SONGWE: Serikali yaingilia tuhuma za wauguzi kusababisha kifo cha kichanga kwa uzembe

JanguKamaJangu

JF-Expert Member
Feb 7, 2022
2,309
5,464
Wauguzi katika Kituo cha Afya Tunduma, Wilayani Momba wanatuhumiwa kusababisha kifo cha mtoto aliyezaliwa kituoni hapo, huku mzazi (jina limehifadhiwa) Mkazi wa Kata ya Uwanjani, Tunduma akidai mtoto huyo alikutwa na jereha kichwani licha ya kujifungua salama.

Taarifa zilizopatikana kituoni hapo na baadaye kuthibitishwa na Bibi wa kichanga kilichofariki, Ness Mwazembe, Mkazi wa Kata ya Uwanjani, alisema mjukuu wake alifariki Mei 5, 2022 mchana huku akiwa na jeraha na uvimbe kichwani.

Anasema mwanaye alijifungua siku ya Mei 4, 2022 saa sita usiku, lakini kichanga hakikulia kama ilivyo kawaida ndipo wauguzi waliokuwa zamu walikichukua kichanga hicho na kukipeleka chumba cha 'Oksijeni' hadi asubuhi walipokabidhiwa mtoto akiwa analia muda wote.

Kwa upande wake mama wa mtoto aliyefariki akizungumza kwa uchungu na hisia kali huku akiomba jina lake lisiandikwe gazetini, alisema wakati akihangaika kwa uchungu hakupatiwa huduma nzuri.

Anasema wauguzi waliomhudumia walikuwa ni wanafunzi ambao hawakutoa huduma nzuri kwake licha ya kuwaita mara kwa mara baada ya mtoto kuanza kutoka.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Omary Mgumba amethibitisha kupokea taarifa za malalamiko hayo na tayari amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Momba, Fakh Lulandala kuunda timu ya kuchunguza tukio hilo.

"Hili sio tukio la kwanza wala la pili katika Hospitali ya Mji Tunduma, Serikali hatupuuzi malalamiko ya wananchi ambao ndio tunawaongoza, baada ya uchunguzi utakaofanyika tutatoa majibu ya kifo cha mtoto huyo ili wahusika kama walifanya ni uzembe wachukuliwe sheria," alisema.

Aidha, Mgumba aliwataka watumishi wa Serikali hasa wahudumu wa afya kutoa huduma nzuri na lugha nzuri pindi wanapotoa huduma za kitabibu kwa wananchi.


Source: Majira
 
Back
Top Bottom