Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema amesema amesoma alama za nyakati na kuona kwamba ipo haja ya kuachana na siasa za kugombea urais na badala yake ameamua kuwania ubunge katika Jimbo `lake` la Vunjo katika Uchaguzi Mkuu mwakani.
Hata hivyo, alisema uamuzi huo ambao ameuchukua baada ya kuombwa na kusumbuliwa kila mara, lazima upitishwe na vikao vya TLP.
Mbali na Mrema, kuna kila dalili kwamba viongozi wa Wakuu wa Vyama vya upinzani nchini, wameamua kukacha kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu ujao kama ilivyozoeleka, na badala yake wamepanga kugombea ubunge.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi na baadaye kuhojiana na viongozi hao, umeonyesha kwamba safari hii wapinzani wamepania kuwekeza nguvu zao katika ubunge.
Lengo la kufanya hivyo ni kutaka kupata viti vingi bungeni ili kuongeza upinzani katika chombo hicho cha kutunga sheria na mhimili muhimu.
Mrema, ambaye mwaka 1995, alishauriwa na Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Nyerere awanie ubunge badala ya urais, sasa amesema amekubali wito huo.
Mrema ambaye amegombea urais mara tatu bila mafanikio, alisema hatua hiyo inazingatia zaidi matakwa ya Watanzania na wanachama wa TLP. Alifafanua kwamba amekuwa mtumishi wa umma miaka yote hivyo kila wakati analenga kufanya jambo ambalo litakuwa na faida kwa watu wengine na si kwake binafsi.
Hata hivyo, alisema japokuwa suala hilo (la kuachana na kugombea urais) ameliridhia, lakini lazima liamuliwe na mkutano Mkuu wa TLP unaotarajia kufanyika mapema Aprili, mwaka huu.
Mrema alisema suala la kugombea ubunge hakuwa nalo ila ameombwa na aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo 2000- 2005 Meja Jesse Makundi.
Alipoulizwa kama anaweza kushinda ubunge Jimbo la Vunjo, alisema mgombea wa TLP mwaka 2005, alipata zaidi ya kura 26,000, Chadema 8,000 na NCCR- Mageuzi kura 6,000.
Alisema kura hizo zikijumlishwa zinapita zile za mgombea wa CCM aliyeshinda kwa kura 30,000.
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995, Mrema aligombea kupitia NCCR-Mageuzi na kushika nafasi ya pili kwa kupata kura milioni 1.8 nyuma ya Benjamin Mkapa wa CCM.
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, Mrema aligombea kupitia TLP na kushika nafasi ya tatu kwa kupata kura 600,000 nyuma ya Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF aliyeshika nafasi ya pili na Mkapa aliyeshika nafasi ya kwanza.
Chati ya Mrema iliporomoka katika uchaguzi wa mwaka 2005 baada ya kushika nafasi ya nne kwa kupata kura 80,000 nyuma ya Freeman Mbowe wa Chadema, aliyeshika nafasi ya tatu, Profesa Lipumba aliyeshika nafasi ya pili na Rais Jakaya Kikwete aliyeongoza.
Alisifu hekima za Meja Makundi na kusisitiza kwamba bila TLP kusimama `Buldoza` kuna hatari jimbo hilo likaendelea kushikiliwa na CCM na `washirika wake`.
Habari za ndani kutoka kwa vyama hivyo zinasema hatua hiyo ya viongozi wa upinzani, (ya kugombea urais kila mara) ambayo ilikuwa ikilalamikiwa mno, inalenga kujiimarisha ili kuweza kuchukua nchi mwaka 2015.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Freeman Mbowe, alisema suala la chama hicho kusimamisha au kutosimamisha mgombea urais, litategemea maamuzi ya wanachama ambayo yatazingatia maoni ya Watanzania walio wengi.
Alisema Chadema hakipo kwa ajili ya maslahi ya mtu au kikundi kimoja, bali kwa ajili ya Watanzania wote, hivyo mikakati yake ya kisiasa na uamuzi, lazima ufuate matwaka ya wananchi.
Alipoulizwa kama suala la kuacha kuwania urais na kugombea ubunge Jimbo la Hai kama inavyosema lina maslahi kwa Taifa, Mbowe alikubali.
Japokuwa hakuwa tayari kukanusha au kukubali, Mbowe alisema yupo tayari kugombea nafasi yoyote atakayoteuliwa na chama hata kama ni ubunge.
Kuna habari kwamba Mbowe amejipanga kuwania ubunge katika Jimbo la Hai, ambalo alipata kuliwakilisha mwaka 2000 hadi 2005, alipogombea urais na kushindwa.
Kwa upande wa NCCR-Mageuzi, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa chama hicho, Faustine Sungura alisema kwa utamaduni wa kwao, si lazima Mwenyekiti wao James Mbatia awanie urais.
Ili kuondoa msuguano kati yake na Mrema, Mbatia ambaye pia ni mzaliwa wa Vunjo, inasemekana anapanga kugombea ubunge Jimbo la Kawe, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, japokuwa Mbatia hakupatikana kuzungumzia suala hilo, Sungura alisema ni haki ya kiongozi huyo kugombea mahali anapotaka.
Naye Mwenyekiti wa CUF, Ibrahim Lipumba hakupatikana kuzungumzia jambo hilo baada ya wasaidizi wake kueleza kwamba alikuwa anashughulikia kusafirisha wajumbe waliokuja jijini kuhudhuria Mkutano Mkuu wa chama hicho uliomalizika juzi.
SOURCE: Nipashe