SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya............31-32
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047
ILIPOISHIA...
"Dayana mbona kama hauko sawa" David aliuliza wakati wakipiga hatua kusonga mbele lilipo pango hilo.
"Huwezi kuamini David moyo wangu hauna amani kabisa, napata hisia mbaya sana. Sidhani kama huku tunakokwenda ni salama" Alisema Dayana.
SASA ENDELEA...
"Huo ndiyo uchawi sasa kama hutaki kwenda ni heri ukabaki sawa Dayana" Zungu alifoka akionekana kutofurahishwa kabisa na kauli ya Dayana.
"Jamani sasa kwani mimi kusema vile najisikia ni kosa?" Dayana alijitetea.
"Sawa lakini hakuna ambaye hana hisia mbaya hapa, kila mtu anaogopa ila tunafanya kwa sababu tumechoshwa na maisha ya humu bondeni"
"Oya! yaishe basi jamani tu-focus kwenye lengo, kwanza mnapiga kelele tu hapa" David aliingilia kati.
Waliendelea kutembea na kusonga mbele huku mwanga wa mwezi ukiwa ni msaada mkubwa kwao. Baada ya mwendo kama wa dakika saba hivi mwisho Zungu alisimama ghafula.
"Ni hapa, inabidi tupite kwenye huo uchochoro hapo mbele" Alisema Zungu akinyoosha kidole chake kuelekea kwenye ukuta wa bonde hilo mahali kulipokuwa na ufa mkubwa.
"Tunapita kwenye huo ufa?" Aliuliza Dayana.
"Ndiyo ila kuweni makini kuna shimo hapa mbele inabidi turuke kwanza..." Alisema Zungu akiwa ndio wa kwanza kuruka.
David alisimama na kulitazama lile shimo macho yake yakionekana kuwa na wasiwasi.
"Unaanza au nitangulie mimi?" Dayana alimuuliza mara baada ya kuona David ni kama anasita
"Aa..we..we anza tu" Alijibu David huku akijaribu kuficha wasiwasi aliokuwa nao.
Dayana akaruka hadi upande wa pili kule alipo Zungu. Sasa ikawa ni zamu ya David. Ajabu ni kwamba David alionekana kuogopa sana kiasi cha kuwashangaza Zungu na Dayana. Shimo halikuwa kubwa sana la kutisha hata mtoto mdogo wa miaka kumi akijitahidi sana anaweza kuruka lakini kwa David ilionekana kuwa mtihani mgumu.
"Oya acha utani basi ujue tunakusubiri wewe" Zungu aliongea akihisi labda David anawatania, mwisho japo kwa taabu sana David aliruka hadi upande wa pili, lakini alikuwa akihema sana huku mapigo yake ya moyo yakimuenda mbio isivyo kawaida akawa ameinama na kushikilia magoti yake. Mara baada ya David kuruka Zungu aliendelea na safari lakini Dayana alimfuata David akamshika mgongoni.
"Davii.. shida nini unaumwa?"
"Hapana niko poa" Alijibu David huku akiinuka, akavuta pumzi ndefu na kuitoa taratibu, kisha akampa ishara Dayana kuwa waendelee kwenda.
"Sitaki kuamini kama kuruka lile shimo ndio unahema kiasi hicho?"
"Aah! We acha tu, ni historia ndefu"
"Historia tena?" Aliuliza Dayana lakini wakakatisha mazungumzo yao mara baada ya kumfikia Zungu.
Sasa wakaanza kupenya kwenye ule uchochoro mahali ambapo kuta za bonde hilo zilikuwa zimeachana na kuacha ufa mkubwa. Walitembea kwa tahadhali kila mmoja akiwa makini asije kukanya kitu chochote cha kudhuru mwili.
Baada ya hatua kama arobaini hivi mara waliona pango kubwa mbele yeo. Pango liliokuwa na giza nene ndani yake.
"Ni hapa, hii ndiyo njia yenyewe David" Alisema Zungu. David akapiga hatua mbele akawa anaangalia kwa makini.
"Kwa hiyo tunatakiwa kulifuata uelekeo wa hili pango mpaka litakapoishia?"
"Ndiyo David"
"Vipi kuhusu hili giza, tutaonaje mbele tunapokwenda?"
"Mbele kuko salama, niliingia mchana, lakini hata hivyo kuna mwanga upo utatusaidia. Nilishaandaa kila kitu msijali. Subirini hapa" Alijibu Zungu, akapiga hatua kusogea mbele akaingia ndani zaidi kwenye lile pango, akawa haonekani kabisa kutokana na giza nene lililokuwepo mle ndani.
Dayana na David walibaki wamesimama pale nje ya pango wakimsubiri kiongozi wao Zungu aseme neno.
"Sio muoga kabisa huyu jamaa.." Alisema David.
"Inaonekana wazi harakati zake hazijaanza leo" Alijibu Dayana na mara hiyo walisikia sauti za mawe yakigongana mle pangoni. Haukupita muda wakaona mwanga wa moto. Zungu alikuwa amewasha moto kwenye nyasi na baadae akaweka kipande cha mti ambacho juu yake alifunga majani fulani mabichi lakini hushika moto na kuwaka kwa muda mrefu. Aliwasha kipande cha kwanza kisha cha pili.
"Njooni basi" Zungu aliita.
David na Dayana walisogea wakaingia mle pangoni. Zungu akampatia David kile kipande cha mti chenye moto juu yake, yeye akabaki na kile kipande kingine.
"Hizi ndio tochi zetu kwa leo, haya twendeni..." Alisema Zungu.
Safari ikaendelea. Vijana hawa watatu wakawa wanakatisha ndani ya pango lile la kutisha. Hii yote ikiwa ni Katika harakati za kupambana kuhakikisha wanajitioa kwenye mikono ya Magnus.
"Unajua nini David" Alisema Zungu
"Niambie kamanda"
"Natamani sana kama tutafanikiwa kwenye hili basi tuwatoe watu wote mle bondeni"
"Yeah! Ni kweli yaani umewaza kama mimi Zungu, kama tukifanikiwa basi tusiwaache wenzetu" David aliongezea.
"Mmh! Ndugu zangu vipi tena, yaani mambo ndio kwanza yaanza mshaanza kuweka mipango. Nyie ndio huwa mnapigia bajeti hela za kubeti hata kabla hamjashinda" alisema Dayana.
"Kwa hiyo umeona hapa tunabeti au sio?" Aliuliza Zungu kisha wote wakacheka kwa furaha. Licha ya kwamba walikuwa kwenye eneo la kutisha lakini hawakuacha kuleta utani wa hapa na pale na hii iliwasaidia sana kuwaondolea hofu.
Waliendelea kusonga mbele wakifuata uelekeo wa lile pango. Safari ilikuwa ni ndefu na ngumu mno huku ile miale ya moto waliyobeba ikiwasaidia kuwaangazia. Kwa bahati nzuri katika pango hilo hakukuwa na vitu vyovyote vyenye kutishia usalama wao kama Zungu alivyosema. Hali ilikuwa ni shwari kabisa. Sasa walianza kupanda juu kufuata uelekeo wa pango hilo.
"Tumeshavuka kule kwa Magnus hapa tunapanda ule mlima wenye walinzi kibao" Zungu alitoa maelezo.
"Dah! Hii ni hatari kweli kweli, imenikumbusha filamu ya kirikuu. Alipita kama hivi chini ya nyumba ya mchawi karaba" Alisema Dayana.
"Hahaha! Kwa hiyo Magnus ndio mchawi karaba mwenyewe tumepita chini ya nyumba yake au sio" Zungu akaongezea.
"Alafu kitu kingine hata kirikou alikuwa uchi kama sisi hivi" David naye akaongezea, wote wakacheka kwa sauti.
"Kaka kumbe na huwa unaangalia katuni?"
"Aah! Zungu kuna katuni nyingine nzuri hata mtu mzima unaweza kuangalia. Zipo nzuri kuliko hata muvi zenu za kibongo"
"Hahaha zile muvi ni hatari lakini salama"
Baada ya kupandisha kwa zaidi ya dakika tatu hatimae pango hilo likawa tambalale tena. Zungu, David na Dayana wakazidi kusonga mbele.
"haya tumefika ndugu zangu" Hatimae Zungu aliongea na kusimama, wote wakasimama.
"Mnaona lile jiwe pale mbele, sasa chini ya lile jiwe ndio kuna ile barabara niliyowambia. Ni barabara inayotoka ufukweni mwa bahari hadi kule kwenye majengo ya Magnus lakini imepita chini ya mlima huu" Alieleza Zungu
Baada ya hapo wote walisogea hadi kwenye lile jiwe analolisema Zungu. Kwa pamoja walisaidiana kuliinua lile jiwe waliweka pembeni.
Amini usiamini chini ya lile jiwe kulikuwa na uwazi mkubwa uwazi ambao chini yake ilionekana barabara inayokatiza chini ya mlima huo. Ilikuwa ni ile ile barabara ambayo hutumika kuwaleta mateka wanaoshushwa na meli kuwaingiza ndani ya himaya ya Magnus.
David, Dayana na Zungu waliinama kuchungulia chini wakishuhudia mafanikio makubwa waliyoyapa hadi kufika eneo hilo. Katika kuta za barabara hiyo kulikuwa na miale ya moto pembeni hivyo ilikuwa inaoneka vizuri.
"Inatakiwa tushuke hapo chini tutafuata hiyo barabara mpaka tutakapofika ufukweni" Alieleza Zungu.
"Sasa tunashukaje hapa?" Aliuliza Dayana
"Tutatumia kamba ipo niliiandaa" Alijibu Zungu huku akianza kutafuta sehemu aliyoihifadhi kamba hiyo. Dayana naye akasimama kumsaidia.
"Uliitoa wapi hiyo kamba?" Dayana aliuliza swali lingine lakini kabla Zungu hajajibu mara ghafula wote wawili walishangaa kumuona David anasimama taratibu huku macho yake yakionekana kuwa na wasiwasi mwingi. Ni hali ileile kama iliyomkuta wakati ule wanaruka juu ya shimo muda mfupi uliopita. Sasa kwa mara nyingine tena baada ya David kutazama chini ilipo ile barabara anapatwa na kizunguzungu cha ajabu akaanza kurudi nyuma taratibu huku akiyumbayumba.
Ilikuwa ni hatari kubwa kwani alikokuwa anaelekea kudondokea ndipo kuna ule uwazi(shimo).
Zungu hakutaka kujiuliza mara mbili mbili alikimbia haraka na kwenda kumsukuma David pembeni. Huu ulikuwa ni msaada tosha kwa David kwani alimbadilishia uelekeo David akaanguka pembeni badala ya kudondokea ulipo ule uwazi. Lakini wakati Zungu akifanya hivyo kwa bahati mbaya na yeye akateleza na kuangukia moja kwa moja kwenye ule uwazi huku miguu ndiyo ikitangulia kwenda chini. Licha ya kujitahidi kujizuia lakini ilikuwa ni ngumu kwani tayari alishakosa balance.
Sasa Zungu akawa ameshikilia pembeni kwenye kingo za ule uwazi lakini tayari mwili wake wote ulikuwa umetoka, akawa anabembea kutumia mikono yake. Laiti kama kungekuwa na mtu kule chini barabarani angeweza kumuona.
Hadi dakika hii Dayana alikuwa katika hali ya mshtuko mkubwa mara baada ya kushuhudia tukio hilo la David kutaka kuanguka lakini Zungu anamsaidia mwisho na yeye anateleza na kuangukia shimoni kwenye ule uwazi.
Dayana aliiona mikono ya Zungu akining'inia huku akipambana kupanda juu, kwa bahati mbaya mikono yake ilikuwa ikiteleza kutokana na hali ya unyevu mahali pale.
Zungu alihitaji msaada, tena msaada wa haraka sana la sivyo angeangukia kule chini barabarani jambo ambalo lilikuwa ni hatari kwa usalama wake.
Wakati Dayana anakimbia haraka ili awahi kuishika mikono ya Zungu tayari alikuwa amechelewa kwani ndio kwanza mikono ya Zungu ilikuwa ikiteleza na kuishia.
"Zuuuuunguuu" Dayana aliita kwa sauti huku akiweka mikono yake kichwani, aliogopa mno.
Kufumba na kufumbua mara alimuona David akiruka kwa kasi kama mshale. Wakati Zungu akiwa anakwenda chini mara David alimuwahi na kumshika mkono wake mmoja. Lakini jambo baya na la kutisha ni kwamba hata David naye hakuwa amejishikilia kikamilifu kwani nusu ya mwili wake ilikuwa tayari imetoka nje kwenye ule uwazi kilichobaki huku juu pangoni ni miguu pekee ambayo ndiyo iliyokuwa ikimpa nguvu kidogo sana ya kuweza kumzuia Zungu asiende chini.
Dayana alikimbia na kwenda kushika miguu ya David kumzuia asianguke. Sasa ikawa kama mchezo wa kuokoana.
Zungu ambaye mwili wake wote ulikuwa ukielea alikuwa ameshikwa mkono wake wa kulia na David. Lakini hata David naye karibu nusu ya mwili wake ulikuwa nje na isingekuwa Dayana kumshika miguu yake kule juu basi David na Zungu wote wangeangukia kule chini barabara. Hali ilitisha mno wakati huo.
Sasa mtihani ukawa ni namna gani Zungu ataweza kupanda na kurudi juu. Si kweli kwamba Dayana angeweza kuwavuta wote wawili kuwarudisha juu, hakuwa na nguvu hizo.
"David jitahidi usiniachie jamaa yangu" Zungu aliongea huku akianza kutafuta namna yakupanda juu, lakini ilikuwa ni ngumu tena ngumu mno.
"Nimekushika Zungu..." Alisema David huku kijasho chembamba kikimtoka. David alionekana kuweweseka sana licha ya kujikaza na kumshika Zungu lakini bado hakuwa sawa hata kidogo.
Tukio kama hili liliwahi kumtokea miaka kadhaa iliyopita wakati akiwa bado ni mdogo, tukio lililopelekea David kumpoteza kaka yake ambaye alitumbukia na kupotelea majini.
Leo tena inajirudia kwa mara nyingine huku safari hii akiwa si kaka yake bali ni Zungu mtu muhimu sana kwake.
Tukio hilo lilikuwa likijirudia kwenye akili ya David na kumuumiza kichwa. Hii ndiyo sababu akawa katika hali ya kuweweseka. Ni tukio ambalo lilipelekea David akapatwa na ugonjwa wa kisaikolojia ambao kitaalam unaitwa 'Acrophobia' yaani hofu ya Urefu au hofu ya kilele.
Watu wenye tatizo hili hawawezi kupanda juu ya kitu chochote kilicho mbali kutoka ardhini. Hata kupanda juu ya meza huwa ni tatizo, wanakuwa wanaogopa sana.
Hii ndiyo sababu David alipata shida sana wakati ule wanaruka lile shimo. Hakuliweka wazi tatizo lake isipokuwa aliishia kumwambia Dayana kuwa ni historia ndefu.
Hata wakati huu alipopata kile kizunguzungu cha ghafula ni baada ya kuchungulia chini barabarani kupitia ule uwazi kwa muda mrefu. Tatizo la hili la Acrophobia lilimpata na kupelekea janga zito walilonalo wakati huu.
Dayana alikuwa akijitahidi kuivuta juu miguu ya David lakini bado kazi hiyo ilionekana kumzidi uwezo. Wakati huo Zungu naye akawa anajitahidi kuushika mkono wa David kwa nguvu ili apande juu lakini bado hali ilikuwa ni tete, na tayari alishaanza kuchoka.
Mara ghafula katika hali wasiyoitegemea Zungu, David na Dayana walisikia muungurumo wa gari linakuja. Ni gari ambalo lilikuwa nilakwenda kuwachukua mateka wapya ufukweni mwa bahari walioletwa na meli usiku huo.
Wote watatu walitoa macho kwa mshangao ulioambatana na hofu, walijua kwa vyovyote vile lazima Zungu na David wataonekana wakielea pale juu.
"Mungu wangu tumekosa nini" Alisema Dayana akionekana kukata tamaa.


Wakati hayo yakiendelea katika kisiwa cha Magnus, upande wa pili usiku huo huo Mama yake David alionekana amekaa nje ya nyumba yake akilia kwa uchungu mkubwa mno. Kama utakumbuka jioni ya siku hiyo Mama David alipata ugeni wa ghafula nyumbani kwake. Alitembelewa na Mwanamke Hustana kutoka kundi la kigaidi MG Family.
Haikujulikana ni nini hasa kilitokea nyumbani kwa mama David lakini kwa namna ambavyo mama huyu alionekana akilia kwa uchungu usiku wa giza nene ni wazi hali si shwari hata kidogo.
Lakini hali si shwari pia hata kwa mwanae anayemtegea David akiwa kule kisiwani kwa Magnus.


Wakati huo Ndege aliyopanda Felix iliendelea kupasua mawingu angani. Yalikuwa yamesalia masaa machache sana pale ndege hiyo itakapotua na kugusa ardhi ya Tanzania.
ITAENDELEA...
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047