Taxi - (96)
ILIPOISHIA
Tunu akamtaka dereva wake azime injini ya gari, yule dereva alikuwa mwepesi kuelewa, akafanya kama alivyoagizwa. Kisha Tunu akamuuliza kuhusu kiasi cha fedha alichokuwa anadai kama malipo ya umbali wa kutoka Ilala alikokodiwa hadi pale.
Yule dereva akamwambia kiasi cha fedha na bila kupoteza muda Tunu alimlipa na kumzidishia ili kujenga uaminifu kwa yule dereva. Yule dereva alizipokea zile fedha huku akishukuru sana. Tunu alitulia mle garini kwa muda akijaribu kulichunguza eneo lile kwa makini na mara akamwona yule mrembo akifungua mlango na kushuka toka kwenye lile gari
Toyota Verossa, akaliendea geti la mbele la ile nyumba na kutoa ufungo, akafungua na kuzama ndani ya ile nyumba huku geti likifungwa haraka.
Muda huo huo lile gari
Toyota Verossa likaonekana kugeuza na kuondoka likirudi lilikotoka na kuwapita kwa kasi, kisha likatokomea kizani. Tunu aliiangalia ile nyumba kwa shauku, akageuza shingo yake kumwangalia yule dereva wa taxi na kumwahidi kuwa angerudi baada ya dakika therathini ila endapo asingetokea katika muda huo basi angekuwa huru kuondoka zake.
Akiwa katikati ya udadisi na shauku alishuka toka ndani ya ile taxi, na kuanza kupiga hatua taratibu na kwa tahadhari kuelekea kwenye ile nyumba huku moyo wake ukienda mbio sana, hakuweza kuhisi nini ambacho kingemtokea mbele yake, hata hivyo, hilo halikumzuia kuendelea na harakati zake.
“Liwalo na liwe,” Tunu aliwaza huku akizidi kujongea kwenye ile nyumba.
SASA ENDELEA...
Kabla hajafika mbali akasikia sauti fulani ya tahadhari ikimwita nyuma yake, “Sister!” Alipogeuka akamwona yule dereva wa taxi iliyomleta akimjia haraka. Tunu alisimama akamtazama kwa mshangao. Yule dereva alikuwa akimjia haraka.
“Kuwa makini sana, Sister,” yule dereva alimwambia Tunu sentensi fupi yenye uzito kisha akaanza kurudi haraka kwenye gari lake. Tunu alibaini kuwa alikuwa anamaanisha anachokisema kwa namna alivyomtazama. Naye kwa kumwonesha kuwa wapo pamoja, alibetua kichwa chake kukubali kisha akaanza kuondoka.
Wakati akitembea, aligeuka tena kutazama nyuma, akamwona yule dereva akiwa ametulia kwenye gari lake lakini akiwa makini kufuatilia kule alikokuwa Tunu.
Tunu aligeuka kutazama pembeni yake, hakuweza kumwona mtu yeyote aliyemtilia shaka. Akashusha pumzi na kuendelea na safari yake bila kuonesha wasiwasi wowote akiwa kama mtu aliyekuwa anapita zake. Aliitupia jicho la wizi nyumba ile kuutathmini usalama wa eneo lile. Mwanga wa taa kubwa juu ya ukuta wa ile nyumba ulimwezesha kwa kiasi fulani kuyasoma mazingira ya eneo lile.
Aliziona kamera mbili zilizokuwa juu ya geti zenye uwezo wa kunasa picha ya kitu chochote mbele ya nyumba. Alipofika mwisho wa ule ukuta, akachepuka na kuzunguka upande wa nyuma ambako nyumba ile ilikuwa imezungukwa na miti mirefu na mikubwa ya kivuli ambayo matawi yake yalikuwa makubwa yaliyokuwa yametengeneza vichaka vilivyosababisha kiza fulani.
Alisimama kwenye kiza kwa tahadhari akaendelea kuitazama ile miti mikubwa kwa utulivu huku hisia zake zikimweleza kuwa mtu yeyote mwenye hila angeweza kujibanza nyuma ya miti ile na kuitimiza adhma yake mbaya.
Alipojiridhisha kuwa hali ilikuwa salama, akaukwea kwa tahadhari mti mmoja mkubwa na kufanikiwa kufika juu, akachungulia ndani. Akayaona mazingira mazuri ya nyumba ile. Ilikuwa nyumba ya kisasa iliyozungukwa kwa bustani nzuri ya maua na nyasi zilizokatwa vizuri. Kulikuwa na magari mawili yaliyokuwa ndani ya banda la wazi la kuegeshea magari.
Gari moja ni aina ya
Mercedes Benz E-class limousine jeusi lililokuwa na milango sita na gari jingine ni Nissan Patrol jeupe. Akiwa pale juu alichagua tawi moja zuri lililokuwa limening’inia ndani ya ukuta wa ile nyumba kule nyuma ya nyumba. Alijilaza juu ya tawi lile na kuanza kusota kwa tumbo taratibu akishuka kuelekea mle ndani ya ule ukuta.
Kiza kilichosababishwa na matawi makubwa ya miti ya vivuli iliyoizunguka nyumba ile kilimpa nafasi nzuri ya kufanya mjongeo makini na wa utulivu akionekana kama kivuli kwani alitembea kwa tahadhari kubwa, akiwa na uhakika kuwa ingehitaji mtu makini sana kugundua uwepo wake.
Alifika kwenye varanda ndogo katika sehemu ya nyuma ya ile nyumba na kusimama huku macho yake yakiwa makini kuangaza huku na huko, varanda ile ilikuwa na mlango wa nyuma wa kuingilia jikoni. Aliusogelea mlango na kusimama kwa utulivu akitazama huku na kule katika namna ya kusikiliza kama angeweza kusikia kitu lakini hali bado ilikuwa ya ukimya mno.
Pembeni ya ule mlango kulikuwa na dirisha moja la sehemu ya jiko la ile nyumba upande wa kushoto. Tunu alilisogelea lile dirisha na kuchungulia ndani, japo dirisha lilikuwa limefunikwa na pazia kwa ndani lakini kupitia uwazi mdogo pembeni ya dirisha lile aliweza kuona mle ndani. Hakuona dalili ya kuwepo mtu yeyote.
Alijaribu kulifungua lile dirisha lakini hakufanikiwa kwani lile dirisha lilikuwa limefungwa ndani kwa komeo. Hakuona kama kulikuwa na namna nyingine yoyote ya kuweza kuingia mle ndani isipokuwa kuvunja sehemu ndogo ya kile kioo cha lile dirisha.
Mara akahisi uwepo wa kiumbe kingine eneo lile, akashtuka na kugeuka kutazama nyuma yake na macho yake yakakutana na macho ya yule mrembo akiwa ameshika bastola mkononi akimwelekezea. Tunu alishikwa na taharuki ambayo hakuitarajia kabisa.
Yule mrembo alikuwa bado amevaa nguo zilezile alizotoka nazo kule ELLI’S, sketi fupi nyeusi yenye miraba myeupe, blauzi nyeupe ya mikono mirefu na viatu vya flati, na alikuwa amekunja sura yake huku akimtazama Tunu kwa macho makali.
Tunu alimtazama kwa makini, sura yake ikajaa usoni kwake, ghafla akaonekana kumkumbuka.
“Lisa!” Tunu aliita kwa mshangao mkubwa.
Yule mrembo kwanza hakumjibu, aliendelea kumnyooshea bastola huku akiwa amekunja sura yake. Akili ya Tunu ikaanza kufanya kazi haraka akitafuta namna ya kujinasua toka katika mikono ya Lisa. Alitazama kando yake na kuliona kopo dogo lililopandwa maua.
“Niambie, Tunu, nini kilichokuleta hapa?” Lisa aliuliza kwa ukali.
“
We need to talk, Lisa, nilikuja hapa kuongea na wewe na tumalize tofauti zetu...”
“Usinifanye mimi ni mjinga, Tunu! Natambua kinachoendelea,” Lisa alisema na kuendelea, “Nilifahamu tu kuwa ungenifuata hapa na ulivyo na kichwa cha panzi umeshindwa hata kuushtukia mtego hafifu kama huu. Dereva wako uliyemkodi kakuchuuza. Yule ni mwenzetu.”
“Umekosea sana, Lisa, kwa hiki unachotaka kukifanya,
we are friends...” Tunu alisema huku akimwangalia Lisa kwa uchungu, moyoni alijua kuwa amenasa kwenye mtego kwa kumwamini yule dereva kirahisi. Lisa aliangua kicheko cha dharau.
“Tunu, Nafahamu vyema wewe ni nani, unamfanyia nani kazi na upo hapa Dar es Salaam kwa kazi gani! Sishangazwi na hilo kwani hata mimi nipo hapa kwa maslahi ya ninayemfanyia kazi kama ilivyo kwako,” Lisa alisema kwa kujiamini.
“Kwa hiyo bado unamfanyia kazi Mr. Oduya? Hivi unaamini kabisa atakuwa rais wa nchi hii?” Tunu aliuliza huku akimkazia macho Lisa.
“Mimi huwa sina kawaida ya kujibu maswali ya kipumbavu toka kwa watu wa sampuli yako,” Lisa alisema kwa dharau. Kisha kikatokea kitambo kifupi cha ukimya.
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf red apple the-sniper