Mzee Mwanakijiji
Platinum Member
- Mar 10, 2006
- 33,710
- 40,777
Makala hii imetoka kwenye gazeti la Tanzania Daima (hard copy) lakini kwenye mtandao haikuwekwa.
Ningependa kuungana na waandishi wengine wengi leo ambao wameandika kuhusu kikao cha NEC Butiama na maana yake kwa Taifa. Nikiwa mmoja wa waliofuatilia kwa karibu naomba nikwepe kufanya hivyo kwa sasa ili nipate muda wa kuchambua hasa kile kilichojiri. Nirudi kidogo kwenye suala la EPA na madai kuwa yawezekana Tanzania iko mikononi mwa maghaidi.
Uwezekano kuwa nchi yetu iko mikononi mwa maghaidi na kuwa vyombo vyetu vya usalama vinatambua hivyo, ni uwezekano ambao lazima umshtue Mtanzania yeyote yule kwani kama ni kweli, basi tunachopigania siyo hali yetu ya maisha ya kuwa huru na wenye kufanikiwa bali tunapigania uhai wetu kama Taifa.
Bila shaka umepigwa na butwaa unashangaa hili limetoka wapi tena hata hivyo kama umekuwa mfuatiliaji wa habari unajua kabisa nini niniachozungumzia. Mapema mwezi uliopita Inspekta Jenerali wa Polisi akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa Kamati inayofuatilia wizi wa EPA alisema kuwa suala la wizi wa EPA linaweza kufananishwa na utekaji nyara wa ndege ambapo vyombo vya usalama vinalazimika kuzungumza na wateka nyara hao ili kunusuru maisha ya abiria.
Ni katika maelezo hayo na jinsi alivyotumia mfano huo ndipo leo ninajikuta najiuliza kama yumkini kuwa nchi yetu imetekwa nyara na maghaidi wa EPA na sasa tunafanya nao majadiliano ili wasitulipue? Kama kweli tumetekwa nyara basi tufanye nini tujinasue au tukubali tu yaishe na tusalimike?
Binafsi sitaki kuamini hata kidogo kuwa tumetekwa nyara; lakini dalili zote zinaonesha kuwa tumechukuliwa mateka na mafisadi wa EPA. Kwanza kabisa lazima tukumbuke kuwa hawa jamaa waliokwapua fedha za EPA ni kama majambazi ambayo yameingie Benki na kuchota fedha toka Chumba Kikuu na huku wakipepea mabomu na silaha zao wakatokomea mafichoni.
Na sasa baada ya polisi kujua ni kina nani walioiba benki wanagundua pia kuwa siyo walikwapua na vipande vya dhahabu na kuondoka na baadhi ya wafanyakazi kama bima y ao. Sasa polisi wanakabiliwa na swali wavamie nyumba kuokoa fedha na watu au wakae katika meza ya majadiliano na majambazi ili waokoe fedha na watu?
Kwa mujibu wa IGP Mwema uamuzi ni huu wa kukaa na majambazi na wateka nyara ili kupata suluhu wasije wakailipua nchi.
Sasa kama hili ni kweli lazima tujiulize kwanza, walinzi wa benki zetu walikuwa wapi hadi majambazi yakaingia hadi Benki Kuu na kuchota fedha na kutuchukua mateka? Wakati mafisadi wa EPA wanaingia mikataba ya wizi na kuunda makampuni ya geresha wale walinzi walioapa kuilinda nchi hii walikuwa wanalala wapi? Jibu siyo gumu.
Ndugu zangu, taifa letu limechukuliwa mateka kwa sababu walinzi wa Taifa hilo na hasa vyombo vilivyotakiwa kusimamia usalama wa Taifa hili wanadaiwa kuwa ni sehemu ya wezi hao. Kwamba, waliokula njama kuiibia nchi hii na kututeka mateka walifanya hivyo mbele ya vyombo vya usalama na vyombo hivyo havikufanya lolote kuzuia.
Tumetekwa mateka kwa sababu Jeshi la Polisi na vitengo vyake vyote ambavyo vimepewa jukumu la kulinda raia na mali zao walishindwa kufanya hivyo. Kama Jeshi la Polisi lilishindwa kuanzisha uchunguzi wa kihalifu muda wote wa tuhuma za wizi wa EPA kwanini leo walalamike kuwa tumetekwa mateka?
Kama Jeshi la Polisi ambalo lina maofisa wenye nyota nyota, magari ya vingora na mbwa wa kunusa walishindwa kuzuia wizi wa Benki Kuu mchana kweupe ni jinsi gani tunaweza kulalamika kuwa tumechukuliwa mateka? Lakini binafsi siwapi mzigo mzito wa lawama polisi isipokuwa chombo kimoja ambacho kwa hakika siyo tu hakina budi kupanguliwa lakini viongozi wake kuwajibishwa kwa kuacha nchi yetu itekwe nyara na mafisadi
Chombo hicho ni idara ya Usalama wa Taifa ya Tanzania. Kama kuna chombo ambacho siyo tu kimeliangusha Taifa letu bali pia kimeonesha udhaifu mkubwa wa kuwajibika ni idara hii ya Usalama wa Taifa ambayo imekaa kana kwamba inafanya kazi wakati wa vita baridi.
Kwa mujibu wa sheria iliyounda idara hiyo ina majukumu makubwa manne ambayo yote yanahusiana na mambo ya usalama wa Taifa na kukusanya habari za kijasusi na kutoa taarifa kwa vyombo husika. Katika kufanya hivyo idara hiyo inajukumu la kuangalia mambo ya wizi wa siri za serikali kupeleka kwa adui, habari za kighaidi, kuvuruga vitu, na pia mambo mengine kama hayo.
Idara hiyo inakatazwa kisheria kusimamia usalama moja kwa moja na pia inakatazwa kuanzisha uchunguzi au ujasusi dhidi ya mwananchi yeyote wa Tanzania kwa sababu ya shughuli halali za mtu huyo kupinga au kutokubali maamuzi fulani ya serikali akitelekeza haki zake za kikatiba.
Idara hii ilitakiwa kuhakikisha kuwa inakusanya taarifa zote za kijasusi ambazo zinaweza kusaidia kuwa hakuna ghaidi ambaye anaweza kupenya na kufanya uovu na hivyo ni jukumu la idara hiyo kutoa taarifa kwa vyombo husika ili vichukue hatua madhubuti. Kwa maneno mengine, Usalama wa Taifa wanatakiwa kushughulikia ukusanyaji wa taarifa za kijasusi na siyo ulinzi wa viongozi au mipango ya viongozi.
Yawezekana kuna sababu ya Usalama wa Taifa kuonekana wanashughulikia ulinzi wa viongozi lakini kisheria jukumu hilo naamini halipo mikononi mwao; wao jukumu lao ni kushughulikia mambo ya kijasusi.
Ni kwa sababu hiyo basi naweza kusema pasipo shaka kuwa wizi uliotokea Benki Kuu kuanzia huu wa EPA, na ndugu zake wa Deep Green, Meremeta, Tangold, na Mwananchi Gold yote yametokea kwa sababu TISS ilishindwa vibaya kabisa kukusanya taarifa za kijasusi. Hii ni aibu kwa taifa hili.
Kama watu wanaolipwa kukusanya habari za kijasusi walishindwa kugundua kuwa kuna fedha zimeibwa toka Benki Kuu ni nani basi tunaweza kumuamini? Lakini swali jingine ni kuwa je yawezekana kuwa TISS haikushindwa lakini ilikuwa ni sehemu ya uchafu na ufisadi huo?
Mpendwa msomaji kama unakumbuka utaona kuwa wakati Bi. Meghji ameidhinisha fedha za kuilipa kampuni ya Kagoda aliambiwa na Balali kuwa fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya shughuli za Usalama. Hadi leo hii, hakuna chombo cha usalama ambacho kimekana kuhusika na wizi wa fedha hizo. Siyo Polisi, JWTZ au Usalama wa Taifa ambao wamesimama na kusema hawakuhusika na wizi huo au kutoa baraka zao kama ilivyodaiwa kitu ambacho mwenye fikra anaweza kujua ina maana gani. Wakati mwingine ukimya una maana ya kukubali.
Usalama wa Taifa hawakushindwa wajibu wao kwenye suala la EPA tu bali pia kwenye suala jingine la Richmond. Hivi hadi Watanzania tunaingia kwenye mkataba huu wao Usalama wa Taifa (TISS) walikuwa wapi? Hivi ni kitu gani ambacho kinahatarisha nchi kama suala la nishati kuchezewa?
Wakati tumepata dharura ya nishati ilihitajika uangalizi mkubwa wa nini tunafanya tusije kukurupuka kualika wasiotutakia mema kuja kutuletea umeme. Mara baada ya tetesi kuwa Richmond ni kampuni feki zimeanza (na zilianza zamani) TISS walifanya nini kuhakikisha kuwa usalama wa nchi yetu hauwi mikononi mwa kikundi cha watu wachache? Hakuna.
Katika ripoti ya Kamati ya Bunge iliyoongozwa na Dr. Mwakyembe hatuoni ni jinsi gani watu wa Usalama wa Taifa walishiriki katika kuhakikisha kuwa Richmond haipewi tenda hiyo. Kwa mujibu wa sheria iliyounda taasisi hiyo nina uhakika wanazo nguvu za kuangalia habari za kijasusi ambazo zinaweza kutishia usalama wa nchi yetu. Ninaamini TISS ingeweza kutumia nguvu walizonazo katika ibara ya 5(b) ya sheria hiyo ya Idara hiyo. Hawakufanya hivyo.
Sasa hivi kuna suala zima la fedha za dola zilizokosewa karibu miaka nane iliyopita karibu dola milioni tatu; fedha zile ziliishia wapi baada ya kukataliwa? Hakuna anayejua na hakuna taarifa iliyotolewa lakini wakusanya habari za kijasusi wetu wanaendelea na maisha yao wakiombea kuwa Tanzania iko salama.
Idara hii inahitaji kufanyiwa mabadiliko ya haraka na ya lazima ili kuinusuru na kuipa nguvu ya kulinda maslahi ya Taifa hili. Ndugu zangu, roho ya usalama wan chi yetu iko mikononi mwa taasisi hii na inaposhindwa kutimiza wajibu wake siyo tu viongozi wake wanahitaji kuwajibika lakini wao wenyewe wakiwa waungwana wangeweza kuwajibika.
Hivi Mkurugenzi wa Idara hiyo anaweza vipi kupata usingizi huku akijua kuwa taasisi yake imeshindwa kazi ya kukusanya habari za kijasusi? Na hapa simaanishi kutafuta nani ni nani wa Jambo forums! Nina maana kukusanya habari ambazo zingesaidia kuzuia Taifa kutekwa nyara na mafisadi? Yeye na waziri wake (sijui waziri wa Usalama wa Taifa ni nani.) wanaweza vipi kunywa chai, na kula kuku kwa mrija wakati wahuni wachache wanatuingiza mjini na kampuni hewa hadi Taifa linaadhirika kwa kujiuzulu waziri Mkuu?
Tunaweza kuchezea mambo mengine lakini hili la usalama wa Taifa letu siyo jambo la kuchezea hata kidogo au kuchukulia kwa wepesi. Idara inayotengewa mabilioni ya shilingi inaposhindwa kugundua ufujaji mkubwa benki kuu siyo tu imeshindwa kazi bali pia imeihatarisha nchi na kwa hakika viongozi wake lazima wawajibishwe.
Mabadiliko makubwa yanahitajika katika kuiboroesha idara hii. Kwanza kabisa ni kubadilisha sheria ya TISS ili kukipa chombo hicho jukumu la wazi la kufuatilia habari za kijasusi katika utendaji kazi wa idara na wizara mbalimbali za serikali na kuhakikisha kuwa habari hizo zinafanyiwa kazi aidha kwa kutoa taarifa za ndani au kutoa taarifa kwa Kamati ya Usalama ya Bunge na kwa Rais (yaani Rais asitaarifiwe bila Kamati ya Bunge nayo kupatiwa taarifa).
Jingine ambalo naamini linaweza kutusaidia huko mbeleni ni kuhakikisha kuwa idara hiyo haijajaa ndugu, jamaa, na marafiki wa familia za viongozi kwani siyo tu ni hatari lakini maslahi ya watu yanaweza kupiku maslahi ya Taifa. Sijui sasa hivi idara ilivyo lakini kama kuna dalili yoyote ya undugunization basi ni chumvi inayokoleza kushindwa kwa taasisi hiyo kugundua maovu (itaweza vipi kuchimba ofisi anayosimamia baba au mama)!? Hivyo, idara hii irudi kwenye uwezo na uwezo pekee na ianze tena kutafuta watumishi wake hata nje ya jamaa, ndugu, na marafiki. Ninasema hili nikiwa najua mambo fulani jinsi ya watu walivyopata kazi kwenye idara hiyo nyeti.
Pamoja na hayo, idara hii lazima ipewe uwezo wa kujipenyeza katika taasisi mbalimbali kama ilivyokuwa miaka ile ambapo wale watumishi waliipenda nchi kuliko. Leo hii hata waliojipenyeza wengi wanajulikana na siyo siri kama ilivyokuwa zamani. Kama tungekuwa na watu waliojipenyeza Benki Kuu na wanajua jukumu lao sijui kama kina Kagoda wangeweza kuiba na kututeka nyara! Kama tungekuwa na watu wa Usalama Idara ya Madini sijui kama leo tungekuwa na vibangusilo vinavyolia lia!
Hapa simaanishi kujaza watu wa usalama kila kona na kuanza kulifanya Taifa liishi kwenye hali ya wasiwasi bali kuhakikisha kuwa wale wote wanaofanya kazi na serikali au kuingia mikataba na serikali wajue kuna hatari ya kutiwa pingu. Hivyo, watu hao wa Usalama naamini wakati umefika wapewe nguvu ya kupekua na kukamata (search and seizure) ili katika mazingira fulani basi wawe na uwezo wa kutia mbaroni wahujumu wa uchumi wetu kabla hawajatoroka.
La mwisho ambalo naamini linaweza kusaidia idara hii ni mahusiano yake na wananchi wa kawaida katika kukusanya taarifa nyeti. Idara hii lazima ihakikishe inafanya kazi na wananchi kwa ukaribu hata kama kwa siri ili iweze kupata habari nyeti. Suala la Richmond na suala la EPA ni uthibitisho kuwa idara hii iko mbali na wananchi.
Ni nani basi atawaambia wana Usalama wetu kuwa kuna tatizo na wafanye uchunguzi? Hivi IGP Mwema na Mkurugenzi Rashid Othman wanaweza kufanya uchunguzi kuhusu makampuni hayo bila kuomba kibali ikulu? Hivi tulipotekwa mateka wao walifanya nini? Kama Rais asingeamuru wafanye uchunguzi huo wao wangefanya nini? Ni wazi kuwa hawawezi kufanya au kuanzisha uchungu wao wenyewe isipokuwa hadi wapate baraka toka Ikulu ndio maana leo tumetekwa nyara na wao hawana cha kufanya isipokuwa kupiga magoti katika altare ya mafisadi na kujaribu kujitoa mhanga kama bangusilo wa mafisadi. Usalama uamka na kuwa kweli usalama wa Taifa, tusije kuwa na taasisi ya usalama ambayo yenyewe si salama.
Kama tunataka kweli kulinda rasilimali zetu hatuna budi kuimarisha usalama wa Taifa ili usiwe usalama wa wenye matumbo ya Taifa bali usalama wa hazina, mali, na raslimali za Taifa. Kama wale waliodhaminiwa kusimamia usalama wa taifa hili wameshindwa kufanya hivyo, kama waliopo katika safu za usalama wa taifa weshindwa kulinda usalama wa Taifa na badala yake wanahangaika na kutafuta watu wasiowahusu na kushiriki kwenye michezo michafu ya kisiasa basi waachie ngazi tu ili tukodi watu wengine waje watulindie usalama wetu kwani ndugu zetu wenyewe wametuuza!
Vinginevyo, tunapofanya majadiliano na hawa mafisadi waliotuteka ni nani ana nguvu basi? Ni wazi nguvu ya mjadala haiko na timu ya Mwanyika bali na wateka nyara maana katika utekaji nyara mwenye nguvu ni aliyeshika silaha.
Swali ambalo naogopa jibu lake ni kuwa hawa walioiteka nchi na kututishia kuwa tukipega kelele watailipua wameshika kitu gani cha thamani kiasi kwamba tunashindwa kuwatia pingu na kufanya majadiliano nao?
Hoja yangu nimejenga, kaditamati natama,
Kwa maneno nilopanga, inahusu usalama,
Mwenye kutaka kupinga, namruhusu kusema,
Usalama wa taifa, mbona kama wa fisadi.
Niandikie: mwanakijiji@klhnews.com
Ujumbe: 248 686 2010
TAIFA LILIPOTEKWA NYARA, USALAMA WA TAIFA WALIKUWA WAPI?
Na. M. M. MwanakijijiNingependa kuungana na waandishi wengine wengi leo ambao wameandika kuhusu kikao cha NEC Butiama na maana yake kwa Taifa. Nikiwa mmoja wa waliofuatilia kwa karibu naomba nikwepe kufanya hivyo kwa sasa ili nipate muda wa kuchambua hasa kile kilichojiri. Nirudi kidogo kwenye suala la EPA na madai kuwa yawezekana Tanzania iko mikononi mwa maghaidi.