Simulizi: Sasha Mlinzi wa Nafsi - 1

SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........08
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...

Wakati gari waliyopanda David na Tesha ikizidi kwenda kwa kasi, upande wa pili Sasha akiwa juu ya farasi alionekana akiendelea kwenda mbele kwa kasi akipita katikati ya msitu ule mnene asijue huku nyuma alikotoka barabara ilikuwa ikijifunga.
Je nini kitafuata?

SASA ENDELEA....
Femi na Zucc wanawake waliotumwa na Handan kuhakikisha wanamuua David walionekana wakiwa wamesimama pembeni ya barabara. Tayari walikuwa wameshapanga ni namna gani watatekeleza mauaji ya kijana huyo ambaye amejikuta anaingia matatani tangu pale alipolishika boksi la Sasha kwa mikono yake.

"Wanakuja" Alisema Femi.
Zucc akiwa anatazama pembeni aligeuka kutazama upande wa pili wa barabara kwa mbali akaliona lile gari la Tesha ambalo kwa sasa David pia alikuwa ndani yake linakuja kwa kasi sana.
Femi na Zucc walikuwa wamepanga kusababisha ajali ambayo baadae itapelekea kifo cha David ili lengo lao litimie.

"Jitahidi kuwa makini Femi, ni NAFSI ya David pekee ndio tunaihitaji, hatakiwi kufa mtu mwingine tofauti na David"
"Usijali Zucc, ndani ya gari kuna watu wawili na watatu ni David, ni rahisi kuwalinda wengine na kumuua mmoja" Alisema Femi huku akisogea na kusimama katikati ya barabara.
Gari la Tesha likiwa limekaribia kufika pale walipo, Femi aliinua mkono wake wa kushoto akasogeza kiganja chake karibu na mdomo wake. Mara kuna moshi mweupe ukajitokeza juu ya kiganja cha mkono wake. Femi akavuta pumzi ndefu akiwa tayari kuupuliza ule moshi ambao ungekwenda moja kwa moja kwa dereva wa Tesha kisha kumchanganya na mwisho kusababisha ajali. Ajabu ni kwamba dereva wa Tesha hakuwa akimuona Femi pale katikati ya barabara.
David naye ambaye pengine angeweza kumuona hakuwa akitazama mbele, yeye alikuwa amejiinamia huku habari za mama yake kulazwa hospitali zikionekana kumchanganya sana.

"Femi achaaaa....!!" Mara Zucc alipiga kelele kumzuia mwezake.
Kwa kasi ya ajabu Femi aliruka na kusogea pembeni ya barabara tayari alishajua ni kwa nini mwenzake kamzuia asisababishe ajali ile waliyokusudia.
Kulikuwa na basi la abiria linakuja kutoka upande wa pili nyuma ya Femi, na endapo kama angelisababishia ajali gari la Tesha basi kulikuwa na hatari ya kutengeneza ajali nyingine ya basi hilo lililokuwa karibu kabisa.
Mwisho basi lile pamoja na gari la Tesha vilipishana salama salmini bila shida yoyote. Hii ikawa ni mara ya pili David ananusurika kuuawa.
"Huyu mtu inaonekana ana bahati ya pekee" Alisema Femi huku akionekana kukasilika mara baada ya kuipoteza nafasi ile.
"Tumfuate, safari hii tunamuondoa" Alijibu Zucc kisha wakashikana mikono wakapaa umbali wa mita kadhaa kisha wakapotea ghafula.

Upande wa pili katikati ya ule msitu mnene Sasha aliendelea kwenda kwa kasi akiwa juu ya farasi wake. Tayari alikuwa ameshaingia ndani sana ya msitu huo baada ya kwenda kwa zaidi ya dakika kumi.
Akiwa katika mwendo mara ghafula farasi akasimama. Ilikuwa ni hali iliyomshangaza Sasha kiasi, akajaribu kumpiga farasi wake asonge mbele lakini farasi akagoma kusogea, akajaribu tena na tena hali ikawa ni ile ile.
"Ooh! nini shida kipenzi changu" Alisema Sasha huku akimpapasa farasi wake lakini ghafula farasi alimrusha na kumtupa pembeni. Sasha alianguka chini akaumia mgongo, kabla hajafanya lolote farasi wake alikimbia huku akilia kwa sauti akatokomea kwenye msitu mnene.
Sasha akiwa pale chini ndipo aliposhtuka baada ya kugundua kuwa ile barabara aliyokuwa akiifuata imepotea ghafula, sasa alikuwa mwenyewe katikati ya msitu mnene.
Alijikongoja na kusimama kisha akawa anaangaza macho yake huko na kule. Hakuwa akiogopa hata kidogo mazingira kama hayo kwake yalikuwa ni ya kawaida, hayakumtisha.
Sasha alikuwa amedhamiria kwa dhati kuonana na Bi Noha kwa ghalama yoyote ile, alikuwa na shauku kubwa ya kuonana na mtu huyo.
Mara taratibu upepo ulianza kuvuma, upepo ambao ulikuwa ukiongezeka kadri muda unavyozidi kwenda. Sasha aliendelea kusimama imara huku akiangalia pande zote kwa ajili ya usalama wake. Hatimae upepo ukawa ni mkali sana kiasi cha kusababisha kimbuka kikubwa eneo lile.
Sasha alikimbia na kwenda kujificha nyuma ya mti mmoja mkubwa lakini hii haikutoshosha kimbunga kilikuwa ni kikali kiasi cha kuanza kung'oa miti iliyopa juu kama vipande vya karatasi, hali ilitisha mno. Sasha aliendelea kuushikilia ule mti lakini mwisho nao uling'oka na kupaa juu. Ajabu ni kwamba Sasha yeye hakubebwa na kile kimbunga, alibaki amejikunyata pale chini kwa zaidi ya dakika 5 mwisho hali ilianza kutulia na baadae kukawa na ukimya wa ajabu.

Sasha aliinua uso wake taratibu kutazama, alishangaa kuona mazingira ya eneo hilo yamebadilika kabisa. Lilikuwa ni eneo jeupe sana kila mahali kulikuwa kweupe, sakafu juu na pembeni kote kulikuwa kweupe. Mbele yake aliona mlango wa mbao ukifunguka akatoka mwanamke mmoja aliyevaa gauni refu lenye rangi ya machungwa. Alimtazama Sasha kisha akaachia tabasamu pana.

"Haujachelewa Sasha" Alisema yule mwanamke huku akimuonyesha Sasha ishara kuwa asimame na kumfuata. Bila woga Sasha alifanya hivyo, akapiga hatua na kuingia ndani kupitia ule mlango, baada ya kuingia yule mwanamke akaufunga.

Upande wa pili tayari David na Tesha walifika hospitali mahali alipolazwa mama yake David kama alivyoelezwa kwenye simu.
David alishuka kwenye gari upesi akawa anaelekea ndani ya hospitali hiyo. Tesha naye alishuka sekunde chache baadae, akawa anaongea na simu huku akipiga hatua taratibu sana kuingia hospitali.
David akiwa mwenye haraka tayari alishapata maelekezo chumba alicholazwa mama yake akawa anapiga hatua ndefu ndefu kuelekea huko.
Ilikuwa ni wodi ya wagonjwa wa kike chumba namba saba. David alifika akasimama mlangoni, akavuta pumzi ndefu kisha akaitoa taratibu. Alinyonga kitasa cha mlango akafungua taratibu na kuingia.
Uso kwa uso David akagonganisha macho yake na macho ya mdogo wake wa kike, aitwae Tatu. Wakati huo akawaona madaktari zaidi ya watatu wakiwa wamesimama kukizunguuka kitanda alicholazwa mama yake.

Upande wa pili nako mara baada ya Sasha kuingia ndani kupitia ule mlango wa mbao, sasa alikuwa ndani ya chumba kimoja kipana sana, mbele yake aliona wanawake watatu wakiwa wamesimama kukizunguuka kitanda ambacho juu yake alilala bibi kizee moja aliyeonekana kuzeeka sana.
Mara baada ya Sasha kuingia wale watu waliosimama waligeuka kwa pamoja kumtazama. Mmoja kati yao alikimbia nakwenda kumkumbatia Sasha kwa nguvu.

Tatu mdogo wake David alipomuona kaka yake ameingia alikimbia na kwenda kumkumbatia kwa nguvu huku akilia machozi.

Yule mwanamke aliyemkumbatia Sasha naye alikuwa akilia machozi.

"Kaka" Tatu aliita
Wakati huo daktari mmoja akasogea pale walipo
"Wewe ndio David?"
"Ndio mimi Daktari"
"Mama yako alikuwa akikusuburi sana tunakuacha ufanye naye mazungumzo kisha uje ofisini" Alisema daktari

Upande wa pili...
"Sasha" Yule mwanamke aliyemkumbatia Sasha aliita.
"Abeee"
"Bi Noha, amekusuburi kwa zaidi ya miaka 10, aliamini lazima ipo siku utakuja kabla ya kifo chake, hatimaye leo umekuja, haujachelewa Sasha. Tunakuacha ufanye naye mazungumzo muhimu" Alisema yule mwanamke.

Je, nini kitafuata?

Ni nini kinaendelea kati ya matukio haya mawili ya sehemu mbili tofauti lakini yenye kufanana?
Nini maana yake?
Hii ni SASHA MLINZI WA NAFSI sehemu ya 8 tukutane sehemu ya 9.


RIWAYA HII YA KUSISIMUA INAPATIKANA YOTE KWA TSH 1000 TU NJOO WHATSAPP NAMBA
0756862047.
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........09
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
"Kaka" Tatu aliita
Wakati huo daktari mmoja akasogea pale walipo
"Wewe ndio David?"
"Ndio mimi Daktari"
"Mama yako alikuwa akikusuburi sana tunakuacha ufanye naye mazungumzo kisha uje ofisini" Alisema daktari


Madaktari wote walitoka nje wakamuacha David afanye mazungumzo na mama yake pale kitandani kama alivyoomba. Mwili wake ulionekana kudhoofika sana, wakati huo hakuwa na uwezo hata wa kijitikisa.

"Da..david mwanangu" Mama David aliongea kwa taabu kidogo
"Naam mama niko hapa, pole sana mama Mungu atakusaidia utapona"
"Asante, so..sogea karibu mwanangu"
David akakaa kitandani na kusogea karibu na mama yake.
"David"
"Naam mama"
"Naomba ufanye kitu kimoja mwanangu"
"Kipi mama? Nakusikiliza.."
"Oa mwanangu"
Ilikuwa ni kauli iliyomfanya David atoe macho kwa mshangao, hakuwa ametegemea kama mama yake ataongea kitu kama hicho.
"Umesema?" David Aliuliza akahisi labda amesikia vibaya
"Mama yako nakaribia kufa David, sina mda mrefu sana wakuishi. Natamani sana kukuona unaoa kabla sijafa moyo wangu uta...."
"Mama unaongea nini, huwezi kufa"
"David, najua unajua kabisa mimi sio wa kuishi muda mrefu, za...za...zawadi yangu ya pekee ninayotamani kuiona kutoka kwako ni kukuona ukioa mwanangu"
"Lakini mama mimi bado sijawa tayari kuishi na mwanamke kwa sasa napambana kuwahudumia wewe na mdogo wangu Tatu"
"Achana na mimi, ugonjwa wangu hautibiki hata hivyo umri wangu umeenda. Tafuta mwanamke atakaye saidiana na wewe kumtibu mdogo wako Tatu" Mama David aliongea kwa msisitizo.


Wakati maongezi haya yakiendelea bado Tesha alikuwa amesimama mbele ya mlango wa kuingia ndani ya hospitali hiyo akiwa anaongea na mtu kwenye simu, baadaye akamaliza maongezi na kukata. Punde wakatokea waandishi wa chombo kimoja cha habari.

"Mambo vipi Miss Tesha" Alisalimia yule dada mwandishi akionyesha uchangamfu wa hali ya juu huku mpiga picha akiwa makini na kazi yake.
"Poa poa mambo vipi" Tesha aliitika
"Tunaweza kufanya mahojiano kidogo please kama hutojali?"
"No no, hapa ni hospitali shoga, sio mahala pake"
"It's okay tupo kazini pia, kuna watu tumekuja kuchukua taarifa zao hapa walinusurika na ajali ya treni, just a minute Tesha.. tupe muda kidogo tu"
"Sawa dakika moja"
"Poa poa.."
"Siku hizi huonekani, wala hufanyi promo ya mitindo yako mipya kama tulivyo kuzoea... Shida ni nini au umepumzika? watu wameenda mbali na kusema Tesha ni mjamzito je, kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?"
"Hao ni watu sio mimi...Kila mmoja ana uhuru wa kuongea kila anachofikiri ni sahihi. Ukweli ni kwamba nilisimama kidogo na ishu za kikazi ila watu wangu bado waliendelea kuwajibika so hakuna kilicho haribika na habari njema ni kwamba wiki hii nimeingia ubia na kampuni kubwa ya mavazi na mitindo nchini Marekani GMK Fashion Group, kwa hiyo tegemeeni makubwa kutoka kwangu..."
"Na vipi kuhusu msimamo wa mahusiano yako kwa sasa, still upo single kama unavyosema siku zote?"
"Hahahah Nooo! Am not single... soon nitaenda kumuweka wazi mkalia ini wangu"
"Wow tutegemee lini miss Tesha..."
"Nimesema soon, so ni suala la kukaa na kusubiri, as you know mimi nikiongea kitu lazima nikitimize"
"Sawa Tesha, Hivi karibuni umekuwa uki...."
"Hapana jamani inatosha next time"
Alisema Tesha akikatisha mahojiano yale mara baada ya kumuona David anatoka kinyonge sana nje ya hospitali. Waandishi wa habari walimshukuru kwa ushirikiano wake na mwisho wakaondoka wakati huo David akafika pale alipo.
"Vipi David kwema?" Aliuliza Tesha, David akawa kimya
"Mama anaendeleaje?"
"Tunaweza kukaa mahali tuongee kidogo Tesha?" Badala ya kujibu swali David naye akauliza swali
Tesha alitulia kwa muda kisha akakubali ombi hilo. Walitoka na kuongozana hadi kwenye mgahawa mmoja karibu na hospitali hiyo, wakatafuta sehemu iliyotulia wakakaa tayari kwa mazungumzo.
"Nambie David" Tesha alianzisha mazungumzo baada ya kuona David amekaa kimya kwa muda mrefu. Wakati huo mhudumu alileta vinywaji walivyo agiza na kuondoka.

Wakati huo huo wale wanawake wawili wasioonekana machoni pa watu yaani Femi na Zucc walitokea ghafula kwenye kona moja ya mgahawa huo. Wakawa wanamtazama David akiwa kwenye mazungumzo muhimu na Tesha.

"Tesha" David aliita
"Nambie"
"Nimekubali kuifanya kazi yako ila na mimi nina sharti langu moja.."
"Woow! Mchumba si ndio huyu, haya niambie ni sharti gani? Au unataka nikuongezee pesa kwa ajili ya matibabu ya mama yako. Sio shida niambie tu ni kiasi gani wanahitaji"
"Hapana sio hivyo Tesha"
"Owk! Ni sharti gani hilo?"
"Badala ya kuishia kuigiza uchumba kama unavyotaka tunaweza kuigiza hadi ndoa pia, yaani tukaoana kabisa" Alisema David kauli iliyomfanya Tesha aliyekuwa anakunywa kinywaji apaliwe ghafula.
"Eti nini?"
"Ndiyo, tu-fake ndoa... Na harusi iwepo" David alisisitiza.
Tesha alimtazama David usoni akaona kabisa anamaanisha kile anachokisema.
"Mungu wangu" Aliwaza Tesha...
Awali Tesha alitaka kuigiza mahusiano na David kwa ajili tu ya kumnasa mwanaume wake Felix ili amrudie lakini sasa David naye anakuja na wazo jipya la ndoa akiwa na lengo la kumridhisha mama yake mzazi kama alivyomuomba.


Upande wa pili...
Wale wanawake waliokuwa wamekizunguuka kitanda alicholala yule bibi mzee sana walitoka wote na kumuacha Sasha pekee.
Sasha alimtazama yule bibi kwa sekunde kadhaa kisha akapiga hatua kumsogelea. Akiwa amekaribia kumfikia Sasha akasimama.

"Sogea binti yangu usiogope" Alisema yule bibi(Bi Noha) huku akiwa bado ameyafumba macho yake.
Sasha akasogea karibu zaidi, yule bibi akafungua macho yake.

"Nimekuwa nikikusubiri kwa miaka mingi sana mwanangu, nilijua ipo siku utakuja kabla sijafa"
"Bila shaka wewe ndio Bi Noha?"

"Ndio mimi mjukuu wangu, haya niambie kwa nini unataka uniona?" Aliuliza Bi Noha.
Sasha akawa kimya, ni kweli kwa kipindi kirefu alikuwa anashauku kubwa ya kuonana na Bi Noha lakini katu hakuwahi kuwaza ni kwa nini hasa anatamani kuonana na bibi huyo.
"Hahahah, hahahah hujui...umekuwa ukitamani tu kuniona na hujui kwa nini hahah" Bi Noha alicheka sana kiasi cha kumfanya Sasha aone ndani ya kinywa cha bibi huyo kilichokuwa na upungufu wa meno karibu yote.

"Ngoja nikusaidie kujibu mjukuu wangu... HATIMA.... Hatima ndio imekufanya uje hapa mjukuu wangu, ilikuwa ni lazima tu uje kuonana na mimi uyasikie maneno yangu. Ni Hatima yetu mimi na wewe kukutana ndio maana na mimi sijafa mpaka sasa"

"Unamaana gani kusema Hatima Bi Noha?"

"Kila kitu na kila mtu ataishi kulingana na Hatima yake Sasha umekuja kwa sababu ni hatima yako. Sasha mjukuu wangu kwa sasa ISRA ipo mikononi mwako pamoja na wanadamu ambao tunazilinda NAFSI zao"
Alisema Bi Noha, Sasha akawa hajamuelewa kabisa. Bi Noha akajikongoja akainuka na kuketi kitandani kisha akaendelea kuongea.

"Sasha mjukuu wangu, unakazi kubwa ya kufanya katika ISRA wewe na huyu kijana...Mnaweza kuamua kuharibu au kutengeneza" Alisema Bi Noha huku akinyoosha kidole chake kuelekea ukutani, Sasha akatazamana uelekeo wa kidole cha bi Noha. Ukutani ilijitokeza picha ya kijana mmoja ambaye sura yake haikuwa ngeni machoni kwa Sasha, alikuwa ni David. Picha mfano wa runinga ilionyesha wakati ule Sasha alipokutana na David pale uwanja wa uhuru wakati akikusanya machozi.
Naam, ni David huyu huyu ambaye kwa sasa anaomba kufungua ndoa ya kuigiza na mwanadada mrembo Tesha.

"Huyu mwanadamu hakikisha unamlinda kwa gharama yoyote ile, bila yeye ISRA itateketea na kupotea kabisa. Nitakwambia ni kwa nini..." Alisema Bi Noha.

ITAENDELEA...

0756862047
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........10
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
"Huyu mwanadamu hakikisha unamlinda kwa gharama yoyote ile, bila yeye ISRA itateketea na kupotea kabisa. Nitakwambia ni kwa nini..." Alisema Bi Noha.



Sasha aliitazama picha ya David pale ukutani ambayo ilitumia kama sekunde 30 mwisho ikatoweka, akageuka na kumtazama Bi Noha.

"Sijakuelewa Bi Noha, huyu mwanadamu anahusiana vipi na ISRA kuteketea?" Aliuliza Sasha.
Bi Noha alitulia kwa muda kisha akaongea..

"Inaonekana hujui chochote Sasha... Hebu nikuulize kwanza swali mjukuu wangu, unajua kazi ya hayo machozi uliyoagizwa na baba yako ukayakusanye kutoka kwa wanadamu?"

"Hapana, baba aliniambia atanieleza kila kitu pindi nitakaporudi"

"Hahah! Gu Gamilo hajahawi kubadilika... Sawa, nakuuliza swali lingine Sasha unajua ni kazi gani kubwa tunayoifanya sisi WALINZI WA NAFSI, kazi ambayo ilitufanya tukapewa nguvu zaidi ya wanadamu, kisha tukatengwa huku ISRA?"
Sasha alitulia kwa muda akionekana kufikiri jambo kisha akajibu...
"Tunalinda NAFSI za wanadamu"
"Nafsi zipi?"
"Zipi?"
"Ndiyo zipi? Si kila nafsi tunapaswa kuilinda.."
"Hapana hilo simfahamu Bi Noha"
"Ni sahihi lazima usijue kitu, baba yako amefanya makosa makubwa kukufungia Ikulu kwa kipindi chote hiki, bado unamengi sana ya kujifunza...hujui kitu. Sikiliza Sasha kwa miaka mingi sana nimekaa hapa nikisubiri siku kama ya leo ifike siku ambayo nitakutana na mtu ambaye ameibeba hatima ya ISRA"

"Kivipi bibi, naomba unielekeze tafadhali..."

"Nitakuhadithia simulizi moja ya miaka mingi iliyopita kabla hata hujazaliwa..." Alisema Bi Noha lakini kuna kitu cha tofauti Sasha alikigundua kutoka kwa Bi Noha.
Kadri muda unavyozidi kwenda ngozi ya Bi Noha ilizidi kuongezeka makunyazi na kubadilika rangi kuwa nyeupe. Hata sauti ya yake ilianza kukwaruza na kufifia taratibu sana. Sasa hakuwa na nguvu tena ya kuendelea kukaa, akalala kama alivyokuwa mwanzo. Kitu pekee ambacho aliendelea kufanya ni kuongea. Alisema...

"Hapo awali mji wa ISRA ulikuwa ukiongozwa na watu wawili, wa kwanza alikuwa ni baba yako Gu Gamilo wa pili alikuwa ni baba yako mkubwa yaani kaka yake na baba yako aliitwa MAGNUS. Kwa bahati mbaya Magnus aliingiwa na tamaa ya uongozi, akatamani kila kitu kiwe cha kwake.
Hakuwa kiongozi mzuri kama wengi walivyo tarajia, alivunja taratibu nyingi na miiko ya Walinzi wa nafsi kwa makusudi kabisa. Mwisho tamaa yake ikazidi kuwa kubwa akaupeleka utawala wake hadi kwa wanadamu ambao ni dhaifu sana kwetu. Magnus hakuishia hapo alitamani kuitawala ISRA akiwa yeye peke yake. Akatengeneza njama ya kufanya mapinduzi lakini kwa bahati nzuri baba yako aliweza kumzuia kabla hajaleta madhara makubwa ndani ya ISRA. Magnus alikamatwa akanyang'anywa kila kitu na baadae akatupwa nje ya ISRA. Magnus hakuwa na uwezo wa kurudi tena ISRA lakini tayari alikuwa ameshatengeneza jeshi kubwa na matabaka ndani ya ISRA. Wale waliokuwa wanamtii waligeuka na kuwa waasi, na huo ndio ukawa mwanzo wa uvunjifu wa amani na kuwepo kwa uasi ndani ya ISRA, ni hao ambao mpaka leo wanapambana na baba yako kila kukicha. Lakini si kwamba habari za Magnus ziliishia hapo la hasha, kwa miaka yote hii Magnus amejificha katikati ya wanadamu na anajipanga upya kuja kupambana kwa mara nyingine kuuludisha utawala wake. Magnus ni nyoka hatari ndani ya ISRA, huko aliko anaanda jeshi kubwa la kupambana na sisi lakini pia hata ndani ya ISRA pia analo jeshi kubwa ambalo linasubiri siku atakayolejea kwa mara nyingine"
Bi Noha alieleza mambo ambayo ama kwa hakika yaliibua maswali mengi kichwani kwa Sasha.

"Kwa hiyo Bi Noha ni lini Magnus amepanga kuja kuivamia ISRA? Kama amekuwa akijipanga kwa muda mrefu kwa nini mpaka leo hajawahi kuvamia?" Aliuliza Sasha

"Hana uwezo wa kuingia ISRA na mtu pekee ambaye anaweza kumzuia Magnus asirudi ISRA milele ni huyu mwanadamu niliyekuonyesha, ndio maana nimekwambia unatakiwa kumlinda huyu kijana kwa gharama yoyote ile" Alisema Bi Noha

"Lakini nawezaje kumlinda mwanadamu ikiwa mimi niko huku ISRA?"

"Sasha mjukuu wangu Hatima ndio itaamua kila kitu, kitu muhimu na cha pekee ambacho nataka kukukumbusha ni kwamba hautakiwi KUPENDANA na mwanadamu. Katu usije kuruhusu hisia zako zikampenda mwanadamu" Bi Noha aliongea kwa msisitizo na hapo ngozi yake ya mwili ikawa ni nyeupe sana na nyepesi kiasi cha kuanza kuchanika katika baadhi ya maeneo mwilini mwake. Lakini Bi Noha bado hakuacha kuongea, hapo ndipo Sasha alipogundua kuwa kadri bibi huyo anavyoongea ndivyo anavyozidi kuchoka na kunyong'onyea.

"Bi Noha usiendelee kuongea tafadhali" Alisema Sasha.
"Usijali mjukuu wangu, ni salama..."
Alisema Bi Noha kisha akaachama mdomo wake na kuuacha wazi.

"Amekufa" Ilisikika ya kike kutokea nyuma ya Sasha. Alipogeuka akawaona wale wanawake aliowakuta awali ndani ya chumba hicho wanarudi tena mkononi mwao wakiwa wamebeba jeneza. Ni kweli Bi Noha alikuwa amekufa.



Upande wa pili...
Bado maongezi kati ya David na Tesha yalikuwa yakiendelea.

"Badala ya kuishia kuigiza uchumba kama unavyotaka tunaweza kuigiza hadi ndoa pia, yaani tukaoana kabisa" Alisema David kauli iliyomfanya Tesha aliyekuwa anakunywa kinywaji apaliwe ghafula.
"Eti nini?"
"Ndiyo, tu-fake ndoa... Na harusi iwepo" David alisisitiza.

Tesha alimtazama David usoni akaona kabisa anamaanisha kile anachokisema.

"Mungu wangu" Aliwaza Tesha, kisha akauliza.

"Kwa nini, mbona ghafula hivyo?"

"Kama wewe ambavyo hujaniambia sababu ya kutaka tuigize mahusiano ya uchumba na mimi sitokuambia kwa nini nataka tuigize ndoa" Alijibu David.

"No! Lakini mimi jambo langu ni rahisi Uchumba huwezi kulinganisha na ndoa, ujue nitatakiwa kukwita mume wangu. Unaona ni rahisi?"

"Tesha unaogopa labda unahisi baadae nitasema tuachane alafu nitake nusu ya mali zako, hapana sio hivyo. Tunaweza kuingia mkataba kama ukitaka" Alieleza David, lakini bado ulikuwa ni mtihani mgumu kwa Tesha kuamua.

"Nahitaji muda wa kufikiri David hili jambo sio dogo, na wala sijui ni kwani nini wewe unalirahisisha namna hii" Alijibua Tesha.

Lakini wakati wakiendelea na mazungumzo haya kwa mbali alionekana mwanaume mmoja aliyevalia nguo nyeusi na kofia inayoziba uso wake akiwapiga picha Tesha na David kwa siri pale mgahawani.

Zucc na Femi nao pia walikuwa hawachezi mbali, bado waliendelea kurandaranda mle mgahawani kuangalia ni namna gani wanaweza kutengeneza tukio ambalo litapelekea kifo cha David.
Ajabu ni kwamba licha ya wao kuwa na nguvu zaidi ya binadamu wa kawaida lakini hawakuruhusiwa kuua moja kwa moja, hii ilikuwa ni kinyume kabisa na taratibu zao (walinzi wa nafsi). Sheria yao ni kwamba hawaruhusu kuua mwanadamu kwa mikono yao bali kutengeneza tukio ambalo litasababisha kifo cha mwanadamu.

"Basi ni heri tuwekane wazi tu kwa nini nataka uchumba na wewe kwa nini unataka ndoa ili twende sawa maa..." Alisema Tesha lakini mara simu yake iliyokuwa ndani ya mkoba wake mdogo ilianza kuita, wakati akitaka kuichukua kwa bahati mbaya akasukuma ule mkoba wake ukawa unadondoka chini. David aliwahi haraka kutaka kuudaka lakini tayari Tesha alishaushika David akaishia kuudaka mkono wa Tesha.
Walibaki wanatazamana kwa sekunde kadhaa huku mkono wa David ukiwa juu ya mkono wa Tesha. Taratibu Tesha akahisi mapigo yake ya moyo yanaanza kubadilika. Sasa ilikuwa ni mara ya pili kwa Tesha kupatwa na hali hii..

Whatsap 0756862047.

Je nini kitafuata?
Nini kinaendelea kati ya Tesha na David?
Ni nani anawapiga picha kwa siri?
Femi na Zucc watatengeneza tukio gani kumuua David?
Vipi kuhusu Sasha?
Je ni kweli Magnus yupo?
Na kama yupo ni nani na yuko wapi?

ITAENDELEA...
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........11
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Walibaki wanatazamana kwa sekunde kadhaa huku mkono wa David ukiwa juu ya mkono wa Tesha. Taratibu Tesha akahisi mapigo yake ya moyo yanaanza kubadilika. Sasa ilikuwa ni mara ya pili kwa Tesha kupatwa na hali hii...
Je nini kitafuata?

SASA ENDELEA....
Haraka Tesha alitoa mkono wake kutoka kwenye mkono ya David huku akijikohoresha na kujifanya kama hakuna kitu kilichotokea.
"Mi naondoka..." Alisema Tesha
"Mbona ghafula?" Aliuliza David wakati huo tayari Tesha alishasimama.
"Ninadharula" Tesha alidanganya, kisha akachukua mkoba wake na kuanza kuondoka.
"Nitakupigia David tutaongea wakati mwingine..."
""Lakini hauna namba ya..." Alisema David, lakini alishindwa kumalizia sentesi yake kwani tayari Tesha alishafika mbali.

Tesha alitembea haraka haraka mara baada ya kutoka nje ya mgahawa huo alimpigia dereva wake simu akamataka asogeze gari. Sekunde chache baadae gari ilifika Tesha akafungua mlango na kuingia ndani. Baada ya kukaa kwenye kiti Tesha alivuta pumzi ndefu na kuitoa taratibu, bado mapigo yake ya moyo yalikuwa hayajatulia kabisa.

"Vipi bosi uko sawa?"
"Eeh! Niko sawa kwani vipi?" Tesha alijibu huku akijaribu kuvunga kama hakuna kilichotokea lakini ukweli hakuwa sawa. Hata yeye alikuwa akijishangaa ni kwa nini anapatwa na hali hiyo mara zote anapotazamana na David usoni au hata akimgusa.

"No haiwezi kuwa hivyo...bado nampenda Felix wangu" Tesha alijisemea mwenyewe kwa sauti ya chini mara baada ya kuwaza kuwa pengine hisia zake zinataka kuhamia kwa David.
Aliamini haikuwa rahisi hata kidogo kwa 'super star' kama yeye kuzama penzini na kijana wa mtaani asiye na mbele wala nyuma. Licha ya kwamba tayari alishamsifia sana David kwa kaka yake kuwa ataweza kumfanya mpenzi wake Felix kupata wivu na kurudi haraka Tanzania.


David alibaki ndani ya mgahawa ule akiwa amekaa vile ile kama alivyoachwa na Tesha.
"Sasa shida yangu nini... Au nimekosea kumshika? Lakini mbona ilikuwa ni bahati mbaya tu?" Alijiuliza David huku akiutazama mkono wake aliotumia kumshika Tesha.
"Hivi ni kwamba mimi ni masikini sana hadi kuugusa mwili wake nakuwa nimekosea?" David aliendelea kujiuliza maswali.
Lakini wakati akiendelea kujiongelesha mwenyewe mara alipotazama chini aliona pochi ndogo sakafuni. Kumbe wakati ule Tesha amekaribia kuudondosha mkoba wake ile pochi ilichomoka kutoka kwenye mkoba huo ikadondoka chini, hakuna aliyeona.

"Ohoo!" Alisema David wakati akiangaza macho yake pande zote kuangalia kama kuna anayemuona ndani ya mgahawa ule kisha taratibu akaivuta ile pochi kwa mguu wake wa kulia, akainama na kuiokota.
Licha ya kwamba David alifahamu fika kuwa pochi hiyo ni ya Tesha lakini hakusita kuifungua na kuangalia vilivyomo ndani.

"Woow! Mambo ya dollar..." Alisema David huku akitabasamu mara baada ya kuona noti nyingi za kigeni(dollar) zikiwa zimepangwa vizuri ndani ya pochi hiyo, akaendelea kupekuwa.
Baadae aliichomoa picha moja ndogo iliyokuwa ndani ya pochi hiyo ya Tesha. Ilikuwa ni picha iliyokatwa upande mmoja, na upande uliobaki ulimuonyesha Tesha akiwa ameweka pozi moja mujarabu huku akiwa amevalia nguo nyepesi za beach. Alikuwa amevaa Chupi na sidiria pekee huku akiwa ameweka pozi la kujibinua kiasi, alipendeza sana na kufanana na wale wanawake wa Kibrazili pale Ipanema Beach.

"Ooh! Mashallah Mungu fundi jamani... Huyu dada ni mzuri hakuna mfano...eti anataka tuwe wachumba kwa kuigiza nitaweza kweli? hebu muangalie lips zake mmh! Au ni malaika na hatujui" David aliendelea kujiongelea mwenyewe huku akimalizia kinywaji kilichosalia katika glasi aliyotumia Tesha . Kwa muda mfupi alijikuta anasahau habari za mama yake kule hospitalini.
Akazidi kuipekuwa pochi ya Tesha, mara akakutana na kitu ambacho hakutegenea. Ilikuwa ni paketi mbili za mipira ya kiume(Condom).

"Huhuuu hahahaha Tesha Tesha.... hahahha" David alicheka sana.

Wakati huo Zucc na Femi walikuwa nyuma yake hatua kadhaa kutoka pale alipokuwa, wakawa wanamtazama huku Femi akionekana kifurahishwa sana na Tabia za David, akawa anatabasamu kila wakati. Tofauti na Zucc yeye alikuwa amevaa sura ya kazi, wakati wote alikuwa akimtazama David kwa macho makali huku akipiga hesabu ni namna gani atayaondoa maisha ya mwanadamu huyo ambaye mpaka sasa tayari walikuwa wamepoteza nafasi mbili za kumuua.

Mwisho David alirudisha kila kitu mahali pake ndani ya ile pochi, akawaza aihifadhi tu atampatia Tesha watakapoonana kwa mara nyingine. Akaiweka ile pochi mfukoni kisha akainuka tayari kwa kuondoka.

"Samahani kaka haujalipa?" Mara sauti ya mhudumu wa kike ilisikika kutokea nyuma yake. David akasimama na kumtazama dada huyo ambaye alipiga hatua na kusimama mbele yake.
"Mbo..mbona yule dada niliyekuwa naye alishalipa" David alijibu huku akijiumauma, ukweli hakuwa hata na senti tano mfukoni, aliogopa.
"Hapana hajalipa kaka yangu"
"Sasa kwa nini hamkumdai anapoondoka?" David alifoka huku akiangalia njia akiwaza pengine akimbie.
"Tuna mdai vipi wakati wewe upo na ulibaki hapa?"
"Aaaah! Sawaa.. umesema sijalipa eeh!" Alisema David huku safari hii akiachia tabasamu pana kiasi cha kumshanga yule dada, tayari alikumbuka kuwa mfukoni anayo pochi ya Tesha yenye pesa za kutosha.
Kwa mbwembwe sana akaingiza mkono mfukoni akatoa ile pochi na kuifungua, akachomoa noti moja na kumpatia yule.

"Keep change" Alisema David,
Kauli hii ilimnyima uhuru Femi akajikuta nacheka kwa sauti, hakika David alionekana kumfurahisha sana.
Sauti hii ya kicheko ilipenya vizuri kwenye masikio ya David akageuka haraka kutazama. Mara hiyo Zucc na Femi wakapotea ghafula.
David aliangaza macho yake huku na kule hakuona mtu, kulia kushoto mbele nyuma kote hakukuwa mtu.
"Wewe ndio umecheka?" David alimuuliza yule dada muhudumu ambaye aliikunja sura yake akionekana ushangazwa na swali la David. Yeye hakuwa ameisikia sauti hiyo ya kicheko, kama ilivyokuwa kwamba ni David pekee ndiye aliyekuwa na uwezo wa kuwaona watu hao wa ajabu vivyo hivyo hata sauti zao aliweza kuzisikia yeye peke yake.
"Kwa hiyo haujacheka si ndiyo...!!" David alijijibu swali lake mara baada ya kuona yule dada ameonyesha hajui kitu.

Baada ya Zucc na Femi kupotea ghafula walitokea pembeni ya mlangoni nje ya mgahawa.
"Unakuwa kichaa sasa Femi, ni kipi kimekuchekesha?"
"Nisamehe bure Zucc huyu mwanadamu anavituko sana, kanifurahisha..."
"Yaani badala ya kuumiza kichwa kufikiria tunamuua vipi wewe unacheka kweli Femi?"
"Nimesema samahani Zucc, vipi umeshapata jibu tunamuua vipi?"
"Hapana, nimewaza tumuue moja kwa moja bila kutafuta sababu za kibinadamu la sivyo tutachelewa kurudi ISRA"
"Nini? Unataka tumuue moja kwa moja, hapana hatutakiwi kufanya hivyo Zucc tunavunja sheria" Alisema Femi wakati huo David alionekana akitoka mgahawani akawa anaondoka zake. Hakuwaona Zucc na Femi pale pembeni ya mlango.

Zucc alichomoa kile kisu chake kidogo akawa anapiga hatua kumfuata David kwa nyuma.
"Zucc usifanye hivyo tafadhali.." Aliongea Femi akijaribu kumzuia mwenzake, lakini Zucc hakumjali.

Je nini kitafuata?
David atakuwa salama?
Vipi kuhusu Sasha kule kwa Bi Noha?
Ni nani aliwapiga picha David na Tesha pale mgahawani?

ITAENDELEA....
0756862047
 
SASHA MLINZI WA NAFSI
Sehemu ya..........12
Mtunzi: Saul David
WhatsApp: 0756862047

ILIPOISHIA...
Zucc alichomoa kile kisu chake kidogo akawa anapiga hatua kumfuata David kwa nyuma.
"Zucc usifanye hivyo tafadhali.." Aliongea Femi akijaribu kumzuia mwenzake, lakini Zucc hakumjali.

SASA ENDELEA...

Upande wa pili, msituni alipo Sasha....
"Amekufa" Ilisikika sauti ya kike kutokea nyuma ya Sasha. Alipogeuka akawaona wale wanawake aliowakuta awali ndani ya chumba hicho wanarudi tena mkononi mwao wakiwa wamebeba jeneza. Ni kweli Bi Noha alikuwa amekufa.
Wale wanawake waliweka jeneza chini kisha wakaubebe mwili wa bibi kizee(Bi Noha) na kuuweka ndani ya jeneza lile baada ya hapo wakaliinua jeneza na kuingia nalo ndani ya chumba cha pili.

Sasha alibaki katika hali ya kuduwaa asijue afanye nini, kila kitu kilichokuwa kinatokea kilikuwa ni kigeni kwake. Kwanza kabisa alikuwa akiyatafakari maelezo ya Bi Noha ambaye kwa sasa ni marehemu. Ni maelezo yaliyokuwa na mafumbo makubwa kiasi cha kumfanya Sasha atamani kujua zaidi lakini ndio hivyo Bi Noha hakuwepo tena.

Bado hakujua ni namna gani ataweza kutekeleza jukumu alilopewa la kuhakikisha anamlinda kijana David ambaye ni mwanadamu wa kawaida tofauti kabisa na yeye.

Wakati akiwa bado amesimama mara kikasikika kishindo kikubwa kikiambatana na mtikisiko mnene wa ardhi. Wale wanawake wakatoka haraka hadi pale alipo Sasha, walionekana kuwa kwenye hali ya mshtuko kama ilivyo kwa Sasha. Wakampita na kutoka nje kabisa ya chumba kile.

"Msitu wetu umefikia kikomo chake...!!" Alisikika mmoja kati ya wale wanawake akiongea. Wakawa wanatazama juu.
Hali ya hewa ilikuwa inabadikika taratibu, ule mwanga mweupe ulitoweka, huku mawingu yakionekana kwenda kasi sana angani. Upepo nao ukazidi kuongezeka kiasi cha kuyafanya magauni marefu waliyovaa wale wanawake yapepe mithiri ya bendera kwenye mlingoti wake.
"Tumtoe Sasha hapa haraka..." Mwanamke mwingine akadakia. Wakati huo tayari Sasha naye alikuwa ametoka nje. Alistaajabu kuona hali ya hewa ilivyobadilika ghafula.

"Sasha..!" Mwanamke mmoja kati ya wale wanne aliita na kumsogelea Sasha, akamshika mikono yake yote miwili kisha akaongea kwa hisia sana.

"Sasha, mwisho wetu umefika...tayari Bi Noha ameikamilisha kazi yake. Hakikisha unayafuata na kuyatimiza yale yote aliyokwambia bila kukosea. Umepewa jukumu zito ambalo kuna wakati utaona kama linakuelemea, usikate tamaa endelea kupambana kwa ajili ya ISRA. Kuna mambo mengi makubwa na magumu utakutana nayo kuanzia dakika hii ukiwa ISRA na hata utakapotoka nje ya ISRA. Utakutana na vita ya kila aina kutoka kwa ndugu zako pamoja na Wanadamu. Wewe ni MLINZI WA NAFSI Hatima ya walinzi wa nafsi wote wa ISRA umeibeba wewe..."
Aliongea yule mwanamke huku maelezo yake yakikatishwa na mtikisiko mkubwa wa ardhi ulioanza taratibu na kuongezeka kadri muda ulivyozidi kwenda

"Muondoe hapa haraka, muondoeeee......" Wale wanawake wengine walipiga kelele kali mno kwa pamoja, kelele zilizopasua anga na kusikika upande wa pili nje kabisa ya msitu huo.


Handan mwanamke mahiri aliyepewa jukumu la kulinda usalama wa Sasha mtoto wa mkuu wa ISRA Gu Gamilo alionekana pembeni ya msitu alioingia Sasha. Uso wa Handan pamoja wa na wale wanawake wawili alioambatana nao ulionyesha kuwa na wasiwasi mwingi.
Tayari walishamaliza kupambana na wale viumbe wa ajabu ndipo wanapogundua kuwa Sasha hayupo amewatoroka.
Baada ya kufuatilia nyayo za farasi wakagundua kuwa Sasha aliingia msituni jambo ambalo hakuruhusiwa kabisa kufanya.
Handan alikuwa akiogopa sana kwani alimjua Mkuu wa ISRA ni mtu asiye na masihara hata kidogo endapo akigundua kuwa Handan amefanya uzembe na kumuacha Sasha akaingia ndani ya msitu huo basi kifo kilikuwa ni halali yao.

"Sasha huyu mtoto!!" Handan alilaani huku akipiga hatua kwenda mbele na kurudi nyuma, alikuwa amechanganyikiwa si kidogo.
"Tutanyaje Handan" Aliuliza mmoja kati ya wale wanawake wawili
"Tufanyaje sasa! Tutamsubiri atoke, na iwe kheri tu atoke salama la sivyo Mkuu atatuua wote..." Alijibu Handan.
"Kwa nini tusijaribu kumfuata tukamtafute kuliko kuendelea kusubiri hapa"
"Nini?" Handan Aliuliza huku akimtazama yule mwanamke kwa macho makali
"Aa.. na..naogopa anaweza kupatwa na jambo baya wakati tuna nafasi ya kuingia msituni kumsaidia"
"Kwani huzijui sheria za ISRA? Tangu lini ikaruhusu kuingia kwenye huu msitu bila ruksa, hata Mkuu Gu Gamilo mwenyewe akitaka kuingia ni lazima atoe taarifa kwa viongozi wote ISRA. Iweje sisi tuingie? Na usije thubutu kuufungua mdomo wako kuongea mbele za watu kuwambia kama Sasha aliingia kweye huu msitu. Itakuwa ni kesi kubwa ambayo hata Gu Gamilo mwenyewe hawezi kuibeba" Handan aliongea kwa msisitizo, akatulia kwa muda kisha akaendelea...

"Unajua adhabu atakayopata Sasha kama ikifahamika kuwa ameingia kwenye huu msitu? Unajua? Hujui... Ni kifo, watamuua... Sasa unahisi baba ataweza kumuhukumu mtoto wake kifo? Na kama akishindwa unajua nini kitatokea? Viongozi maadui wa Gu Gamilo wataleta shinikizo la Sasha kuuawa kitakachofuata ni vita. Alafu kwanza unaongea ongea tu tumfutate tumfutate, tunamfuata kupitia njia gani wakati njia haipo imepotea" Handan alizidi kufoka.
Ni kweli maelezo yake yalikuwa sahihi kabisa, kama utakumbuka wakati Sasha akikimbia na farasi wake kuingia msituni njia ilikuwa ikijifunga. Na hii ndio ilikuwa alama pekee kuashilia kama kuna mtu kaingia ndani ya msitu huo wa ajabu.

Wakati Handan na wenzake wanahangaika wasijue cha kufanya ghafula unatokea msafara wa watu karibu ishirini wakiwa na farasi wakija kwa kasi.

"Ooh! Mambo yameharibika sasa" Alisema Handan mara baada ya kuuona msafara huo.
"Ni akina nani kwani?" Aliuliza mmoja kati ya wale wanawake aliokuwa pamoja nao.
"Ni DUMAYO mjomba wake Sasha. Huyu mwanaume ni nuksi tupu, ni moja kati ya watu wenye nguvu na ushawishi mkubwa sana hapa ISRA" Alijibu Handan wakati huo msafara wa Dumayo ukawa karibu kuwafikia, wakapunguza kasi za farasi wao.

"Hakikisha mahuonyeshi wasiwasi wowote, Dumayo hatakiwi kujua kama Sasha kaingia ndani ya huu msitu" Alisema Handan na mwisho Dumayo na msafara wake wakafika walipo, wakasimama.
Handan na wale wanawake wawili waliinamisha vichwa vyao chini kwa heshima.
Dumayo akiwa katikati ya msafara huo aliwatazama Handan na wenzake mmoja baada ya mwingine huku uso wake ukionekana kujawa na dharau ya kiwango cha juu.

"Handan mwanamke shujaa mlinzi wa Sasha... Ni wapi mnatoka wakati huu? Usiniambie leo hii kwa mara ya kwanza Sasha karuhusiwa kutoka nje ya Ikulu?" Aliuliza Dumayo
Handan akainua uso wake na kumtazama Dumayo usoni, alionyesha kuwa na chuki kali dhidi ya mtu huyu. Ukiacha yule Magnus aliyekuwa na tamaa ya uongozi na baadae kufanya uasi lakini akaishia kufukuzwa na kutupwa nje ya ISRA, Dumayo naye alikuwa mmoja kati ya watu waliokuwa na tamaa ile ile kama Magnus.

"Si nje ya Ikulu tu, ametoka hadi nje ya ISRA..." Alijibu Handan kauli iliyomshtua kiasi Dumayo. Alibinua midomo yake kisha akatoa ishara fulani akiwataka watu wake wasonge mbele, nao walikuwa wakielekea Ikulu vilevile.
Waliendelea na safari lakini baada ya kupiga hatua kadhaa Dumayo akasimamisha farasi wake tena, ni kama vile aliona kitu kisicho cha kawaida. Akageuka na kuanza kurudi pale walipo akina Handan.

Kabla hajawafikia Dumayo akawa anaangaza macho yake kuelekea msituni, ni kama kuna jambo alikuwa anahakikisha. Mwisho akawafikia akina Handan

"Iko wapi njia ya kuelekea kwa Bi Noha? Kunamtu kaingia msituni? Ni nani? Sasha?" Dumayo aliuliza maswali mfululizo, Handan na wenzake wakainamisha vichwa vyao chini, hakuna aliyejibu.
Tayari Dumayo alikuwa na jibu sahihi. Aliamini kwa vyovyote vile lazima kuna mtu kaingia msituni na lazima atakuwa ni Sasha. Na huo ndio ulikuwa ukweli wenyewe. Dumayo akatabasamu na kuwaza...

"Hii ni nafasi nyingine ya kumnasa Gu Gamilo, kwisha habari yake...Anampenda sana Sasha hawezi kuchomoka kwenye hili.... Sasa ni yeye au Sasha mmoja wao ni lazima afukuzwe nje ya ISRA kama walivyomfanya Magnus. Nitahakikisha nashikilia hili suala mpaka kieleweke..." Aliwaza Dumayo

Mara ghafula wote walihisi miguu yao ikitetemeka, farasi wakaanza kupiga kelele na kurudi nyuma. Ilikuwa ni tetemeko la ardhi lililoanza ghafula.
Kufumba na kufumbua waliona kimbunga cha ajabu kikichomoza na kupanda juu kutokea katikati ya msitu ule, kimbunga hicho kiliambatana na mtikisiko mkubwa wa ardhi kiasi cha kusababisha ardhi kuanza kutengeneza mpasuko na kutitia chini katikati ya msitu ule.
Hali ilikuwa inatisha sana. Si Handan si Dumayo wala wafuasi wake, wote walipanda farasi na kukimbia mbali kabisa na msitu huo ambao sasa ulikuwa kwenye majanga makubwa. Miti ilikuwa iking'orewa na kurushwa juu huku mingine ikititia na kuzama ardhi. Msitu wa Bi Noha ukawa unatoweka kwa namna ya ajabu mno.

"Maskini Sasha! Nini kimetokea huko...? Ooh! Jamni naogopa mimi... Tafadhali toka ukiwa salama we binti" Aliwaza Handan.
Tukio hili liliutikisa mji wa ISRA, ndani ya dakika tano tu tayari ISRA yote ilikuwa na taarifa za kile kinachoendelea katika msitu wa Bi Noha.
Mkuu wa ISRA Gu Gamilo baba yake Sasha alionekana akiingia haraka haraka katika mkokoteni wake maalumu unaovutwa na farasi wanne wenye rangi nyeupe tayari kwenda kushuhudia tukio hilo la ki historia ndani ya mji wa ISRA.

Turudi upande wa pili...
Wakati dereva wa gari la Tesha akizidi kukanyaga mafuta kumrudisha bosi wake nyumbani mara Tesha alimtaka asimame ghafula.
"Nini tena bosi?"
"Nimedondosha pochi yangu pale mgahawani..."
"Mmh! Kwa hiyo turudi au? Si atakutunzia yule jamaa wako David sijui" Alisema Dereva
Tesha hakujali sana kuhusu pesa zake, lakini alipokumbuka vitu vingine vilivyomo kwenye pochi yaani ile picha ya utupu na ile mipira ya kiume(condom) akaona asimpe David nafasi ya kuikagua pochi yake, ni aibu.
"Hapana turudi" Alisema Tesha na mara hiyo dereva akageuza gari na kuanza kurudi.
Hakuna aliyejua kuhusu majanga mazito yanayokaribia kumkuta David ambaye yuko njiani kuuliwa na wale wanawake wa ajabu kutoka ISRA Zucc na Femi.

0756862047

Je nini kitafuata?
Sasha atakuwa salama?
Dumayo atafanya nini?
Magnus ni nani na yuko wapi?
Nini Hatima ya David, Tesha na Sasha?

ITAENDELEA....
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom