na Schola Athanas
WAZIRI wa Nishati na Madini, Nazir Mustafa Karamagi, jana alidai kwamba aliokolewa na Spika wa Bunge, Samuel Sitta kutoka katika kibano cha wabunge wakati wa kuchangia hotuba ya bajeti ya makadirio ya wizara yake.
Akizungumza katika kipindi cha Bunge Wiki Hii, kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TvT) na kuongozwa na Tido Mhando ambaye ni mkurugenzi wa kituo hicho, Karamagi alisema Sitta alimuokoa baada ya kuvunja baadhi ya vipengele katika kanuni za Bunge, vinavyowawezesha wabunge wengi kuchangia.
Mjadala ulikuwa mkali kidogo, si kwa nia mbaya, ni kwa nia ya kuboresha, ni kweli, vyombo vya habari viliandika kuwa niliokolewa na Spika, hii ni kutokana na Spika kuvunja baadhi ya vipengele katika kanuni za Bunge, vinavyowawezesha wabunge wengi kuchangia, alisema Karamagi.
Alisema wabunge wengi walikuwa na hamasa ya kuchangia ili wapate umeme katika maeneo yao, hivyo kulikuwa na maswali mengi.
Akizungumzia baadhi ya hoja za wabunge zilizotolewa katika mjadala wa wizara yake, alisema suala la wageni pekee kufanya utafiti wa awali wa madini si la kweli kwa kuwa kuna Watanzania 5,800 wanaofanya utafiti huo na wamekwishapewa leseni za kazi ya kuchimba madini.
Bado wizara inaendelea kutoa leseni kwa Watanzania ambao waliingia katika maeneo ya wachimbaji wenye leseni kubwa, hawa tunawaondoa katika maeneo hayo na kuwatafutia maeneo mengine ilimradi wafuate sheria, alisema Karamagi.
Kuhusu mikataba kuharakishwa na kubadilishwa, alisema huwa inabadilishwa na inatofautiana kati ya mikataba ya zamani na ya sasa.
Akizungumzia agizo la rais la kupitia upya mikataba ya madini, alisema si jambo rahisi kuiondoa haraka kwa sababu mikataba ina taratibu zake, hivyo inapaswa kuwasiliana na wenye kampuni ili kuwaomba wakubali kuibadili kwa hiari yao.
Mikataba ya mwanzo ilikuwa kwa ajili ya kuwavutia wawekezaji, hivyo kwa kuwa soko la madini la Tanzania limeishajulikana, tutabadilisha vipengele kwenye mikataba ambavyo tuliviweka kwa ajili ya kuwavutia.
Na hata mafuta na gesi, kuna kampuni 19 ambazo zinafuatilia, nishati hizi zimeshagundulika katika maeneo ya Songosongo, Mnazi Bay, Mkuranga na Kigoma Bay, alisema Karamagi.
Akizungumza katika kipindi hicho, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), alisema serikali iliahidi kuwa mikataba ya madini itabadilishwa na kamati itaundwa, cha kushangaza bado mikataba inaendelea kusainiwa kinyume cha azma ya serikali na rais mwenyewe.
Mikataba inatakiwa kubadilishwa haraka kwani kuchelewa kunasababisha kampuni kushindwa kulipa kodi haraka ambayo ni asilimia 30, kutokana na kuondolewa kwa vipengele katika sheria ya mwaka 2001-2002, kuna kampuni ambazo zilitakiwa kuanza kulipa kodi ikiwemo Barrick, lakini inashangaza kuona wakisaini mkataba mwingine, alisema Kabwe.
Gema Akilimali kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), alisema wawekezaji wanaokuja kuchimba madini wanakuja kunyanganya maeneo kwa sababu wanawakuta wananchi wanachimba madini katika sehemu hizo, hivyo hawafanyi utafiti kama inavyodaiwa katika mikataba hiyo.
Nashauri wavune madini, lakini badala ya kuyauza nje kama madini, vitengenezwe vito vya thamani na viuzwe ili taifa lipate faida zaidi, alisitiza Akilimali.
Katika mjadala wa makadirio ya wizara yake, Waziri Karamagi ambaye ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, alibanwa kwa kiasi kikubwa na wabunge, wengi wakitaka maelezo ya kina juu ya kero ya umeme, mikataba ya madini na mambo mengine kadha wa kadha.
Hata hivyo, kutokana na idadi kubwa ya wachangiaji ambao kila mmoja alionekana kuwa na hoja nzito, Spika alilazimika kuingilia kati mara kwa mara na hatimaye kufanikisha kupita kwa mbinde kwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.