Stori ya kusisimua - Taxi

Stori ya kusisimua - Taxi

Taxi - (88)

ILIPOISHIA

Sammy alimchukua Tunu hadi kwenye nyumba aliyokuwa amepanga eneo la Makumbusho, Kijitonyama. Siku hiyo Tunu alikuwa amevaa blauzi na kaptula ya kitenge. Kaptula ile iliishia juu ya magoti yake na kuifichua minofu ya miguu na mapaja yake yaliyonona.

“Nimekuja mara moja tu kukusalimia, sitakaa muda mrefu,” Tunu alisema huku akiitazama saa yake ya mkononi mara tu walipoingia ndani. Hata hivyo, Tunu alikuwa akimtazama Sammy kwa macho ya wizi, macho yake yalikuwa yamelegea kama aliyekuwa amekula kungu, sura yake ilionekana wazi kumsubiri Sammy afanye kitu.

Sammy aligundua kuwa Tunu alikuwa amekolea ingawa haikuwa rahisi kwake kukubali moja kwa moja, akamshika mkono. Hakuleta pingamizi lolote, kwani alionekana kutojiweza na uso wake aliuinamisha chini kwa aibu. Alimvutia kifuani kwake akamkumbatia. Tunu alijigandamiza kwenye mwili wa Sammy na kutulia huku akihema kwa nguvu.

Sammy hakuendelea kusubiri, alimbeba hadi kitandani, akamwangusha kama mzigo. Tunu pumzi zilimpaa! Kilichofuata baada ya hapo kilimfanya ahisi kuchanganyikiwa. Alijikuta akiwa taabani huku akiyashuhudia maumivu ya kupendeza yaliyokuwa yakimuua taratibu kama mgonjwa taabani. Yote yaliyotendeka kwenye mwili wake hakuwahi kuyaona ndotoni au hata kuyafikiria.

ENDELEA...

Hakujimudu na wala hakuweza kuvumilia, alitapatapa kama samaki anayekaangwa hai, akaanza kulia. Kilikuwa kilio cha faraja kilichotokana na adhabu aliyojitakia mwenyewe ambayo wala hakuijutia. Alilia na machozi yakamtoka, sauti ikamkauka. Ilikuwa ni siku ya aina yake kwake, siku ambayo kamwe isingepotea katika fikra zake.

Mechi ilipoisha Tunu hakuweza hata kumtazama Sammy machoni, alikuwa anatweta kama aliyemaliza mbio ndefu za kilomita arobaini na mbili baada ya kuvunja rekodi ya dunia. Aliyafuta machozi yake kwa kiganja cha mkono na kushusha pumzi ndefu.

“Pole mpenzi, pole sana…” Sammy alimpa pole Tunu huku akicheka kimoyomoyo, kilikuwa kicheko cha ushindi.

“Mmh, hakyamungu ungeniua,” Tunu alisema kwa sauti legevu ya chini huku akipiga miayo.

“Usijali, mpenzi wangu, utazoea tu. Hata hivyo, umenifurahisha sana, you’re a real gift to me. Kuanzia leo sitakuita Tunu bali wewe ni Gift…”

Tunu aliitazama saa yake na kushtuka, ilikuwa imeshatimu saa mbili na nusu usiku, akaamua kuaga na kuondoka, alikuwa hoi. Sammy alimsindikiza hadi kituo cha daladala, wakapeana mabusu motomoto ya kuagana kisha akampandisha daladala la kuelekea Sinza huku wakiahidiana kukutana baada ya siku tatu, lakini tangu siku hiyo Sammy hakuweza kumtia tena machoni Tunu! Bahati mbaya hakuwa akijua Tunu aliishi Sinza ipi, maana Sinza ni kubwa ati!

Sammy alikuwa kama mwehu, alizunguka mji mzima kumtafuta Tunu, alifika kila pembe ya Sinza na viunga vyake, aliuliza watu aliodhani wangeweza kuwa na taarifa za Tunu, lakini hakuna alichoambulia ambacho kingeweza kumsaidia kujua alipo. Alimfuata Grace, dada wa Elli ambaye alisoma darasa moja Tunu, lakini pia hakupata habari zake.

Kutokuonekana kwa Tunu katika maisha ya Sammy kulimwathiri sana kisaikolojia na hata kuathiri utendaji wake wa kazi za kila siku. Alijikuta akiwa na mwili wa mgonjwa akisubiri kifo ili arudi mavumbini, ubongo upo hospitali na nafsi kwa Mungu. Tabibu pekee wa kuutibu ugonjwa wake alikuwa mmoja tu, Gift!

Alimuwaza yeye tu muda wote. Mbele ya uzuri wa kiumbe aliyemwita Gift, Sammy alijiona kama limbukeni wa mapenzi. Gift alikuwa amemwachia shimo kubwa sana moyoni liitwalo mapenzi. Shimo ambalo hakukuwa na mtu mwingine wa kuliziba isipokuwa yeye tu. Kwa miaka miwili Sammy hakujiweza, kutwa kucha alimwaza Gift tu! Alishangaa, iweje mrembo yule apotee ghafla katika kipindi ambacho alimhitaji mno?

Katika kipindi cha miaka miwili tangu kutoweka kwa Tunu, Sammy alishindwa kabisa kumwondoa moyoni mwake, mawazo kuhusu Gift yalimpitia kila siku na kila alipolikumbuka jina lake moyo wake ulimwenda mbio kama mtu aliyekuwa na ugonjwa wa wasiwasi. Alijiuliza iwapo hali ile ilikuwa ni matokeo ya kumpenda sana Gift, ingekuwaje pindi angesikia kuwa ameolewa na mwanamume mwingine?

Yako wapi yale macho yake mazuri yenye mvuto wa ajabu yaliyomtia utumwani? Hivi iliwezekanaje kwa msichana kama Gift, aliyeamini ni zawadi yake kutoka kwa Mungu, kutoweka ghafla na kumwacha yeye katika kipindi kama kile? Kuachwa si kioja, laiti angelipewa nafasi ya miaka kadhaa kusema na roho yake pengine angeweza kuwa na uamuzi mzuri zaidi, ingawa ni ajabu sana kwa donda ndugu kupona!

Baada ya miaka miwili ya maisha ya mateso, Sammy alijiambia kuwa ilikuwa imetosha, huo sasa ulikuwa ni wakati mwafaka wa yeye kuanza maisha mapya kwani hakuweza kuendelea kumsubiri mtu ambaye hakujua yupo wapi, kama ni mzima au amekufa. Ni katika kipindi hicho ambacho Sammy alikutana na Joyce wakati akitoka Tanga kutembelea mapango ya Amboni. Kipindi ambacho Joyce alikuja kwenye maisha yake kama malaika mwokozi aliyeshushwa kumwondolea machungu ya kukimbiwa na Gift. Yote yaliyokuja kutokea baadaye yamebaki kuwa historia…

“Sammy!” sauti nyororo ya Tunu ilimzindua Sammy kutoka kwenye lindi la mawazo. Sammy alimtazama Tunu akamwona akiwa anamtazama kwa utulivu huku akitabasamu.

“Gift!” Sammy alimudu kusema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani. “Ninahitaji kujua ukweli na tafadhali naomba usiniongopee. Niambie ukweli hata kama ukweli huo utaniumiza sana,” Sammy alimwambia Tunu huku akimtazama usoni kwa makini.

“Unataka kujua nini, Sammy?” Tunu aliuliza huku akiwa makini kusikiliza alichotaka kuambiwa.

“Kwa nini ulinikimbia? How could you do this to me? ” Sammy aliuliza huku akimtazama Tunu kwa uchungu mkubwa. “Maybe I was not important to you at all,” aliongeza kabla Tunu hajasema neno.

Kwa sekunde chache Tunu alibaki kimya akimtumbulia macho Sammy akiwa hajui niseme nini, hakuweza kabisa kumjibu bali alibaki kimya huku akimtazama kwa makini. Kila alipotaka kujieleza alihisi kukosa ujasiri.

“Kwa nini ukaamua kutupa jongoo na mti wake! Tunu I need to know the truth,” Sammy alisema huku akiwa ameyatuliza macho yake kwenye uso wa Tunu.

I’m so sorry…” Tunu alisema kwa sauti ya chini.

Sorry? Baada ya miaka yote hii ya kunipa mateso leo unaniambia kirahisi rahisi tu, eti I’m so Sorry! Sorry for what? I’m disappointed, very disappointed,” Sammy alishindwa kuvumilia akaanza kuzungumza kwa sauti kubwa na kuwafanya watu wengine wageuze shingo zao kuwatazama kwa mshangao.

Enough! Can you please stop blaming me?” Tunu naye alikuja juu na kusema kwa sauti ya ukali huku akikunja sura yake.

Kwa kitambo fulani hali ya mahali pale ilikuwa tete, walibaki kimya wakiwa wanaangaliana kama majogoo yaliyotaka kupigana. Tunu alishusha pumzi za ndani kwa ndani.

Inaendelea...
 
Taxi - (89)

I’m sorry for everything, I’m real very sorry,” Tunu alimwambia Sammy huku akijitahidi kutengeneza tabasamu la kumlainisha Sammy.

Sammy alitaka kusema lakini akatishwa na simu yake iliyoanza kuita kwa fujo. Aliitazama kwa makini kisha akaitupia jicho saa yake na kushtuka. Akashusha pumzi.

“Mke wangu anapiga simu,” Sammy alisema huku akionekana kama aliyekuwa akijishauri iwapo aipokee au aipotezee.

Nyumbani kwa Sammy, Joyce alikuwa anapiga simu huku amewekewa kisu shingoni na Spoiler akimtishia kumchinja endapo angeshindwa kumshawishi Sammy arudi nyumbani. Spoiler alikuwa ameghadhabika kwelikweli.

“Na usijaribu kufanya jambo lolote la kipumbavu kumshtua, vinginevyo nitawaua wewe na mwanao…” Spoiler alisema kwa ghadhabu.

“Tafadhali naomba msimdhuru mwanangu…” Joyce alisema kwa woga huku akilia, alimkodolea macho Dulla aliyekuwa kamwelekezea Pendo bastola kichwani. Wakati huo Pendo alikuwa amebandikwa gundi maalumu ya karatasi mdomoni ili asiweze kupiga kelele.

Kwenye mgahawa wa ELLI’S, Sammy aliendelea kuiangalia ile simu huku akijiuliza angemjibu nini mkewe baada ya kupokea, simu iliita hadi ikakatika akiwa bado anaikodolea macho. Akashusha pumzi. Mara ikaanza kuita tena, hakusubiri akaipokea huku akimtupia jicho Tunu na kuipeleka moja kwa moja kwenye sikio lake. “Hallo!

“Baba Pendo, njoo nyumbani haraka, hali ya Pendo ni mbaya sana,” Joyce alisema huku analia, sauti yake ilipenya kwenye ngoma ya sikio la Sammy na kumfanya ashtuke sana.

Sammy alisimama bila kujijua. Alibana pumzi huku akionekana kunyong’onyea sana kisha akashusha pumzi taratibu. Tatizo la Pendo lilionekana kumnyima raha.

“Baba Pendo! Mbona huongei, kwani uko wapi?” sauti ya Joyce ilimzindua tena kutoka kwenye mawazo.

“Fanya hivi, naomba chukua teksi tukutane hapo hospitali ya…”

“Siwezi, njoo nyumbani,” Joyce alimkatisha Sammy, alikuwa analia kilio cha kwikwi.

Sammy alitaka kusema neno lakini akagundua kuwa simu ilishakatwa. Aliogopa sana, alihisi mwili wake ukiishiwa nguvu na hakujua afanye nini. Tunu alionekana kuguswa sana na mabadiliko ya Sammy, alimtazama kwa makini akitaka kujua alichoambiwa na mkewe. Sammy alianza kukusanya vitu vyake, simu na funguo iliyokuwa juu ya meza huku akimtazama Tunu kwa huzuni kidogo.

“Samahani, Gift, nalazimika kuondoka, hali ya mwanangu nyumbani si nzuri kabisa,” Sammy alisema kwa huzuni na kuanza kuondoka lakini akakumbuka na kutoa kadi yake ya kibiashara, akampa Tunu, “Naomba tuwasiliane.”

Tunu aliitazama ile kadi kwa makini na alipoinua uso wake Sammy hakuwepo, akaduwaa asijue la kufanya. Muda huo huo aliwaona wale wanaume waliokuwa wameketi meza ya tatu kutoka meza yake, Bob Chopa na mwenzake wakiondoka haraka haraka kuelekea nje.

Huko nje, Sammy alilifikia gari lake na kufungua mlango, akaingia ndani ya gari na kuwasha injini ya gari, akasubiri kwa sekunde chache huku akiliacha gari likiunguruma taratibu. Simu yake ya mkononi ikaanza kuita, aliiangalia kwa makini na kugundua kuwa ilikuwa ni namba ngeni. Aliipokea kwa pupa huku moyo wake ukienda mbio kwa wasiwasi, “Hallo… Hallo!” alisema lakini upande wa pili wa simu ulikuwa kimya. Kimya kabisa! Sammy aliita tena lakini kimya kilitawala upande wa pili wa simu, mara simu ikakatwa.

Sammy alishangaa, akataka kupiga ili kujua ni nani aliyekuwa akimpigia halafu haongei, akaona kuwa ingempotezea muda na hivyo hakuipa umuhimu, akili yake ilikuwa mbali, alidhamiria kuwahi nyumbani kwake kwani hakujua kama Pendo alikuwa bado yu hai au amekufa. Akaachia breki taratibu na gari likaanza kuserereka. Wakati gari likianza kuyaacha maegesho, Sammy aliwaona wanaume wawili wakimsogelea huku wakipunga mikono yao juu kumsimamisha.

Alikanyaga breki na kuwatazama kwa makini, macho yake yakagongana na yao, Sammy akawatambua. Walikuwa ni wale wanaume waliokuwa wameketi meza ya tatu kutoka meza ya Tunu. Yule mwanamume mfupi alionekana kama aliyechoka sana au mgonjwa. Kila dalili ya kuomba msaada ilijionesha kwenye macho yake na alikuwa ameshikiliwa na mwenzake aliyekuwa mrefu mwenye mwili ulioshiba.

Wale wanaume waliangalina katika namna ya ‘nani aseme’ kisha wakamwangalia Sammy kwa unyonge. “Samahani, ndugu, unaweza kutuacha hapo mbele?” yule mwanamume mrefu mwenye mwili ulioshiba alisema.

Sammy aliwatazama kwa makini akionekana kusita sana, akatingisha kichwa chake kukataa. “Samahani sichukui abiria sasa hivi, kuna sehemu natakiwa kuwahi.”

Wale jamaa wakageuka kuangaliana tena kwa namna ambayo Sammy hakuweza kuielewa. Hata hivyo, walionekana kukata tamaa. Bob Chopa, yule mwanamume mfupi akapandisha juu mabega yake na kuyashusha huku akimkabili Sammy. Aliikunjia kifuani mikono yake katika namna ya kuomba msaada.

“Basi unaweza kutuacha hapo mbele tu, halafu uendelee na safari yako, tafadhali sana…” alisema huku akionesha kwa kidole sehemu wanakotaka kuelekea.

Sammy hakuwa na muda wa kupoteza wala kujishauri, alishusha pumzi ndefu na kubetua kichwa chake kukubali huku akiwaashiria waingine. Walionesha furaha na kuingia, wakaketi kwenye siti ya nyuma ya gari.

Cadillac DeVille likaingia barabarani likiwa katika mwendo wa kasi. Sammy alikuwa anaendesha gari kama mtu aliyechanganyikiwa, ingawa alionekana kuwa makini barabarani.

* * * * *

Winifrida alikuwa amejikunyata kwa hofu kwenye eneo finyu lililokuwa juu ya kabati la nguo lililo ukutani. Alikuwa na mashaka makubwa na hakujua aliwezaje kunusurika mbele ya yule mtu aliyekuwa na uchu kama fisi aliyeona mzoga, hata hivyo aliamini kuwa bado hali haikuwa salama kwake, kwani yule mtu angeweza kurudi tena kule chumbani kumtafuta.

Winifrida alikuwa anaweweseka huku akijaribu kusikiliza kwa makini kama angeweza kusikia chochote kilichokuwa kinaendelea kule sebuleni, ambako wifi yake Joyce na Pendo walikuwa chini ya ulinzi wa majahili wasio na huruma.

Inaendelea...
 
Taxi - (90)

Winifrida alikuwa ameponea kwenye tundu la sindano baada ya kupata wazo la kupanda kule juu na kujificha, lilikuwa eneo ambalo ingekuwa vigumu kwa mtu asiye mwenyeji wa chumba kile kufahamu kuwa kulikuwepo eneo finyu ambalo lingeweza hata kumficha mtu, hasa mwenye umbile dogo kama lake. Lile eneo lilikuwa limezibwa na mfuniko wa ubao mteke (plywood) uliopakwa rangi sawa na ile iliyopakwa ukutani na kupafanya paonekane kama sehemu ya ukuta.

Hakuwa na namna nyingine isipokuwa kujificha pale baada ya kuhisi kuwa angeonekana kama angetaka kutoka mle chumbani. Kilichomtisha zaidi ni kauli aliyoisikia baada ya wale watu kuelezana kuchunguza kila chumba ili kuwabaini wote waliokuwemo mle ndani. Bahati nzuri walianzia katika vyumba vingine na kile chumba kikawa cha mwisho. Hiyo ilimpa nafasi nzuri ya kujinusuru.

Alikuwa amefikiria kujificha pamoja na Pendo lakini akachelea kufanya hivyo kwa hofu kuwa eneo lile lisingetosha kuwaweka wote wawili na endapo wale watu wangeingia chumbani na wasikute hata mtu mmoja, wangepata shaka na matokeo yake ingekuwa rahisi kugundulika.

Winifrida alikuwa akiwaza afanye nini kuwanusuru Joyce na Pendo ilhali hofu nayo ilizidi kumtomasa maungoni na kumchachafya. Wakati akiwaza hayo, mwili nao ulikuwa unamuuma kama kidonda. Alishajikunyata pale juu kwa muda wa kutosha na sasa mwili wote ulikuwa umekufa ganzi. Pamoja na hayo bado hakuacha kuwaza. Alijiuliza wale watu ni akina nani na kwa nini walikuwa wanamtaka Sammy?

Pamoja na hofu aliyokuwa nayo lakini alikumbuka kumwona yule mtu aliyeingia mle chumbani, japo kwa taabu, kupitia upenyo mdogo. Aliweza hata kuiona sura yake wakati yule mtu alipogeuka na kuelekea upande ule wa kabati alikokuwa amejificha. Mavazi na umbile lake vilimjulisha Winifrida kuwa alikuwa kipande cha mtu. Winifrida alihisi kuwa aliwahi kumwona yule mtu sehemu fulani. Alimwona wapi?

Vinyweleo vya mwili vikamsimama baada ya kuikumbuka ile sura. Ilikuwa ni sura ile ile aliyoiona kwenye video ya mauaji aliyoikuta kwenye memory card aliyoitoa ndani ya gari la Sammy. Alihisi baridi kali ya hofu ikipenya hadi kwenye mifupa. Sasa aliamini kuwa lilikuwepo jambo lisilo la kawaida likiendelea ambalo hakulijua. Je, walikuwa wanaitafuta ile memory card aliyokuwa nayo? Alitishika. Tena alitishika si kidogo.

Hili lilimwongezea mashaka zaidi na kujiona kuwa hakuwa salama kabisa endapo ingegundulika kuwa ni yeye aliyeichukuwa ile memory card. Mapigo ya moyo wake yalikuwa yanakimbia kwa kasi ya ajabu. Alihisi yalikaribia kukitoboa kifua chake chenye mifupa miteke na kuchanja mbuga nje ya mwili wake.

Alianza kuweweseka kwa hofu na kufumba macho yake, akaanza kuomba Mungu ili amnusuru yeye na jamaa zake dhidi ya wale watu walioonekana kubobea kwa unyama ulioweza kumtisha hata ibilisi. Baada ya maombi mafupi ghafla alijikuta akiuvaa ujasiri. Akafumbua macho yake na kutazama pale alipokuwa amesimama yule mtu. Patupu!

Hakukuwa na mtu tena wala kivuli chake. Na hata Pendo hakuwepo kitandani! Amempeleka wapi? Alijikuta akiishiwa nguvu. Mara akamsikia yule mtu akimhoji Joyce ni wapi aliko mtoto mwingine kwa kuwa walikuwa wameambiwa mwanzoni kuwa mle ndani kuna watoto wawili.

Hata hivyo, Winifrida hakusikia Joyce alijibu nini, alichoweza kuambulia ni kuwasikia wale watu wakimlazimisha Joyce ampigie simu Sammy kumtaka arudi nyumbani haraka na kumwonya asifikirie kufanya ujanja ambao ungeyagharimu maisha yake na mtoto Pendo. Wakati huo Joyce alikuwa analia kilio cha kwikwi.

Winifrida alihamanika sana. Alipepesa macho yake pale alipokuwa amejikunyata huku akiwaza jinsi ya kufanya ili kuwanusuru Joyce na Pendo toka katika mikono ya wale majahili. Aliamua kufanya jambo la hatari lakini la kishujaa. Aliamua kumpigia simu Sammy na kumweleza ukweli wa kile kilichokuwa kinaendelea pale nyumbani. Lakini angeanzaje?

Bahati ilikuwa upande wake, simu yake ilikuwa imefichwa kule kule juu ya kabati alikokuwa amejikunyata. Ni kama vile Mungu alikuwa amemwongoza kuificha ile simu juu ya kabati. Kwa hofu kubwa aliichukua na kuitafuta namba ya Sammy, akapiga na kusikiliza, akasikia simu ikiita upande wa pili na mara ikapokelewa, kisha akaisikia sauti ya Sammy kutoka upande wa pili wa ile simu.

Winifrida akashikwa na kitete na kushindwa kuongea, hofu ilikuwa imemtawala na donge la fadhaa kumkaba kooni. Alimeza funda kubwa la mate kwa nguvu mithili ya mtu anayejaribu kukisukuma kipande cha mfupa kilichokwama kooni. Alitamani sana kupiga yowe lakini sauti yake ikamsaliti. Akajiuliza kwa nini apige yowe? Akili ilimhoji na kumtia ganzi.

Akajikuta akishindwa kabisa kuongea japo alimsikia Sammy akiendelea kuita upande wa pili wa simu. Alishindwa, si kwa sababu ya hofu ya kusikiwa, bali alijiuliza kuwa endapo Sammy angemuuliza simu ile aliitoa wapi angemjibu nini kwani hakuna yeyote aliyejua kama anamiliki simu. Akaikata.

Alianza kujilaumu kwa kutokuzungumza na Sammy, kwani ni hatari zaidi kumwacha Sammy arejee nyumbani na kukutana na wale watu hatari kuliko yeye kutafuta majibu ya wapi ameitoa ile simu. Majuto yalipita haraka kichwani mwake, yalipita kwa kasi mno kiasi cha kumwita Mungu na asimweleze alilotaka amfanyie.

Mara akapata wazo la kupiga tena simu. Lakini kwa wahaka aliokuwa nao, asingeweza kuzungumza na Sammy kwa kuchelea kusikiwa na wale watu. Alishusha pumzi huku akijaribu kusikiliza kwa makini akihofia kuingia kwenye mtego kwa kudhani mmoja wa watu wale, ambao hakujua idadi yao, angeweza kuwa amejificha mle chumbani kumsubiri. Alijitahidi kuangaza macho yake sehemu alizoweza kuzifikia lakini hakuona kitu cha kutilia shaka.

Usikose kufuatilia kila hatua ya kusisimua ambayo Taxi inapitia ili kuyajua yote yaliyojiri. Ciao...
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom