Dk. Slaa akizungumza kwa uchungu alisema mauaji ya Songea yalitokana na uzembe wa hali ya juu wa viongozi wa serikali na vyombo vya dola ngazi ya wilaya na Mkoa wa Ruvuma.
"Napenda kutoa kauli juu ya mauaji dhidi ya raia yaliyofanywa na Jeshi la Polisi huko Songea. Kwa taarifa nilizonazo, mauaji yale yametokea kwa sababu ya uzembe wa hali ya juu na ufinyu tu wa akili ya viongozi, akiwamo mkuu wa Mkoa na polisi wale. Hivi unawaambiaje raia wenye uchungu na vifo vya wananchi wenzao, waliojikusanya na kuamua kuandamana kudai haki, eti wachague kiongozi wa kuonana na mkuu wa mkoa," alisema.
Aliitaka serikali kuunda tume huru ya kuchunguza mauaji hayo ya Songea na kudai kuwa hakuna uhalali wowote wa viongozi wa serikali wa mkoa ambao ni watuhumiwa wa mauaji hayo kuunda chombo cha kuchunguza.
"Tunawapongeza wananchi na hasa vijana wa Songea kwa kuandamana kudai haki. Tunataka ufanyike uchunguzi huru juu ya mauaji hayo, yatakayoihusisha mahakama (Korona) na mkuu wa mkoa na polisi hawana uhalali wa kuunda tume za kuchunguza kwani wao pia ni watuhumiwa katika tukio hilo," alisema.
Katibu mkuu huyo wa CHADEMA alilaani tukio la juzi usiku, ambapo polisi katika mji wa Tunduma wanadaiwa kushusha bendera za chama hicho katika maeneo mbalimbali ya mji huo.
Alisema kitendo hicho ni uchokozi tosha kwa CHADEMA na kimelenga kuleta fujo nyingine zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani.
"Niliwasiliana na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, pia mkuu wa mkoa, niliwaambia mimi sipendi kugombana nao kwa masuala ya hovyo kama hayo, tupo kwa mujibu wa sheria, bendera zetu zinatokana na kodi za Watanzania, wakasema eti zingine ziko sokoni, nikawauliza za CCM huwa zinawekwa wapi?
"Watu hawana maji, hawana zahanati, elimu inashuka, mkuu wa wilaya hajawahi kuamuka usiku, lakini kwenye kushusha bendera za CHADEMA wanaamka usiku wa manane," alisema.
DR. SLAA ni zaidi ya Rais kwa kazi azitendazo. I'm very impressed with his bolded quotes.