Simulizi: Soka Lilivyonikutanisha Na Shetani

Simulizi: Soka Lilivyonikutanisha Na Shetani

Sehemu ya 61

Pamoja na mateso aliyoniachia bado sikuweza kabisa kumtoa nafsini mwangu, sikuwa na funguo wa kumwondoa mwanamke huyo ndani ya moyo wangu. Sura nzuri ya chotara huyo, iliniganda kama gundi.

Ningefanya nini mimi zaidi ya kulipigania penzi langu.
Asubuhi ya siku ya pili, niliamkia mazoezini. Kama kawaida nilijituma na kupambana, nilizidi kumfurahisha kocha mzungu.

Baada ya mazoezi kumalizika meneja alitutangaziwa wachezaji jambo jipya.
Ilikuwa ni kuhusu maisha ya wachezaji wa timu hiyo. Alisema klabu ilikuwa imeazimia kutuweka kambi vijana wote.
Tulielezwa kwamba kuanzia kesho, wachezaji wote wa timu ya Mzizima tungeweka kambi sehemu moja hadi mwisho wa msimu.

Maana yake ni kwamba tungekuwa tunaishi pamoja. Wote kama familia moja. Muda wote hadi msimu utakapo malizika.
“Hii latiba itaanza kesho asubuhi, hivyo kila mchezaji, kesho, achukue kila kitu chake muhimu aje nacho klabuni. Wote tutakutania hapo na kwenda kwenye apartment iliyopangwa.

Katika kambi kutakuwa na taratibu mbalimbali ambazo tutawatangazieni. Lakini moja ya kanuni kubwa ni wachezaji kutotoka kwenda sehemu yoyote bila luksa maalumu,” meneja wa timu aliongea.

Nilihisi tumbo lote linachemka ndani kwa ndani. Ilikuwa ni lazima nishugulike na mambo yangu binafsi haraka iwezekanavyo.

Sikujua kwa nini latiba hiyo mpya ilikuja ghafla vile. Hata hivyo, wakati tupo katika vyumba vya kubadirishia nguo ili kila mchezaji arudi kwakwe ama makwao. Kuna minong’ono ikazuka, minong’ono hiyo ndiyo ikanipa jibu la awali. Juu ya kambi kuitishwa ghafla vile.

“Angalau watu tukaishi kambini. wengine walikuwa wanapata fursa ya kwenda kwa waganga kuroga wenzao ili wavunjike,” mchezaji mmoja aliropoka.

Nilitetemeka. Sikujua kauli hiyo kama ilinilenga mimi ama jamaa alijiropokea tu.
Watu wakacheka. Wengine kama wawili wakashadadia.

“Kweli kabisa.” Mwingine akasema: “Ila dawa ya moto ni moto. Ukirogwa na wewe roga.” Jasho jembamba lilinivuja makwapani. nilitamani kujua wale jamaa walijuaje kama kuna watu katika timu wanakwenda kwa waganga?
 
Sehemu ya 62

Nikaendelea kujiuliza.
Inamaana hata huku kuitishwa kwa kambi ni kutokana na sababu hiyo? Je viongozi wa timu nao wanatambua juu ya suala la wachezaji kurogana?

Kama mambo yote yapo hadhalani je wamekwisha nitambua? Na ni nani ametoboa siri hiyo? Ni cholo? Hapana... Sasa ni nani?

Maswali yote hayo nilijiuliza bila kujua nitapata wapi majibu.

SIKU hiyo nilirudi nyumbani nikiwa nimefadhaika, kitendo cha timu yangu kuwa na fikra za kichawi, tena tukishutumiana sisi kwa sisi wachezaji, ilinifanya nikose amani ya roho.

Jioni hiyo nilizungumza na Cholo kama ni yeye aliyewatonya wachezaji wenzetu juu ya urozi nilioufanya kwa Felix Kisu:
“Hapana. Sijamwambia mtu yeyote jambo hilo. Unajua siwezi kufanya kitu cha namna hiyo Ajibu,” Cholo alinijibu.
“Niliona nyuso zao Cholo. Jamaa wanaonekana kunisema chini chini.

Nadhani wananihisi mimi.”
“Mambo haya ni kawaida kwenye mpira Ajibu. Wewe pambana na mambo yako, hao achana nao.”

Pamoja na maneno ya Cholo lakini bado nafsi yangu ilikuwa ikijisikia vibaya. Ni kweli nilikuwa nimemroga Felix na ni kweli kabisa, nilikuwa nimetokea kuwa muumini sana wa mambo ya kishirikina, ila nilipenda mambo hayo yawe siri.
Usiku ulipoingia niliandaa vitu vyangu vizuri ili kesho asubuhi niwe tayari kwa kuamkia kambini kama ambavyo uongozi ulikwisha amua.

Katikati ya usiku wa siku hiyo, mauzauza yakanikumba. Ilikuwa ni majira ya saa saba za usiku kama sikosei. Nilijiwa na kitu kama ndoto. Nilikuwa naota, eti nipo kwenye uwanja wa mpira, nilikuwa na baadhi ya wachezaji wenzangu ambao tulikuwa kwenye mazoezi ya kawaida tu.
 
Sehemu ya 63

Ghafla nikamwona ng’ombe mwenye pembe ndefu alikuwa akinijia kwa kasi. Kimwonekano ni kama alikuwa ng’ombe kichaa, alikuwa anakuja kwa lengo la kunishambulia.

Alikimbiza huku ameinamisha kichwa chini, pembe yake iliyochongoka ikitishia uhai wa maisha yangu. Nilitimua mbio kumkimbia mnyama huyo.

Wakati tukio hilo linatokea, wachezaji wenzangu wao waliendelea na mazoezi tu, yanii ilikuwa ni kama vile hawakumuona yule ng’ombe. Wala hawakuwa wanajali taharuki yangu.

Mbio zangu hazikufua dafu mbele ya mnyama huyo. Kwa kasi ya ajabu nilipamiwa na dubwasha hilo likanichoma na pembe yake kwenye kifua changu.
Ghaflaa!!....

Nilishtuka kutoka katika usingizi. Ilikuwa ni ndoto ya kutisha. Jasho lilikuwa linanitoka. Ndani ya sekunde hiyo hiyo, nilihisi maumivu makali sana ya ndani kwa ndani kwenye kifua.

Nilipojaribu kuketi kitako kitandani, nilishindwa. Maumivu yalikuwa makali mno kifuani. Akili ilinizunguka. Inakuwaje shambulio la ndotoni liwe kwenye uhalisia halisi. Sikutaka kujiongopea kwamba nilikuwa sifanyiwi mambo ya kishirikina na mbaya wangu Felix Kisu.

Nilipiga kelele kumwita Cholo aliyekuwa chumbani kwakwe anakoroma tu. Hata hivyo, muda ulizidi kuyoyoma Cholo hakutokea chumbani kuja kunipa msaada. Kifua kilizidi kuwaka moto. Yanii nilikuwa nahisi kama naunguzwa na chuma cha moto kwa ndani.

Nilijikaza na kunyanyuka kitandani. Nikawasha taa ya chumbani. Nikapiga hatua kulisogelea jokofu.Nikatoa maji baridi na kumimina kwenye bilauri. Nikanywa maji yale ya baridi nikidhani labda ningetuliza hali ile.

Hakuna nilichotibu.
Ajabu yale maji ilikuwa ni kama vile naongeza joto ndani ya kifua changu. Hali ilizidi kuwa mbaya, nikarudi kitandani na kujibwaga. Muda mchache badaye nikawa nahisi kama nabanwa mbavu kwa nguvu. Nikazidi kukoroma huku nikimwita Cholo. Jamaa hakuamka kabisa.

Sikujua nifanye nini usiku huo. Nilihisi kama ninakaribia kufa usiku huo wa saa saba. Wakati nagaagaa kitandani nikawa nahisi kama kuna uwepo wa kivuli cha mtu mule ndani kando ya kitanda.

Maumivu jumlisha hofu ya kivuli cha mtu ilikuwa ni patashika. Mtu huyo sikuweza kumwona vizuri kutokana na mkandamizo mkubwa wa maumivu niliyokuwa nayo.
 
Sehemu ya 64

Niliamini hakuwa Cholo, nilitambua walikuwa ni Felix Kisu.
Kwa kweli vita niliyokuwa napigana ilikuwa ngumu kwa upande wangu, na nilisalimu amri. Maji yalinifika shingoni.

Kwa mara ya kwanza katika maisha nikajutia kitendo cha kujiingiza kwenye vita ya kichawi katika mchezo wa soka dhidi ya watu nisio wajua barabara.

Nakumbuka nilibakia kwenye wakati mgumu kuanzia usiku ule wa saa saba hadi alfajiri. Mara nyingi Cholo alikuwa na desturi ya kudamka asubuhi sana kufanya ibada.

Hivyo alikuwa mara nyingi anapoamka lazima apite chumbani kwangu kuniamsha, wakati yeye anafanya ibada mimi nilikuwa naanza mazoezi mepesi.

Alipoingia ndani na kunikuta nipo kwenye hali tete, alichanganyikiwa mno.
“Ajibu una nini?” aliuliza uso wake ukisawijika kwa taharuki.
“Kifua...mbavu.” nilimjibu nikiwa dhofulhali.

“Hali hii imeanza saa ngapi?”
“Usiku.” Upesi Cholo alijitarayarisha kwa ajili ya kunipeleka Hospitali ya Palesitina.
Alipokuwa akifanya maandalizi ya kutafuta usafiri wa kunipeleka hospitali, mule ndani bado nilihisi uwepo wa kivuli cha mtu asiyeonekana.

Mbali na uwepo wa kivuli cha mtu, naeleza kulikuwa na uwepo wa mtu mule ndani ni kutokana na dalili moja nyingine. Kuna wakati nilikuwa nasikia kabisa mtu akihema, akivuta na kushusha pumzi, pia kuna muda nilikuwa nikisikia aidha chafya au kikohozi cha mtu.

Cholo aliporudi, alikuwa na dereva tax. Walisaidia na yule dereva na kunitoa kitandani, wakanibeba hadi ndani ya gari, safari ya kwenda Palesitina ikaanza.

Tukiwa kwenye gari nilitamani nimwambie Cholo juu ya kile ninachokidhani mimi. Sikuamini kabisa kama ugonjwa ule ulikuwa ni wa hospitalini kutokana na mazingira yake.

Lakini pia, nilitaka nimwambia hata kuhusu uwepo wa kivuli cha mtu ndani ya chumba changu. Lakini nilisita kutokana na uwepo wa yule dereva. Dakika kumi badaye, nilikuwa Palestina kwenye foleni ya kuonana na daktari. Cholo aliwasiliana na uongozi wa timu na kuwaeleza kila kitu kuhusu hali yangu.

“Anaendeleaje?”
Meneja wa timu alimuuliza simuni.
“Hali yake sio nzuri, tupo kwenye foleni ya kuonana na daktari.”
“Poleni sana, tutafika kumwona badaye.”
“Sawa.”
 
Sehemu ya 65

Nusu saa badaye, nilikuwa ndani ya ofisi ya daktari, alikuwa ni mwanamke mmoja wa makamo. Alionekana alikuwa na muda mrefu kwenye taalumu ya uganga.
“Tatizo nini?” aliniuliza. “Kifua kinauma.”
Nilipomjibu akaandika kwenye kitabu chake. Akaniuliza tena:

“Kinaumaje?”
“Ni kama kinawaka moto ndani kwa ndani.”
“Unamawazo?” alizidi kuniuliza. Nikatafakari kidogo swali lake kisha na mimi nikamuuliza.

“Kuna binadamu asiye na mawazo dokta?”
“Nina maanisha unamsongo wa mawazo kwenye maisha yako, hasa kwa siku za hivi karibuni?”

“Hapana.” Nilimjibu. Akaniuliza tena:
“Unafanya kazi gani?”
“Mimi ni mchezaji wa mpira.”
“Tatizo limeanza lini?”
“Usiku wa kuamkia leo.”
Akaendelea kuandika majibu yangu kwenye tabu lake la kumbukumbu.
“Kuna dawa nitakupa, zisipokusaidia rudi tena hapa. Sawa?”

“Sawa dokta.”
Aliniandikia tembe za vidonge fulani vitatu vya aina tofuati. Siwezi kabisa kusahau majina ya zile dawa. Tembe moja ilikuwa inaitwa Ampidox , nyingine inatwa Predistone pamoja na Panadol.

Nazikumbuka vizuri kabisa.
Tuliondoka na kurudi nyumbani tayari kwa kuanza dozi ya dawa hizo. Hali yangu ilikuwa bado ni tete, kila wakati nilikuwa nahisi maumivu makali na kifua kikitaka kulipuka kwa joto kali.

Tulipowasili, Cholo aliniacha sebuleni nipumzike, kisha yeye akaondoka na kwenda kuripoti klabuni. Nilichukua chupa ya maji safi na kumeza tembe hizo.

Ilikuwa ni kama baada ya dakika 20 baada ya kutumia vidonge hivyo... Nilipatwa na muamivu makali nashindwa hata kuyaelezea mfano wake.

Ndani ya mwili wangu kulikuwa ni kama vile kuna uji wa plastiki umemwagwa kwenye mifupa yangu. Nilikuwa nalia kama mtoto mdogo. Jasho lilikuwa linanichuruzika kama maji mwilini mwangu. Dunia ilikuwa inazunguka kwa kasi kama panga boi.

Ndani ya muda mchache nilipoteza fahamu, pumzi nazo zilikuwa zinakata kama utambi wa mwisho kwenye mshumaa unaovyoishilizia. Sasa dalili ya malaika mtoa roho ilikuwa waziwazi mbele yangu. Katika hali hiyo, nikawa nahisi kama kuna kundi la watu wameingia mule ndani kisha wamenizinguka.

Wakati fahamu zinanipotea kabisa, nikawa nahisi kama lile kundi la watu linaniangalia namna ninavyozama kwenye wingu la giza nene,
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom