Stori ya kusisimua - Kizungumkuti!

Stori ya kusisimua - Kizungumkuti!

Kizungumkuti! - 29

Na Bishop Hiluka

“Muda!” alijikuta akiwaza tena, lakini safari hii alitamka kwa sauti kama vile alikuwa akiongea na mtu.

Ni mara ngapi Yusuf alikuwa akiuona “muda” ukipita mbio mbele yake mithili ya duma mwenye kasi! Kuna kipindi aliitamani kuusimamisha ili afurahie maisha bila kuwa na wasiwasi.

Lakini siku hiyo ambayo ilikuwa muhimu sana katika maisha yake “muda” ulionekana kumnyima raha, ulikuwa ukinyiririka taratibu kwa madaha na maringo kama kinyonga. Zaituni ndiye aliyekuwa mchawi wa huo “muda”. Alikuwa na mamlaka ya kuuamuru uwe duma mwenye kasi ama uwe kinyonga.

Endelea...

Yusuf alimuwaza Zaituni muda wote, mbele ya uzuri wa kiumbe huyo aliyeitwa Zaituni, Yusuf alijiona kama limbukeni wa mapenzi. Mawazo yalimpitia na moyo ulimwenda mbio kama mtu aliyekuwa na ugonjwa wa kihelehele. Alijiuliza iwapo hali ile ilikuwa ni matokeo ya kumsubiri Zaituni, ingekuwaje pindi angeingia ndani mwake?

Alijiambia kuwa kama ni mateso yalikuwa yametosha, huo sasa ulikuwa ni muda muafaka wa kumaliza utata. Aliitupia tena jicho saa yake, ilionesha kuwa saa 7:56. Wasiwasi ukazidi kwa kadiri muda ulivyokaribia. Aliendelea kusubiri lakini muda ulivyozidi kusogea ndivyo alivyozidi kuhisi mabadiliko katika akili na mwili wake.

Saa 7:57, Yusuf akaanza kupanga jinsi atakavyompokea Zaituni. Ikamjia picha akilini mwake ya Zaituni akiteremka katika basi la Shabiby na kumfuata lakini akaishiwa nguvu na kuanguka. Picha hiyo haikumpendeza kabisa Yusuf.

Saa 7:58, mwili mzima wa Yusuf ulijaa moto, alihisi joto kali sana likitambaa mwilini kwake kama vile alikuwa amewekwa kwenye tanuru la kuokea mikate. Kijasho chembamba kikaanza kumtoka!

Saa 7:59, vidole vya mikono yake vilianza kutetemeka kama vile damu ilikuwa ikienda mbio kwenye mishipa. Saa 8:00 alikuwa amebadilika kabisa na yeyote ambaye angemuona kwa wakati huo asingeshindwa kubaini kuwa Yusuf alikuwa katika wakati mgumu sana.

Hata hivyo, alipiga moyo konde na kusubiri ujio wa mrembo wa shani aliyekusudiwa kuumbwa malaika lakini akateremshwa duniani kimakosa. Muda ulianza kuyoyoma na Yusuf hakukata tamaa, aliendelea kumtizamia Zaituni kwa dakika zingine ishirini huku akichungulia kwenye kila gari lililoingia pale Ubungo.

Kichwa chake kilizunguka, na ndani yake mseto wa hamu, hofu na tamaa vilianza kumtambaa taratibu na kuyafanya maungo yake yageuke. Mara akaliona basi la Shabiby kutoka Dodoma likiingia katika Kituo cha mabasi cha Ubungo.

Muda ule Yusuf alikuwa amejiandaa vyema kumkabili Zaituni, alijiandaa kwa kila hali kuanzia kimavazi, namna ambavyo angempokea na kumsalimia kisha angemkaribisha jijini na hata namna ambavyo angemweleza jinsi alivyokuwa akimpenda kwa dhati.

Alisimama kutoka kwenye benchi baada ya kuliona lile basi likisimama na abiria kuanza kushuka, akasogea karibu huku akiweka sawa tai yake shingoni kisha akakaza macho yake kuwatazama kwa makini wale abiria walioshuka kutoka ndani ya basi la Shabiby.

Mara akamuona msichana mrembo aliyeshuka kutoka kwenye lile basi la Shabiby akiwa ameshika begi dogo jeusi la safari na kuanza kupiga hatua zake kwa madaha akielekea upande ule ambao yeye alikuwa amesimama.

Yule msichana ambaye alikiri kuwa hadi wakati huo alikuwa hakuwahi kumuona msichana wa namna ile katika pitapita zake, alikuwa amevaa vazi la kitambaa cha bazee lililoshonwa na kudariziwa vizuri kwa nyuzi za dhahabu na lilikuwa limenasa vyema kwenye kiuno chake chembamba kilichoshikilia mzigo mkubwa wa makalio na minofu ya mapaja yake.

Miguuni alivaa viatu vyekundu vyenye vikanyagio virefu vya mchuchumio na nywele zake nyeusi za kibantu alikuwa amezisuka mtindo wa rasta na kuzifunika kwa kilemba, hivyo kumfanya aonekane mzuri wa asili.

Mkono wake wa kushoto alikuwa amevaa saa nzuri ndogo ya kike iliyotengenezwa kwa namna ya kupendeza na hivyo kuongeza ziada nyingine katika uzuri wake. Begani alikuwa amening’iniza mkoba mzuri mwekundu.

Yusuf akajikuta akipiga hatua zake kumfuata yule mrembo, alisahau kabisa kuwa aliambiwa kuwa atakuwa ameweka ua waridi jekundu katika titi lake la kushoto. Alipokumbuka akasita na kusimama ghafla huku akimkodolea macho ya matamanio, na wakati huo huo yule msichana akampita kwa mwendo wa kasi passipo kumjali na kujichanganya kwenye umati wa watu.

Yusuf alibaki akiwa ameduwaa na alipokuwa bado anashangaa mara akamuona mwanamke mtu mzima aliyezidi miaka 60 akiwa amesimama akiangaza macho yake huku na kule kama vile alikuwa akimtarajia mtu. Yule bibi alikuwa amevaa gauni zuri la kitenge na miguuni alivaa viatu vya flat visivyo na visigino virefu. Yusuf alipomtazama vizuri akaliona ua waridi jekundu katika titi lake la kushoto.

Dah! Alijikuta akiishiwa nguvu, alihisi kana kwamba mwili wake ulikuwa umegawanywa katika mapande mawili, akataka aondoke zake na kumwacha yule bibi kwenye mataa, hata hivyo, hakuona kama ni busara kuondoka bila kuongea naye, hivyo akamfuata na kujitambulisha kwake huku akimuonesha kile kitabu.

"Naitwa Yusuf Akida, nimefurahi sana kukutana na wewe ana kwa ana, Bi Zaituni. Ninaomba kwanza nikupeleke ukapate chakula cha mchana kabla hatujaongea," Yusuf alisema huku akimtazama yule mwanamke kwa tabasamu.

Hata hivyo, alishangazwa sana kuona yule mwanamke hakuwa akimtambua yeye wala kile kitabu alichoshika na alimtazama kwa mshangao mkubwa kana kwamba aliona kitu kigeni cha ajabu kutoka sayari nyingine.

“Kwa kweli vijana mnazidi kunichanganya,” alisema yule bibi, “lakini kuna msichana mmoja alivaa ngyuo ya bazee na kilemba kichwani alielekea huko aliniomba nivae hili ua kwenye kifua changu. Na alisema kama mwanamume yeyote ambaye angenipokea nimuambie kuwa amekwenda kumsubiri katika hoteli ya Landmark. Alisema kuwa hili ni jaribio kuona kama kweli mwanamume huyo ana upendo wa dhati,” alisema yule bibi na kumuacha Yusuf akiwa mdomo wazi.

Haraka sana Yusuf aliondoka na kuelekea Landmark Hotel alikomkuta Zaituni akimsubiri, wakala pamoja chakula cha mchana na huo ndiyo ukawa mwanzo wa mahaba mazito na hatimaye ndoa… Yusuf aliwaza sana na mara akajikuta akipitiwa na usingizi pale pale kwenye kochi…

______

Mama Jasmine aliendelea kukaa kule nje akipiga soga na shoga zake hadi ilipotimia saa moja na ushee ndipo akaamua kuingia ndani na macho yake yakatua kwa mumewe aliyekuwa kauchapa usingizi palepale kwenye kochi, kiganja cha mkono wa kulia kikiwa shavuni.

Macho yake yalihama na kumtazama mwanawe Jasmine ambaye pia alikuwa kauchapa usingizi palepale kwenye kochi. Runinga ilikuwa bado inaonesha vipindi vya katuni.

Mama Jasmine alimfuata mwanawe na kumbeba kisha akaingia naye chumbani na kumlaza kitandani. Akarudi tena sebuleni na kusimama akimtazama mumewe kwa chuki na kuchukua remote kisha akaizima ile runinga.

Yusuf akashtuka na kufumbua macho yake, macho yake yakaanza kutambaa katika mwili wa mkewe, yakianza na mapaja yaliyonona kuelekea juu kisha yakakutana na nyonga zilizofinyangwa barabara.

Macho yake yakatuwama kwa muda katikati ya mapaja ya mkewe, kisha yakafunga safari kuelekea kiunoni yakakutana na kiuno kilichobonyea na kuacha fursa ya nyonga kuchanua zilivyotaka. Kiuno kilirembwa na tumbo dogo ambalo lilikana kuwa wakati fulani lilishabeba kiumbe kwa muda wa miezi tisa.

Hamu haikuishia hapo, macho yalielekea kwenye kifua kilichobeba matiti madogo yaliyokuwa yamesimama kana kwamba hakuwahi kunyonyesha hapo kabla. Hamu ya mapenzi ikamjaa juu ya mkewe.

Macho yake hayakuishia hapo bali yalipanda hadi kwenye uso wa mkewe, akauona uso wa mkewe ukiwa mkavu usio na tashwishwi yoyote. Yusuf akatweta na hamu ya mapenzi ikamuisha mara moja.

Mambo ndo' yanazidi kunoga, endelea kufuatilia stori hii ya kusisimua "Kizungumkuti" ili kuujua mwisho wake...
Hahahaa kitendo alichofanyiwa yusuph na jasmine kwa bibi kizee umfanyie mwanaume wa jf thread itakuhusu
 
Hahahaa kitendo alichofanyiwa yusuph na jasmine kwa bibi kizee umfanyie mwanaume wa jf thread itakuhusu
Hahahahahahahaaa, hujakosea kabisa. Ungeona tuu uzi unaosema "wadada wa jf mnayotufanyia Mungu anawaona. We mdada tuliepanga kukutana ubungo rudisha nauli nliyotumia kuja kukupokea. Nakupa siku 1". Afu kwa msisitizo anamalizia kabisa kuwaomba mods wasifute uzi wake[emoji2][emoji2][emoji2]

the Legend☆
 
Hahahahahahahaaa, hujakosea kabisa. Ungeona tuu uzi unaosema "wadada wa jf mnayotufanyia Mungu anawaona. We mdada tuliepanga kukutana ubungo rudisha nauli nliyotumia kuja kukupokea. Nakupa siku 1". Afu kwa msisitizo anamalizia kabisa kuwaomba mods wasifute uzi wake[emoji2][emoji2][emoji2]

the Legend☆
Hahaha na matusi juu
 
Nipo nyumbani wala sijawahi kuondoka...

Naanzaje kuwa mbali wakati Jacky wetu yupo.. Jacky ni grisi tosha ya kulainisha vigumu....
Hahahahahaa, leo imekuaje sasa, mbona bila bila?

the Legend☆
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom