SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya............28
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047
ILIPOISHIA...
"Bosi kuna tatizo tena tatizo kubwa, nimepewa taarifa na shushushu wetu kutoka ofisi za usalama wa Taifa kuwa wanampango wa kumkamata Felix mara tu Ndege aliyopanda itakapotua kesho asubuhi..."
Magnus alitoa macho mara baada ya kuipokea taarifa hiyo, kisha akaikunja sura yake mithiri ya mtu aliyeramba limao.
SASA ENDELEA...
Magnus alihisi kuchanganyikiwa, hakuwa na nguvu tena za kuendelea kuzungumza na mateka wake, akageuka haraka na kuondoka, wale wanawake pembeni yake,walinzi na yule msaidizi wake wa kazi wakamfuata nyuma.
"Mkuu atajibu maswali yenu kwa wakati mwingine, kwa sasa amepata dharula ndogo" Alisema yule mtangazaji ambaye awali ndio aliwaambia mateka wale wasogee.
Dayana, David pamoja na mateka wengine walirudi kwenye nafasi zao huku baadhi yao wakilalamika. Maswali aliyouliza yule mama msukuma yalikuwa ya muhimu mno. Kila mmoja alitamani kujua kwa nini ametekwa? Kwanini yuko ndani ya bonde lile? Nini hatima yake?. Lakini kwa bahati mbaya mambo yanaingiliana na kumfanya Magnus kushindwa kujibu maswali hayo.
Wakati huo mvua ilianza kunyesha, mateka hawakuwa na mahali pa kujificha zaidi ya kujibana kwenye kuta za bonde hilo. Hii ndiyo ilikuwa hali halisi ya maisha ya mateka wale mle bondeni. Mvua na jua vyote vilikuwa vyao.
"Felix ameanza safari saa ngapi kutoka Marekani?" Aliuliza Magnus wakati akipiga hatua kuingia ndani ya jengo moja kubwa.
"Kaanza safari leo saa kumi na moja alfajiri ambayo ni sawa na saa sita mchana huku kwetu" Alijibu yule msaidizi wake.
Baada ya kuingia ndani Magnus alikaa juu ya kiti chake kilichotengenezwa mithiri ya viti wanavyokaa wafalme.
"Katika vitu sipendi ni kapambana na Binadamu. Sipendi na sitaki, bado nini safari ndefu. Nahangaika usiku na mchana kutafuta namna ya kurudi ISRA alafu kirahisi tu mtu anafanya uzembe kunivurugia mipango yangu. Hebu kwanza niambie imekuwaje hadi Felix anatafutwa na polisi?"
"Mkuu kama utakumbuka miaka kadhaa iliyopita ulikuwa ukimfundisha Felix kuwa jasiri. Alikuwa akitoka mara kwa mara kwenda kuwaleta mateka kwa bahati mbaya alirekodiwa na kamera za CCTV" Yule msaidizi alieleza kwa ufupi.
"Ona, ni upuuzi mtupu. Inakuwaje arekodiwe na kamera? Hakuvaa helmet?. Mtoto mjinga sana huyu kwanza alivunja utaratibu akaanza kutafuta wanawake, akawa na mahusiano sijui na nani yule wanamwita, kile kisichana kinaitwa nani...!!"
"Tesha"
"Eeh! Huyu Tesa sijui Tesha. Bado najiuliza hizo kamera zilimnasa vipi, na mbona nizamani sana kwa nini iwe sasa?"
"Alivaa, lakini aliivua kabla ya kuingia ndani ya gari. Askari walianza kumtafuta kwa siri tangu kipindi hicho. Hadi leo ndio wamefanikiwa kujua alipo kwa bahati nzuri shushushu wetu akapata taarifa pia"
"Shezi kabisa, Naomba waite MG Family sasa hivi wambie nawahitaji" Magnus alitoa agizo
"Sawa napiga simu sasa hivi"
"Waambie wafanye haraka"
"Sawa mkuu".


Upande wa pili hospitali kule alipo Tesha na Mama yake David.
Tesha alionyesha kuchanganyikiwa mara baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Mina kuwa yupo pamoja na Kipenzi chake Felix ndani ya Ndege moja inayotoka nchini Marekani kuja Tanzania.
"Mwanangu nini shida? Uko sawa kweli?" Mama David alirudia tena swali lake.
"Ukweli siko sawa mama" Alijibu Tesha.
"Nini tatizo mwanangu?"
"Nitakweleza mama" Alijibu Tesha akihangaika kupiga simu kwa kaka yake Godfrey, simu iliita mara kadhaa ikapokelewa.
"Nambie Tesha, uko home?" Sauti ya Godfrey Ilisikika simuni akiuliza swali
"Sikia kaka nina shida kubwa hapa"
"Shida gani?"
"Ni kuhusu Felix...!"
"Ooh! Ushaanza na huyo Felix wako, haya kimetokea nini"
"Nitakweleza, kwa sasa naomba unisaidie kitu kimoja wasiliana na yule dada wa airport mulize ni ndege gani imeondoka majira ya saa sita kutoka Marekani, inakuja moja kwa moja Tanzania. Mulize pia itafika saa ngapi?"
"Dada gani huyo unamuongelea?"
"Si yule mpenzi wako anafanya kazi airport kaka jamani"
"Unaamanisha Khadija, mbona nilishaachana naye mda sana"
"Sasa kaka si unamuliza tu jamani kwani akiwa X wako tayari ni adui"
"Aah! Usirahisishe basi huwezi kujua mazingira gani tuliachana, anyway dakika kumi nakupa jibu"
"Kumi?"
"Eh! Tano basi" Alijibu Godfrey akakata simu.
Wakati huo pale walipo aliwafuata nesi mmoja akampa taarifa mama David kuwa daktari anataka kumuona.
Baadae alipewa ruhusu ya kutoka hospitali huku Tesha akiwa ndio msimamizi wa kila kitu. Tesha alikuwa anasubiri simu kwa hamu kutoka kwa kaka yake Godfrey, lakini hadi dakika 10 zinakwisha bado alikuwa hajampigia.
"Lakini mwanangu kwani David yeye yuko wapi?" Hatimae mama David aliuliza swali wakati wanatoka hospitali.
Tesha aliwaza haraka haraka amjibu nini, ilikuwa sio rahisi kumwambia moja kwa moja kuwa David ametekwa na watu wasiojulikana siku ya jana. Isitoshe hata polisi nao walifanya siri.
"Aah! David kuna kazi nimempatia Mama, amesafiri ameenda nje ya Dar, usijali nitakupeleka mwenyewe hadi nyumbani kwako" Tesha alidanganya.
Waliingia ndani ya gari la Tesha yeye pamoja na mdogo wake David yaani Tatu, safari kuelekea nyumbani kwa mama David ikaanza. Wakati huo Tesha alikuwa akiitazama simu yake mara kwa mara kuangalia kama kaka yake kamtumia hata ujumbe wa maandishi lakini bado Godfrey alikuwa kimya.


Upande wa pili ndani ya lile bonde, Dayana na David walionekana wamekaa na kujikunyata ukutani, wakati huo mvua ilipungua na sasa yalibaki manyunyu pekee ingawa baridi ilikuwa ni kali mno eneo hilo.
David alionekana kuwa na mawazo sana, aligeuka pembeni yake akamtazama Dayana akamuona anatetemeka mno kutoka na baridi kali.
David alimuonea huruma mno. Akamsogelea karibu kisha akazunguusha mkono wake nyuma ya mgongo wa Dayana akamlaza kifuani pake. Aliweza kuuhisi mwili wa Dayana namna ulivyokuwa ukitetemeka.
Kimya kilitawala kwa muda, mwisho Dayana akauvunja ukimya huo.
"Unawaza nini David? haupo sawa kabisa"
"Nawezaje kuwa sawa Dayana..."
"Ni sahihi lakini kuna wakati lazima ukubali matokeo"
"Sio kwamba sijakubali Dayana, lakini siwezi kuvumilia kuendelea kuwepo hapa. Siwezi kabisa, nakuapia sito maliza wiki humu ndani" Alisema David akimaanisha, Dayana akatabasamu huku akijiweka vizuri kwenye kifua cha David.
"Unajua nini Davi..."
"Nambie..."
"Sahau"
"Nisahau nini?"
"Namaanisha sahau kutoka humu huwezi David, na ukitaka kulazimisha sana utaishia kupoteza maisha. Naomba usifanye hivyo tafadhali sitaki nikupoteze na wewe" Alisema Dayana.
"Kwani nini cha ajabu cha kunizuia kutoka Dayana, kila tatizo lina ufumbuzi wake. Umemuona hata huyo mnaemwita Magnus anamapungufu kibao ndio maana ameondoka ghafula bila kusema kitu, inamaanisha hata yeye mnaemuona Mungu mtu kuna mambo yake hayaendi sawa, na nikwambie kitu Dayana... Ukitaka kumshinda adui yako tafuta udhaifu wake. Magnus anao udhaifu lazima anao" Alieleza David.
"Sasa huo udhaifu wa Magnus wewe utaujuaje, sikia David. Hata ukifanikiwa kutoka kwenye hili bonde bado huko nje tumezunguukwa na msitu wenye walinzi kibao hadi ufike ufukweni, na bado hata ukifika ufukweni utapata wapi usafiri wa majini kukutoa kwenye hichi kisiwa. David futa hilo wazo"
"Siwezi kufuta Dayana, mimi sio kama ninyi mnaokaa hapa na kusubiri miujiza ya Mwenyezi Mungu, hata maandiko yanasema jisaidie na mimi nitakusaidia" Alisema David.
Mara wote walishtushwa na sauti ya Zungu akifoka.
"Inamaana ninyi mmekaa mmekumbatiana hapo mmeacha kuni zimelowana tutaota moto gani usiku.."
Dayana na David walikurupuka na kugeuka.
"Kwa hiyo tungefanyaje sasa, tuzikumbatie hizo kuni zisilowane?" Dayana alijibu swali kwa swali. Wakawa wanatazamana na Zungu kwa macho makali yaliyojaa hasira lakini hawakuweza kustahimiri mwisho wote wakaangua kicheko.
Zungu alikimbia akitaka kumvaa Dayana, Dayana naye akainuka haraka na kuanza kukimbia. Wakaanza kukimbizana huku wakicheka kwa furaha, hawakujali tena yale manyunyu ya mvua.
Dayana hakufika mbali akateleza na kuanguka chini kwenye tope, Zungu alimfikia na kulala juu yake.
"Wewe ni wakunikazia macho mimi!!" Alisema Zungu huku akicheka.
"Sasa kama unauliza maswali ya hovyo nifanyaje" Dayana alijibu huku naye akicheka.
Sasa wote wakawa wamelala chali na kutazama juu angani huku wakionekana kuwa na furaha moyoni.
David aliwatazama naye akajikuta anatabasamu. Si David tu hata mateka wengine waliowaona Dayana na Zungu walijikuta wakitabasamu pia. Tabasamu lenye uchungu ndani yake.
Licha ya kuwa kwenye mazingira magumu lakini bado waliitafuta furaha na kuipa.


Haukupita muda mara walisikia muungurumo wa helikopta iliyokuwa angani ikiwasili kisiwani hapo.
Naam, walikuwa ni GM Family wakiwasili.
Je nini kitafuata?
GM Family ni watu gani?
Harakati za kumkamata Felix zinakwendaje?
Magnus na GM Family watafanya nini?
ITAENDELEA...
Simulizi ni shillingi 1,000/= lipia kwa mpesa namba 0756862047 jina saul au Airtel money namba 0788967317 jina saul kisha njoo WhatsApp inbox namba hizo hizo