Simulizi: Sasha Mlinzi wa Nafsi - 1

SASHA MLINZI WA NAFSI.
Sehemu ya............1-2

Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

UTANGULIZI...
Majira ya mchana wa jua kali mwanaume mmoja anaonekana akitembea kwa taabu sana katikati ya jangwa moja kubwa. Upepo mkali ulikuwa ukivuma kiasi cha kusababisha vumbe jingi kutanda hewani hali iliyopelekea mwanaume huyo kutembea na kuanguka chini mara kadhaa, hata mwili wake pia ulionekana kuwa dhaifu mno, hakuwa na nguvu za kutosha. Wakati huo katika mikono yake alikuwa amembeba mtoto mchanga mwenye umri yapata kama wiki mbili hivi. Alijitahidi kumfunika mtoto huyo ili asipigwe na lile vumbi kwa kutumia vipande vya nguo zilizo chakaa.

Hali ya mwanaume huyo aitwaye David ilionekana kuwa mbaya sana, alitembea akijikokota huku usoni akiwa na michirizi ya damu iliyokauka. Hakujua anakokwenda wala alipotoka, jangwa lilikuwa ni kubwa isivyo kawaida haukuonekana mwanzo wala mwisho wa jangwa hilo.
Baada ya kupiga hatua kadhaa David alisimama na kumtazama mtoto aliyekuwa amevalishwa kidani shingoni mwake, David alikifungua kidani hicho kilichokuwa na picha ya mwanamke mmoja mrembo sana ndani yake. Akawa anaitazama picha hiyo kisha akaachia tabasamu hafifu.

David aliinua macho yake na kutazama juu kisha akaongea akisema....

"Duniani kuna mambo mengi sana yanatokea, yapo tunayoyajua na kuyaona katika maisha yetu ya kila siku, lakini pia yapo mambo yanayoendelea ambayo hatuyajui na wala hatuamini Kama yapo. Mimi David nimefanikiwa kuishi na kuyaona yale mambo tusiyoyajua, mambo ambayo katu sikuwahi kuwaza kama yapo katika huu ulimwengu wetu. Haikuwa rahisi hata kidogo kwangu kuyakabiri maisha haya mapya, lakini kwa msaada wa SASHA mwanamke niliempenda naye akanipenda nimeishi na nitaendelea kuishi nikiwa na kiumbe huyu mikononi mwangu. Sitokufa kabla ya kukamilisha jukumu ambalo pengine nilizaliwa kwa ajili ya kulikamilisha.

Na hii ndiyo ilikuwa siku yangu ya kwanza kukutana na SASHA, sasa tuanze...

๐’๐€๐’๐‡๐€ ๐Œ๐‹๐ˆ๐๐™๐ˆ ๐–๐€ ๐๐€๐…๐’๐ˆ

MWANZO....

Ilikuwa ni siku iliyojaa simanzi na majonzi kwa WATANZANIA wote hasa wale waliokuwa wamekusanyika siku hiyo katika uwanja wa uhuru jijini Dar es salaam wakiuaga mwili wa aliye kuwa Rais wa Tanzania Dk John pombe magufuli.
Mwili wa shujaa huyo wa watanzania ulikuwa ukizungushwa uwanjani hapo kwa ajili ya kuagwa na maelfu ya watanzania waliokuwa wamekusanyika eneo Hilo.
Kilio cha watanzania kilisikika huku baadhi wakipunga mkono wa kwa heri kwa shujaa huyo wa aina yake kuwahi kutokea nchini Tanzania.
David alikuwa ni miongoni mwa watanzania waliofika kwenye uwanja wa uhuru kutoa heshima hizo za mwisho. uso wake ulionekana kujaa majonzi mno.

Wakati zoezi hilo likiendelea, binti mmoja mrembo akiwa amevaa gauni jekundu refu linaloburuza mpaka chini alionekana akiwa anatembea tembea kule walipokuwa waombolezaji akiwa ameshikilia kichupa kidogo chenye rangi nyeupe mkono wa kulia na mkono wa kushoto aliishikilia boksi dogo lenye rangi nyeupe pia.
Binti huyo alikuwa akikinga matone ya machozi yaliyokuwa yakiwatoka waombolezaji hao kwa kutumia ile chupa yake.
Kila alipokuwa akimkaribia mtu yeyote anaelia alisubiri hadi tone la machozi litoke ndipo alikinga na tone hilo kuangukia ndani ya chupa yake, cha ajabu hakuna mtu yeyote aliyeweza kumuona binti huyo, aliendelea na shughuli yake kama kawaida pasipo kuonekana.

wimbo wa maombolezi ulibadirishwa na wimbo wa zuchu -Magufuli, ulianza kupigwa...

Magufuli hai !!
Hai!!
Hai hai hai!
Hai.....!!

Hapo watu wengi waliacha kulia na kuanza kuruka ruka ikiwa Kama sehemu ya kuenzi miongoni mwa nyimbo pendwa za Rais magufuli wakati wa ziara zake.
Yule binti aliacha zoezi lake la kukusanya machozi akawa anasubiri nyakati za majonzi ili aendelee.
Alitazama chupa yake ilikuwa imefika katikati kwa ujazo wa machozi aliyokusanya.
Wakati akifanya hivyo mara kwa bahati mbaya kale kaboski kake keupe kalimponyoka na kuanguka chini, kakaporokoka kwenye ngazi katikati ya watu.
Yule binti alipatwa na mshituko mkubwa baada ya kuangusha lile boski kwani Sasa alikuwa anaonekana na kila mtu, ilionyesha kuwa lile akini boski ndilo lililokuwa likimfanya asionekane.
kwa bahati hakuna mtu aliyeshtuka binti huyo kuonekana ghafula kutokana na msongamano mkubwa wa watu.
***

David akiwa ni sehemu ya waombolezaji, mara aliona kuna kijiboksi kidogo cheupe kimedondokea miguuni pake.

Aliliangalia kwa sekunde kadhaa na taratibu akainama kutaka kuliokota.

"Achaa, usishikeee"
Sauti ya kike ilisikika kutoka nyuma yake, David aligeuka kutazama.
Akamuona binti mmoja mrembo sana amevaa gauni jekundu mkoni akiwa ameshikiria chupa nyeupe.

" Kwa hiyo unaona Mimi ni mwizi au" alisema David huku akiinama kuokota lile boksi.

"Achaaaaa"
Yule binti alipaza sauti kwa mara nyingine kumzuia David lakini haikusaidia kwani tayari David aliinama na kulichukua lile boksi, kisha akamtaka aje kulichukua.

Yule binti alibaki katika hali ya kuduwaa huku akiwa amemkodolea macho David.
David nae akiwa haelewi chochote kwa nia njema tu alitaka mkumsaidia yule binti lakini hakuja ni kwa nini Yule binti anamzuia kwa nguvu kubwa.

Wakati wakizidi kushangaana mara David alipigwa shoti ya ghafula kwenye ule mkono alokuwa ameshika lile boksi, akatetemeka na kuliachia likadondoka.
David alihisi mkono wake umekufa gazi, alimtazama Yule binti ambae nae alionekana kuduwazwa na tukio hilo.
Haraka yule binti aliinama na kuliokota boski lake akaanza kuondoka.

David akiwa bado ana maumivu kiasi, alimsindikiza yule binti aliyekuwa anaondoka kwa kasi akipotelea kwenye umati wa watu.
David hakuweza kusema lolote zaidi ya kubaki anashangaa tu, lakini jambo ambalo hakulielewa ni kwamba baada ya yule binti kulishika lile boski lake kwa mara nyingine ni yeye pekee ndiye aliyekuwa anamuona.
Watu wengine waliokuwa kwenye msiba huo hawakuwa wakimuona zaidi ya David pekee lakini yeye hakujua hilo.

Baada ya yule binti kupotea machoni kwa David, Kijana huyu aliutazama mkono wake uliopigwa na shoti ya ajabu mara baada ya kulishika boksi lile akaona uko salama. Kichwani alibaki na maswali mengi akijiuliza msichana yule ni nani? Kwa nini alimzuia kuokota kile boksi kidogo? Kwa nini mara baada ya kuokota amepigwa na shoti ya ajabu. Bado David hakuwa na majibu ya maswali yake, mwisho aliamua kupotezea tukio lile akiamini pengine kulikuwa na vitu vyenye asili ya umeme ndani ya kile kijiboksi ndio sababu alimzuia. Hakutaka kulizingatia sana tukio lile ambalo kiasi lilikuwa na maajabu yake.


Dakika 45 baadae...
Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Julias Nyerere kundi kubwa la watu walionekana wakikimbia mara baada ya kuvunja geti, wakawa wanaelekea kwenda kushuhudia mwili wa Rais wao kipenzi ukiingizwa ndani ya ndege tayari kusafirishwa. Licha ya serikali kutoa siku mbili za kuuwaga mwili wa marehemu lakini hazikutusho kuwazuia maelfu wa Watanzania waliojitokeza hadi uwanja wa ndege kumsindikiza huku wakiimba na kulitaja jina la shujaa huyo.

Watu walifika uwanjani hapo walikuwa ni wengi mno, ikiacha idadi kubwa ya Watanzania waliojipanga pembeni ya barabara kutoka uwanja wa mpira wa uhuru hadi kufika uwanja wa ndege bado hawakufikia idada ya hawa waliofulika uwanjani hapo.
Licha ya kuwekwa utaratibu maalumu uwanjani hapo lakini ilikuwa ni ngumu kuwazuia Watanzania hao ambao baadae walivunja geti na kuanza kukimbia wakiingia ndani zaidi ya uwanja wa ndege. Hali hii ilipelekea wengine kuanguka na kuanza kukanyagana. Ilikuwa ni hatari sana hasa kwa wanawake na vijana wadogo walikuwa miongoni mwa waombolezaji hao.

David akiwa mmoja kati ya maelfu ya watu waliofika mahali hapo, alishuhudia kundi kubwa la watu likivunja geti na kuingia ndani ya uwanja wa ndege kwa kasi. David akiwa hatua kadhaa kutoka hapo, alijikuta akitabasamu na kuwaza moyoni.

"Huu ni upendo wa ajabu wanaouonyesha Watanzania kwa Rais wao, haijawahi tokea mahali popote Dunia, hakika walimpenda mno"
Aliwaza David na wakati akiwaza hayo ndipo alipoona tukio lingine la ajabu.

Katikati ya lile kundi kubwa la watu waliokuwa wakikimbia kwa mara nyingine tena alimuona yule binti mwenyewe gauni jekundu. David alitoa macho kwa mshangao baada ya kuona binti huyo akifanya mambo ya ajabu. Si kwamba alikuwa akikimbia kama wengine la hasha, yeye alikuwa bize akiwainua wale watu waliokuwa wakianguka chini kuwazuia wasikanyagwe. Alikuwa akiifanya kazi hiyo kwa kasi sana. Anaenda kushoto anamuinua huyu anarudi kulia, anakwenda mbele anarudi nyuma huku kasi yake ikionekana kutokuwa ya kawaida kabisa.
Yule binti aliendelea kuifanya kazi hiyo katikati ya ule umati mkubwa wa watu. Jambo la ajabu ni kwamba hakuna aliyekuwa akimuona zaidi ya David peke yake.
"Oo..oya mwanangu" Alisema David huku akimgusa begani mwanaume mmoja aliyekuwa amesimama pembeni karibu yake.

"Nambie" aliitika

"Unamuona yule msichana anachokifanya pale?"

"Msichana yupi?"

"Yule pale" David akanyoosha kidole katikati ya ule umati wa watu wanaokimbia

"Sasa watu wote wale nitajua ni mtu gani unamzungumzia" aliuliza yule mwanaume huku akimtazama David usoni kwa mshangao.

"Namaanisha yule Dada amevaa gauni jekundu kwani huoni anavyofanya katikati ya wale watu?"

"Eeh.. we jamaa mi sikuelewi bana" Alisema yule mwanaume huku akimuona David kama mwendawazimu, akazuga kama anapokea simu akaenda zake pembeni.

"Mbona anaonekana kwamba haoni nini pale?" David alijiuliza hukua akiamini kwa mtu mwenye macho yenye afya kamili kama yake asingeshindwa kumuona yule msichana mwenye gauni jekundu.

Wakati David akizidi kutazama mara ghafula akaona tukio lingine la ajabu. Kilishuka kitu cheusi kutoka juu angani kikaanguka chini katikati ya ule umati wa watu na baadae akasimama mtu mmoja aliyevalia mavazi meusi tii kuanzia juu hadi chini. Hata yeye alikuwa na ngozi nyeusi tii kama nguo zake. Alikuwa amevaa koti kubwa jeusi lenye kofia pana kichwani. Koti lake lilikuwa refu mno kiasi cha kugusa chini na kufanya miguu yake isionekane.
Mkononi alikuwa ameshikilia mkuki mrefu, akawa anatembea kumuelekea yule binti anayefanya kazi ya kuinua watu waliodondoka.
Yule mtu mwenye mavazi meusi naye alikuwa akipishana na watu pasipo kuonekana yaani alikuwa ni David pekee ndiye aliyekuwa akiwaona watu hao wa ajabu.
Yule mtu aliendelea kutembea akawa anamueleka yule binti, kwa bahati mbaya yule binti hakuwa amemuona kabisa na alipo mkaribia aliinua mkuki wake juu akiwa amedhamiria kuuzamisha kwenye mgongo wa yule binti aliyekuwa ameinama wakati huo.

David alishuhudia yote haya akiwa kwa mbali asielewe ni nini hasa kilikuwa kinaendelea. Alifumba macho kwa hofu asishuhudie tukio lile la kutisha. Kuna wakati alihisi kama yuko ndotoni lakini kila alipojaribu kuzinduka kutoka usingizini ndipo alipogundua kuwa haikuwa ni ndoto bali kila alichokiona na kukishuhudia kilikuwa ni kweli tupu.

Wakati yule mtu akiushusha kwa nguvu mkuki wake ghafula kufumba na kufumbua wakatokea wanawake wengine watano waliovaa mavazi mekundu sawa na alivyovaa yule binti. Mmoja kati yao akasimama mbele ya yule binti na wakati huo huo yule bwana mwenye mavazi meusi akausindilia mkuki wake kwenye mwili wa yule mwanamke aliyesimama mbele ya binti yule kumkinga, nikama mwanamke yule alikuwa amejitoa muhanga kuzuia mkuki usimpate yule binti na badala yake ukazama kwenye kifua chake na akatokea mgongoni.
David alipokuja kufumbua macho yake kuangalia kwa mara nyingine akakutana na tukio lingine la kutisha, aliona ule mkuki ukiwa umezama kwenye mwili wa mwanamke mwingine ambaye hakujua ametokea wapi huku wale wengine wanne wakiwa wamesimama imara kumzunguuka yule binti. David hakujua watu hawa wamefikaje fikaje mahali hapo na wametoka wapi. Kila alichokiona kilizidi kumchanganya na kumuacha mdomo wazi.
David alishuhudia yule mwanamke aliyechomwa mkuki akipukutika kama mchanga na baadae akawa moshi mweupe uliopotelea hewani. Wakati huo huo wale wanawake wanne waliosalia wakawa bado wamesimama kumzunguuka yule binti ambaye aliacha kufanya kile alichokuwa akikifanya sasa akawa anaelewa kuwa yuko hatarini kushambuliwa na yule mtu mwenye mavazi meusi.
Ajabu ni kwamba licha ya idada ya wale watu wa ajabu kuongezeka lakini bado ni David pekee ndiye aliyekuwa akiwaona. Watu wengine wote walikuwa bize na harakati za msiba wa Mheshimiwa Rais.

Yule binti alikuwa amesimama katikati huku akiwa amezinguukwa na wale wanawake wanne ambao kila mmoja alikuwa na kisu kidogo mkononi mwake kilichofungwa utepe mwekundu. Yule binti alipenya kati kati ya wale wanawake waliomzunguuka akapiga hatua kumsogelea yule mwanaume mwenye mavazi meusi.

"Tafadhali usimsogelee ni hatari" Aliongea mwanamke mmoja kati ya wale wanne.

"Acha niongee naye"

"Hapana Sasha anaweza kukudhuru" Yule mwanamke alisisitiza.
Naam, hilo ndilo jina halisi la binti huyo, aliitwa SASHA.
Wakati yote hayo yakiendelea David alikuwa kwa mbali akishuhudia. Alishangaa ni vipi anaona vitu ambavyo ama kwa hakika ni yeye pekee ndiye alikuwa na uwezo wa kuona lakini watu wengine hawakuelewa lolote. David hakujua ni vipi amepata uwezo huo, lakini mambo yalibadilika tangu pale alipoliokota lile boksi la SASHA akiwa ndani ya uwanja wa uhuru wakati ule wa kuuga mwili wa Mheshimiwa Rais.

Je nini HATIMA ya mkasa huu wa kusisimua?

Ni vipi kijana David anajikuta ameingia katika jukumu zito mno ambalo linaibua vita kali, Vita ya Mapenzi, vita ya Kisasi, Vita ya kupambania uhai wake na uhai wa watu wengine anaowapenda.

Siri zilizofichwa zinafichuka, mazuri na mabaya yanawekwa bayana, Chuki inazaliwa, Michezo na drama za kutumia akili kubwa zinapelekea Damu kumwagika.

Endelea kufuatilia Simulizi hii ndani ya uzi huu humu humu Jamii forum napatikana WhatsApp namba 0756862047.

ITAENDELEA...
Good
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom