Simulizi ya kweli: Mpaka kieleweke

Simulizi ya kweli: Mpaka kieleweke

Story: Mpaka Kieleweke
Mtunzi: Nira Saire
SEHEMU YA 16

Ilipoishia...

"wanyama wapo ila hutumika kwa ruhusa ya Magugi, mtunzaji wa wanyama wale ni bwana mmoja katili sana ambaye ni mtiifu kwa Magugi kama walivyo watu wote wa Muifufu" alielezea bwana yule!..
nikachukua ule mkoba k niliopewa na Mnaro na kuchukua ule mkate ambao alinielezea kuwa endapo ningemlisha mtu yeyote basi angefanya chochote ambacho ningemwambia! nikakata kidogo na kumkabidhi yule bwana.. "hakikisha mtu huyo anakula mkate huu, kisha tunaweza kumtuma na hakuna mtu ambaye atamuelezea juu ya hilo" bwana yule akapokea kipande kile bila ubishi wala maswali, kisha akatoka akinitaka kupumzika, kwaajili ya safari ya usiku!..
nilibaki nikiwa na wasiwasi mwingi kwakuwa sikuwa nimejaribu kutumia mbinu ile ambayo alinifundisha Mnaro ambaye yeye mwenyewe hakuwa na uhakika kama bado huku Muifufu kuko kama ambavyo alipaacha.. vipi kama huyo bwana anayepelekewa mkate ule atakuwa ana nguvu ya kuzidi uchawi ule na hivyo kugundua dhamira yetu?! niliwaza na kubaki kuomba tu mambo yaende kama ambavyo tulihitaji....

Endelea

nilibaki pale ndani nikifikiria mengi na katikati ya mawazo nikakumbuka adhma kuu ya kuwepo Muifufu, mke wangu kipenzi!.. sijui atakuwa wapi Samia wangu!, niliwaza na kujikuta nikitembea kutoka nnje ya eneo lile bila ya kujua nilikuwa nakwenda wapi, nikajikuta nafuata njia ileile ambayo ilinileta katika nyumba ile nikimfuatilia Sauda, nadhani ni kutokana na kutopajua pengine popote!..
nilifika mpaka kwenye uwanja ambao tulikuwepo masaa machache yaliyopita lakini kitu cha ajabu ni kuwa lile jumba la kifahari ambalo ndio makazi ya Magugi halikuwepo tena pale ambapo lilikuwepo mwanzo! uwanja ulikuwa mtupu, nilistaajabishwa kwa muda mfupi juu ya kutokuwepo kwa jumba lile, nikafikia kudhani kuwa pengine nilikuja eneo tofauti lakini nikajiridhisha kuwa sikuwa nimepotea, ni penyewe haswa ila uchawi ulikuwa umefanyika tayari bila shaka ni uchawi wa aina ileile ambao uliuficha mji wa Muifufu ukakosa kuonekana duniani ikiwa upo humohumo!.. Nikaamua kuwa ni bora nirudi tu kwenye yale makazi yangu ya muda kuliko kuwepo kwenye mazingira yale yasiyoeleweka na mwisho wake kunasa mikononi mwa Magugi kirahisi!...
muda huu kagiza kalikuwa kameanza kuingia, hali ya Muifufu ilikuwa ni tulivu mno, hakukuwa na watu wengi kama iwavyo dunia ya kawaida hasa mida hii ya jioni kila mtu akirudi nyumbani kutoka kwenye shughuli mbalimbali!...
nilipokaribia nyumba ile ambayo ndipo nilipokuwa nimewekewa makazi ya muda niliona kundi kubwa la watu wakiwa wamekusanyika pale! lilikuwa ni kundi kubwa kama ambalo lilikuwepo pale kwa Magugi wakati wakinitafuta!. Nikasogea kwa taadhari sana na kugundua kuwa nyumba ile ambayo nilifikia ilikuwa ikiwaka moto! kwa mbali pia niliona watu wawili wakiwa wamefungwa kwenye miti ambayo bila shaka ilichimbiwa pale chini kwa shughuli ile kwani haikuwepo mwanzo!..
pembeni ya watu wale kulikuwa na jitu lenye misuli mikubwa mno likimchapa mmoja wa watu wale kwa fimbo za mfululizo kisha lilipumzika na kufanya mzungumzo kwa muda mfupi na baadae likamchapa yule mtu mwingine na kufanyanaye mazungumzo pia! sikuweza kuwatambua watu wale ambao walikuwa kwenye mateso yale makali lakini hisia ziliniambia kuwa alikuwa bwana yule ambaye Sauda aliniacha kwake, bwana Mkude!.. Nikafikiria kwenda kujumuika kwenye kundi lile ili kujiridhisha juu ya watu wale ni akina nani na kujua nini hasa chanzo cha mateso yale kwa watu wale!.
Lakini itakuwaje kama tayari wanaijua sura yangu na kufika kwangu pale ikawa kujikamatisha? je kama watu wale wanateswa ili kuonesha nilipo na hawaoneshi kwakuwa hawajui nilipo kwenda kwangu si itakuwa pona yao na matatizo kwangu?! nilijiuliza na kufikia uamuzi wa kujisogeza kwa taadhari mpaka kwenye kichaka kidogo ambacho kilikuwa karibu zaidi na umati ule!, angalau kutokea pale niliweza kushuhudia na kusikia sauti za juu ya kilichokuwa kinaendelea pale!..
"sogezeni hapa zile kuni" nilisikia akiagiza bwana yule mwenye kutoa adhabu na watu ambao walikuwa wamevaa sare wakakimbia na kusogeza mzigo mkubwa wa kuni miguuni mwa watu wale!..
"sheria za Muifufu ni lazima ziheshimiwe, na yeyote mwenye kujaribu kuzivunja adhabu yake ni kifo, nipe moto" alisema mtu yule kisha akaagiza apewe moto na akapewa ukuni uliokuwa ukiwaka moto mkubwa kiasi cha kutoa mwanga naye akakiangushia kwenye kuni zile ambazo zilianza kushika moto kwa kasi na hatimaya kufanya moto mkubwa ambao ulianza kuwaunguza watu wale ambao niliwagundua kuwa walikuwa wale wenyeji wangu huku umati ule ukishangilia tukio lile!...
kwa upande wangu roho iliniuma sana... niliumia kwakuwa sikuwahi kushuhudia ukatili kama ambao ulitendeka pale, lakini pia niliumia mno kwakuwa niliona waziwazi kuharibika kwa mambo ambayo yalikuwa yamepangwa hapo mwanzo!..
nilibaki pale nikishuhudia watu wale wakitapatapa katikati ya moto ule mkali mpaka wakatulia na miili yao kuteketea motoni "nadhani mmeshudia madhara ya kuwa adui wa Muifufu" alianza kuongea tena mtu yule na washangiliaji wakawa kimya ghafla kumsikiliza.. "mtukufu Magugi ameahidi huyo mtu ni lazima apatikane na kuanguka kwakwe kutakwenda na wafadhili wake wote ndani ya Muifufu pamoja na familia zao! tawanyikeni mkaendelee na shughuli zenu" alimaliza bwana yule na watu wakaanza kutawanyika wakionekana kufurahishwa na jambo ambalo limetokea!
nilibaki pale kichakani nikiwa na hofu kubwa, mpaka kufikia hapo sikuwa na muongozo tena, hata kutoka kwenye kichaka kile niliogopa nikihofia kuonekana na kupoteza maisha kama ambavyo imetokea kwa wenyeji wangu wale muda mfupi uliopita! lakini mara nilipata ujasiri nikasimama na kuanza kutembea kuelekea ambako sikuwa nikipajua, njiani nilipishana na watu wachache ila kila mmoja alikuwa na mambo yake nikaenda mpaka eneo ambalo lilionekana kuwa ni eneo la mashamba na kuanza kurandaranda kwenye mashamba ya watu bila mpango maalumu!..
nikiwa katikati ya shamba la mahindi nilihisi kama kulikuwa na minong'ono mbele kidogo ya ambapo nilikuwepo, nikaamua kusogea ili kujua alikuwa nani na alikuwa akifanya nini mashambani usiku ule "hakikisheni tunampata kabla yao na anavuka mlima Kalingisi kabla hakujakucha, ardhi hii sio salama kwake" alikuwa akiongea mwanamke ambaye nilimtambua kuwa alikuwa Sauda na vijana watatu ambao mavazi yao yalifanana na watu wale ambao waliagizwa kuleta kuni ili bwana Mkude na mkewe wateketezwe kwa moto!..
sikuona sababu ya kuendelea kujificha ikiwa watu wale walikuwa wakipanga kuhusu usalama wangu. Nikajitokeza mbele yao na wote wakashituka wakidhani wamefumaniwa katika mbinu zao lakini baada ya kunitambua Sauda akatabasamu "umewezaje kujua kama tuko hapa?" aliuliza swali ambalo lilinifanya na mimi kujiuliza ni kwanini sikwenda pengine popote bali pale ambapo ndipo hasa walikuwepo watu pekee ambao ni salama kwangu, tukianacha na hili, niliwezaje kuondoka pale nyumbani kwa Mkude huko nyuma watu wa Magugi wakafika na kuteketeza nyumba? bila shaka ni kazi ya Mnaro!. Nilikumbuka kuwa aliahidi kuniongoza akisema mimi ni silaha yake! nafikiri ulikuwa muongozo wake..
"hapa sio salama tena kwako, inakubidi kuondoka usiku huu, Mkude alikwenda kujaribu kukupatia usafiri kama ambavyo mlikuwa mmekubaliana lakini alikuta tayari wamegundua juu ya yeye kukuhifadhi nyumbani kwake ikawa chanzo cha kifo chake, afadhali hawakukukuta walipokwenda kusachi kwa Mkude sote tulijua tumekwisha" alielezea Sauda nikiwa kimya kuwasikiliza wao toka kuwasili kwangu eneo lile "sasa jamani mimi naondoka ila hakikisheni mnampa kila kitu kama ambavyo nimewaelekeza na kisha mumpeleke mpaka kwenye mlango wa mlima Kalingisi, kisha nyie mrudi"aliagiza Sauda nikaondoka nikiongozana na watu wale, tukapitia kwenye kijumba cha ajabu ambacho hakikuonekana kama kilikuwa kikitumika, tukachukua furushi fulani ambalo sikujua lilikuwa na nini kisha safari ikaendelea!..
tulikwenda mpaka tukaufikia mlima ule ambao ulikuwa mbali kidogo kutoka ambapo mji ulikuwepo, tukakaa na bwana ambaye alikuwa amebeba furushi akalifungua na kutoa mfuko na kunikabidhi "hicho ni chakula, kula upate nguvu kabla ya kuanza kazi ya kupanda mlima! ni mbali sana" alisema bwana yule huku akinipa na kibuyu ambacho kilikuwa na maziwa!..
nikala harakaharaka chakula kile ambacho kilikuwa nyama ya kuku aliyebanikwa, nikashushia na yale maziwa na kujiona kuwa nilikuwa vizuri!..
"humu kuna nguo, maji ya kunywa na nyama ya ng'ombe iliyokaushwa, itakufaa safarini na utakapokuwa nyuma ya mlima maana huko ni kukame na kuna njaa sana! alielezea bwana yule nami nikachagua nguo na kuvaa, maana muda wote huu nilikuwa uchi, kisha nikabeba furushi langu na kuanza safari nikiacha watu wale wakirudi Muifufu..

kazi ya kupanda mlima ule ilikuwa ngumu sana kama ambavyo nilitegemea, hasa kutokana na kutokuwa na njia za kupita huku kilima kile kikiwa na vichaka ambavyo nilipaswa kuvipenya mara kwa mara ili kusonga mbele. Ugumu pia ulichangiwa na giza ambapo mara kadhaa nili jikwaa na kujeruhiwa na miti ambayo ilikuwa na miba mikali sana kwenye vichaka vile vidogovidogo! nikawa nikikazana kupanda huku nikipumzika na kupata maji ya kunywa kila ambapo nilipata sehemu ambayo haikuwa na muinuko mkubwa sana..
Safari yangu ikawa hivyo huku nikijitahidi na kujiambia kuwa sikupaswa kukata tamaa! masaa yakakatika katika hali ile na hatimaye nikawa nimefika katika kilele cha mlima ule ambao ulionekana wa mbele lakini hatua kama kumi kutoka nilipokuwa niliona kilima kingine cha kupanda ambacho kilikuwa kimeungana na hiki na kuwa kama kilima kimoja!..
baada ya kunywa maji na kupumzika kidogo nikaamua kukikabili kilima kile cha mbele yangu nikiamini ilikuwa kazi ndogo tu kwani hakikuwa kirefu kama ambavyo kilikuwa kile ambacho nilikuwa nimekimaliza. Nikaianza kazi ya kupanda mlima ule wa pili kwa kasi, haikuwa kazi rahisi pia kwani ulikuwa mlima huu haukuwa hata ni vichaka ambavyo vingeniwezesha kushika kama ilivyokuwa kwa ule wa awali, hivyo mara kadhaa nilinusurika kuporomoka nikajitahidi kuongeza umakini na kusonga mbele! safari ikaendelea kwa masaa mengi sana lakini sikufika juu!..
pamoja na kutokuwa na saa nilijua fika kuwa ni masaa mengi yamepita lakini kwanini nilikuwa sifiki juu! nikageuka na kuangalia chini nilikotoka, sikuridhishwa na umbali ambao nilikuwa nimepanda!. Ilikuwa ni kama ambaye nimepoteza muda mwingi bila kufanya jambo lenye manufaa!.. nikiwa bado nimegeuka nikiangalia chini na kushangaa kazi ambayo nilikuwa nimeifanya ambayo haikufanana hata kidogo na matarajio yangu, nikashangaa nimesukumwa na kuporomoka mpaka chini nikatua na makalio huku nikipatwa na maumivu makali sana!...
ghafla nikasikia sauti za vicheko huku wenye kucheka vichoko hivyo wakisogea nilipo...

usikose sehemu ya kumi na saba!..

mawasiliano:
+255653686008
nirasaire@gmail.com
facebook.com/nira.saire
@nira_saire (instagram)
 
Haitoshi kuniaminisha kwa maneno kua wew sio mchawi au hujawahi kua mchawi kwa hadithi hii.... Yumkini kama sio kwa bibi basi ni kwa shangazi ambaye ni mbobezi na nguli wa uchawi ulipopata taarifa hizi nyeti za wachawi. Kuendesha nyau, kupita ukutani, kutembea uchi na bila kuonekana, kuamini na kitu kuwa ,vyote hivyo vinashuhudia wewe u mzoefu wa mambo hizi...,,, Though very interesting...,,


Na hakika mwisho wa hii hadithi tutakua tumeiva kwa kuloga..!!
hahahaha hayo yote ni mambo ya kufikirika, sidhani kama ndivyo wachawi wanavyofanya kweli
 
Back
Top Bottom