (royalty) kutoka katika makampuni ya kuchimba madini yaliyopo nchini kwetu, toka mwaka 2000 mpaka 2004. Pia alilieleza hilo Bunge kuwa mwaka 2003 Serikali ya Tanzania ilitia saihi mkataba na kampuni ya Kimarekani Alex Stewart (Assayers), kuyafanyia uchunguzi makampuni ya madini yaliyoko nchini mwetu ili kujua ni kiasi gani wanapashwa kulipa kama (royalty fees). Mpaka Februari 2006, Serikali yetu ilikwisha ilipa Alex Stewart dola za kimarekani 30, 915, 642 na senti 80.

Kwa tafsiri yangu, katika kipengele cha (royalty) peke yake, wastani wa mapato ya Serikali kwa mwezi toka 200 mpaka 2004 na wastani wa mwezi wa gharama tunazoilipa Alext Stewart, Serikali inabakia na dola za kimarekani 282,180 na senti 27. Lakini Jarida linalotolewa na (Tanzania Chamber of Minerals and energy 2006), linasema kwamba madini yenye thamani ya dola za kimarekani milioni 693 yalisafirishwa nje ya nchi kwa mwaka mmoja peke yake wa 2004. Lakini toka mwaka 1997 mpaka 2005, Serikali ilikusanya mapato ya dola za kimarekani 255.5 kutokana na kodi za aina zote katika madini. IMF na WB ndio walituwekea masharti ya kusamehe kodi za makampuni yanayopora madini yetu. Wakati huohuo, wanatukopesha fedha ili tuwe na mifumo ya kisasa ya utozaji kodi. Sasa tukiwa na hiyo mifumo ya kisasa, tutamtoza nani hiyo kodi? Kinachotakiwa sio kwenda kukopa fedha ili kuleta haki na uadilifu katika mfumo wa utozaji kodi, bali ni kuipitia hii mikataba na kukusanya kodi.

June 8, 2004 Serikali ya Tanzania ilipata mkopo wa dola za kimarekani milioni 43.8 kutoka katika Benki ya Dunia kwa sababu ya mpango wa dharura wa kupunguza makali ya mgao wa umeme uliokuwa ukilikabili taifa letu. Hata hivyo, kadili ya Ripoti iliyotolewa na (Transparency International), Serikali ya awamu ya tatu iliridhia na kukubali Tanesco isaini mkataba wa kuilipa IPTL dola za kimarekani 2.5 kila mwezi kwa muda wa miaka 20, hata kama Tanesco hainunui umeme au inanunua. Kambarage na Sokoine si wanaruka kichura chura huko waliko. Mzee JokaKuu, Kambarage na Sokoine, hawakuwa na makosa ya kukataa masharti ya IMF na WB. Tumefika hapa tulipo sio kwa sababu ya matendo yao ya kukataa masharti, bali ni kwasababu ya umasikini wetu wa mawazo. Ebu fanya mahesabu hapo juu kati ya mkopo tunaowatwisha wananchi wetu, na fedha tunayowalipa IPTL kila mwezi.

Kila mkopo hapo juu unajitegemea. Kadiri ya Benki ya dunia, makubaliano ya kila mkopo niliyoiongelea hapo juu ni pamoja na ada ya uazimaji (commitment fee) asilimia 0.35, gharama ya kuhudumia mkopo (service charge) asilimia 0.75 kwa kipindi chote cha miaka 40 ya ukomavu (maturity) na kipindi cha madahiro (grace period) cha miaka 10. Hivi ni viwango vya Jumuia ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA). Baada ya miaka 40, hakuna kiongozi yeyeto wa sasa atakayekuwa hai. Ndio maana wanafanya huu ushetani kwa kushirikiana na Majangiri wa IMF na WB.
 
kyoma

nna ombi kama inawezekana tupatie hiyo speech ya Mh sokoine ya kuliahirisha bunge il;i tuweze kujifunza zaidi
 
Kafara,
Sokoine alisoma wakati akipata "matibabu" huko YUGOSLAVIA. Vilevile aliporudi Tanzania na hata alipokuwa Waziri Mkuu alikuwa akisomea masters chuo kikuu cha DSM.

Sidhani kama kipindi alichoacha Uwaziri Mkuu na kwenda "kutibiwa" kinatosha kupata shahada ya kwanza. Nadhani UDSM walimruhusu kuchukua masters degree kwa kuzingatia uzoefu wake ktk uongozi na siasa.

Mzee ES,
Hawa viongozi ni watu kama mimi na wewe. Huyo Sokoine mtu wa watu wanawe wamesoma ngambo pia. Sokoine mtu wa watu alipougua alikwenda YUGOSLAVIA kutibiwa. Kama Sokoine, na Kawawa, walikwenda Yugoslavia, na Uchina kwa matibabu, nini kinachowazuia viongozi wa sasa hivi kutibiwa nje?

Tukiendelea kuwabeba viongozi wenye "nia nzuri" lakini kazi mbaya basi Taifa letu halitaendelea. Watanzania tunapaswa ku-raise standards za kupima utendaji kazi wa viongozi wetu. So far Tanzanians have set the standards so low.

Hawa kina kawawa ,sokoine walienda kutibiwa huko Nchi za mashariki kama msaada kwa viongozi hao wa kikomunisiti wakati huo.Ni viongozi wetu hao mara nyingi walikuwa wanatibiwa Muhimbili wakati huo na pale wanapopata Ofa kutoka kwa wakomunisti ambao walitoa hata nafasi nyingi za kimasomo kwa watanzania wakati huo ndiyo walienda kutibiwa bila ya kutugharimu fedha yetu walipa kodi.Kuhusu Kawawa hata hivi Leo Mara nyingi ni Mgonjwa Lakini si kila mara anaenda kutibiwa nje Mara nyingi anapata tiba Muhimbili pamoja na uwezo wa kuomba apelekwe Ulaya upo.Viongozi wetu wa leo Hakuna anayekanyaga Muhimbili wakati muungwana anauotea Urais ndiyo alikuwa akionekana viwanja vya muhimbili kutembelea ndugu na jamaa na Mke wake amewahi kulazwa Muhimbili na watoto kusoma Bongo Lakini Baada ya kupanda kazi ameanza kupeleka watoto nje..................... Kutibiwa sijui vile vile au la ,sina hakika!Hakuna anayejali sana Hospitali zetu na kuzibweresha ili siku moja wajivunie kupata matibabu Bora kwenye hizo Hospitali zetu.
 
Waheshimiwa,

Hapa nilipo inakaribia saa kumi na mbili asubuhi. Kuna mtu amenipigia simu na kuacha ujumbe kuwa jumbe zangu ninazoandika Jambo Forums zitanitia matatizoni. Sijuhi ni nani, na amepata wapi namba yangu, na amejuaje utambulisho wangu. Ngoja kwanza niwasiliane na provider wangu wa simu ili nijue hiyo simu imetoka wapi, kwa sababu haionyeshi namba kwenye call Id, pia, hata nikiwa nasikiliza ujumbe, namba haitajwi. Mtu mwenyewe anaongea Kiingereza lakini sio lafudhi ya kitanzania.

ujumbe wenyewe sio mzuri, una vitisho.
 
Waheshimiwa,

Hapa nilipo inakaribia saa kumi na mbili asubuhi. Kuna mtu amenipigia simu na kuacha ujumbe kuwa jumbe zangu ninazoandika Jambo Forums zitanitia matatizoni. Sijuhi ni nani, na amepata wapi namba yangu, na amejuaje utambulisho wangu. Ngoja kwanza niwasiliane na provider wangu wa simu ili nijue hiyo simu imetoka wapi, kwa sababu haionyeshi namba kwenye call Id, pia, hata nikiwa nasikiliza ujumbe, namba haitajwi. Mtu mwenyewe anaongea Kiingereza lakini sio lafudhi ya kitanzania.

ujumbe wenyewe sio mzuri, una vitisho.
Hapo juu nimependa ulivyoanisha ripoti mbali mbali za hayo mashirika majangili na jinsi yanavyoathiri Dhamira ya Nchi MASIKINI Kujikwamua Kiuchumi.Kazi Nzuri!Kuhusu swala la vitisho lifanyie uchunguzi Lakini Usitishike ni watu wanataka kukunyamazisha tu .Wapuuze hawakuwezi!
 
Back
Top Bottom