Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,399
- 39,550
Leo ni miaka 23 tangu Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine atutoke ghafla na kuacha simanzi na wingu la huzuni. Siku ile ya machozi na majonzi imebakia katika kumbukumbu za Watanzania wengi kama vile jana. Mfano wake ni kumbukumbu ya Wamarekani waliposikia habari za kuuawa kwa Rais John F. Kennedy.
Kila mtu aliyekuwa mtu mzima wakati ule anakumbuka vizuri siku hiyo alikuwa wapi na alikuwa anafanya nini. Je pengo aliloliacha marehemu limeanza kuzibwa?
Je, kuna kiongozi yoyote ambaye anakaribia sifa na utendaji kazi wa Marehemu Sokoine? Leo tunamkumbuka Edward Sokoine.
Pata kidogo chini hapa toka kwa mkuu Kyoma:
Kila mtu aliyekuwa mtu mzima wakati ule anakumbuka vizuri siku hiyo alikuwa wapi na alikuwa anafanya nini. Je pengo aliloliacha marehemu limeanza kuzibwa?
Je, kuna kiongozi yoyote ambaye anakaribia sifa na utendaji kazi wa Marehemu Sokoine? Leo tunamkumbuka Edward Sokoine.
Pata kidogo chini hapa toka kwa mkuu Kyoma:
Wazee, heshima yenu kwanza,
Mimi natofautiana na nadhalia ya kumfananisha Moringe Sokoine na Ngonyani Lowasa au Lyatonga Mrema. Sokoine alikuwa na sifa ya Uongozi, kwa maana ya kudhamilia kuonyesha njia. Pia, alikuwa ni mfanyakazi mwenye juhudi na maarifa. Dhamila ya Sokoine ilikuwa haimsuti katika utendaji wake wa kazi, ndio maana alifanikiwa kuthubutu kupunguza kero zilizowasibu watanzania. Mrema na Lowasa hawana sifa ya Uongozi, bali wana sifa ya kutawala. Pia, Mrema na Lowasa hawana sifa ya kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, bali wana sifa ya kushughulika. Dhamila zao wote wawili zinawasuta katika utendaji wao wa kazi, ndio maana hawawezi kufanikiwa, sio tu kupunguza, bali hata kugusa kero zinazowasumbua watanzania.
Lowasa na Sokoine wanafanana katika mantiki ya kuwa wote wameshika cheo cha uwaziri mkuu, lakini tofauti ni kuwa Sokoine alikitumia hicho cheo kuongoza watanzania, na Lowasa anakitumia hicho cheo kutawala watanzania. Katika michango yangu ya nyuma, nilikwisha elezea kwa kinaga ubaga tofauti kati ya cheo na uongozi, kwa maana ya kuwa uongozi si cheo, na cheo si uongozi. Hii ndio tofauti ya msingi kati ya ndugu yetu marehemu Moringe Sokoine ambaye aliunganisha cheo na uongozi katika nafsi yake, na kiongozi wetu mheshimiwa Ngonyani Lowasa ambaye amepata cheo cha uwaziri mkuu. Ili tuwajue hawa viongozi watatu, lazima pia tufahamu tofauti kati ya shughuli na kazi. Shughuli si kazi, na wala kazi si shughuli.
Kwa sababu nina mengi ya kuongea kuhusu Lowasa, naona nimuweke kiporo kwa leo, na nianze na tofauti kati ya Mrema na Sokoine. Mwaka 1973, nchi yetu ilikumbwa (off-guard) na ongezeko la bei ya mafuta ya petroli duniani. Hii iliathili ubadilishaji wa fedha ya kigeni. Mwaka huo huo mpaka 1974, tulikumbwa na ukame usio na kikomo, hivyo kusababisha upungufu wa chakula. Sukari, Mahindi, Unga wa ngano, na vifaa vya ujenzi ka simenti, na mabati vilikuwa hadimu. Serikali ililazimika kuingilia mgao wa chakula pamoja na mafuta ya Petroli kwa kutoa vibali kwa wale waliotaka kununua ili kulinda wananchi waliokuwa hawana uwezo wa kuchuana.
Tulichechemea mpaka mwaka 1977 wakati jumuia ya nchi za Afrika ya Mashariki ilipovunjika. Serikali ililazimika kutumia fedha ili kugharamia huduma ambazo mwanzoni zilikuwa zinatolewa na jumuia. Kumwaga tindikali kwenye kidonda, mwaka 1978 tukajiingiza kwenye vita dhidi ya Idi Amin. Kwa kiasi kikubwa, ile vita tuliigharamia sisi wenyewe bila ya fedha za mikopo. Resources zote zilienda kwenye vita, hivyo, uhaba wa kweli wa bidhaa ukaifadhaisha nchi yetu (kumbuka Sembe ya njano kwa foreni).
Tatizo kubwa lililozaliwa ni baadhi ya maafisa watendaji wa serikali katika ngazi za mikoa na wilaya, kutumia udhaifu wa uhaba wa bidhaa kwa kujilimbikizia mali. Mtindo waliotumia ulikuwa ni rushwa, kwa maana ya watendaji kuongwa na wafanya biashara ili wapewe vibali vya kulangua bidhaa zote hadimu katika bei ya serikali, na kuzificha hizo bidhaa mpaka kipindi fulani, alafu wanakuja kuziuza kwa bei ya magendo na kupata faida maradufu, wakati wananchi wakiteseka. Wafanyabiashara walipata faida isiyo kifani, na watendaji wa serikali walipata hongo kutokana na kuwauzia vibali walanguzi. Sokoine alikuwa kiongozi wa kwanza kustukia hiyo janja ya watendaji wa serikali walioshirikiana na walanguzi.
Sokoine alitoa matamko kuwa katika hali ya uchumi tuliokuwa nayo, mkate wa umasikini ilibidi ugawanywe kwa wote. Alisema, watu wanaolangua bidhaa zote na kuzificha kwapani, alafu wananchi wakiuliza tatizo ni nini wenyewe wanasema eti hali ya uchumi ni mbaya, lazima wasakwe mijini na vijijini. Akaimarisha jeshi la polisi ili liweze kupambana na hiyo tabia. Ili watu wanaojihusisha na vitendo hivyo wapate adhabu kali, akaliomba bunge kupitisha muswada kwamba wale wanaouza vibali na kulangua bidhaa hadimu wapatikane na hatia ya kuhujumu uchumi badala ya kosa la kula rushwa. Akaifanya iwe kampeni ya kitaifa.
Niliwahi kusoma paper ya Maliyamkono T. na Bagachwa, M.S.D (1990) ambayo haikumuongelea Sokoine lakini iliyoonyesha dhamila ya serikali ya kupambana na wahujumu uchumi. Inaonyesha idadi ya watu toka mwaka 1980 mpaka 1983 waliokamatwa, fikishwa mahakamani, na kufungwa jela baada ya kupatikana na hatia. Kwa Sokoine, hii haikuwa shughuli, bali ilikuwa ni kazi, kwa maana kuwa aliona kero, akaimarisha taasisi ya jeshi la polisi kwa kuiwekea mazingira ya kisheria baada ya kupata kibali kutoka katika taasisi ya bunge.
Kazi ya waziri au waziri mkuu ni kuimarisha taasisi zote anazoziongoza. Mwalimu aliwahi kusema kuwa, nchi inaongozwa na sheria. Watu lazima wajue kuwa sheria zimebadilika ili waweze kuzitii. Nchi haiongozwi na akili za mtu. Mambo ya kuona kiongozi anatoka kwenye vilabu vya pombe, au anaamka usingizini na kuanza kutoa hamri, au kufungia taasisi mbalimbali bila mpangilio, ni mishughuliko sio kazi.
Kifo cha Sokoine, kilikatisha watu huondo wa mechi kati yake na Msuya, ambapo mwamuzi alikuwa Nyerere na Kawawa. Sheria ya kuhujumu uchumi ilikuwa ni msumeno, na yeye hakuwa na hitilafu ya kuhofia. Inasemekana vijana wenye Land lover zilizokuwa ma matunubali walionekana nje ya nyumba ya Msuya. Waliulizwa wamepata wapi mamlaka ya kumpekua waziri, lakini vijana walimuonyesha kibali cha kufanya upekuzi. Inadaiwa Kawawa ndiye aliwaondoa vijana nyumbani kwa Msuya, kitendo kilichomuhudhi Sokoine. Nyerere alimwambia Moringe kuwa mambo mengine yanahiyaji tuyafanye taratibu, na Moringe akamjibu kuwa sheria lazima zichukuwe mkondo wake. Alisema kama tunaamua kuwa wajamaa, basi iwe hivyo, vinginevyo tufatute sera zingine.
Sokoine hakutumia vyombo vya habari kutangaza aliyokuwa akifanya. Tena mambo yake mengi yalikuwa hayatangazwi mpaka alipokufa.
Mrema alipokuwa waziri wa mambo ya ndani aliongoza vyombo vilivyopashwa kusimamia haki, sheria, usalama wa raia na mali zao. Hata hivyo, kipindi cha uangalizi wake, tulishuhudia utawala uliokiuka misingi ya sheria, usio tenda haki, na ulioshindwa kusimamia usalama wa raia. Badala ya kuimarisha taasisi ya jeshi la polisi, alitoa amri za kuwalazimisha raia kulala nje wakiliwa na mbu eti wanajilinda pamoja na mali zao kwa mtindo wa jadi wa Sungusungu. Polisi walibaki maofisini wakila rushwa, kulinda wahalifu waliohujumu nchi yetu, na kuota vitambi. Raia walikuwa na nondo, majembe, mapanga, visu vya jikoni, uma na vijiko, bila hata kupata mafunzo ya aina yoyote, wakingoja usiku kucha kupambana na majangiri yenye bunduki za SMG. Kwa Mrema, eti huo ndio ulikuwa usalama wa raia na mali zao. Watu wanasema huko ndiko kuchapa kazi kwa Waziri wa mambo ya ndani.
Mwaka 1993, chini ya uangalizi wake, Paspoti mpya za Tanzania 10,000 zilipotea wakati zinakabidhiwa wizara ya mambo ya nje kutoka uhamiaji (gazeti la Uhuru januari , 14 1993). Hapakuwepo na uzembe, bali vilikuwa ni vitendo vya rushwa ambavyo vilipelekea taifa kupata fedhea kwani hizo paspoti ziliangukia mikononi mwa raia wa Somalia na wale wabeba madawa ya kulevya. Hakuna aliyekamatwa. Packets 2,000 za madawa ya kulevya ‘Mandrax" ziliyeyuka zikiwa chini ya uangalizi wa polisi (Uhuru Januari 7 1994), Kilometa za mraba 4666 ziliuzwa kwa msukumo wa rushwa (Mfanyakazi januari 20 1993). Kila siku ya Mungu, magazeti yalikuwa yakiandika wizi upolaji wa mali ya Umma, na vitendo vya rushwa, huku Mrema akinguruma kutisha raia wasiokuwa na hatia kwa kutumia vyombo vya dola. Matukio yote makubwa yaliandikwa na kupita bila kumkamata mtu.
Sasa hivi mambo ya kuhujumu uchumi ni ya kawaida, lakini kipindi cha uwaziri wa mambo ya ndani wa Mrema, kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, uchumi wa nchi ulikuwa unahujumiwa chini ya uangalizi wake. Yeye ndiye alipalilia msamiati wa vigogo, alipojifanya polisi pale airport kwa kuingilia mali za wakubwa zikiwa zinatoloshwa nje ya nchi. Kwake yeye, sheria zilibagua vigogo na hazikutakiwa kuchukua mkondo wake. Hata wakati sheria zilipobadilishwa ili kuruhusu mfumo wa vyama vingi, aliongoza vyombo vya dola kuwapiga mabomu ya machozi viongozi wote wa vyama vya upinzani. Aliwanyima haki ya msingi ya kuhutubia wananchi kwa kuwakatalia vibali vya mikutano. Majuzi wakati anahojiwa na Radio Butiama, akasema alifanya hivyo kwasababu alikuwa akimtumikia kafili, lakini hakusema mradi wake alioupata ulikuwa ni upi? Sokoine alikuwa hamtumikii kafili, bali aliwatumikia wananchi.
Aliyavalia njuga matokeo ya uhalifu kwa kujenga vituo vya polisi kila kona ya nchi, ili kuzuia vibaka na kuwaacha ‘vigogo' ambao ni wezi wa kweli wakipeta. Badala ya kufanya kazi ya kuliwezesha jeshi la polisi kuwa na uwezo wa kuwakamata wahalifu wote ili wafikishwe mahakamani, akaanzisha utaratibu wa kutoa siku kumi kumi. Aligeuza ofisi na nyumbani kwake kilalacha kuwa kituo cha polisi, mahakama, na jela. Hakuna mhalifu hata mmoja aliyeitwa nyumbani au ofisini kwake, alafu akafikishwa mahakamani. Wizara zina miongozo, sheria pamoja na taratibu ambazo zinatakiwa kuheshimiwa na kiongozi yeyote. Alizinyamazisha taasisi za Mahakama na Polisi, badala yake hizi taasisi zikaanza kuwa mapango ya wala rushwa. Wahalifu walitakiwa kupelekwa polisi sio nyumbani kwa Waziri. Eti watu wanasema huku ndiko kuchapa kazi.
Akaanzisha tabia mbaya ya kulala uvunguni mwa vitanda vya wanandoa. Hizi ni busara alizokopa kutoka kwa mabibi wa kijadi waliokuwa wanataka kuhakikisha kama mke aliyeolewa na mjukuu wao ana bikira au la!. Waziri unamwita mke wa mtu ofisini kwako, tena kupitia kwenye vyombo vya habari? Kwa nini Waziri anaingilia ndoa za watu? Kwa nini asiimalishe taasisi zinazoshughulika na mambo ya jamii? Nchi inaporwa, vyombo vya dola vimewekwa kibindoni, Waziri anayeongoza taasisi zote hizo yuko ofisini na mke wa mtu akisuluhisha ugomvi wa makonde yatokanayo na wanandoa kunyimana uroda, au kufumaniana. Hizi zote ni shughuli na sio kazi.
Kwa nini Mrema alipata umaarufu wakati ule na sio sasa hivi?
Kila Mrema alipokwenda, alilakiwa na ‘umati mkubwa" wa watu ukiongozwa na kitengo cha umoja wa vijana, huku wakijivinjari na mapikipiki, bendera, pamoja na jezi zao za kijani na nyeusi. Ikasadikikika kuwa Mrema alikuwa na ‘mvuto wa watu". Yote haya yalitangazwa kila siku na vyombo vya habari. Alipojiengua CCM, na kuamua kugombea uraisi mwaka 1995, matangazo ya Radio Tanzania na magazeti ya chama yalienguliwa pia. Mrema aliendeleza matangazo yake ya kuwa na mvuto wa watu kupitia kitengo cha vijana wa NCCR –Mageuzi.
Walitueleza kuwa Mrema alikuwa na mvuto wa watu kiasi cha kubebwa kila anapotokeza. Wengine walimlilia Mrema kama wafanyavyo wapenzi wa Michael Jackson. Matangazo mengine yalisema Mrema alikuwa njiani kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma, lakini wakazi wa Dodoma wametembea kwa miguu kutoka Dodoma mpaka Chalinze ili kumpokea. Matangazo hayo yalionekana kuishawishi serikali kutumia vyombo vya dola ili kuzuia watu wasiende kupokea kipenzi chao. Hata hivyo, kinara wa mizengwe, Mwalimu Kambarage, aliona hiyo janja ya nyani na wakati akifungua kampeni za Mkapa pale Jangwani 1995, aliwaambia viongozi wa Serikali kuwa ‘Muacheni". ‘Kama mtu anapenda sana kubebwa, na watu wa kumbeba wapo, hata wakipokezana maili kumi kumi kama jeneza, waacheni".
Baadae Mrema alianza kuona haya, na mambo ya kubebwa bebwa yakayeyuka. Hakuwa na fedha wala ujanja wa kuendeleza matangazo yaliyokuwa yanavutia watu. Yeye hakuwa na sifa ambayo ingeendelea kuwapendeza, kuwashikilia na kuwavutia watu.
Kama mtu ana sifa fulani, mvuto wa watu unakuwepo hata kama matangazo yanakoma. Ni vema kutofautisha kati ya mvuto wa matangazo na mvuto wa sifa ambapo vyote viwili vinajenga mvuto wa watu. Matangazo yaligunduliwa ili kujaribu kuchukuwa nafasi ya sifa ambacho ni kiini katika mvuto wa watu. Hivyo basi, mvuto wa watu halisi sio sifa ya msimu kama ilivyo Kiangazi na Kipupwe, bali ni sifa ambayo mtu anakufa nayo kama Sokoine. Lakini hiyo sifa ikiwa ni matokeo ya kilemba cha ukoka kama ilivyokuwa kwa Mrema, ndipo inakuwa na tabia za msimu. Ndio maana amedolola kwa sasa.