Kizungumkuti! - 30
Na Bishop Hiluka
ILIPOISHIA
Yusuf akashtuka na kufumbua macho yake, macho yake yakaanza kutambaa katika mwili wa mkewe, yakianza na mapaja yaliyonona kuelekea juu kisha yakakutana na nyonga zilizofinyangwa barabara.
Macho yake yakatuwama kwa muda katikati ya mapaja ya mkewe, kisha yakafunga safari kuelekea kiunoni yakakutana na kiuno kilichobonyea na kuacha fursa ya nyonga kuchanua zilivyotaka. Kiuno kilirembwa na tumbo dogo ambalo lilikana kuwa wakati fulani lilishabeba kiumbe kwa muda wa miezi tisa.
Hamu haikuishia hapo, macho yalielekea kwenye kifua kilichobeba matiti madogo yaliyokuwa yamesimama kana kwamba hakuwahi kunyonyesha hapo kabla. Hamu ya mapenzi ikamjaa juu ya mkewe.
Macho yake hayakuishia hapo bali yalipanda hadi kwenye uso wa mkewe, akauona uso wa mkewe ukiwa mkavu usio na tashwishwi yoyote. Yusuf akatweta na hamu ya mapenzi ikamuisha mara moja.
Endelea...
Akiwa bado anatafakari jinsi ya kuanzisha maongezi na mkewe mara akamuona mkewe akiondoka haraka na baada ya muda akarudi akiwa amebeba jagi lililokuwa na maji ya kunawa na beseni dogo la kunawia, akaviweka pale mezani na kuondoka tena na baada ya muda akarudi akiwa amebea sahani ya chakula na kukitenga pale mezani bila hata kusema kitu, kisha akaelekea chumbani na kufunga mlango.
Yusuf alimtazama kwa kila hatua aliyopita bila kusema neno kisha akakaa pale kwa kitambo kirefu akikiangalia kile chakula, muda wote hakuwa akihisi njaa. Japo kile chakula kilikuwa kimepikwa vizuri sana lakini hakuweza kula. Alibaki kukikodolea macho akiutazama wali uliokolea nazi, samaki wa maji baridi, mboga za majani na maharage.
Baada ya kitambo kirefu cha ukimya huku akikitazama kile chakula hatimaye aliamua kula japo matonge kadhaa ili isionekane kuwa alikuwa amesusa chakula, kisha alikifunika na kuinuka akaingia chumbani kumfuata mkewe. Alipoingia chumbani alimkuta mkewe ameketi kwenye pembe ya kitanda akiwa kajiinamia anawaza na mara alipomuona mumewe alimtazama kwa jicho kali sana.
“Mama Jasmine, hivi ni mambo gani haya yasiyoisha? Nimeshakuomba samahani zaidi ya mara tatu lakini naona mwenzangu bado una kinyongo…” Yusuf aliongea kwa sauti ya chini na ya kusihi.
“Hayawezi kuisha kirahisi kama unavyodhani!” Mama Jasmine alisema kwa sauti tulivu lakini yenye hasira.
“Kwa hiyo tutaishi maisha haya hadi lini?” Yusuf aliuliza tena huku akimwangalia mkewe kwa huzuni.
“Niache bwana, nahitaji kupumzika. We nenda kwa huyo huyo malaya wako,” Mama Jasmine alijibu kwa hasira na kujilaza kitandani.
“Dah, natamani hii siku ifutike kabisa akilini mwangu. Hata kama ikibaki niione kama ndoto tu. Nahisi kama vile unanichukia sana,” Yusuf alimweleza mkewe bila kumtazama wala kusubiri jibu, akatoka zake kimya kimya.
Alifungua mlango wa chumbani akapita sebuleni na kuelekea nje hadi barazani. Muda ule alikuwa bado hajavua saa yake ya mkononi. Hivyo aliitazama na kugundua kuwa ilishatimu saa tatu na ushee.
Alisimama pale nje akainua macho yake kutazama angani. Anga lilikuwa wazi na la rangi ya samawati liking’arishwa kwa wingi wa nyota na mwezi mkubwa uliokuwa umevaa rangi nyekundu aliouona vizuri kutokea pale alipokuwa amesimama.
“Mwezi mwandamo huanza mchanga, pole pole hukua na kuwa mpevu na huweza kuonekana kwa wote hata wale waonao ukungu mbele ya macho yao, na baadaye huwa mwekundu na huogopesha manyani porini,” Yusuf aliwaza akiyakumbuka maneno ya mwanazuoni mmoja aliyemsoma kitabuni wakati akiwa sekondari.
Aliendelea kuutazama ule mwezi mwekundu, akaanza kutafakari kuhusu masimulizi aliyowahi kuyasikia kuwa ukifikia hatua hiyo huogopesha manyani porini.
Muda huo upepo wa usiku uliipuliza ngozi yake na kumfanya ajisikie vizuri na hapo ndipo alipogundua kuwa ngozi yake ilinata kutokana na jasho. Alitamani kuingia ndani akachukue maji na kuelekea bafuni kuoga, hata hivyo, hakuwa na hamu ya kurudi ndani.
Donge la fadhaa lilimkaba kooni hasa alipohisi kuwa huenda mkewe aliamua kumchukia na wala hakutaka kumsamehe. Akawaza nini cha kufanya ili kuurudisha upendo katika familia yake. Mara akakumbuka msemo kuwa “hakuna mkate mgumu mbele ya chai” hii ilimaanisha kwa Yusuf kuwa njia pekee ilikuwa ni kupata fedha nyingi ambazo zingeweza kurudisha heshima na furaha ndani ya nyumba.
Alipowaza suala la pesa mara akamkumbuka Jacky ambaye yeye alimtambua kwa jina la Belinda. Alijilaumu kwa kuiacha simu yake ndani angempigia ili ingalau asikie sauti yake ya kubembeleza, huenda ingempunguzia stress. Alitamani kuingia ndani akachukue simu yake lakini alisita.
“Dah, Belinda ameyateka mawazo yangu na akili yangu yote inamuwazia yeye tu. Katika mazingira kama haya nahitaji kuwa naye tu karibu nimkumbatie mikononi mwangu, nikimbembeleza kama mtoto mdogo huku nikiisikia miguno yake na sauti yake nyororo anapolalama kwa raha…” Yusuf aliwaza na kushusha pumzi.
“Ki ukweli Belinda yuko tofauti sana na wanawake wengine wote na ana mvuto wa ajabu mno, pia amebarikiwa vitu vya kipekee ambavyo ni vigumu hata kuvielezea…” Yusuf alizidi kusumbuliwa na mawazo juu ya Jacky, kwa muda mrefu alimuwazia Jacky tu. Mara akachoka kusimama na kuamua kukaa kwenye ngazi za baraza.
Alipoitazama tena saa yake akashtuka kuona kuwa ilikuwa imeshatimia saa sita na dakika kumi na tano usiku! Ilikuwa imeshaingia siku nyingine akiwa anapigwa na ubaridi pale nje. Aliamua kukiegemeza kichwa chake kwenye nguzo ya ukuta na kufumba macho kwani uchovu ulimuelemea sana, na mbu nao hawakumwacha salama.
Mama Jasmine akiwa chumbani amelala kitandani alishtuka na kuangaza macho yake huku na kule, Yusuf hakuwepo ndani. Akapuuzia na kufumba tena macho yake kulala, hata hivyo, alijikuta akianza kupatwa na wasiwasi.
“Mke mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe, lakini mwenye busara huijenga na kuiboresha nyumba yake,” Mama Jasmine alijikuta akiyakumbuka maneno hayo kutoka ndani ya Biblia ambayo aliwahi kuyasikia kutoka kwa mchungaji mmoja wa kanisa lililokuwa jirani na nyumba waliyokuwa wakiishi.
Japo hakuwa Mkristo lakini maneno yale yalikuwa yamemuingia na aliyakariri japo hakujua yalipatikana wapi ndani ya hiyo Biblia. Mara akajikuta akiinuka kutoka pale kitandani na kutoka, akamwangalia mumewe pale sebuleni hakumuona, akafungua mlango na kumwangalia kule uani, hayupo!
Sasa akaingiwa na hasira akidhani kuwa labda aliondoka kwenda kulala kwa kimada wake waliyekesha wote kabla hajarudi nyumbani asubuhi, akipanga kumkomoa.
Akatoka nje na kumkuta Yusuf akiwa amejikunyata pale kibarazani kwenye ngazi akiwa chakula cha mbu, alijikuta akiingiwa na huruma, alisimama akimtazama kwa huruma na kuamua kumwamsha kwa kumpiga piga taratibu mgongoni huku akimwita. Yusuf alishtuka na kuamka, mkewe akamuinua na kumuongoza ndani.
Yusuf alipoingia chumbani alivua fulana yake na kujitupa kitandani, wala hakuwa tena na wazo la kuoga. Dakika mbili baadaye alikuwa anakoroma.
Mama Jasmine alisimama pale akimtazama mumewe kwa makini kisha akarudishia chandarua vizuri na kuzima taa halafu akapanda kitandani na kulala pembeni ya mumewe.
Itaendelea...