Mafisadi washika hatamu CCM
Monday, 17 August 2009 16:43
*Aundiwa fitna za kung'olewa
Na John Danieli, Dodoma
Majira
HALI ya kisiasa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imezidi kuwa tata, baada ya kundi linalodaiwa kuwa na mlengo wa 'kubeba' mafisadi, kutaka Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta awajibishwe kwa madai ya kukisumbua chama hicho kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya wazembe serikalini.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho (NEC) kinachoendelea hapa, Mjini Dodoma, zilieleza kwamba mara baada ya kuanza jana majira ya saa 12 jioni wajumbe waliopangwa walisimama mmoja mmoja na kueleza kwamba bila CCM kumwondoa kiongozi huyo wa Bunge, mambo ya kisiasa hususani hatima ya CCM katika uchaguzi mkuu ujao itakuwa mashakani.
Hivyo dawa pekee ni kumwondoa katika nafasi yake ya uspika na kumfukuza uanachama wa CCM hoja ambayo hata hivyo ilipingwa vikali na kundi la wajumbe linalopinga ufisadi, huku wakitaka kabla ya kiongozi huyo kuchukuliwa hatua, watuhumiwa wote wa ufisadi wakamatwe na wafukuzwe uanachama wa CCM kwanza.
"Hawa watu walijipanga wiki mbili zilizopita kabla ya NEC, walifanya vikao vyao, wakatenga mabilioni ya pesa........ (anamtaja mmoja wa wajumbe wa NEC, jina tunalihifadhi kwa sasa), akatumwa kwenda Zanzibar akagawa pesa kwa baadhi ya wajumbe wa NEC kutoka Zanzibar, sasa wamekuja kwenye kikao na ajenda moja tu, nayo ni kutaka kumg'oa Spika Sitta," kilisema chanzo chetu ndani ya NEC na kuongeza.
"Baada ya hapo watawashughulikia wafuasi wake wote wanaopinga ufisadi, lakini tunajua tatizo ni nini, tunatambua uongozi wa huyu spika Sitta umewabana na kuwakosesha amani, lakini tunasubiri uamuzi wa kikao, na mwenyekiti, lakini wakishindwa kuwadhibiti mafisadi hawa tumekwisha," kilisema chanzo hicho.
Habari zaidi zilieleza kwamba kundi hilo linaloaminika kudhaminiwa na watuhumiwa ufisadi ndani ya CCM, linaongozwa na mmoja wa Manaibu Waziri, Mwenyekiti wa CCM Mkoa na Katibu wake pamoja na wajumbe kadhaa kutoka Kanda ya Ziwa pamoja na Zanzibar.
Kutokana na ajenda hiyo kuzua mjadala mkali, jana siku nzima wajumbe wa NEC walishinda wakijadili ajenda moja tu ya hali ya kisiasa nchini huku mafisadi wakionekana kuzidi kujiimarisha zaidi ndani ya CCM
Baada ya mashambulizi kuongezeka zaidi kwa siku nzima dhidi ya Spika Sitta na wafuasi wake wanaopinga ufisadi, ilielezwa kuwa juhudi za baadhi ya wajumbe wanaofurahishwa na kasi ya Spika Sitta zilionekana kutokuzaa matunda hadi jana jioni kutokana na kundi hilo la mafisadi kuonesha dalili toka awali kutaka kuteka kikao cha NEC, kwa hoja zao ambazo kwa nje zilionekana kutaka kudai maslahi ya CCM, lakini kwa ndani zinaonekana kuipeleka CCM kaburini kama ilivyofanyika kwa Chama cha KANU nchini Kenya.
Ilielezwa kuwa licha ya Spika Sitta, kutakiwa kung'olewa kwenye wadhifa wake, pia Spika wa Baraza la Wawakilishi, Bw. Pandu Kificho, naye hakuweza kuepuka dhahama hiyo, baada ya wajumbe kadhaa kutaka naye awajibishwe kwa kung'olewa kwenye wadhifa wake kutokana na Baraza lake kutuhumiwa kumtukana Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali kwa ujumla pamoja na Bunge la Muungano.
"HIvyo ndivyo hali ilivyokuwa ndani ya NEC, hata sisi hatukutegemea. Wajumbe walimtaka Kificho naye ang'olewe kwa kuwa Baraza lilimtukana Waziri Mkuu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano na hata Bunge. Kama hali itaendelea hivi, ni wazi kwamba CCM inachungulia ilipo KANU kwa sasa, lakini yote hayo bado ni mchango wa wajumbe, tusubiri mamuzi ya kikao leo usiku (jana)," kilisema chanzo chetu ndani ya NEC.
Ilielezwa kwamba chanzo cha Spika Sitta kutaka kutolewa inatokana na itikadi yake kutokuyumba katika masuala mazito yanayohusu ufisadi kama vile Richmond, TRL, TICTS,na kukataliwa kwa mswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali.
Hali hiyo imeelezwa kufanya baadhi ya mawaziri kumchukia kwa kuwa kasi yake inawapa wakati mgumu bungeni. Jumla ya mawaziri 7, wametajwa kuwa wanahusika na kuungana na kundi la mafisadi kutaka kiongozi huyo ang'olewe.
"Bunge chini ya Spika Sitta linajadili maslahi ya watanzania wanaokadiriwa kuwa milioni 40 kwa sasa, anayezungumza kuwa Sitta anawasaliti CCM anajali maslahi ya kundi lake, watoto wake, marafiki zake na ndugu zake. Tunaelkea kufikia ndoto ya Mwalimu Nyerere, kuwa CCM ikiyumba nchi itayumba. NI wazi sasa ufisadsi unayumbisha CCM, kama hatutawang'oa nchi itayumba," alisema mmoja wa wajumbe wa NEC bila kufafanua.
Hadi tunakwenda mitamboni, kikao cha NEC kilikuwa bado kinaendelea japo wajumbe kadhaa walionesha kutoridhika na mwenendo wa kikao hicho.