Katika hali isiyo ya kawaida, Kwa kauli na mienendo yake ya hivi karibuni, Anna Tibaijuka ameonesha wazi kukosa haya kwa kiwango cha kutisha, anafanya mambo ambayo hata mtoto mdogo hawezi kufanya.
Ni jambo la kusikitisha na la hatari kuona kiongozi wa umma mstaafu akitoa matamshi yanayochochea dharau dhidi ya mhimili wa mahakama. Kauli zake, zinazo hamasisha vurugu, fujo na uasi kama njia ya kufikia malengo ya kisiasa, si tu zinapotosha historia ya harakati za uhuru, bali pia zinahatarisha amani na mshikamano wa taifa.
Kauli za namna hii si za kubezwa, ni mbegu za machafuko. Ni fikra hatarishi zinazoweza kuligharimu taifa kwa damu, mali na mustakabali wa vizazi vijavyo. Hakuna kiongozi mwenye akili timamu anayeweza kusimama hadharani na kuhalalisha vurugu kisha ajione yuko sahihi.
Cha kushangaza zaidi, inaonekana Tibaijuka anaamini kuwa athari za vurugu hazitamgusa, kwa fedha zake anaweza kukimbilia nje ya nchi na kuyaacha madhara kwa wananchi wa kawaida. Huu si tu mtazamo mufilisi, bali ni dharau ya wazi kwa Watanzania na uhai wao.
Na si mara ya kwanza kwake kuonyesha dharau na kauli za hovyo. Historia yake imewahi kugubikwa na tuhuma nzito za ufisadi, ambazo alizipuuza kwa kauli nyepesi akidai fedha hizo zilikuwa “hela ya mboga.” mtu huyu anapaswa kutazamwa kwa jicho la kipekee.
Tangu alivyoshindwa katika harakati zake za kisiasa amegeuka mbogo na yuko tayari kwa lolote, ikiwemo kuhamasisha vurugu. Aina hii ya siasa za jazba na kejeli kwa taasisi kama Mahakama haina nafasi katika taifa linalojenga misingi ya utawala wa sheria na maendeleo endelevu.