Stori ya kusisimua - Kizungumkuti!

Stori ya kusisimua - Kizungumkuti!

Kizungumkuti! - 76

Na Bishop Hiluka

ILIPOISHIA...

Liston na Kabwe walitazamana kisha wakawatupia macho ASP Komba na Sajenti Mapambano huku wakiwatazama kwa makini na hatimaye wakamgeukia tena Jacky.

“Hebu acha kutuwekea mkwara wa kitoto, unataka kutuchezea picha sisi. Hadhulumiwi mtu hapa,” Kabwe alisema huku akimnyooshea kidole Jacky kwa hasira.

“Wala hakuna anayetaka kuwachezea picha, mnataka au hamtaki lakini huo ndiyo ukweli wenyewe…” Jacky alimwambia Kabwe huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

Muda ule ule kabwe aliinuka ghafla kwa pasipo kutegemea alichomoa bastola yake iliyokuwa imehifadhiwa kiunoni. Aliikamata vyema ile bastola na kuielekezea kwenye kichwa cha Jacky huku akionekana kugadhabika sana. Muda ule midomo yake ilikuwa ikimtetemeka kwa hasira.

Endelea...

ASP Komba alikwisha ihisi hatari ambayo ingeweza kutokea mbele ya macho yao muda wowote, hivyo aliwahi kuinuka na kuruka juu akajibetua kwa sarakasi ya samasoti na kumchapa Kabwe pigo moja takatifu la flying kick lililomtia udhaifu mkubwa kifuani na kichwani kwake.

Pigo lile lilimfanya Kabwe arudi kinyumenyume na kupepesuka ovyo huku akipiga mayowe ya hofu. ile bastola ikamtoka na kuanguka kando. ASP Komba hakutaka kumkawiza, kwa haraka aliruka tena hewani na kumchapa pigo lingine la teke la kijapani ambalo lilikata mzizi wa fitina, kwani Kabwe aliangukia juu ya kiti kikubwa ambacho kilivunjika vipande viwili.

Kuona vile Liston alitaharuki na kunyanyuka haraka huku akiitoa bastola yake tayari kwa mapambano kisha aliielekeza kwa ASP Komba. Kwa haraka sana Sajenti Mapambano alikusanya nguvu za kutosha kisha kufumba na kufumbua aliruka juu na kutua karibu na Liston, akajibetua na kuuzungusha chini mguu wake wa kulia akimchota mtama maridadi wenye ufundi wa hali ya juu.

Liston alishikwa na taharuki ya aina yake wakati alipokuwa akirushwa hewani na alipotua chini akajikuta tayari ameenea vizuri kwenye kabari matata ya Sajenti Mapambano iliyomnyima nafasi ya kuhema vizuri, huku macho yake yakiwa yamemtoka pima kama mjusi aliyebanwa na mlango.

Tukio lile lilikuwa limesababisha hata ile bastola yake mkononi imponyoke na kuangukia mguuni kwa Sajenti Mapambano. Mahesabu ya Sajenti Mapambano yalikuwa yameenda vizuri kwani kwa haraka aliinama na kuiokota ile bastola huku Liston akiendelea kufurukuta bila ya mafanikio.

Wakati Liston akiwa kadhibitiwa vyema na Sajenti Mapambano, Kabwe alijaribu kuinuka huku akigugumia kwa maumivu makali na kujiweka sawa kumkabili ASP Komba, kisha akaanza kumfuata kwa hasira kama Mbogo aliyejeruhiwa.

ASP Komba alikusanya nguvu za kutosha kisha alimtandika kichwa cha nguvu na kuupasua vibaya mwamba wa pua yake. Kabwe alipiga yowe kali la maumivu huku akiyumba, na hapo ASP Komba akamtupia pigo jingine kali la kareti shingoni lililomfanya apepesuke na kurushwa juu, akapiga yowe kali la maumivu wakati alipojipigiza kichwa chake kwenye ukuta wa ile fensi ya nyumba kisha akaanguka chini na kutulia kimya.

Shingo yake ilikuwa imevunjika na damu ilikuwa inamtoka puani, mdomoni na masikioni. Jacky aliziba macho yake huku akitoa ukelele hafifu wa hofu. Watu waliokuwa wamekuja pale msibani walianza kukaa mbali na eneo lile na wengine kupanda juu ya ukuta wa fensi huku wakichungulia kile kilichokuwa kikiendelea pale nyumbani kwa Jacky wakati ASP Komba na Sajenti Mapambano wakiwadhibiti wale wahuni.

Mara eneo lote likageuka kuwa kisiwa chenye ukimya wa kutisha, hakuna cha nyimbo za maombolezo wala vilio, watu wote walikuwa kimya kabisa. Liston alikubali yaishe na hivyo kusalimu amri mbele ya wale maofisa wa polisi wenye mafunzo maalumu katika sanaa ya mapigano. Wakamfunga pingu mikononi na kumtuliza pale chini, kisha ASP Komba aliwaita makachero Haji Adam na Sebastian Masesa waliokuwa sehemu ya wale waombolezaji.

Kisha akatoa simu yake akawapigia kituoni akiwafahamisha kilichotokea pale nyumbani kwa Jacky na kuwaomba walete haraka gari la kubebea maiti. Muda ule ule wale makachero makachero Haji Adam na Sebastian Masesa walimnyanyua Liston wakamkokota msobe msobe hadi kwenye gari la polisi na kuondoka naye.

ASP Komba aliutazama kwa makini mwili wa Kabwe uliokuwa umelala pale chini ukiwa hauna uhai na kuminya midomo yake, kisha akampa maelekezo Koplo Victor ya kubaki hapo hadi gari la kubebea maiti litakapofika na kuuchukua ule mwili.

ASP Komba akamtazama Jacky kwa makini na kushika vyema bastola yake, akamuelekezea kichwani.

“Haya sasa nieleze, ziko wapi?” ASP Komba alisema kwa sauti iliyokuwa imebeba hasira.
“Nini, afande?” Jacky alimuuliza ASP Komba huku akionekana kugwaya sana.

“Fedha, mmezificha wapi?” ASP Komba alimuuliza Jacky huku sura yake ikiwa mbali kabisa na mzaha, safari hii sura yake haikuonesha aina yoyote ya utani wala kubembelezana.

“Zipo kwenye kabati maalumu ndani ya chumba maalumu cha ofisi ya siri.” Jacky alisema na kuwafanya ASP Komba na Sajenti Mapambano watazamane.

“Tupeleke haraka kwenye hicho chumba cha ofisi ya siri,” ASP Komba alimuamuru Jacky.
Bila ubishi wowote, Jacky akaanza kupiga hatua taratibu kuelekea ndani ya lile jumba huku akifuatwa na wale maofisa wa polisi, wakaivuka ile sebule kubwa ya lile jumba iliyokuwa imejaa waombolezaji ambao waliwatazama kwa wasiwasi wale maofisa wa polisi ambao muda wote walikuwa wamemuelekezea Jacky bastola kichwa wakati wakipita, wakaelekea katika chumba cha chakula.

Kule kwenye chumba cha chakula wakavuka na kuelekea jikoni ambako waliukuta mlango mwingine ulioonekana kama mmoja wa milango ya makabati ya ukutani ambao juu yake kulikuwa na taa ndogo nyekundu na pembeni yake kulikuwa na kisanduku kilichokuwa na namba.

Walipoufikia ule mlango Jacky aligeuza shingo yake kuwatazama ASP Komba na Sajenti Mapambano na kuiona ile mitutu ikiwa bado imemuelekea kichwani, akashusha pumzi na kubonyeza namba nne za siri kwenye kile kisanduku kilichokuwa pembeni ya mlango kisha akaweka dole gumba la mkono wake wa kulia katika sehemu maalumu iliyokuwa ikiwaka taa ya kijani.

Thank you, Jackline Mgaya, you’re welcome…” sauti maalumu kwenye spika ndogo pembeni ya mlango ikasikika ikimkaribisha Jacky huku ikiambatana na maandishi “Welcome Jackline Mgaya” na mara mlango ule ukafunguka.

ASP Komba na Sajenti Mapambano wakatazamana na kutweta, kisha wakaingia ndani ya kile chumba wakimfuata Jacky huku wakiendelea kumuelekezea bastola zao kichwani, wakiwa tayari kwa lolote. Na hapo walijikuta wakiwa ndani ya ofisi ya siri iliyoonekana kama ofisi ya kawaida tu yenye samani chache za kiofisi ikiwa na kiyoyozi aina ya Singsung kilichokuwa kikisambaza hewa safi.

Ofisi ile ilikuwa na zulia zuri la rangi nyekundu sakafuni, meza kubwa ya kiofisi ambayo juu yake kulikuwa na kompyuta mbili, IMac Retina 5K ya inchi 27 na PC aina ya Acer i5 yenye kioo cha flat.

Kwenye kona moja ya ile ofisi kulikuwa na mashine iliyokuwa ukutani mfano wa zile mashine za kutolea fedha (ATM), lakini hii ilikuwa ikisoma alama za vidole.

Jacky alishusha pumzi huku akionekana kujishauri, kisha akaingiza tena namba nne za siri na kuweka kiganja cha mkono wake wa kulia mahala palipochorwa alama ya vidole na baada ya sekunde kumi ile mashine ikasoma na kuwaka taa ya kijani huku maandishi yakitokea kwenye kioo, “Thank you, Jackline Mgaya, Now the door will open in a few seconds”.

Ndani ya sekunde tano mlango fulani uliokuwa unafanana na ule ukuta ukaanza kusogea ukifunguka taratibu, na hapo wakaliona kabati la ukutani likijitokeza, na begi kubwa la magurudumu lililoonekana kwenye kamera za usalama za benki likaonekana likiwa limehifahiwa kwenye shelfu za lile kabati la ukutani.

Bila wasiwasi wowote, Jacky akalivuta lile begi na kubonyeza namba fulani zilizokuwa juu ya lile begi, likafunguka. Mabunda ya fedha ya noti nyekundu nyekundu yaliyopangwa vizuri yakaonekana ndani ya lile begi kubwa. ASP Komba na Sajenti Mapambano wakapigwa butwaa.

Ghafla Jacky akafanya jambo ambalo hakuna yeyote aliyekuwa amelitarajia, aliruka hewani kutoka pale alipokuwa amesimama na kutua nje ya kile chumba na kubonyeza namba fulani kwenye kile kisanduku kilichokuwa na namba kando ya ule mlango wa ofisi. ASP Komba alishtuka na kuruka juu kumfuata Jacky, bastola ikiwa mkononi, lakini alikuwa amechelewa! Mlango ukajifunga.

Kwa sekunde kadhaa ASP Komba na Sajenti Mapambano wakachanganyikiwa wasijue wafanye nini, fahamu zilipokuja kuwarudia, ASP Komba alishusha pumzi ndefu kana kwamba alikuwa ametoka kwenye mbio ndefu za marathoni.

Itaendelea...
 
Kizungumkuti! - 77

Na Bishop Hiluka

Ghafla Jacky akafanya jambo ambalo hakuna yeyote aliyekuwa amelitarajia, aliruka hewani kutoka pale alipokuwa amesimama na kutua nje ya kile chumba na kubonyeza namba fulani kwenye kile kisanduku kilichokuwa na namba kando ya ule mlango wa ofisi. ASP Komba alishtuka na kuruka juu kumfuata Jacky, bastola ikiwa mkononi, lakini alikuwa amechelewa! Mlango ukajifunga.

Kwa sekunde kadhaa ASP Komba na Sajenti Mapambano wakachanganyikiwa wasijue wafanye nini, fahamu zilipokuja kuwarudia, ASP Komba alishusha pumzi ndefu kana kwamba alikuwa ametoka kwenye mbio ndefu za marathoni.

Endelea...

What are we going to do?” (Tutafanyaje) Sajenti Mapambano aliuliza kwa wasiwasi.

The bastard has escaped. We must do something to get out of here,” (Mwanaharamu katoroka. Lazima tufanye kitu tutoke humu) ASP Komba alisema huku akijaribu kuufungua ule mlango uliokuwa umejifunga bila mafanikio.

“Inaonekana chumba hiki kina mambo makubwa tusiyoyafahamu. Tunachotakiwa ni kutafuta namna ya kujiokoa kutoka humu ndani haraka kabla hayajatukuta makubwa,” ASP Komba alimwambia Sajenti Mapambano huku akionesha kukata tamaa.

Kisha kama mtu aliyekumbuka jambo alichukua simu yake kisha akapiga simu ofisini kwake akiwafahamisha kilichotokea na kuwaomba waongeze nguvu na wamlete mtaalamu wa Tehama.

* * * * *

Saa kumi na mbili jioni, ndani ya ofisi za Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu, kwenye jengo la kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam, ASP Komba alikuwa ameketi kwenye kiti chake cha kuzunguka.

Mkononi alikuwa ameshika faili kubwa ambalo alikuwa akilipitia na kuhakiki zile taarifa. Mara mlango wa ile ofisi ukagongwa mara moja na kufunguliwa, kisha Nassos Chatzopoulos, mkurugenzi mkuu wa The Jacarandah Group akaingia na kutembea taratibu huku akionekana mnyonge sana.

ASP Komba alimtazama Nassos Chatzopoulos na kuachia tabasamu huku akimuelekeza kiti. Nassos aliketi kwenye kile kiti huku akimtazama ASP Komba kwa umakini.

I’m sorry to bother you, Mr Nassos, but I’ve called you to give you a final report of our case on the part of the investigation,” (Samahani nimekusumbua, bwana Nassos, lakini nimekuita ili nikupe taarifa ya mwisho ya kesi yetu kwa upande wa upelelezi) ASP Komba alimweleza Nassos huku akiendelea kutabasamu.

Okay, officer, but I'm desperate to get back my money, however, I don't know where you've got?” (Sawa, afande, lakini mimi nimeshakata tamaa kabisa ya kuzipata fedha zangu, hata hivyo, sijui mmefikia wapi?) Nassos Chatzopoulos alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

All your money was found…” (Fedha zako zote zimepatikana…)

Impossible, all!” (Haiwezekani, zo-te!) Nassos aliuliza huku akinyanyuka kutoka kwenye kile kiti kwa mshtuko mkubwa, alimkodolea macho ASP Komba kwa mshangao akiwa haamini kile alichokisikia.

All and have been stored within the central police cabinet of the stolen money. You’ll be given once the case has ended,” (Zote na zimehifadhiwa ndani ya kabati kuu la polisi la fedha zilizoibiwa. Utakabidhiwa mara tu kesi itakapomalizika) ASP Komba alisema huku akishusha pumzi.

When?” (Lini?) Nassos aliuliza kwa shauku kubwa.

It won't take long. The defendants will be brought to court tomorrow morning, and we’ll make sure the case goes quickly because all the evidences are there,” (Haitachukua muda. Washtakiwa watakafikishwa mahakamani kesho asubuhi, na sisi tutahakikisha kesi inakwenda haraka maana vielelezo vyote vipo) ASP Komba alimwambia Nassos huku akilifunga lile faili na kuliweka kwenye droo ndogo ya meza yake.

How many defendants are there?” (Kwani washtakiwa wenyewe ni wangapi?) Nassos alimuuliza ASP Komba kwa shauku huku sura yake ikianza kuonesha nuru.

They were three defendants but now they are only two. Yusuf Akida, the employee of the Commercial Bank and the notorious criminal called Liston George. The first defendant, a woman who was the key arranger of all strategies, called Jackline Mgaya has managed to escape,” (Walikuwa watatu lakini kwa sasa wapo wawili tu. Yusuf Akida, yule mfanyakazi wa Benki ya Biashara na mhuni maarufu anaitwa Liston George. Mshtakiwa wa kwanza mwanamke aliyekuwa mratibu mkuu wa mipango yote, anayeitwa Jackline Mgaya amefanikiwa kutoroka) ASP Komba alisema na kumfanya Nassos kushangaa kidogo.

I heard even my attendant, Jasmine Kombo is involved in theft! Will she not be brought to court?” (Si nilisikia hata yule mhudumu wangu, Jasmine Kombo kuwa amehusika kwenye wizi! Kwani yeye hatafikishwa mahakamani?) Nassos aliuliza kwa mshangao.

She’d have been brought if she were present,” (Kama angekuwepo angefikishwa) ASP Komba alisema huku akizilamba kingo za midomo yake kwa ulimi.

If she were present! What do you mean, officer, I’ve heard she’s admitted in hospital?” (Kama angekuwepo! Unamaanisha nini, afande, si nimesikia amelazwa hospitali?) Nassos aliuliza huku akizidi kushangaa. ASP Komba alivuta pumzi ndefu kisha akazishusha taratibu.

She has also escaped this midday after the interrogation,” (Pia katoroka leo mchana baada ya mimi kutoka kumhoji) ASP Komba alisema, Nassos akaguna. Wakatazamana kwa kitambo kifupi na kuangua kicheko.

Kicheko chao kilikatizwa na simu ya ASP Komba iliyoanza kuita, ASP Komba alitaka kuipuuza ile simu lakini alipoitazama kwa makini akashtuka sana baada ya kugundua kuwa ilikuwa inatoka kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Evance Hiza. Akaipokea haraka na kuiweka sikioni.
Hello!” ASP Komba alisema kwa unyenyekevu.

“Habari yako, ASP?” sauti nzito ya IGP Hiza ikasikika kutoka upande wa pili wa ile simu.

“Nzuri, afande!” ASP Komba alijibu kwa sauti ya ukakamavu.

“Umefikia wapi huko?” IGP Hiza aliuliza kwa shauku.

“Tumekamilisha kazi, afande,” ASP Komba alijibu kwa ukakamavu.

“Unasema…?”

“Nasema tumekamilisha ile kazi, afande.”

“Mmefanikiwa kuzipata fedha zote zilizoibwa?”

“Ndiyo, afande, fedha zote zipo salama na zimehifadhiwa ndani ya kabati kuu la polisi la fedha zilizoibiwa,” ASP Komba alisema huku akimtupia jicho Nassos.

“Vipi watu walioshiriki katika wizi wa mabilioni pale benki, mmefanikiwa kuwakamata?”

“Ndiyo, afande, tunao watuhumiwa wawili na mmoja ametoroka… wengine watatu wamekufa katika operesheni,” ASP Komba alisema huku akishusha pumzi za ndani kwa ndani.

IGP Hiza alinyamaza kwa sekunde kadhaa, kisha akaibuka, “Mbali na wewe, ni nani mwingine alikuwa mstari wa mbele katika kuongoza upelelezi huo?”

“Msaidizi wangu, Sajenti Mapambano.”

“Yupo ofisini sasa hivi?”

“Hapana, nimempa mapumziko ya siku mbili, ataingia kazini keshokutwa asubuhi. Vipi afande?” ASP Komba aliuliza huku akionekana kupata shaka kidogo.

“Wanasema mcheza kwao hutunzwa. Kuna nafasi zimetoka za askari kwenda masomoni Toronto, Canada mwezi ujao, nataka nimpe nafasi hiyo Sajenti Mapambano akaongeze ujuzi…” IGP Hiza alisema na kushusha pumzi za ndani kwa ndani.

“Na wewe jina lako tayari lipo mezani kwa Rais, utakuwa mmoja wa maofisa wa polisi watakaopewa kamisheni na Rais wa Tanzania kuwa Makamishna wasaidizi wa Polisi, kwa hiyo utapanda nafasi mbili zaidi kutoka Mrakibu Msaidizi wa Polisi hadi Kamishna Msaidizi wa Polisi. Na ukishapewa kamisheni tu nakuhamishia Arusha kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa,” IGP Hiza alisema na kumfanya ASP Komba akenue meno yake kwa furaha.

“Ninashukuru sana, afande, ninashukuru sana…” ASP Komba alisema kwa nyenyekevu. IGP Hiza akakata simu.

MWISHO.
0685 666964
 
Mwisho wa safari hii ndefu iliyojaa "KIZUNGUMKUTI" ndiyo mwanzo wa safari nyingine itakayotufanya tujiulize, mambo haya "HADI LINI!" Usikose kufuatilia stori hii...
Nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kazi nzuri hata jina la hadithi linajieleza vyema kuwa kweli ilikuwa kizungumkuti wacha nitie mkazo Senkyuu vele machi
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom