Taxi - (74)
ILIPOISHIA
“Kaondoka?” Maximilian alimuuliza yule mhudumu wa kiume.
“Eeh! Ila kakasirika huyo! Amesema mtakutana mahakamani,” yule mhudumu alisema, kisha akamgeukia Tunu, “Anti, nikusaidie?”
Tunu aliyekuwa akimtazama Maximilian alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kugeuza shingo yake kumtazama yule mhudumu mara moja.
“Nilitaka kumuulizia huyu kaka, bahati nzuri nimemuona,” Tunu alimwambia yule mhudumu kwa sauti tulivu na kumkabili Maximillian, “Samahani, kaka’angu!”
Maximilian aligeuza shingo yake kumtazama Tunu kwa makini. Tunu aliachia tabasamu pana la kirafiki huku akimsogelea. Maximilian naye alijikuta akiachia tabasamu, huku akionekana kuvutiwa na Tunu. Walitazama kwa sekunde chache kila mmoja akiwa kimya. Macho yao yaliongea mengi kuliko ambavyo wangeweza kuongea kwa mdomo.
SASA ENDELEA...
“Enhe, nikusaidie!” hatmaye Maximilian alimudu kumuuliza Tunu.
Tunu alishusha pumzi za ndani kwa ndani na kuonekana kama aliyekuwa akitafuta neno la kuongea.
“Jana usiku katika kipindi chako nimeliona gari aina ya Cadillac DeVille nikawa
very interested…” Tunu alianza kujieleza, akasita na kuzungusha macho yake kuwaangalia watu waliokuwa wameketi kwenye eneo la kusubiria pale mapokezi. Wale wahudumu wa mapokezi na Maximillian wakatazamana, kisha wakamtazama Tunu kwa makini.
“Nahitaji kuonana na mmiliki wa gari hilo, sijui utanisaidiaje kaka’angu!” Tunu alisema huku akishusha pumzi. Maximilian alishusha pumzi na kulamba midomo yake.
“Mmh… hata sijui nisemeje, sina namba zake na hadi sasa tuna ugomvi. Alikuwepo hapa na ameondoka dakika chache tu zilizopita, nadhani mmepishana hapo nje,” Maximilian alisema huku akiegemeza kiwiko cha mkono wake juu ya meza ya mapokezi.
Tunu alishika kiuno chake na kukunja sura yake akionekana kuwaza kidogo. Kisha alimtazama Maximilian, “Hakuna sehemu yoyote unayoijua labda naweza kumpata?”
Maximilian alifikiria kidogo akionekana kujishauri, kisha alivuta pumzi ndefu na kuzishusha taratibu.
“Nenda pale kwenye mgahawa wa kisasa wa Elli’s, Ilala Sharif Shamba, mara nyingi huwa anakuwepo pale kwa rafiki yake. ila usimwambie kama mimi ndiye nimekuonesha,” Maximilian alimwambia Tunu.
“Usijali, kaka’angu. Nashukuru sana, nikiwa na chochote nitarudi tena kwako,” Tunu alisema na kuanza kupiga hatua taratibu kuondoka eneo lile huku macho ya Maximillian na wale wahudumu wa mapokezi yakimsindikiza hadi alipotoka nje ya jengo.
Alifika kwenye maegesho ya magari ya lile jengo la kituo cha televisheni ya Mzizima na kuingia ndani ya gari, alimkuta Victor akiwa amejiegemeza kwenye siti yake akiwa anasinzia.
“Twen’zetu. Naomba nipeleke Sinza nikapumzike,” Tunu alisema huku akifunga mkanda wa siti yake.
“Umempata uliyekuja kumtafuta?” Victor aliuliza kwa shauku huku akimkazia macho Tunu.
“Sijampata, nitamfuatilia tena baadaye!” Tunu alijibu kwa kifupi kisha akajiegemeza kwenye siti yake na kufumba macho.
Victor hakuongeza neno jingine, aliwasha gari na kuliondoa taratibu, akaingia barabara ya Lumumba na kwenda mbele alikokutana na barabara ya Morogoro, akakunja kuingia kushoto akiifuata barabara ile ya Morogoro. Ilikuwa ni safari ya kuelekea Sinza.
* * * * *
Saa tano ya asubuhi Joyce alikuwa ameketi kwenye sofa sebuleni kwake akitazama runinga, hata hivyo macho yake yalitazama runinga lakini akili yake haikuwa kwenye runinga, alikuwa mbali sana kimawazo, japo alionekana mtulivu sana.
Siku ile hakujisikia kutoka kwenda sehemu yoyote, alitaka kubaki ndani akipumzika baada ya kile kilichotokea kati yake na mumewe usiku wa siku iliyotangulia. Alishusha pumzi na kujilaza juu ya sofa.
Siku ile ilionekana kuwa ndefu sana kwa Joyce kuliko kawaida, hadi wakati huo alikuwa hajatia kitu chochote tumboni na hakuwa akihisi njaa, alikuwa peke yake nyumbani baada ya Sammy kutoka kwenda kazini kwake na watoto kwenda shule. Alijihisi mpweke sana.
Katika upweke ule alijikuta akizama kwenye tafakari, alikumbuka jinsi alivyokutana na Sammy kwa mara ya kwanza, walivyoanza uhusiano wao hadi walipofunga ndoa.
Alikumbuka kuwa alikutana na Sammy kwa mara ya kwanza miaka minane iliyokuwa imepita akiwa safarini kutoka Tanga akielekea jijini Dar es Salaam kuanza kazi ya ukatibu muhtasi baada ya kumaliza masomo yake ya uhazili katika Chuo Cha Uhazili tabora.
Ni siku hiyo hiyo Sammy alikuwa anatoka kutembelea vivutio vya mapango ya Amboni yaliyopo umbali wa kilomita 8 kutoka jijini Tanga katika barabara kuu inayoelekea Mombasa.
Ilikuwa saa kumi na mbili na dakika tano alfajiri ya siku ya safari yake ilimkuta akiwa bafuni anaoga na alitakiwa kuondoka saa kumi na mbili na nusu. Huaminika kuwa wanawake huchukua muda mrefu sana katika kujiandaa, kuanzia kuoga, kujipodoa na hata kuvaa nguo. Joyce alimaliza kuoga katika muda usiozidi dakika kumi, kisha alitoka haraka, akaingia chumbani mwake.
Kwa mara ya tatu, aliitupia jicho la wasiwasi saa yake ya mkononi iliyokuwa juu ya meza ya vipodozi, akajifuta maji haraka haraka. Zilikuwa zimebaki kama dakika tano tu tu kabla ya muda wa basi kupita uliokuwa umeandikwa kwenye tiketi yake, basi hilo lilikuwa likitokea jijini Tanga.
Kwa kawaida kutoka nyumbani kwao hadi kituo cha basi ingemchukua zaidi ya dakika arobaini na tano kama angetembea kwa miguu, lakini ilimchukua dakika tatu tu kufika kituo cha basi. Dereva wa pikipiki iliyomchukua kumpeleka hapo kituoni alikuwa ni kama nusu kichaa kutokana na mwendo wake wa kasi.
Joyce hakuamini kwamba angeweza kuwahi na kujiunga na wasafiri wenzake katika kituo cha basi kabla ya basi la Tahmeed halijapita.
Alipofika kituoni alitafuta sehemu nzuri akasimama. Siku ile alikuwa amevaa gauni zuri la kitenge cha wax lililokuwa limeshonwa na kudariziwa kwa nyuzi za dhahabu na kuushika mwili wake huku likilichora vyema umbo lake maridhawa na kichwani alikuwa amevaa kilemba kikubwa.
Kama ilivyokuwa imeandikwa, ndani ya dakika mbili tu basi la Tahmeed likawafikia na kusimama kituoni, Joyce akajiunga na wasafiri wengine kupanda ndani ya lile basi. Wakati akiingia kondakta wa lile basi alijikuta amebabaishwa sana na uzuri wa Joyce kiasi cha kusahau hata majukumu yake.
Kondakta alijikuta akipiga mluzi mdogo wa mshangao uliowafanya baadhi ya abiria walioketi jirani na mlango kumtazama kwa mshangao kabla ya macho yao kuhamia kwa Joyce. Si wanawake wala wanaume, wote walijikuta wakimkodolea macho Joyce huku wakiyasanifu mengi ya huba mbele ya hua aliyejitanashati kikweli kweli mbele ya macho yao!
Inaendelea...
CC
the_legend Norshad bobefu zoefu Pablo PAKAYA Ibney blackstarline Bryece Tater Bigjahman moneytalk marybaby nipo2 ram kisukari Smart911 Madame S carbamazepine Astelia culture gal Prisoner of hope Mine eyes kuku mweus Thad hearly Shunie moneytalk Tumosa Mine eyes Kudo swahiba92 ludist Toyota escudo Clkey macson3 boga la kiangazi LEGE Smart911 Richard irakunda skfull popie Krizy Beat hearly nipo2 MWINDAJI HARAMU kakhulu Katavi Norami mbududa iron2012 popie Bughy Harry Mlenge Kacheda mjasiliamali Laki Si Pesa cocochanel kinusikwetu big jambo mludego Shupavu Kacheda mjasiliamali Mweweso Songa Heri esiankiki mnadhimu mkuu wa jf