Na Romana Mallya
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Laurence Masha amesema suala la Spika wa Bunge, Samuel Sitta, la kuomba kuongezewa ulinzi bado wanalifanyia kazi.
Masha alisema jana kuwa, kwa sasa wanachokifanya ni kujua sababu za Sitta kuomba ulinzi na kama zitaonekana zina uzito wa kuongezewa ulinzi watafanya hivyo.
Alisema kwa kawaida viongozi wote hupewa ulinzi na kwamba hakuna hata siku moja viongozi hao walishaachwa kulindwa.
Alisema ikiwa Sitta aliomba ulinzi wa ziada, wao hawana pingamizi lakini lazima wapate maelezo ya kutosha kutoka kwake na wayafanyie kazi ili kujua kama kuna sababu za kupatiwa ulinzi huo.
Sitta alitoa ombi hilo bungeni Alhamis wiki iliyopita kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Alisema kuwa ulinzi alio nao haumtoshi kutokana na kuadamwa na wabaya wake kwa njia mbalimbali, zikiwemo za kumchafua kupitia katika mitandao.
Aidha, Jumapili ya wiki hii, Sitta akizungumza na Nipashe alisema kuwa, alitakiwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma na Usalama wa Taifa wa mkoa huo kupelekea maelezo hayo.
Chanzo: NIPASHE