Taxi - (91)
ILIPOISHIA
Winifrida akashikwa na kitete na kushindwa kuongea, hofu ilikuwa imemtawala na donge la fadhaa kumkaba kooni. Alimeza funda kubwa la mate kwa nguvu mithili ya mtu anayejaribu kukisukuma kipande cha mfupa kilichokwama kooni. Alitamani sana kupiga yowe lakini sauti yake ikamsaliti. Akajiuliza kwa nini apige yowe? Akili ilimhoji na kumtia ganzi.
Akajikuta akishindwa kabisa kuongea japo alimsikia Sammy akiendelea kuita upande wa pili wa simu. Alishindwa, si kwa sababu ya hofu ya kusikiwa, bali alijiuliza kuwa endapo Sammy angemuuliza simu ile aliitoa wapi angemjibu nini kwani hakuna yeyote aliyejua kama anamiliki simu. Akaikata.
Alianza kujilaumu kwa kutokuzungumza na Sammy, kwani ni hatari zaidi kumwacha Sammy arejee nyumbani na kukutana na wale watu hatari kuliko yeye kutafuta majibu ya wapi ameitoa ile simu. Majuto yalipita haraka kichwani mwake, yalipita kwa kasi mno kiasi cha kumwita Mungu na asimweleze alilotaka amfanyie.
Mara akapata wazo la kupiga tena simu. Lakini kwa wahaka aliokuwa nao, asingeweza kuzungumza na Sammy kwa kuchelea kusikiwa na wale watu. Alishusha pumzi huku akijaribu kusikiliza kwa makini akihofia kuingia kwenye mtego kwa kudhani mmoja wa watu wale, ambao hakujua idadi yao, angeweza kuwa amejificha mle chumbani kumsubiri. Alijitahidi kuangaza macho yake sehemu alizoweza kuzifikia lakini hakuona kitu cha kutilia shaka.
ENDELEA...
Kisha akapata wazo jingine. Sasa alikata shauri, liwalo na lilwe lakini asingeweza kuendelea kujikunyata pale juu ilhali alikuwa na uwezo wa kunusuru ile hali. Aliazimia kupiga simu, kuwapigia polisi kwa kutumia ile namba yao ya dharura na kuwaleleza kilichokuwa kinaendelea kwenye nyumba yao.
* * * * *
Sammy aliendelea kuendesha gari lake katika barabara ya Uhuru kwa mwendo wa kasi akiyapita magari mengine. Sasa alikuwa anazivuka taa za kuongozea magari barabarani za Buguruni Shell na kuingia barabara ya Mnyamani, mara akaonekana kugutuka na kuwauliza wale watu aliokuwa amewapa msaada wa usafiri bila kugeuka wala kuwatazama. “Kwani mnashukia wapi? Mimi napitia barabara ya Mnayamani.”
Kimya!
Sammy akashangaa na kugeuza shingo yake kuwatazama. Akapigwa na butwaa na kushtuka sana. Akanywea. Yule mwanamume mrefu aliyepanda hewani kisawasawa na mwenye mwili ulioshiba alikuwa amemnyooshea bastola huku akiwa makini sana.
Uso wa Bob Chopa, yule mwanamume mfupi kiumbo lakini mkakamavu na mwenye sura ya unyenyekevu ulikuwa umepambwa na tabasamu la kifedhuli.
“Sasa sikiliza, utafuata maelekezo yangu,” yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba alisema kwa ukali.
Sammy alionekana kubabaika sana. Alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kubana midomo yake, hakujua afanye nini.
“Ni nini mnakitaka toka kwangu?” Sammy aliuliza kwa sauti tulivu huku akipunguza mwendo wa gari kuwakwepa wapiti njia.
“Hatuna shida ya kukudhuru wala kuchukua gari lako ila kuna kitu tunakihitaji ndani ya hili gari, tukikipata tutakuacha uende zako,” yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba alimwambia Sammy.
“Na msipokipata?” Sammy aliuliza huku akipata shaka, hakuiamini ile kauli ya yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba.
“Tutajua cha kufanya…”
“Kwani kitu gani mnachokihitaji kwangu?” Sammy aliuliza huku akimtupia jicho la wizi yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba.
“Utajua baadaye, kwa sasa endesha gari hadi nitakapokwambia usimame,” yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba alimwambia na Sammy pasipo kubisha aliendesha gari lake pasipo kuhoji. Muda huo akili yake ilikuwa inafanya kazi haraka ili kujinusuru toka katika mikono ile ya watekaji.
Yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba aliikoki bastola yake na kuisogeza katika kichwa cha Sammy. Sammy alibana pumzi baada ya kuuhisi ubaridi wa bomba la bastola. Aliuma meno yake akionekana kuzuia donge la hasira lililoanza kumchonyota kooni. Waliivuka reli ya kuelekea Ubungo na hapo Sammy akataka kugeuza shingo yake kuwatazama.
“Endesha na usigeuze shingo yako kutazama nyuma,” yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba alimwambia Sammy kwa ukali.
Muda wote Bob Chopa alikuwa ameketi katika siti yake akiwa mtulivu mno, alikuwa anatabasamu kama ambaye hakuhusika na lile tukio. Alikuwa anashuhudia kila hatua, jinsi ambavyo yule mwenzake mrefu mwenye mwili ulioshiba alivyokuwa makini kuhakikisha Sammy hafanyi jambo lolote ambalo lingeweza kuwagharimu.
Maara simu yake ikaanza kuita, Bob Chopa aliitazama kwa makini na kupokea mara moja baada ya kuliona jina la mpigaji. “Hallo, boss,” alisema mara baada ya kuiweka sikioni.
“Vipi, Bob, mmefikia wapi?” sauti upande wa pili wa simu ilisikika ikiongea kwa wasiwasi.
“Bado, hatujafika eneo sahihi,” Bob Chopa alijibu na kushusha pumzi.
“Kuweni makini, nadhani kuna mtu anawafuatilia, pia hakikisheni huyo bwana haumii nitamhitaji baadaye kwa matumizi ya nyumbani, tumeelewana?”
“Sawa, boss,” Bob Chopa alisema huku akiachia kicheko hafifu, alikwisha fahamu nini maana yake. Akakata simu huku akimwangalia Sammy kwa makini na kusema. “Kazi kwelikweli!”
“Vipi, kamanda?” yule mwenzake mrefu mwenye mwili ulioshiba alimuuliza Bob Chopa kwa shauku.
“Disko limeingiliwa na Mmasai,” Bob Chopa alijibu huku akiendelea kutabasamu. “Ila usijali, nitacheza naye muziki wowote anaoutaka,” akaongeza huku akiendelea kutabasamu.
“Ongeza mwendo!” yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba alimwambia Sammy baada ya kuona mwendo wa gari umepungua, wakati huo walikuwa wanavuka eneo la Kidarajani.
Simu ya Sammy ikaanza kuita. Sammy akashtuka na kuitupia jicho katika hali ya kukata tamaa kwa kuwa alijua asingeweza kuipokea bila kuruhusiwa na wale watu. Simu yake ilikuwa imewekwa kwenye
dashboard. Ilikuwa ni simu kutoka kwa Joyce aliyetaka kujua alikuwa amefika wapi.
Yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba aliitupia jicho la haraka ile simu kisha akayarudisha macho yake kumtazama Sammy kwa makini. Aliamua kuihamisha bastola yake toka kwenye kichwa cha Sammy na kuigandamiza kwenye mbavu zake. Hofu ilizidi kumsonga Sammy. Akaitupia tena jicho simu yake iliyoendelea kuita. Akaanza kuomba Mungu utokee muujiza.
Mara wakaliona gari moja likija kasi nyuma yao, lilikuwa ni gari aina ya Nissan Patrol la rangi nyeusi.Sammy akashusha pumzi za ahueni huku akiendelea kuomba Mungu. Bob Chopa alitoa bastola yake kutoka mafichoni na kujiweka tayari kwa lolote, macho yake aliyakaza kuliangalia kwa makini lile gari lililokuwa linawasogelea.
Wakati huo walikuwa wanalivuka soko la Vingunguti Kwa Simba. Lile gari aina ya Nissan Patrol jeusi likawafikia na kuanza kuwapita huku dereva wake akipiga honi kuonesha kuwa alikuwa na haraka. Wote walilitupia macho na kuyaona maandishi makubwa ya ‘POLISI’ ubavuni. Moyo wa Sammy ukapiga kite. Pah!
Bob Chopa akawa makini kuangalia ndani ya lile gari. Kulikuwa na maofisa wawili wa polisi. Sammy akataka kujaribu bahati yake, akaongeza mwendo ili kwenda sambasamba na lile gari la Polisi huku akigeuza shingo yake kuwatazama wale maofisa wa polisi kwa jicho la kuomba msaada.
Inaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple