Tume ya Hakijinai kukagua Vituo vya Polisi, Magereza, kuhoji Wafungwa, Wananchi na Askari

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,120
maxresdefault.jpg

JF SUMMARY

Tume ya Kuboresha Taasisi za Hakijinai Nchini itaanza ziara ya siku 12 katika Mikoa 13 kwa kutembelea Magereza Makuu 14 na Makazi ya Askari ili kupata maoni kutoka makundi mbalimbali wakiwamo Wananchi na Askari wa Vyeo vya chini.

Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mkuu Mstaafu #OthmanChande ameagiza Wakuu wa Magereza na Polisi kutoandaa mazingira yoyote kuanzia Wafungwa, Hali za Magereza na Mahabusu kwasababu wanataka kuona na kusikia uhalisia wa mambo.

Mikoa iliyotajwa ni Tabora, Kigoma, Katavi, Kagera, Mtwara, Mbeya, Morogoro, Ruvuma, Tanga, Arusha, Mwanza, Shinyanga, Visiwani Zanzibar, Dar es Salaam na Dodoma.

===============

TUME ya Kuangalia Jinsi ya Kuboresha Taasisi za Hakijinai nchini, inataraja kuanza ziara ya siku 12 katika mikoa 13, ambako itatembelea magereza 14 na vituo vya polisi, kupata maoni kutoka makundi mbalimbali wakiwamo wafungwa, mahabusu na askari wa vyeo vya chini.

Ziara hiyo inafanyika wakati tume hiyo ikiwa imeshakutana na wakuu wa Mahakama, Magereza, Polisi, Tume ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, alisema lengo la ziara hiyo ni kujionea hali halisi kutoka kwa wananchi, ili kutoa mapendekezo mazuri ya kuboresha mfumo wa haki jinai.

Jaji Chande alisema ziara hiyo itaanza Jumatatu ijayo na kuwaomba wananchi wa mikoa husika kujitokeza kutoa maoni na mapendekezo.

Alisema wajumbe wa tume watakutana na wafungwa na mahabusu moja kwa moja na kulitaka Jeshi la Polisi na Jeshi la Magereza kutoandaa watu wa kuzungumza na tume.

“Tutahojiana moja kwa moja na wafungwa na mahabusu ndani ya magereza 14 makuu na madogo. Tumeelekeza mamlaka husika, yaani Magereza na Polisi, wasiandae. Tunataka tukute hali kama ilivyo.

“Tukute kituo cha polisi kama kilivyo. Kama hakina miundombinu basi hakina, kisiwe na miundombinu kwa sababu tume inakwenda pale…tumewaelekeza wasisafishe njia, watuachie sisi wenyewe tuone, tuongee…ndipo tutaweza kupendekeza,” alisema.

Jaji Chande alisema katika ziara hiyo, tume itatembelea vituo na makazi ya polisi na magereza ili kujionea hali halisi na kuhoji askari wa vyeo vya chini wa majeshi hayo.

Alisema nia ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuunda tume hiyo ni kufanya maboresho makubwa ya kutatua changamoto zinazokabili taasisi za haki jinai nchini kwa miaka mingi ijayo.

Jaji Chande alisema kutengeneza mazingira ya kuficha taarifa hakutasaidia kutimia kwa azma hiyo.

MAKUNDI MIKOANI
Chande alisema kutokana na jiografia ya nchi, tume itagawanyika katika makundi matatu na kwamba kundi la kwanza litatembelea mikoa ya Tabora, Kigoma, Katavi na Kagera.

Alisema kundi la pili litatembelea mikoa ya Mtwara, Mbeya, Morogoro na Ruvuma; wakati kundi la tatu litaenda katika mikoa ya Tanga, Arusha, Mwanza na Shinyanga.

Kwa mujibu wa Jaji Chande, tume pia itafanya ziara visiwani Zanzibar na katika majiji ya Dar es Salaam na Dodoma.

Aidha, wajumbe hao watatembelea vyuo vya polisi vya Moshi na kile cha maofisa Kidatu mkoani Morogoro.

“Katika kila mkoa, wajumbe watapata fursa ya kutembelea wilaya mbili kuwasikiliza viongozi wa taasisi za haki jinai, viongozi wa dini, asasi zisizo za kiserikali na askari wa kawaida,” alisema Jaji Chande.

Kwa upande wa wananchi, Jaji Chande alisema tume itafanya mikutano ya hadhara kwenye kila wilaya ili kutoa nafasi kwa wananchi kuwasilisha maoni, ushauri na mapendekezo.

Katika kutekeleza hayo, alisema tume hiyo imeandaa madodoso ambayo yatawapa wananchi na askari nafasi ya kutoa maoni yake kwa uhuru akiwa faragha na kwamba sio lazima mhusika ataje jina lake.

Alisema Machi 13, mwaka huu, tume itakutana na Kamati za Kudumu za Bunge za Katiba na Sheria pamoja na ile ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.

Awali, Jaji Chande alieleza kwamba tume imekutana na wakuu wa taasisi za haki jinai ambao wametoa ushirikiano mkubwa.

Alisema tume imekutana na taasisi saba ambazo zinahusiana na mfumo wa haki jinai ambazo ni Tume ya Kurekebisha Sheria, Jeshi la Uhamiaji, Mganga Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).

Jaji Chande alisema kwa upande wa Zanzibar, tume hiyo imeshakutana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Kamishna wa Polisi, Chuo cha Mafunzo, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Kamishna wa Uhamiaji na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Alisema wiki hii tume inasikiliza taasisi na asasi zisizo za kiserikali zinazohusika na haki za binadamu na utawala bora, vyuo vikuu, mawakili, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Maofisa wa Taasisi za haki jinai wastaafu.

Kwa mujibu wa ratiba ya tume hiyo, leo itakutana na wakurugenzi wastaafu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Adadi Rajabu na Robert Manumba na makamanda wastaafu wa polisi, Jamal Rwambow na Leonard Rwabuzara.

Leo pia tume itakutana na makamishna wawili wa Magereza wastaafu, Juma Malewa na John Minja pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Huduma kwa Jamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

NIPASHE
 
Hii itaibua mengi hadi rais ataona aibu , mahakama za mwanzo ndio zinaongoza kwa kufunga watu

USSR
 
Katavi wafungwa wamejazana imefikia hatua Afande wanaoingia zamu na wafungwa nao wanabadilishana zamu ya kulala, kama ulikua umelala sasa inafika zamu ya kusimama.
 
Back
Top Bottom