Namkumbuka miaka ya 90 mwishoni mwishoni huko kipindi nikiwa kijijini kwa babu huko migombani migombani moshi, kipindi hicho nikiwa kwenye level ya juu kabisa ya utundu na ukurofi, yaani nikiambiwa kitu mi nafanya kinyume chake, yaani chochote kilicho hatarishi mi ndo akili ilinituma nicheze nacho, sumu sumu za kahawa hizi zilishanifanyia booking kama mara 2 hivi Ila safari zikaahirishwa, nyuki nao hawana adabu kabisa, tena hawa nyuki wa kwenye mapango mapango ni washenzi sana . ila hii kupenda penda asali nayo bana daaaah!! alikufa ng'ombe mi nikapelekwa hospitali,
Sasa kuna siku moja bana, nakumbuka ilikuwa kipindi cha kiangazi nimerudi zangu kutoka skuli jua kali mbaya halafu nina njaa kama ya wiki hivi, nyumbani sioni mtu na hakuna dalili na jikoni pamenuna, nikaona isiwe tabu nikachukua zangu manati nikazama migombani. Kwenye pitapita zangu huko kwenye mikahawa na migomba nikaona kapapai kapo juuu kule karibia kabisa na izraeli mtoa roho anakoishi, shetani alivyo mwehu akaniambi "wewe ni mwanaume panda faster" nikavua chachacha zangu kiroho safi, nikaanza kupanda, daaaah! Kumbe kale kapapai kalikuwa mtego sijui ndo chambo bana! mpapai wenyewe ni ile mipapai sijui ni ya enzi gani maana imekaakaa kama ile minazi ilopandwa enzi za sultan Said sayeed kule zanzibar. Nikajitutumua mtoto wa kiume, shetani nae ananambia "pambana", nikajivuta mtoto wa kiume, shetani nae anakazia "Nenda..." nikafika katikati kuna matawi, nikakaa kwenye tawi nikapumzika, baada ya kama dk 5 safari ikaendelea, mtoto wa kiume nikapambana mzee, nikajikunja mwanaume, nikajivuta sana, shetani nae anakazia "twende tu" daaah, nikafika kwenye vitawi vya pili nikapumzika tena, shetani akanipa wazo, "hebu simama ujaribu kama utafikia, nikasima nikajinyooosha lakini wapi! Nikajivuta lakini wapi...!!
Nyie!!. Shetani mhuni sana, nikakumbatia mpapai nikaendelea na safari, nikajituma sana, nikajinyoosha sana tu, aisee!! Daaah nikafika! Daaaah nikaukumbatia mpapai kwa nguvu then nikakanyoosha mkono wa kushoto nichukue nilichofata, aisee nyie watu. Nakumbuka tu sauti ya kukatika Ule mti wa mpapai Ila baada ya hapo sijui nini kiliendelea. Hadi leo mapapai huwa sili.