Simulizi: Sasha Mlinzi wa Nafsi - 1

SIMULIZI RIWAYA

JF-Expert Member
Feb 19, 2022
348
1,045
SASHA MLINZI WA NAFSI.
Sehemu ya............1-2

Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

UTANGULIZI...
Majira ya mchana wa jua kali mwanaume mmoja anaonekana akitembea kwa taabu sana katikati ya jangwa moja kubwa. Upepo mkali ulikuwa ukivuma kiasi cha kusababisha vumbe jingi kutanda hewani hali iliyopelekea mwanaume huyo kutembea na kuanguka chini mara kadhaa, hata mwili wake pia ulionekana kuwa dhaifu mno, hakuwa na nguvu za kutosha. Wakati huo katika mikono yake alikuwa amembeba mtoto mchanga mwenye umri yapata kama wiki mbili hivi. Alijitahidi kumfunika mtoto huyo ili asipigwe na lile vumbi kwa kutumia vipande vya nguo zilizo chakaa.

Hali ya mwanaume huyo aitwaye David ilionekana kuwa mbaya sana, alitembea akijikokota huku usoni akiwa na michirizi ya damu iliyokauka. Hakujua anakokwenda wala alipotoka, jangwa lilikuwa ni kubwa isivyo kawaida haukuonekana mwanzo wala mwisho wa jangwa hilo.
Baada ya kupiga hatua kadhaa David alisimama na kumtazama mtoto aliyekuwa amevalishwa kidani shingoni mwake, David alikifungua kidani hicho kilichokuwa na picha ya mwanamke mmoja mrembo sana ndani yake. Akawa anaitazama picha hiyo kisha akaachia tabasamu hafifu.

David aliinua macho yake na kutazama juu kisha akaongea akisema....

"Duniani kuna mambo mengi sana yanatokea, yapo tunayoyajua na kuyaona katika maisha yetu ya kila siku, lakini pia yapo mambo yanayoendelea ambayo hatuyajui na wala hatuamini Kama yapo. Mimi David nimefanikiwa kuishi na kuyaona yale mambo tusiyoyajua, mambo ambayo katu sikuwahi kuwaza kama yapo katika huu ulimwengu wetu. Haikuwa rahisi hata kidogo kwangu kuyakabiri maisha haya mapya, lakini kwa msaada wa SASHA mwanamke niliempenda naye akanipenda nimeishi na nitaendelea kuishi nikiwa na kiumbe huyu mikononi mwangu. Sitokufa kabla ya kukamilisha jukumu ambalo pengine nilizaliwa kwa ajili ya kulikamilisha.

Na hii ndiyo ilikuwa siku yangu ya kwanza kukutana na SASHA, sasa tuanze...

𝐒𝐀𝐒𝐇𝐀 πŒπ‹πˆππ™πˆ 𝐖𝐀 ππ€π…π’πˆ

MWANZO....

Ilikuwa ni siku iliyojaa simanzi na majonzi kwa WATANZANIA wote hasa wale waliokuwa wamekusanyika siku hiyo katika uwanja wa uhuru jijini Dar es salaam wakiuaga mwili wa aliye kuwa Rais wa Tanzania Dk John pombe magufuli.
Mwili wa shujaa huyo wa watanzania ulikuwa ukizungushwa uwanjani hapo kwa ajili ya kuagwa na maelfu ya watanzania waliokuwa wamekusanyika eneo Hilo.
Kilio cha watanzania kilisikika huku baadhi wakipunga mkono wa kwa heri kwa shujaa huyo wa aina yake kuwahi kutokea nchini Tanzania.
David alikuwa ni miongoni mwa watanzania waliofika kwenye uwanja wa uhuru kutoa heshima hizo za mwisho. uso wake ulionekana kujaa majonzi mno.

Wakati zoezi hilo likiendelea, binti mmoja mrembo akiwa amevaa gauni jekundu refu linaloburuza mpaka chini alionekana akiwa anatembea tembea kule walipokuwa waombolezaji akiwa ameshikilia kichupa kidogo chenye rangi nyeupe mkono wa kulia na mkono wa kushoto aliishikilia boksi dogo lenye rangi nyeupe pia.
Binti huyo alikuwa akikinga matone ya machozi yaliyokuwa yakiwatoka waombolezaji hao kwa kutumia ile chupa yake.
Kila alipokuwa akimkaribia mtu yeyote anaelia alisubiri hadi tone la machozi litoke ndipo alikinga na tone hilo kuangukia ndani ya chupa yake, cha ajabu hakuna mtu yeyote aliyeweza kumuona binti huyo, aliendelea na shughuli yake kama kawaida pasipo kuonekana.

wimbo wa maombolezi ulibadirishwa na wimbo wa zuchu -Magufuli, ulianza kupigwa...

Magufuli hai !!
Hai!!
Hai hai hai!
Hai.....!!

Hapo watu wengi waliacha kulia na kuanza kuruka ruka ikiwa Kama sehemu ya kuenzi miongoni mwa nyimbo pendwa za Rais magufuli wakati wa ziara zake.
Yule binti aliacha zoezi lake la kukusanya machozi akawa anasubiri nyakati za majonzi ili aendelee.
Alitazama chupa yake ilikuwa imefika katikati kwa ujazo wa machozi aliyokusanya.
Wakati akifanya hivyo mara kwa bahati mbaya kale kaboski kake keupe kalimponyoka na kuanguka chini, kakaporokoka kwenye ngazi katikati ya watu.
Yule binti alipatwa na mshituko mkubwa baada ya kuangusha lile boski kwani Sasa alikuwa anaonekana na kila mtu, ilionyesha kuwa lile akini boski ndilo lililokuwa likimfanya asionekane.
kwa bahati hakuna mtu aliyeshtuka binti huyo kuonekana ghafula kutokana na msongamano mkubwa wa watu.
***

David akiwa ni sehemu ya waombolezaji, mara aliona kuna kijiboksi kidogo cheupe kimedondokea miguuni pake.

Aliliangalia kwa sekunde kadhaa na taratibu akainama kutaka kuliokota.

"Achaa, usishikeee"
Sauti ya kike ilisikika kutoka nyuma yake, David aligeuka kutazama.
Akamuona binti mmoja mrembo sana amevaa gauni jekundu mkoni akiwa ameshikiria chupa nyeupe.

" Kwa hiyo unaona Mimi ni mwizi au" alisema David huku akiinama kuokota lile boksi.

"Achaaaaa"
Yule binti alipaza sauti kwa mara nyingine kumzuia David lakini haikusaidia kwani tayari David aliinama na kulichukua lile boksi, kisha akamtaka aje kulichukua.

Yule binti alibaki katika hali ya kuduwaa huku akiwa amemkodolea macho David.
David nae akiwa haelewi chochote kwa nia njema tu alitaka mkumsaidia yule binti lakini hakuja ni kwa nini Yule binti anamzuia kwa nguvu kubwa.

Wakati wakizidi kushangaana mara David alipigwa shoti ya ghafula kwenye ule mkono alokuwa ameshika lile boksi, akatetemeka na kuliachia likadondoka.
David alihisi mkono wake umekufa gazi, alimtazama Yule binti ambae nae alionekana kuduwazwa na tukio hilo.
Haraka yule binti aliinama na kuliokota boski lake akaanza kuondoka.

David akiwa bado ana maumivu kiasi, alimsindikiza yule binti aliyekuwa anaondoka kwa kasi akipotelea kwenye umati wa watu.
David hakuweza kusema lolote zaidi ya kubaki anashangaa tu, lakini jambo ambalo hakulielewa ni kwamba baada ya yule binti kulishika lile boski lake kwa mara nyingine ni yeye pekee ndiye aliyekuwa anamuona.
Watu wengine waliokuwa kwenye msiba huo hawakuwa wakimuona zaidi ya David pekee lakini yeye hakujua hilo.

Baada ya yule binti kupotea machoni kwa David, Kijana huyu aliutazama mkono wake uliopigwa na shoti ya ajabu mara baada ya kulishika boksi lile akaona uko salama. Kichwani alibaki na maswali mengi akijiuliza msichana yule ni nani? Kwa nini alimzuia kuokota kile boksi kidogo? Kwa nini mara baada ya kuokota amepigwa na shoti ya ajabu. Bado David hakuwa na majibu ya maswali yake, mwisho aliamua kupotezea tukio lile akiamini pengine kulikuwa na vitu vyenye asili ya umeme ndani ya kile kijiboksi ndio sababu alimzuia. Hakutaka kulizingatia sana tukio lile ambalo kiasi lilikuwa na maajabu yake.


Dakika 45 baadae...
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Julias Nyerere kundi kubwa la watu walionekana wakikimbia mara baada ya kuvunja geti, wakawa wanaelekea kwenda kushuhudia mwili wa Rais wao kipenzi ukiingizwa ndani ya ndege tayari kusafirishwa. Licha ya serikali kutoa siku mbili za kuuwaga mwili wa marehemu lakini hazikutusho kuwazuia maelfu wa Watanzania waliojitokeza hadi uwanja wa ndege kumsindikiza huku wakiimba na kulitaja jina la shujaa huyo.

Watu walifika uwanjani hapo walikuwa ni wengi mno, ikiacha idadi kubwa ya Watanzania waliojipanga pembeni ya barabara kutoka uwanja wa mpira wa uhuru hadi kufika uwanja wa ndege bado hawakufikia idada ya hawa waliofulika uwanjani hapo.
Licha ya kuwekwa utaratibu maalumu uwanjani hapo lakini ilikuwa ni ngumu kuwazuia Watanzania hao ambao baadae walivunja geti na kuanza kukimbia wakiingia ndani zaidi ya uwanja wa ndege. Hali hii ilipelekea wengine kuanguka na kuanza kukanyagana. Ilikuwa ni hatari sana hasa kwa wanawake na vijana wadogo walikuwa miongoni mwa waombolezaji hao.

David akiwa mmoja kati ya maelfu ya watu waliofika mahali hapo, alishuhudia kundi kubwa la watu likivunja geti na kuingia ndani ya uwanja wa ndege kwa kasi. David akiwa hatua kadhaa kutoka hapo, alijikuta akitabasamu na kuwaza moyoni.

"Huu ni upendo wa ajabu wanaouonyesha Watanzania kwa Rais wao, haijawahi tokea mahali popote Dunia, hakika walimpenda mno"
Aliwaza David na wakati akiwaza hayo ndipo alipoona tukio lingine la ajabu.

Katikati ya lile kundi kubwa la watu waliokuwa wakikimbia kwa mara nyingine tena alimuona yule binti mwenyewe gauni jekundu. David alitoa macho kwa mshangao baada ya kuona binti huyo akifanya mambo ya ajabu. Si kwamba alikuwa akikimbia kama wengine la hasha, yeye alikuwa bize akiwainua wale watu waliokuwa wakianguka chini kuwazuia wasikanyagwe. Alikuwa akiifanya kazi hiyo kwa kasi sana. Anaenda kushoto anamuinua huyu anarudi kulia, anakwenda mbele anarudi nyuma huku kasi yake ikionekana kutokuwa ya kawaida kabisa.
Yule binti aliendelea kuifanya kazi hiyo katikati ya ule umati mkubwa wa watu. Jambo la ajabu ni kwamba hakuna aliyekuwa akimuona zaidi ya David peke yake.
"Oo..oya mwanangu" Alisema David huku akimgusa begani mwanaume mmoja aliyekuwa amesimama pembeni karibu yake.

"Nambie" aliitika

"Unamuona yule msichana anachokifanya pale?"

"Msichana yupi?"

"Yule pale" David akanyoosha kidole katikati ya ule umati wa watu wanaokimbia

"Sasa watu wote wale nitajua ni mtu gani unamzungumzia" aliuliza yule mwanaume huku akimtazama David usoni kwa mshangao.

"Namaanisha yule Dada amevaa gauni jekundu kwani huoni anavyofanya katikati ya wale watu?"

"Eeh.. we jamaa mi sikuelewi bana" Alisema yule mwanaume huku akimuona David kama mwendawazimu, akazuga kama anapokea simu akaenda zake pembeni.

"Mbona anaonekana kwamba haoni nini pale?" David alijiuliza hukua akiamini kwa mtu mwenye macho yenye afya kamili kama yake asingeshindwa kumuona yule msichana mwenye gauni jekundu.

Wakati David akizidi kutazama mara ghafula akaona tukio lingine la ajabu. Kilishuka kitu cheusi kutoka juu angani kikaanguka chini katikati ya ule umati wa watu na baadae akasimama mtu mmoja aliyevalia mavazi meusi tii kuanzia juu hadi chini. Hata yeye alikuwa na ngozi nyeusi tii kama nguo zake. Alikuwa amevaa koti kubwa jeusi lenye kofia pana kichwani. Koti lake lilikuwa refu mno kiasi cha kugusa chini na kufanya miguu yake isionekane.
Mkononi alikuwa ameshikilia mkuki mrefu, akawa anatembea kumuelekea yule binti anayefanya kazi ya kuinua watu waliodondoka.
Yule mtu mwenye mavazi meusi naye alikuwa akipishana na watu pasipo kuonekana yaani alikuwa ni David pekee ndiye aliyekuwa akiwaona watu hao wa ajabu.
Yule mtu aliendelea kutembea akawa anamueleka yule binti, kwa bahati mbaya yule binti hakuwa amemuona kabisa na alipo mkaribia aliinua mkuki wake juu akiwa amedhamiria kuuzamisha kwenye mgongo wa yule binti aliyekuwa ameinama wakati huo.

David alishuhudia yote haya akiwa kwa mbali asielewe ni nini hasa kilikuwa kinaendelea. Alifumba macho kwa hofu asishuhudie tukio lile la kutisha. Kuna wakati alihisi kama yuko ndotoni lakini kila alipojaribu kuzinduka kutoka usingizini ndipo alipogundua kuwa haikuwa ni ndoto bali kila alichokiona na kukishuhudia kilikuwa ni kweli tupu.

Wakati yule mtu akiushusha kwa nguvu mkuki wake ghafula kufumba na kufumbua wakatokea wanawake wengine watano waliovaa mavazi mekundu sawa na alivyovaa yule binti. Mmoja kati yao akasimama mbele ya yule binti na wakati huo huo yule bwana mwenye mavazi meusi akausindilia mkuki wake kwenye mwili wa yule mwanamke aliyesimama mbele ya binti yule kumkinga, nikama mwanamke yule alikuwa amejitoa muhanga kuzuia mkuki usimpate yule binti na badala yake ukazama kwenye kifua chake na akatokea mgongoni.
David alipokuja kufumbua macho yake kuangalia kwa mara nyingine akakutana na tukio lingine la kutisha, aliona ule mkuki ukiwa umezama kwenye mwili wa mwanamke mwingine ambaye hakujua ametokea wapi huku wale wengine wanne wakiwa wamesimama imara kumzunguuka yule binti. David hakujua watu hawa wamefikaje fikaje mahali hapo na wametoka wapi. Kila alichokiona kilizidi kumchanganya na kumuacha mdomo wazi.
David alishuhudia yule mwanamke aliyechomwa mkuki akipukutika kama mchanga na baadae akawa moshi mweupe uliopotelea hewani. Wakati huo huo wale wanawake wanne waliosalia wakawa bado wamesimama kumzunguuka yule binti ambaye aliacha kufanya kile alichokuwa akikifanya sasa akawa anaelewa kuwa yuko hatarini kushambuliwa na yule mtu mwenye mavazi meusi.
Ajabu ni kwamba licha ya idada ya wale watu wa ajabu kuongezeka lakini bado ni David pekee ndiye aliyekuwa akiwaona. Watu wengine wote walikuwa bize na harakati za msiba wa Mheshimiwa Rais.

Yule binti alikuwa amesimama katikati huku akiwa amezinguukwa na wale wanawake wanne ambao kila mmoja alikuwa na kisu kidogo mkononi mwake kilichofungwa utepe mwekundu. Yule binti alipenya kati kati ya wale wanawake waliomzunguuka akapiga hatua kumsogelea yule mwanaume mwenye mavazi meusi.

"Tafadhali usimsogelee ni hatari" Aliongea mwanamke mmoja kati ya wale wanne.

"Acha niongee naye"

"Hapana Sasha anaweza kukudhuru" Yule mwanamke alisisitiza.
Naam, hilo ndilo jina halisi la binti huyo, aliitwa SASHA.
Wakati yote hayo yakiendelea David alikuwa kwa mbali akishuhudia. Alishangaa ni vipi anaona vitu ambavyo ama kwa hakika ni yeye pekee ndiye alikuwa na uwezo wa kuona lakini watu wengine hawakuelewa lolote. David hakujua ni vipi amepata uwezo huo, lakini mambo yalibadilika tangu pale alipoliokota lile boksi la SASHA akiwa ndani ya uwanja wa uhuru wakati ule wa kuuga mwili wa Mheshimiwa Rais.

Je nini HATIMA ya mkasa huu wa kusisimua?

Ni vipi kijana David anajikuta ameingia katika jukumu zito mno ambalo linaibua vita kali, Vita ya Mapenzi, vita ya Kisasi, Vita ya kupambania uhai wake na uhai wa watu wengine anaowapenda.

Siri zilizofichwa zinafichuka, mazuri na mabaya yanawekwa bayana, Chuki inazaliwa, Michezo na drama za kutumia akili kubwa zinapelekea Damu kumwagika.

Endelea kufuatilia Simulizi hii ndani ya uzi huu humu humu Jamii forum napatikana WhatsApp namba 0756862047.

ITAENDELEA...
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
FB_IMG_1675599898856.jpg
 
SASHA, MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........03
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Alishangaa ni vipi anaona vitu ambavyo ama kwa hakika ni yeye pekee ndiye alikuwa na uwezo wa kuona lakini watu wengine hawakuelewa lolote. David hakujua ni vipi amepata uwezo huo, lakini mambo yalibadilika tangu pale alipoliokota lile boksi la SASHA akiwa ndani ya uwanja wa uhuru wakati ule wa kuuga mwili wa Mheshimiwa Rais.

SASA ENDELEA...
"Tafadhali usimsogelee ni hatari" Aliongea mwanamke mmoja kati ya wale wanne waliomzunguuka Sasha
"Acha niongee naye"
"Hapana Sasha anaweza kukudhuru" Yule mwanamke alisisitiza.
"Hawezi" Sasha alijibu kwa kujiamini kisha akasogea na kusimama mbele ya yule mtu mwenye mavazi meusi, bado alikuwa na ule mkuki mkononi mwake.

"Unathubutuje kusimama mbele yangu tena ukiwa na silaha?" Sasha aliuliza akimtazama yule mwanaume kwa macho makali kiasi cha kuyafanya macho yake yang'ae sana.
Yule mwanaume alianza kutetemeka kwa hofu huku akipiga hatua kurudi nyuma,Sasha naye akazidi kumsogelea.
"Nakuuliza... Unapata wapi ujasiri wa kusimama mbele yangu na silaha!?" Sasha alifoka akiwa karibu kabisa na yule mwanaume ambaye alikosa kabisa ujasiri wa kumtazama Sasha usoni.
Wakati akiwa karibu kabisa kumfikia, yule mwanaume aliinua mkuki wake kwa mara nyingine tayari kumchoma Sasha lakini kabla hajafanya hivyo kufumba na kufumbua ghafula alitokea mwanamke mmoja tofuauti na hawa wanne waliosimama nyuma ya Sasha.
Mwanamke huyu alivaa mavazi yale yale sawa na aliyovaa Sasha na wale wanawake nyuma yake. Yule mwanamke aliushika ule mkuki kwa mkono wake wa kushoto kuuzuia, kisha mkono waka wa kulia alishika kisu kidogo ambacho alikisindilia kwa nguvu katikati ya shingo ya yule mwanaume mwenye mavazi meusi. Sekunde chache baadae yule mwanaume alipasuka vipande vipande mithiri ya puto kisha vile vipande vikaanguka ardhini na mwisho vikatoweka.

"Handan!??" Sasha aliita kwa mshangao ni kama hakutegemea kumuona mwanamke huyo mahali hapo. Ingawa gauni refu alilovaa mwanamke huyo lilikuwa na rangi nyekundu kama ilivyo kwa Sasha na wale wanawake wengine, lakini gauni mwanamke huyu lilikuwa na muundo tofauti huku kiunoni akiwa amevaa mkanda mpana uliochomekwa visu vingi kumzunguuka, aliitwa Handan.

"Hivi mnaelewa mnachokifanya!?" Handan aliongea kwa hasira akiwafokea wale wanawake wanne waliosimama nyuma ya Sasha kumlinda.

"Tulimzuia lakini hakutuelewa.." Alijibu mwanamke mmoja kwa unyenyekevu mkubwa huku wengine wote wakiwa wameinamisha vichwa vyao kuonyesha heshima kubwa kwa Handan ambaye sura yake haikuwa na hata chembe ya masihara.
"Sasha nimeagizwa nikurudishe nyumbani haraka" Alisema Handan.
"Hapana bado sijamaliza kazi yangu, angalia chupa yangu ya machozi bado haijajaa" Alisema Shasha huku akiitoa chupa yake kutoka kwenye mfuko wa gauni. Ilikuwa ni ile chupa aliyokuwa anaitumia kukusanya machozi wakati ule ndani ya uwanja wa uhuru.
Wakati huo wote bado David alikuwa akiwatazama watu hao wa ajabu kwa mbali.
"Eeh! Mungu wangu ni nini hiki nakishuhudia leo" David alijisemea mwenyewe kisha akajikuta anakosa nguvu na kukaa chini. Bado alihisi ni kama yuko ndotoni lakini hakika kila alichokiona kilikuwa ni kweli tupu. Jambo lililozidi kumuumiza kichwa ni kwamba wale watu wa ajabu aliwaona yeye peke yake lakini watu wengine waliokuwa maeneo hayo ya uwanja wa ndege hawakuona chochote. Kuna baadhi walipita hadi karibu kabisa na walipo akina Sasha lakini ni kweli hawakuona kitu.

Wakati David akiwa amekaa pale chini alitazama pembeni yake kisha akayarudisha tena macho yake kule walikokuwa wale watu wa ajabu. Lakini wakati David alipotazama pembeni ni kama kuna watu aliwaona miongoni mwa watu wengi waliokuwa maeneo hayo, akageuka tena kuwaangalia, aliwafahamu, walikuwa ni wanaume watatu.

"Ooh! Kumekuchaa..." Alisema David huku akiinuka taratibu na kuanza kuondoka. Alionyesha anawajua vizuri watu hao, na kitendo cha yeye kuinuka na kuanza kutembea haraka haraka kiliashilia wazi watu hawa si wema kwake. David aliendelea kutembea haraka haraka akikatisha katikati ya watu waliokuwa eneo hilo akawa anageuka nyuma mara kadhaa kuangalia akawaona wale watu bado wanamfuata, akiongeza mwendo nao wanaongeza. Mwisho David akaanza kukimbia, wale wanaume watatu nao wakaanza kumfuata wakimkimbiza.

Huku nyuma Sasha na Handan waliendelea na mazungumzo.

"Wameshajua kuwa umetoka nje ya ISRA ndio maana wamekufuata huku ni hatari Sasha naomba turudi nyumbani ISRA" Alisema Handan.
ISRA ilikuwa ni sehemu wanapotoka Sasha pamoja na watu hao wa ajabu.
"Handan hii ni kazi yangu ya kwanza kufanya nje ya Isra siwezi kurudi nyumbani nikiwa na chupa ambayo haijaja machozi, nitamueleza nini baba yangu ambaye ameniamini sana?" Alisema Sasha.
"Hata ukirudi na chupa iliyojaa machozi lakini tayari umeshakosea Sasha" Alisema Handan.
"Nimekosea nini tena!?"
"Leo hii kuna mwanadamu atakufa kwa ajili yako"
"Nani? Mwanadamu gani atakufa?"
"Yule kijana aliyeokota boksi lako la uono" Alisema Handan na hapo Sasha akamkumbuka kijana David aliyeokota boksi alilodondosha wakati ule akiwa anakusanya machozi uwanjani.

"Hapana, hawezi kufa, haiwezekani niwe sababu ya kifo chake" Alisema Sasha
"Huwezi kuzuia Sasha, mpaka sasa yule kijana anauwezo wa kutuona popote pale tutakapokuwa. Ni kinyume na sheria zetu, lazima auawe"
"Lakini kwa nini afe, hana kosa lolote"
"Sasha unatakiwa kuheshimu kanuni na taratibu zetu tofauti na hapo utakuwa unamuudhi baba yako na atakunyang'anya heshima yote aliyokupa, simama kwenye njia anayotaka baba yako, unajua ni kwa nini alikutuma huku peke yako bila walinzi? Alitaka kukujaribu lakini mpaka sasa umeshafanya makosa mawili unataka kuongeza la tatu kwa kumtetea huyo mwanadamu. Naomba usije ukafungua mdomo wako tena kujaribu kupinga, yule kijana ni lazima tumuue" Handan alieleza kwa kina huku sura yake ikionekana kutokuwa na hata chepe ya masihara.


Upande wa pili tayari wale wanaume watatu waliokuwa wakimkimbiza David walifanikiwa kumkata na sasa walikuwa naye ndani ya gari, mmoja akawa kulia mwingine kushoto huku David akiwa katikati yao. Dereva alikuwa akiendesha gari taratibu, David akawa ametulia akitafakari jambo. Akamtazama yule jamaa wa kushoto kisha akamgeukia yule wa kulia, akaongea...

"Jamani hebu subiri kwanza naombeni msinipeleke kwa yule mwanamke atanifanya kitu kibaya naombeni sana eeh! Jamani" David alikuwa akiomba na kukunja mikono yake, akatazama kulia na kushoto hakuna aliyemjali.

Mwisho gari lilifunga breki nje ya nyumba moja kubwa ya kifahari. Wale watu walimshusha David na kumbeba msobe msobe wakamuingiza ndani ya nyumba hiyo.

David alitupwa katikati ya sebule moja kubwa. Mbele yake ulionekana mwanamke mmoja amekaa kwenye kiti karibu na dirisha akiwa amewapa mgongo. Mara baada ya David kutupwa pale chini mwanamke huyo aligeuka taratibu akiwa ameweka pozi la haja.
David aliinua uso wake kwa hofu akatazamana na mwanamke huyo. Alikuwa ni mwanamke mmoja mrembo sana, mwenye uwezo wa kumvutia kila mwanaume atakayemtazama. Ukialichilia mbali mwanadada huyo kuwa na sura nzuri na umbo linalotuvia hata yeye pia alijua namna ya kujiongezea uzuri wake na kuonekana mrembo mara dufu.
Alikuwa amevaa kijisketi kifupi kilichoacha mapaja yake malaini wazi, huku juu alivaa kijinguo fulani chepesi sana kilichoziba chuchu zake zilizonona mithiri ya embe dodo lililoiva na kusubiri kuliwa, tumbo na kitovu lichokuwa na kipini vyote vilikuwa wazi, hakika alipendeza sana. Mwanadada huyu aliitwa Tesha, Naam ni Tesha Andrea Boniage.
Tesha na David waliatazamana kisha Tesha akaachia tabasamu mwanana lililozidi kuupamba uso wake, lakini tofauti na David yeye alimtazama Tesha huku uso wake ukionekana kujawa na mashaka na wasiwasi mwingi. Kwa dakika kadhaa David alikuwa amesahau kabisa habari za wale watu wa ajabu aliowaona uwanja wa ndege dakika chache zilizopita.

Je nini kitafuata?
Tesha ni nani hasa?
Vipi kuhusu mpango wa David kuuawa na wale watu wa ajabu?
Ungana nami katika simulizi hii iliyojaa Mikasa mingi ya kusisimua na kuburudisha. Vita, visasi,vichekesho,ushirikina,mauaji, miujiza bila kusahau love story nzuri sana ndani yake.

Ni mimi mwandishi wako mahiri SAUL DAVID
.
WhatsApp: 0756862047


π“π”πŠπ”π“π€ππ„ 𝐓𝐄𝐍𝐀 πˆπ‰π”πŒπ€π€ ππƒπ€ππˆ π˜π€ 𝐉𝐅
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........04
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Lakini tofauti na David yeye alimtazama Tesha huku uso wake ukionekana kujawa na mashaka na wasiwasi mwingi. Kwa dakika kadhaa David alikuwa amesahau kabisa habari za wale watu wa ajabu aliowaona uwanja wa ndege dakika chache zilizopita.
SASA ENDELEA...

"Nitajaribu kuongea na baba, huenda akanielewa. Sitaki binadamu yeyote afe kwa ajili yangu" Sasha aliendelea kushikilia msimamo wako hakuwa tayari kabisa yeye kuwa ni sababu ya mwanadamu kufa.
"Sawa lakini huyo kijana lazima awe chini ya uangalizi kuanzia sasa, Zucc na Femi mtabaki mkimchunga huyu mtu sisi tunarudi nyumbani ISRA" Alisema Handan. Zucc na Femi walikuwa ni kati ya wale wanawake wanne waliosimama nyuma ya Sasha. Waliinamisha vichwa vyao chini kwa heshima kukubaliana na maagizo ya Handan.
"Tunaweza kuondoka sasa Sasha"
Alisema Handan na mwisho wakubaliana hivyo. Sasha Handan pamoja na wale wanawake wawili walishikana mikono na kuanza kupiga hatua kwenda mbele baada ya hapo walipaa juu kwa namna ya ajabu sana na mwisho wakatoweka ghafula.
Lakini kabla hawajatoweka Handan aligeuka nyuma akawapa ishara fulani Zucc na Femi ishara ambayo ilikuwa sio nzuri akiwa na maana kwamba walitakiwa kumuua David na si kumchunga kama alivyosema hapo awali. Zucc na Femi walitikisa vichwa vyao wakionyesha kuelewa ishara hiyo. Wakati Sasha na wenzake wanapaa na kutoweka, pia Ndege iliyoubeba mwili wa marehemu Mheshimiwa Rais nayo ndio ilikuwa inapaa na kuondoka.

Turudi nyumba aliyopelekwa David baada ya kukamatwa.
Tesha alitoa ishara fulani kwa wale vijana waliomleta David. Wote wakageuka taratibu na kuondoka, wakatoka nje ya nyumba, wakimuacha Tesha akiwa na David pekee ndani ya sebule ile kubwa.
Tesha alitembea kwa madaha huku akijibinua binua makalio yake makubwa akafika na kuchuchumaa mbele ya kijana David. Alipata shida kidogo kutokana na aina ya mavazi aliyoyavaa mwanamke huyo mrembo lakini alijitahidi kubana miguu yake vizuri kujisitili.
"Wewe" Tesha aliita huku akiuinua uso wa David kwa kutumia vidole vya mikono yake. David ambaye awali alikuwa ametazama chini aliinua uso wake taratibu akatazamana na Tesha usoni, bado alionekana mwenye hofu.
"Kwa nini unakuwa msanii! Eti wewe? Umetumia pesa zangu halafu hutaki kufanya kazi tuliyokubaliana kwa nini David" Aliuliza Tesha.
"Tesha ni kweli nilikuwa nahitaji pesa kwa ajili ya matibabu ya mdogo wangu lakini ukweli kazi yako siiwezi, nilichukua pesa zako ili tu niweze kumsaidia mdogo wangu kwa haraka. Kama kuna kazi nyingine unaweza kunipa lakini sio hiyo Tesha tafadhali" David alijaribu kujieleza.
"Sasa kwani hii kazi inaugumu gani David!?" Aliuliza Tesha lakini kabla hajajibiwa mara malango ulifunguliwa. Akaingia mwanaume mmoja aliyevalia suti nadhifu yenye rangi ya kijivu. Alionekana kuwa na haraka sana, lakini alipowaona David na Tesha pale sebuleni aliduwaa kidogo.
"Broo!" Tesha aliita
"What's going on"( nini kinaendelea?) Aliuliza yule mwanaume, aliitwa Godfrey kaka yake Tesha.
Tesha hakujibu kitu, Godfrey aliwapita pale walipo akaelekea chumba kingine huku akimuomba mdogo wake Tesha amfuate.
"Nakuja ole wako ukimbie tena" Tesha alimtisha David kisha akaondoka kuelekea chumbani akimfuata kaka yake
David alibaki amekaa pale chini sebuleni akiwa hajui afanye nini. Nguvu ya pesa aliyokuwa nayo msichana huyu ilikuwa ni ngumu kumkimbia.
"Au nihame Dar?" Aliwaza David lakini akakumbuka alikuwa akiishi na mama na mdogo wake mgonjwa ambao wote wanamtegemea yeye kwa kila kitu.
Wakati David akiwaza hayo ghafula kupitia kioo kikubwa cha dirisha kwa mara nyingine tena aliwaona wale wanawake wa ajabu waliovaa magauni mekundu wakiwa wamesimama nje ya nyumba hiyo wakimtazama. Safari hii walikuwa wawili tu yaani Zucc na Femi. David aliogopa sana, sasa alikosa uvumilivu wa kuendelea kuwatazama wanawake hao ambao awali aliwaona na kuhisi yuko ndotoni lakini sasa walimfuata kila anapokwenda. Na safari hii walikuwa wamekuja kuyaondoa maisha yake kama walivyoagizwa na Handan.

Wakati huo Tesha na kaka yake Godfrey walikuwa ndani ya chumba cha kulia chakula wakifanya mazungumzo.
"Usiniambie kuhangaika kote huku ni kwa ajili ya yule mpuuzi wako Felix?" Aliuliza Godfrey huku akiwa amemtolea macho makali mdogo wake Tesha.
"Of course ni kwa ajili ya Felix kaka" Tesha alijibu
"Ooh! My Goodness, hivi wewe ni mara ngapi nakueleza kuwe Felix hakupendi tena! He's no longer in love with you, hakupendi hakutaki Tesha kwa nini huelewi lakini mdogo wangu" Godfrey alifoka.
"Sawa lakini mimi bado namhitaji kaka! Najua bado ananipenda kuna mahali tu nilimkosea ndio maana amekuwa mgumu kiasi hiki kaka! Can't you think. Ni mwanaume gani anaweza kukupa vitu vyote hivi na bado akawa hakupendi. Amenipa kila kitu nilichonacho sasa, utajiri wangu na wako vyote vimetoka kwake leo hii unadiliki vipi kusema Felix hanipendi" Tesha aliongea huku akirusharusha mikono yake.
"Ndio maana nakwambia mdogo wangu hivi vitu tulivyopata basi tuvitumie yeye si hakutaki basi huna budi kuachana naye, move on! Unamng'ang'ania wa nini? Mbona wanaume wengi tu, istoshe wewe ni mwanamke mwenye pesa zako, unaweza kuchagua mwanaume yeyote unayemtaka"
"Lakini kaka.."
"Kaka kitu gani Tesha"
"Nataka kujaribu njia ya mwisho kama nita prove kweli Felix hanitaki basi nitaachana naye i promise you"
Kimya kikatawala kwa muda...
"Nini unataka kufanya?" Godfrey akauliza
"Nataka nimtishie kuwa nataka kufunga ndoa na mwanaume mwingine, nataka tupige picha za uchumba mimi na David kisha picha hizo zisambae. Nihakikishe hata yeye huko Marekani alikoenda anaziona hizo picha kisha nitaona reaction yake atafanya nini" Alieleza Tesha
"So ndio maana umemleta David hapa?"
"Ndiyo na nilishamlipa tayari"
"Sasa kwa nini umemchagua David na sio mtu mwingine, nasikia umeenda kumteka kijana wa watu huko msibani Tesha why this?" Aliuliza Godfrey, Tesha akatabasamu.
"Unacheka!?"
"No kaka! Ni vile hujanielewa, namtaka David kwa sababu ni kijana mzuri, handsome. Namjua Felix vizuri anawivu sana, nikimtumia David atarudi hapa mkuku mkuku"
"Eee..."
"Yes bro"
"Basi umu..." Alisema Godfrey lakini kabla hajamalizia sentensi yake mara ghafula wanamuona David anakuja walipo huku anakimbia, akafika na kuanguka miguu mwao.

"Kuna watu...kuna watu wa ajabu hapo njee... Wanatisha..wa..wa ...." David aliongea kwa papara kiasi cha kuwafanya Godfrey na Tesha watazamane, wakawa hawamuelewi.


Upande wa pili Sasha Handan pamoja na wale wanawake wawili walionekana wakiibuka kutoka ndani ya maji ya bahari moja kubwa sana ambayo haikuonekana mwisho wake. Macho yao yalikuwa yakiwaka na kutoa mwanga mweupe kwa muda kisha yakarudi katika hali ya kawaida.

Walitembea hadi nchi kavu, walipo kanyaga tu ardhi mavazi yao wote yakabadilika kutoka rangi nyekundu na kuwa meupe tena yaling'aa sana.
Naam, sasa walikuwa ISRA mahali wanapotoka watu hawa wa ajabu.

Je, nini kitaendelea?
David atakuwa salama?
Sasha atafanya nini akigundua Handan kamgeuka?
Huyu Felix ni nani hasa?

ITAENDELEA....
0756862047
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........05
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Walitembea hadi nchi kavu, walipo kanyaga tu ardhi mavazi yao wote yakabadilika kutoka rangi nyekundu na kuwa meupe tena yaling'aa sana.
Naam, sasa walikuwa ISRA mahali wanapotoka watu hawa wa ajabu.

ILIPOISHIA...

"Kuna watu...kuna watu wa ajabu hapo njee... Wanatisha..wa..wa ...." David aliongea kwa papara kiasi cha kuwafanya Godfrey na Tesha watazamane, wakawa hawamuelewi.

Godfrey alipiga hatua akatembea kuelekea sebuleni huku Tesha akimfuata nyuma taratibu, David naye akawa anawafuata akiwa bado mwenye hofu kubwa. Wale watu wenye magauni mekundu walimtisha mno.
Baada ya Godfrey kufika pale sebuleni akaangaza macho yake huku na kule hakuona kitu. Akageuka na kumtazama mdogo wake kisha akamuonyesha ishara kuwa hakukuwa na kitu, hali ilikuwa shwari kabisa.

"Wewe unatuchezea akili sio?" Tesha aliuliza huku akigeuka na kumtazama David kwa macho makali.
"Hapana, nasema kweli Tesha niliona watu hapo dirishani"
"Wako wapi sasa mbona hawaonekani?"

David alipiga hatua akasimama sebuleni kuhakikisha kama ni kweli hakuna kilichoonekana, ajabu ni kwamba hakukuwa mtu tena pale dirishani, wale Zucc na Femi walipotea ghafula.
David aliduwaa kwa muda kisha taratibu akageuka na kumtazama Tesha.
"Unaniangalia nini? Wako wapi hao watu sasa? Acha kucheza na akili zetu David hizo janja janja zako nazijua tangu kitambo ila kaa ukijua kazi yangu utaifanya tu upende usipende kwa sababu pesa yangu umeshachukua" Alisema Tesha.
"Lakini Dada Tesha u..."
"Usiniite hivyo David, mimi sio dadako. Niite mchumba, mchumba wangu... Sawa David, unatakiwa kuzoea hivyo kuanzia sasa, unatakiwa uwe muigizaji mzuri. Sitaki mtu yeyote agundue kuwa uchumba wangu mimi na wewe ni wa kugushi sawa sawa!?"
"Sawa dada Tesha"
"Oh! My Goodness, unakichwa kigumu David..." Sasha alilalamika.
"Tesha...!" Mara Godfrey aliitaa
"Yes bro"
"Hebu angalia pale" Alisema Godfrey akinyoosha kidole chake kuelekea dirisha ambalo awali David ndipo alipowaona wale wanawake wa ajabu.
"Kuna nini?" Aliuliza Tesha akiwa hajaelewa ni nini kaka yake anamtaka atazame, akajitahidi kuangalia kwa makini.
"Kioo! Kioo kimevunjika" Alijibu Godfrey huku akitembea kusogea dirishani, Tesha naye akamfuata.
Ni kweli walipofika dirishani walishuhudia kioo kikiwa kimetengeneza mpasuko. Ilikuwa ni jambo la kushangaza sana kwani vioo hivyo vilikuwa ni vigumu na imara sana haikuwa rahisi hata kidogo kuvunjika kirahisi namna ile.
Godfrey na Tesha walitazamana wakiwa na maswali kichwani mwao yasiyo na majibu kisha wote kwa pamoja wakageuka na kumtazama David. Sasa kwa kiasi walianza kuyaamini maneno yake.
Godfrey akapiga hatua kutoka nje ya nyumba

"Unaenda wapi kaka?"
"Nataka niwaulize walinzi kama wameona lolote" Alijibu Godfrey huku akifungua mlango akatoka nje.


Upande wa pili tayari Sasha na walinzi wake walikuwa wameingia ndani ya mji wao, ISRA.
ISRA ulikuwa mji mkubwa sana huku watu kadhaa na makazi yao wakionekana kuishi ndani ya mji huo. Waliishi maisha yao kama ilivyo kwa binadamu wa kawaida, ingawa ISRA haikufanana na maisha ya Dunia hii ya sasa bali maisha yao yalionekana ni watu wanaoishi maisha ya zamani sana.
ISRA hakukuwa umeme wala maghorofa hakukuwa magari wala ndege, ni maisha ambayo yalionekana kama ni Dunia ya miaka elfu moja iliyopita. Hakukuwa Rais wa ISRA bali kiongozi mkuu wa mji huo ambaye aliitwa Gu Gamilo na huyu ndiye alikuwa baba mzazi wa Sasha.

Zilikuwa zimepita dakika kadhaa tangu Sasha na wenzake waingie ndani ya mji wa ISRA baada ya kuchomoza kutoka ndani ya maji ya bahari. Ajabu ni kwamba wakiwa ISRA hawakuwa na uwezo wa kupotea na kutokea mahali pengine kama iliyokuwa walipokuwa nje ya ISRA.
Sasa walionekana wakiwa wanakatiza katika ya mji wa ISRA kila mmoja akiwa juu ya farasi wake waliotembea taratibu sana. Alitangulia Handan akafuata Sasha na nyuma yake walifuata wale wanawake wawili. Walipita barabarani huku wakiwapungia mikono na baadhi ya watu ambao walikuwa wakiendelea na harakati mbalimbali za maisha ndani ya mji wa ISRA. Mavazi meupe ya kung'aa sana waliyovaa Sasha na wenzake yaliwafanya waonekane tofauti kabisa na watu wa mji wa ISRA. Ni kweli walikuwa ni watu wa tofauti kabisa kutokana na namna walivyokuwa wakisalimiwa kwa heshima na kila waliyekutana naye, watu waliokuwa barabarani walipisha na kusimama mbali wakiuacha msafara huo wa mwana wa Gu Gamilo upite.

"Mama kwani hawa ni akina nani?" Aliuliza mtoto mmoja wa kike yapata umri wa miaka minne hivi yeye na mama yake walitoka sokoni na ndipo hapo walipokutana na msafara wa Sasha, wakawa wanasubiri wapite ndipo nao wavuke barabara.

"Hawa wanaitwa WALINZI WA NAFSI mwanangu" Alijibu yule mama

"Mmh! walinzi? Wanalinda kitu gani?"

"Wanalinda NAFSI zilizopo ndani yaa miili yetu. Maisha yetu yapo mikononi mwao ni wao ndio wanaamua uishi au ufe"

"Kwa hiyo ni watu wabaya!?"

"Hapana mwanangu, hawa ni wazuri saana. Si unawaona jinsi wanavyong'aa hawana ubaya wowote. Bila wao kusingekuwa na AMANI ulimwenguni. Hawa watu wamesimama katikati ya WEMA na UBAYA, katikati ya MWANZO na MWISHO" alieleza yule mama huku akiwa ameachia tabasamu akijua kabisa maneno aliyokuwa akiongea ni magumu kueleweka kwa mtoto huyo mdogo mwenye umri wa miaka minne pekee.

ITAENDELEA...
ISRA kunanini?
Vipi kuhusu usalama wa David?
Hawa WALINZI WA NAFSI ni watu gani hasa?

TUKUTANE TENA KESHO.

Napatikana WhatsApp: 0756862047
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........6-7
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Alieleza yule mama huku akiwa ameachia tabasamu akijua kabisa maneno aliyokuwa akiongea ni magumu kueleweka kwa mtoto huyo mdogo mwenye umri wa miaka minne pekee.

Je, nini kitaendelea...?

SONGA NAYO....
Sasha na msafara wake waliendelea kusonga mbele taratibu. Wakiwa na farasi zao, walitembea umbali mrefu wakiyaacha mbali sana makazi ya watu. Sasa wakawa wanafuata barabara moja iliyopita pembeni ya msitu mnene
"Mbona kuna ukimya sana eneo hili?" Aliuliza Sasha. Ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutoka nje ya ngome (ikulu) ya baba yake na nje ya ISRA pia, hivyo alikuwa hafahamu mambo mengi zaidi ya yale aliyosimuliwa tu.

"Huu msitu haruhusiwi mtu yeyote kusogea wala kuvuka zaidi ya wale wanye vibali vya kuingia Ikulu tu" Alieleza Handan.
"Vipi kuhusu hii barabara inaelekea wapi mbona kama inaingia ndani zaidi ya huu msitu?" Sasha aliuliza swali lingine huku akinyoosha kidole chake kukielekeza ilipo barabara nyingine iliyokuwa ikikatisha kuelekea ndani ya msitu huo wenye miti mirefu isivyo kawaida.

"Hii barabara ni yakuelekea kwa mtu mmoja maarufu sana hapa ISRA, mtu ambaye anajua mambo mengi kutuhusu sisi WALINZI WA NAFSI, mambo mazuri na mabaya" Handan alieleza kwa kifupi.
"Unamaanisha Bi Noha?"
"Ndiyo! Huyo huyo, kumbe unamfahamu?"
"Niliwahi kusimuliwa tu habari zake. Niliambiwa anaweza hata kukueleza hatima yako, yaani mambo yatakayotokea mbeleni?"
"Ndiyo inaaminika hivyo, lakini ni wachache sana ambao waliwahi kubahatika kukutana na Bi Noha, huwa haonekani kirahisi akienda unaweza kutembea msitu mzima na usimpate"
"Kwa nini sasa?"
"Inaaminika kuwa Bi Noha mwenyewe huwa anachagua watu wa kukutana nao na kwa sababu maalum si kila mtu anaweza kumuona, hata baba yako aliwahi kumuona mara moja tu kwa kipindi chote hiki... Na tangu siku baba yako alipoonana na Bi Noha ndipo waasi waliibuka ndani ya mji wa ISRA"
"Waasi gani?"
"Wapo wengi tu, mmoja wapo ni yule aliyetaka kukuchoma mkuki"
Maelezo haya kwa kiasi yalimshangaza Sasha, kwa miaka mingi sana amekuwa akisimuliwa habari za mtu huyo mwenye kuzijua siri nyingi za ISRA na watu wake. Alikuwa akitamani sana kuonana naye lakini kauli ya Handan ilimkatisha tamaa kwa asilimia fulani.

Wakati wakizidi kusonga mbele ghafula katikati hali ya kushangaza waliona vitu vyeusi mfano wa vimondo vikishuka kwa kasi kutoka angani na kufumba na kufumbua walijikuta wamezunguukwa na watu wengi mno walio valia mavazo meusi.
Watu hawa walifanana kabisa na yule mtu aliyetaka kumshambulia Sasha kwa kutumia mkuki wakati ule.
Walivaa makoti meusi yenye kofia kubwa kichwani huku mikononi mwao wakiwa wameshikilia mikuki.

"Nilijua tu hatuwezi kufika nyumbani bila kukutana na hawa jamaa" Alisema Handan huku akichomoa visu vyake na kuvishika sawa sawa, wale wanawake nyuma ya Sasha nao wakafanya hivyo kisha wakashuka kwenye farasi zao.

"Wewe usishuke baki hapo, tutapambana nao" Alisema Handan.
Mji huu wa ajabu ISRA si kwamba ulikuwa na amani siku zote la hasha, bado uongozi wa Gu Gamilo baba yake SASHA ulikuwa ukiingia kwenye vita ya mara kwa mara na viumbe hawa wa ajabu wanaovaa nguo nyeusi. Na hii ndio sababu pamoja na kwamba Sasha aliagizwa na baba yake kukusanya machozi ya watu akiwa peke yake lakini bado alikuwa akifuatiliwa na walinzi wake kwa siri.

Sekunde chache baadaye vita kali ilianza kati ya walinzi wa Sasha wakiongozwa na mlinzi mkuu Handan dhidi ya wale watu wa ajabu waliovalia makoti meusi. Haikuwasumbua sana kupambana nao kwani Handan na wale wanawake wawili walikuwa ni wajuzi wakubwa wa mapigano istoshe walionekana kuwa na nguvu za ajabu ndani yao. Kasi yao ilikuwa si ya kawaida, walitumia visu vidogo viwili lakini katika sekunde moja waliweza kuwaondosha maadui wawili au zaidi. Kila adui waliyemchoma kisu alipasuka vipande vipande kisha kuanguka ardhini na kupotea.

Wakati hayo yakiendelea taratibu Sasha alirudi nyuma na farasi wake akafika hadi pale inapoanzia ile barabara ya kuelekea kwa yule mtu wa ajabu Bi Noha.
Sasha aligeuka nyuma kutazama akaona Handan na wale wanawake walinzi wako bize kupambana na maadui. Haraka Sasha alivuta kamba za farasi wake ambaye alishika njia kuingia msituni kwa kasi sana. Tamaa ya Sasha ilikuwa ni kuonana na Bi Noha, alijua kama akimuomba mlinzi wake mkuu Handan waende wote kumtafuta angemkatalia hivyo aliona autumie mwanya huo kumtoroka.
Farasi wa Sasha alikimbia kwa kasi sana akipenya katikati ya msitu huo mnene. Lakini jambo la kushangaza huku nyuma anakotoka njia ilikuwa ikijifunga na kupote, Sasha hakujua hilo aliendelea kwenda mbele kwa kasi.


Upande wa pili nyumbani kwa mwanamke mrembo Tesha, wanajikuta wanaingia kwenye wimbi la hofu mara baada ya kuona kioo cha dirisha kimepasuka ghafula na wakilinganisha na maelezo ya David kuwa aliona watu wa ajabu pale dirishani, hofu iliwajaa.
Dakika chache baadae Godfrey kaka yake Tesha alirejea tena ndani.
"Walinzi wamesemaje..?" Aliuliza Tesha
"Hawajaona mtu yeyote nao pia wanashangaa kioo kimepasuka vipi ghafula hivi" Alieleza Godfrey kisha akageuka kumtazama David usoni, David akakwepesha macho yake.

"Wewe, unauhakika uliona watu hapa au ni wewe ulipasua hiki kioo ulikuwa unajaribu kutoroka?" Aliuliza Godfrey akiwa amemkazia macho David.
"Hapana mkuu, nimepasua na nini sasa si mngesikia sauti"
"Una uhakika? Hao watu uliowaona wakoje, ulishawahi kuwaona? au ukiwaona tena unaweza kuwakumbuka?"

"Aa..nd...hapana" David alijibu akisita, alijua kama akijibu ndiyo basi angeulizwa maswali mengi asiyo na majibu yake ingawa ni kweli ni kwa mara ya pili anawaona watu hao wa ajabu.

"Tesha si unaona mtu wako anavyo babaika kujibu, hiki kioo kavunja yeye" Alisema Godfrey kisha akaondoka na kuingia chumbani sekunde chache akatoka akiwa na briefcase mkononi akafungua mlango na kuondoka zake.
Tesha na David walibaki kimya wanatazamana kwa dakika kadhaa.
"It doesn't matter umevunja wewe au nani, cha muhimu kwa sasa tujadili namna utakavyoifanya kazi yangu sawa David"
Kimya..
"Unanisikia lakini Dav?"
"Nimekusikia Tesha lakini nikuulize kwanza swali, hivi ni kwa nini unataka tuwe wapenzi wa kuigiza why?" Aliuliza David.
Ni kweli kabisa David alikuwa hafahamu kiundani sababu za Tesha kufanya hivyo, hakuwa akielewa chochote kuwa Tesha anafanya hivyo ili tu kumpima aliyekuwa mpenzi wake yaani Felix ambaye ameonekana hamtaki tena licha ya kwamba amemuachia utajiri mkubwa sana. Tesha alikuwa ni mwanamitindo maarufu sana hapa nchini, alijua wazi kama atayaweka wazi mahusiano yake na David na kutangaza kuwa wanatarajia kufunga ndoa na mwanaume huyo hivi karibuni basi lazima taarifa hizi zingemfikia Felix huko Marekani.

"Nitakwambia sababu za kufanya hivi, ila kwanza kubali kuifanya kazi yangu David.. Au una mpenzi unaogopa atakuacha? it's okay twende tukaongee naye akitaka pesa pia nitampa muhimu akuruhusu na asitoe siri kama mahusiano yetu ni ya kuigiza"
"No,no,no sina mpenzi kwa sasa niko mwenyewe..."
Alisema David huku akiinua mikono yake kuonyesha msisitizo, alipomtazama Tesha akaona anamuangalia kwa macho fulani hivi yanayozungumza, ni kama hakutegemea kupata jibu kama hilo kutoka kwa David.
"Nini?" Aliuliza David baada ya kuona Tesha anamuangalia sana.
"Nothing, sasa kama uko single kwa nini inakuwa ngumu wewe kufanya kazi yangu....?" Aliuliza Tesha lakini kabla David hajajibu swali hilo mara simu yake iliita akaipokea haraka.

"Ndio mimi David...what....sawa nakuja" David aliongea kwa kifupi kisha akakata simu. Alionekana kuwa na huzuni, Tasha aliligundua hilo.
"Nini shida?"
"Mama anaumwa sana kapelekwa hospitali, natakiwa kwenda sasa hivi" Alisema David kisha akageuka tayari kuondoka.
"So unaondoka vipi kuhusu..... mmh! ...okay twende nikusindikize basi tutachukua gari yangu" Tesha aliongea na kubadilisha mada haraka.

Nje ya nyumba ya kifahari ya Tesha, walionekana wale wanawake wawili waliotumwa kumuua David ajabu ni kwamba walinzi waliokuwa wanazunguuka zunguuka eneo hilo wala hawakuwa wakiwaona. Mpaka sasa ni David pekee ndiye aliyekuwa na uwezo wa kuwaona watu hao wa ajabu.
"Inakuwaje tumeshindwa kuingia ndani ya hii nyumba Zucc?" Aliuliza Femi
"Nashindwa kuelewa hii ni mara yangu ya kwanza inatokea kushindwa kuingia ndani ya nyumba ya binadamu, nahisi kuna kitu hakipo sawa" Alijibu Zucc.

Ni kweli kabisa wakati ule David amewaona wakiwa wamesimama dirishani walijaribu kupenya kuingia ndani wakitumia nguvu walizonazo lakini ajabu walishindwa kuingia ndani na mwisho wakajikuta wanaishia kupasua kioo.
"Kuna nguvu ya ziada ipo kwenye hii nyumba, tutauliza wakubwa zetu tukirudi ISRA. Tumsubiri tu huyu mwanadamu atoke tumuue akiwa nje."alieleza Femi. Wakakubaliana wamsubiri David mpaka atakapotoka.
Haukupita muda, mwisho wakawaona Tesha na David wakitoka nje ya nyumba hiyo wakiwa wameongozana wakaingia ndani ya gari moja kati ya magari saba ya kifahari yaliyoegeshwa pale nje, wakakaa siti za nyuma.
"Nawapeka wapi bosi?" Aliuliza Dereva wa Tesha. Tesha akageuka na kumtazama David yeye ndiye alikuwa na jibu la swali hilo, wakatazamana.

"Tupeleke hospitali ya Sanitas, pita barabara ya mwai kibaki" Alisema David.
"Jitahidi kwenda haraka tunawahi" Tesha alisisitiza kisha akageuka na kumtazama David, wakatazamana tena. Tesha akatazama pembeni haraka.
"Ee! Mungu wangu ujinga gani huu nawaza" Aliwaza tesha huku akiweka mkono wake juu ya kifua chake upande wa kushoto.
Wakati huo Dereva aliondosha gari kwa kasi mara baada ya kutoka nje ya geti akafuata barabara aliyoelekezwa. Wote hawakujua kuwa nyuma wanafuatiliwa na wale wanawake wa ajabu waliotumwa kumuua David, yaani Femi na Zucc.


Wakati gari waliyopanda David na Tesha ikizidi kwenda kwa kasi, upande wa pili Sasha akiwa juu ya farasi alionekana akiendelea kwenda mbele kwa kasi akipita katikati ya msitu ule mnene asijue huku nyuma alikotoka barabara ilikuwa ikijifunga.

Je, nini kitafuata?

ITAENDELEA...
(Ndugu msomaji bado tunatengeneza mizizi ya simulizi yetu bomba, jitahidi sana kuzingatia majina ya wahusika wakuu wa simulizi hii ili isikuchanganye...... (David, Tesha, Sasha, Felix, Gu Gumaro, Handan na wengine tutakao kutana nao mbele)
Endelea kufurahia SIMULIZI bomba ya SAUL DAVID... 0756862047.
 

Similar Discussions

9 Reactions
Reply
Back
Top Bottom