Waziri alaumu mabalozi kwa kukiuka taratibu
Faraja Mgwabati
HabariLeo; Saturday,October 06, 2007 @00:02
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amewalaumu baadhi ya mabalozi wa nchi za nje waliopo nchini kwa kuzungumzia masuala ya rushwa kwenye vyombo vya habari, kinyume cha masharti ya Mkataba wa Vienna, badala ya kuzungumza na Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kurejea kutoka ziara na Rais Jakaya Kikwete nchini Marekani, Membe alisema inasikitisha kuona baadhi ya mabalozi hao wanasimama majukwaani na kuisukuma Serikali kutoa maelezo kuhusu masuala ya rushwa bila hata kuiuliza Serikali yenyewe. Baada ya kuzungumza na waandishi wa habari asubuhi ofisini kwake, Waziri Membe, pia alikutana na mabalozi jana mchana kwenye Ukumbi wa Karimjee.
Aliwajulisha kuhusu hatua ambazo serikali inazichukua kuhusu tuhuma hizo na kuwataka mabalozi hao na wananchi kwa ujumla, kuwa na subira kwa kuwa uchunguzi unaweza kuchukua muda, lakini utakuwa ni wa uhakika. Katika mkutano wake na waandishi wa habari, Membe alisema mabalozi hao wanakiuka kifungu namba 34 cha Mkataba wa Vienna unaomtaka balozi ye yote kwenye nchi fulani, kama ana tatizo lolote au haridhishwi na kitu awasiliane na Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje.
Sisi Balozi wetu hawezi hata siku moja kufanya hivyo
balozi wetu wa nchi za nje akifanya hivyo watamrudisha mara moja kwa sababu siyo sahihi kutumia majukwaa kwa balozi, alisema Membe. Membe alisema anashangazwa na mabalozi hao ambao wanakuwa na wasiwasi na Serikali wakati marais wao juzi wameipongeza nchi kwa kupiga vita rushwa na wakaipa Tanzania fedha nyingi kupitia Mpango wa Akaunti ya Milenia ambao uko chini ya Serikali ya Marekani.
Nashindwa kuwaelewa kama mambo wanayozungumza ni yao binafsi au wametumwa na nchi zao kwa sababu nchi zao zinatusifia, wao huku wanakuwa hawatuamini, alisema Mwembe. Alisema serikali haiwezi kufanya mambo kwa kukurupuka kwa kutoa uamuzi ambao utawafurahisha mabalozi, lakini ukawaumiza watu wengine ambao hawahusiki na rushwa. Ndiyo maana suala la mgodi wa Buzwagi na Benki Kuu (BoT) linafanyiwa uchunguzi wa kina ili ukweli sahihi upatikane, alisema.
Its not fare (sio haki) kwa mabalozi hao kuilazimisha serikali kutoa maelezo wakati uchunguzi wa tuhuma za rushwa unaendelea, alisema na kuongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inafanya uchunguzi.
Nimezungumza na PCCB juzi na wameniambia kuwa tuhuma hizo za rushwa zinachunguzwa kwa umakini mkubwa na matokeo yake yatawekwa wazi kwa kila mtu na kama itabainika Membe anakula rushwa, basi atawajibishwa, alisema.
Aliongeza: Tusimlazimishe Rais kutoa uamuzi wakati uchunguzi unaendelea. Hii ni hatari anaweza ku-shoot (kupiga) hata vifaranga wasio na hatia, alisema. Alitoa mfano kuwa wakati fulani baadhi ya jamaa zake walipomlazimisha kupiga ndege aina ya kanga wakati ndege huyo alikuwa ana vifaranga walipokwenda kuwinda kwenye shamba lake mkoani Lindi. Membe alisema katika matokeo ya uchunguzi wa PCCB kama kiongozi ye yote atapatikana na hatia, basi Rais Kikwete hawezi kumwonea haya, atamwajibisha kwa kuwa hakuna kiongozi mwenye ubia na serikali.
Alisema serikali imefanya mambo mengi katika kupambana na rushwa, ikiwa ni pamoja na kuimarisha PCCB kwa kupeleka vijana nje kusomea jinsi ya kupambana na rushwa kitaalamu. Hata Rais Bush (George W. wa Marekani) mwenyewe amemwambia Rais Kikwete juzi kwamba rushwa ipo kila nchi ila kinachotakiwa ni kufanya uchunguzi wa kina kwa tuhuma zinazotolewa dhidi ya serikali, alisema.
Alisema matunda ya juhudi hizo yameanza kuonekana kwa Tanzania kushika nafasi ya 94 mwaka huu duniani kutoka 124 mwaka juzi katika kupambana na rushwa kwa mujibu wa Ripoti ya Shirika la Kimataifa la kupambana na rushwa la Transparency International. Akiwa na mabalozi baadaye jana, Membe alisema: Lazima uchunguzi ufanywe kwa makini ili hata mtuhumiwa naye apate haki ya kujitetea na aweze kusafisha jina lake na huu ndiyo utaratibu unaotumika duniani kote.
Mabalozi walikuwa wakimsikiliza kwa makini. Baada ya maelezo hayo, Membe alikaribisha maswali na wengi wa mabalozi walinyamaza kimya kuonyesha kuridhika na maelezo hayo. Balozi wa Uingereza nchini, Philip Parham alisimama na kuelezea kufurahishwa na maelezo yaliyotolewa na Waziri Membe.
Katika mkutano huo na mabalozi, Membe pia alizungumzia masuala mbalimbali yaliyojitokeza katika ziara yake na Rais Marekani, likiwamo la Zimbabwe. Katika suala la Zimbabwe, Membe aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kuondoa vikwazo kwa nchi hiyo ili wananchi wake wasiendelee kuteseka.
Pia alisema SADC inaamini kuwa kujitoa kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Gordon Brown kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya unaotarajia kufanyika mwezi ujao Ureno, kama Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe atahudhuria siyo suluhisho la matatizo ya Zimbabwe.
Wiki chache zilizopita, Brown alitangaza kuwa hatahudhuria mkutano huo kama Rais Mugabe atahudhuria. Hata hivyo, akijibu hoja hiyo, Balozi Parham alisema kama Brown hatahudhuria kwenye mkutano huo haina maana Uingereza haitawakilishwa na pia kama Mugabe hatakwenda kwenye mkutano huo, nchi itawakilishwa na maofisa wengine wa nchi hiyo.