Taxi - (111)
ILIPOISHIA
“Siku nikimjua aliyefanya hivi, nitakachomfanya naomba Mungu anisamehe...” Madame Norah alisema kwa hasira huku akipitisha kidole chake cha shahada shingoni na kukikung’uta hewani, kisha akamtazama Dk. Mshana. “Dokta, nakuomba fanya kila uwezalo kuhakikisha anaamka. Kama unadhani anahitaji kupelekwa Muhimbili utaniambia...” mara simu yake ya mkononi ikaanza kuita. Madame Norah aliitazama kwa makini na kushusha pumzi kisha akaipokea na kuiweka kwenye sikio.
“Hello, Mr. Mafuru, nipigie baadaye siko kwenye
mood,” Madame Norah alisema kwa sauti yenye kitetemeshi.
“Madame... lakini tulikubaliana kukutana saa hizi kwa ajili ya kuandaa ile...” Mr. Mafuru alianza kujieleza lakini Madame Norah akamkatisha.
“Nisikilize, siwezi kufanya lolote kwa sasa wakati mwanangu yupo kitandani anapigania uhai wake. Sijui umenielewa?” Madame Norah aliongea kwa sauti kali iliyoonesha kukerwa.
“Oh samahani, sikujua. Kwani nani anaumwa maana sina taarifa?” Mr. Mafuru aliuliza kwa sauti iliyoonesha mshangao.
“Binti’angu, anaitwa Joyce. Walivamia nyumbani usiku na watu waliokuwa wanamtaka mumewe kisha wakampiga risasi. Hali yake siyo nzuri hivyo siwezi kufanya lolote kwa sasa...”
“
Oh my God!” Mr. Mafuru alisema na kuongeza, “Dah, ngoja nimweleze Mr. Oduya. Umesema yupo hospitali gani?”
“Amana.”
“
Okay, nashukuru kwa taarifa.
See you later,” Mr. Mafuru alisema na kukata simu.
SASA ENDELEA...
* * * * *
Tunu akiwa katika mwendo wa kasi alijikuta akikanyaga breki ya ghafla na kupunguza mwendo baada ya kuliona daladala linalofanya safari zake kati ya Mnazi Mmoja na Viwandani likiingia katika mtaa wa Lindi pasipo kusubiri magari mengine yaliyokuwa yanapita katika mtaa huo. Gari hilo lilikuwa linatokea eneo la Ilala Boma likiwa katika mtaa wa Tabora.
Tunu alisonya na kulisubiri lipite kisha akakanyaga pedeli ya mafuta kwa nguvu na kulifanya gari lake liserereke na kuongeza mwendo, akalipita gari moja aina ya
Nissan Caravan la rangi nyeupe lililokuwa mbele yake na hivyo kufanya uwepo wa magari mawili katikati yake na gari aina ya
Toyota Alphard jeusi lililokuwa kiasi cha umbali wa mita sabini.
Muda huohuo simu yake ya mkononi iliyokuwa imewekwa kwenye dashbodi ikaanza kuita, Tunu aliitupia jicho na kuliona jina la Victor, rafiki yake na shushushu mwenzake, Victor alikuwa anafanya kazi katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Tunu akaachia tabasamu na kushusha pumzi, alikuwa amepata wazo la kumtumia Victor kufanikisha misheni yake.
“Hallo, Victor, uko wapi!” Tunu aliuliza mara baada ya kuiweka simu sikioni, muda huo alikuwa ameifikia barabara ya Kawawa iliyokuwa inakatisha mbele yao ikitokea eneo la Chang’ombe kuelekea Kinondoni.
“Unanitenga, Tunu, unanitenga...” Victor alianza kulalamika.
“Uko wapi, Victor,
I want to see you right now,” Tunu aliuliza tena kwa sauti iliyoonesha kuwa na haraka, muda huo alikuwa anavuka barabara ya Kawawa na kuufuata mtaa ule wa Lindi. Alikuwa usawa wa
Machinga Complex.
“Nipo hapa
MAK Books and Brains katika jengo la
Mkuki ila nataka kuelekea bandarini mara moja...” Victor alisema.
“Usiondoke, nisubiri hapo nje ya jengo, natokea huku Shaurimoyo,” Tunu alisema kwa sauti iliyomfanya Victor kushikwa na mshangao.
Tunu akapunguza mwendo na kumkwepa mtu mmoja aliyevuka barabara pasipo kuangalia, alikuwa akitokea katika duka moja la vipuri vya magari eneo lile na kuelekea lilipo jengo la Machinga. Lile gari aina ya
Toyota Alphard jeusi nalo lilikuwa linavuka barabara ya Kawawa na kuufuata mtaa ule ule wa Lindi, japokuwa lilikawia kidogo kuvuka.
Hadi hapo Tunu alikwishapata uhakika kuwa walikuwa wakimfuata yeye, hata hivyo kwa namna nyingine ile ilikuwa ni ishara mojawapo ya kumtahadharisha kuwa hakupaswa kujiamini sana bali alitakuwa kuwa makini zaidi.
Aliongeza mwendo hadi alipofika kwenye makutano ya mtaa ule wa Lindi na Shaurimoyo, akaiacha barabara ya Lindi na kungia upande wa kulia kuufuata mtaa wa Shaurimoyo na hapo mwendo wake ukaongezeka tena huku akiyapita magari mawili yaliyokuwa mbele yake. Alikuwa mjanja sana na anayeijua vizuri kazi yake.
Aliivuka reli na alipowa mbioni kufika mwisho wa mtaa ule akageuza shingo yake kutazama nyuma na kuliona lile gari aina
Toyota Alphard jeusi likiwa limeingia katika barabara ile ya Shaurimoyo. Muda huo huo akaliona treni la abiria lifanyalo safari zake ndani ya jiji la Dar es Salaam maarufu kama “
Treni la Mwakyembe” likiwa linapita na kuyafanya magari yote kusimama, hiyo ikawa nafuu kwa Tunu.
Tunu aliingia katika barabara ya Nyerere na kupitiliza moja kwa moja hadi lilipo jengo la Mkuki, akamkuta Victor akiwa amesimama amejiegemeza katika gari lake aina ya
Toyota Prado la rangi nyeupe.
“Nina haraka kidogo, niazime gari lako halafu tumia hili langu, kuna sehemu naenda nikimaliza nitakutafuta tuongee vizuri,” Tunu alisema mara baada ya kushuka toka kwenye gari lake ambalo lilikuwa bado linanguruma taratibu. Victor akaonesha mshangao.
“Unanitenga, Tunu. Umekuja jana tu leo naona una ndinga mpya, tupeane michongo basi, mshikaji wangu,” Victor alisema kwa utani huku akimpa Tunu ufunguo wa gari lake.
“Tutaongea bwana, ngoja niwahi sehemu,” Tunu alisema na kuingia ndani ya lile gari la Victor, akaliwasha na kuliondoa kwa mwendo wa kasi akiifuata barabara ya Nyerere kuelekea eneo la Chang’ombe, alimwacha Victor anashangaa.
Kama kawaida yake, Victor alikuwa amevaa shati zuri la kitenge la mikono mirefu, kofia ya pama, suruali ya dengrizi na miguuni alikuwa amevaa buti ngumu za ngozi. Alishusha pumzi na kuingia ndani ya lile gari aina ya
BMW X6 xDrive 50i jeusi aliloachiwa na Tunu kisha akaliondoa toka katika lile jengo la Mkuki na kuingia katika barabara ya Nyerere, akaelekea uelekeo wa eneo la Kamata. Hakuwa na wasiwasi wowote.
Wakati akiwa analikaribia jengo ambalo awali lilikuwa likitumika kama
Shoprite Supermarket gari aina ya
Toyota Alphard jeusi lililokuwa likiendeshwa na Job ndiyo lilikuwa linaingia katika barabara ya Nyerere.
Victor alipofika katika taa za kuongoza magari barabarani eneo la Kamata akaiacha barabara ya Nyerere na kuingia kulia akiifuata barabara ya Gerezani, kisha akanyoosha moja kwa moja hadi katika mzunguko unaozikutanisha barabara za Gerezani na ile Bandari iliyokuwa inaelekea bandarini.
Wakati huo lile gari aina ya
Toyota Alphard jeusi nalo lilikuwa limezivuka taa za kuongoza magari barabarani za Kamata na sasa lilikuwa katika mwendo wa kasi zaidi kuelekea kule liliko gari aina ya
BMW X6 xDrive 50i. Victor aliuzunguka mzunguko wa barabara na kuelekea kulia kuifuata barabara iliyokuwa inaelekea bandarini kisha akaanza kulivuka daraja ambalo chini yake kulikuwa na reli.
Inaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper MR KUO dan oseko