SteveMollel
JF-Expert Member
- Jul 12, 2015
- 8,803
- 25,442
- Thread starter
- #41
Si wajua vile tufanyavyo.Daah kumbe kumekucha sijatembelea jukwaa hili muda sasa.heko kwako steve maana nasoma kama nacheki movie flani hivi ya kutishatisha.
Si wajua vile tufanyavyo.Daah kumbe kumekucha sijatembelea jukwaa hili muda sasa.heko kwako steve maana nasoma kama nacheki movie flani hivi ya kutishatisha.
Karibu mkuu.Ahsante sana mkuu
Nawe pia.Asante tivie....uwe na siku njema!
*ROHO YAKE INADAI --- 07*
*Simulizi za series*
ILIPOISHIA
.
.
Mume wangu akashtuka sana. Ilikuwa ni kwasababu ya yule mtu aliyemkimbiza ndiyo maana akasahau. Tukapata sana maswali itakuaje, lakini mwishowe tukapuuzia, akinipa moyo kuwa kwasababu Kecie hayupo, basi mambo yatakuwa tu shwari.
.
.
Kumbe tulikuwa tumekosea kabisa kabisa, Alfonso …
.
.
ENDELEA
.
.
Mrs Garett akaweka kituo na kufuata machozi kwanza. Akameza mate na kutazama pembeni akiendelea kusema.
.
.
Basi kwakuwa tulikuwa tumekiuka kile tulichoambiwa na bwana Fringe, tukawa tunaishi kwa hofu kidogo labda pengine mambo yanaweza kukiuka, ila zikapita masiku pasipo jambo lolote kutukia. Tatizo lilikuwa tu kwamba, bado kwa upande wa mume wangu mambo yalikuwa yaleyale.
.
.
Hakuwa anapata kazi popote pale, maisha yalikuwa magumu magumu magumu. Ikafikia kipindi mume wangu akaniambia, mke wangu kwakuwa tulikosea yale masharti, basi tumfuate tena bwana yule tumweleze, labda anaweza kutusaidia. Sikuwa na lingine zaidi ya kumkubalia, akafunga safari na kesho yake akaja naye nyumbani.
.
.
Bwana yule akalalama sana kwa kufanyia uzembe jambo alilotuambia. Akasema kuwa yale yote tuliyoyafanya yalikuw bure, na basi kukata mzizi wa fitna, basi inabidi turudie tena lile swala upya. Lakini tutalirudiaje na wakati Kecie ameshakufa? Nikauliza.
.
.
Yule bwana, Fringe kwa jina, akatuambia ataongozana na sisi kwenda huko msituni, tumfukue Kecie na turejelee zoezi. Niliogopa sana, mosi kwenda msituni, pili kwenda kuona maiti. Nilihisi mwili umekuwa wa baridi, natetemeka kila kiungo, lakini … lakini sikuwa na machaguzi. Ilibidi nifanye tulichokubaliana.
.
.
Tukatoka majira ya saa tisa usiku tukiwa watatu. Nakumbuka siku hiyo mvua ilikuwa inanyesha sana. Baridi lilikuwa kali pia kiasi kwamba barafu zilikuwa zimejaa njiani.
.
.
Nikiwa nimejikunyata, tukaelekea huko msituni, siku hiyo hatukuwa tumebeba taa, wanaume wakachimba shimo na kumfukua Kecie. Mwili wake ulikuwa umejawa na udongo mweusi. Ulikuwa wa baridi mno kama barafu!
.
.
Yule bwana, Fringe, akaniambia niushike mwili huo, nami nikafanya vivyo. Akafungua mkoba wake na kutoa ile chupa yake ya kioo cha duara. Akaipangusa akisema maneno kadha wa kadha, mara ikaanza kuwaka ikiwa ya kijani! Akatutaka tuiwekee viganja chupa yake ile na kusema maneno aliyokuwa anayatamka.
.
.
Basi tukafanya vivyo, mwili wa Kecie ukazamishwa tena ndani ya shimo na mume wangu pamoja na bwana Fringe wakatenda kazi ya kuufukia. Walipomaliza, mume wangu akasema yale maneno ambayo bwana Fringe alimtaka ayatamke kisha kazi ikawa imeishia apo.
.
.
Ila kabla hatujaondoka, Bwana Fringe alituuliza, “Kuna yeyote aliyewaona wakati mnamzika Kecie mara ya kwanza?” mimi na mume wangu tukatazamana, akawahi kujibu, “Hapana. Hamna aliyetuona.”
.
.
Bwana Fringe akatabasamu, ila tabasamu lake lilinitisha zaidi. Mtu yule hakuwa wa kawaida. Kila nilipomtazama nilijikuta natetemeka kwa hofu. Na kila macho yangu yalipokutana na yake, nilihisi moyo wangu umesimama kwa muda. Sikuwa najua kwanini.
.
.
Alitutazama na kutuambia, kwa ajili ya usalama wetu, tutangaze kuwa Kecie amepotelea msituni. Haitakuwa hoja sana kwani watoto kadhaa huwa wanapotelea huko misituni. Lakini nilipata swali, watu wataaminije hilo kwa wepesi?
.
.
Bwana yule, Fringe, katika hali ya kustaajabisha akajua swali langu hilo kichwani, akanitazama na kunambia, “Usijali, Kecie atapotelea msituni na kila mtu ataamini hilo.”
.
.
Sikujua amemaanisha nini, ila jua lilipokucha, nikastaajabu asubuhi ya mapema mlango ukigongwa. Nilipoenda kufungua nikakutana na Kecie mlangoni. Moyo wangu ulishtuka mno. Kwa muda nilijihisi nimepoteza nguvu. Sikuwa najua nini cha kufanya!
.
.
Kecie akazama ndani na kwenda kuketi kitini. Nikiwa katika hali ya bumbuwazi, mara mume wangu naye akaja. Naye akashangazwa sana kumwona Kecie, ila Kecie hakuonyesha muitikio wowote ule. Alikaa pale kitini kana kwamba mdoli.
.
.
Ni baada ya muda kidogo ndipo alinitazama na kuniomba nimletee mdoli wake aupendao. Nikampatia. Na asikae sana, akaenda zake nje. Sikuwa najua anaelekea wapi, nilitaka kumfuata lakini mume wangu akanikataza.
.
.
“Mwache aende. Huwezi jua anaelekea wapi.”
.
.
Ni siku hiyo ndiyo nikaja kuambiwa kuwa Kecie alipotelea kule msituni watu wakiwa wana ushahidi wa kuwa na Faris huko kama mtu wa mwisho.
.
.
Tukiwa na mashaka, tukaenda kutazama lile shimo lake. Ajabu tukalikuta halijafukuliwa, lipo vilevile kama ambavyo tulikuwa tumeliacha. Tukastaajabu alitokaje humo. Lakini pia tukapata shaka sana kuhusu yule mtoto ambaye alikuwa naye kwa mara ya mwisho, yaani Faris.
.
.
Tulijiuliza je atakuwa ameona chochote? Ajabu baadae tukaja sikia taarifa kuwa mtoto huyo amekuwa bubu tangu hapo. Hakuwa anaweza kuongea kabisa isipokuwa kubwatuka vitu ambavyo havieleweki, vitu ambavyo havina maana.
.
.
Ila …
.
.
Mrs Garett akanyamaza kidogo. Akashusha pumzi ndefu kwa pua yake ndefu alafu akajifuta mdomo wake na leso.
.
.
Yule mtoto, Mrs Garett akaendelea kuteta, atakuwa ameona kitu. Ni wazi kuna kitu alikiona. Anataka kusema lakini hawezi. Amekuwa wa ajabu tangu hapo. Amekuwa wa kufungiwa hata leo hii.
.
.
Tulitoa taarifa ya upoteaji wa Kecie. Matangazo yakawa yanabandikwa mara kwa mara lakini tukiwa tunajua kuwa ni bure, lengo lilikuwa ni kulaghai watu tu.
.
.
Lakini mbali na hayo, tangu Kecie alipopotelea, hatukumwona tena. Japo nilisumbuliwa na ndoto za ajabu mara kwa mara hapo karibuni, sikumwona tena mwanangu huyo. Alikuwa ameenda zake.
.
.
Mume wangu akaanza kupata kazi, tena akitafutwa. Ajabu ni kwamba kazi zote alizokuwa anapata zilikuwa ni za kufanya kazi kwenye viwanda vya mbao. Kila alipofanya kazi kwa muda mfupi, akawa anapandishwa nafasi na hata mshahara.
.
.
Maisha yakawa mazuri haswa. Hata hapa katikati tukawa tumemsahau kabisa Kecie, japo kila tulipokuwa tunafanya jitihada za kupata mtoto zikawa zinagonga mwamba. Mpaka leo hii hatujabahatika kupata mtoto, wala dalili. Ndipo tukaona ni vema kutafuta mtoto yeyote wa kukaa naye nyumbani.
.
.
Mrs Garett akamtazama Olivia.
.
.
Ndipo tukampata yule binti yatima, aitwa Oliva.
.
.
Padri Alfonso akasafisha koo lake na kuuliza, “Ina maana matendo uliyoyafanya ndiyo yanakusuta kuja kutubu?”
.
.
Mrs Garett akatikisa kichwa na kusema, “Huenda matendo hayo ningelikuwa nimeyasahau. Ila nilichokujia hapa, ni kikubwa zaidi ya kutubu, kikubwa zaidi ya matendo hayo…”
.
.
“Ni nini hicho?” Padri Alfonso akauliza.
.
.
“Padri,” akaita Mrs Garett. “Nahitaji msamaha kwa Muumba wangu. Lakini pia nahitaji msaada …”
.
.
“Sema nakuskiza,” Padri Alfonso akanguruma.
.
.
.
**
.
.
.
Saa mbili usiku …
.
.
Watu kadhaa walikuwa barabarani. Nyumba ziizokuwa zimepakana na barabara zilikuwa zimewashwa taa kuangazia nuru.
.
.
Wakiwa njiani kutoka kanisani, walikuta gari nje ya nyumba yao. Mrs Garett akasimama ghafla na kumtazama Olivia. “Usiongee kitu chochote, sawa?” akamwonya. Olivia akaitikia kwa kichwa kisha wakaendelea na safari yao iliyokomea mlangoni.
.
.
Walimkuta Mr Garett akiwa ameketi sebuleni, anavuta sigara. Mwanaume huyo alitulia sana kana kwamba hakuna watu walioingia. Kiti alichokuwa amekalia kilikuwa chaenda mbele na kurudi nyuma. Uso wake ulikuwa hauonekani kwa wepesi kwa kujaliwa na moshi wa sigara.
.
.
Mrs Garett akamsalimu, hakuitika. Mwanamke huyo akamtaka Olivia aende chumbani, Olivia akatii. Mrs Garett akaketi na kumtazama mumewe kwa sekunde kadhaa. Mr Garett akasimamisha kiti chake na kuzima sigara akiuliza, “Umetoka wapi?”
.
.
Uso wake haukuwa na lepe la masikhara. Macho yake yalikuwa mekundu, na mdomo wake uliotoka kunyonya sigara ulikuwa mkavu na mweusi.
.
.
“Nimetoka kanisani,” akasema Mrs Garett. Ghafla mumewe akanyanyua kisosi alimokuwa anakung’utia majivu ya sigara, akamrushia mkewe ghafula. Kama si Mrs Garett kukwepa, kisosi hicho kilikuwa kinapasua uso wake. Kilienda kwa kasi na kujibamiza ukutani. Kikapasuka kwenye vipandevipande milioni!
.
.
.
.
***
.
.
.
LAKO JICHO.
Nimeandika tu mkuu, ila kama utangulizi ulivyosema, haya hutukia pia.Steve tafadhali hii hadithi ni based on true story au ya kutunga.maana imekaa km true stori kabisa.
Leo hadi nimekumbuka kuna jamaa zamani tukiwa tunaangalia nae muvi anapata hisia akiamini kwamba yale ni maukweli kabisa!sasa na leo mi hii stori nataka nijue
Kaka shusha chombo hicho arosto kali.Ila halahala, pengine story hii si kama uwazavyo kuwa.

Daaahh kiu haiishiAnayesoma, anajua hii kazi.![]()
*ROHO YAKE INADAI ---- 09*
*Simulizi za Series*
ILIPOISHIA
.
.
“Ndio,” akajibu Dokta, “Hiyo ndiyo maana yake, ndiyo maana nikashangazwa sana na mahali ulipoyatolea hayo maneno. Ebu niambie uliyasikia wapi? Kuwa mkweli, pengine naweza kukusadia.”
.
.
Dkt Hamill alimtazama Brian kwa macho ya kidadisi na hamu. Kabla Brian hajatia neno, akamuuliza, “Umeyasikia maneno hayo ndotoni au msituni?”
.
.
ENDELEA
.
.
“Sijayasikia huko,” Brian akatikisa kichwa chake. “Ni kutoka kwa rafiSki yangu anaitwa Faris. Yeye amekuwa mgonjwa hivi sasa, hawezi kusema jambo lolote akaeleweka. Niliona akiwa ameandika maneno hayo kwenye kingo yake ya kitanda!”
.
.
Dkt akanyamaza asitie neno. Aliminya tu lips zake na kuendelea kumtazama Brian.
.
.
“Dokta,” Brian akaita. “Waweza kunambia maana yake ni nini? Kwanini ameandika maneno hayo?”
.
.
Dokta akameza kwanza mate, kisha akamwambia Brian, “Muda wangu umekwisha. Sina muda tena wa kuongea na wewe. Tuonane kesho majira haya, sawa?”
.
.
“Lakini Dokta,” Brian akataka kuongea. Dkt Hamill akamzuia na kumkumbusha makubaliano yao ya mwanzoni kuwa maongezi hayo ni marefu na vivyo hatoyamaliza yote kwa siku moja. Basi Brian, kishingo upande, akanyanyuka na kuuendea mlango. Dokta akamkumbusha, “Usisahau kuja kesho. Uwe ndani ya muda.”
.
.
Akatikisa kichwa chake kuitikia na kisha akaenda zake. Siku hiyo alikuwa amegundua kitu kikubwa lakini kilichompa hofu zaidi. Alijikuta akitaka kufahamu zaidi kuhusu Halo, na je kuna mahusiano gani kati ya Halo na Faris? Na labda kupotea kwa Kecie msituni?
.
.
Wakati anajiuliza hayo akaona ni vema kama asipomficha kitu Dkt Hamill. Inabidi amweke wazi, labda atakuwa anfahamu kila shaka alilo nalo kichwani. Basi akaapa kesho yake atakapopata fursa ya kuonana na Dkt Hamill atahakikisha analifanyia kazi shauri lake.
.
.
Alipofika nyumbani, baada ya kula na kupumzika kidogo, akatoka pasipo kuaga. Akaenda nyumbani kwa Brewster, mwanaume mzee ambaye alimweleza mama yake juu ya safari yake ya kwenda nyumbani kwa wakina Faris, na pia kumtahadharisha asifanye tena hilo jambo.
.
.
Alitumai atapata mawili matatu kwa mzee huyo. Alikuwa na maswali kadhaa ya kumuuliza.
.
.
Basi kwa mwendo wa robo saa, akawa amefika nyumbani kwa mzee huyo. Ilikuwa ni nyumba ndogo iliyojitenga. Kulikuwa ni kimya sana. Nje ya nyumba kulikuwa kumejawa na majani makavu ya miti. Kibaraza hakikuwa kisafi, pia na vioo vilikuwa vimebadilisha rangi.
.
.
Juu ya paa kulikuwa na kunguru wawili wakimtazama Brian kwa macho ya pembeni kabla hawajalia mara mbili na kupeperusbha mbawa zao.
.
.
“... kuna yeyote ndani?” Brian aliita baada ya kugonga mara tano pasipo majibu. Aliacha kugonga akazunguka nyuma ya nyumba. Huko akakuta banda la nguruwe wawili wadogo. Akapumbazwa kuwatazama rangi zao na namna wanavyokula kwa kufakamia. Ila ghafla akasikia sauti kavu nyuma yake.
.
.
“Hey! We mvulana.”
.
.
Alipogeuka akamwona Brewster. Alikuwa amevalia shati refu na suruali pana. Uso wake ulikuwa mtulivu ila macho yake ya kizee ameyakodoa. Mashavu yake yaliyoanza kudondoka yalikuwa yamemezwa na vinyweleo vya ndevu vilivyosimama. Mdomo wake mwembamba ulikuwa unaonekana kwa hafifu kwasababu ya mustachi.
.
.
“We ni nani na unafanya nini hapo kwa nguruwe wangu?” akauliza Brewster. Brian akamsogelea na kujitambulisha, akamwambia ya kwamba amekuja kumtembelea kwani kuna maneno mawili matatu anataka kuyaongea naye.
.
.
“Ni wewe, Brian!” akastaajabu Brewster. Alikuwa ana tatizo la kuona mbali hivyo Brian alivyosogea karibu na kuongea ndipo akamtambua.
.
.
“Ila sina miadi na wewe,” akasema Brewster. “Pia sina cha kuteta na wewe. Nadhani mama yako alikuambia kila unachostahili kujua, mvulana.”
.
.
“Hapana,” akasema Brian. “Hakuniambia kila ninachokitaka zaidi ya kunipa vitisho. Nataka kujua kwanini? … ulinionaje?”
.
.
Brewster akanyamaza kwa muda. Akamtazama Brian kwa sekunde kadhaa kisha akamsogelea karibu na kuinamisha kichwa chake amtazame machoni. Brewster alikuwa mrefu kuliko Brian, kwahivyo alipofanya vivyo wakawa sawa. Uso wake wa kizee haukuwa unavutia. Macho yake yaliyoanza kufifia kiini yalitazama macho ya Brian na kisha akasema, “Kuna ambacho haukuelewa? … si kila kitu kimejawa na maswali, Brian. Muda mwingine kuwa mwerevu ni kufanya unachoambiwa pasipo kutia mashaka. Ni faida kwako … lakini tu kama unahitaji roho yako.”
.
.
“Kwanini unasema hivyo?” Brian akauliza. “Kwani kuna nini?”
.
.
“Kuna kifo,” akajibu Brewster. “Huko nyuma ya maswali na kutaka kwako kutafutia majibu … kuna kifo. Ni juu yako kuchagua, aidha maisha ama kifo.”
.
.
Brewster aliposema hayo, akaenda zake Brian akimtazama. Alipopiga hatua nane, akageuka na kumtazama Brian. Akamwambia, “Nenda nyumbani. Usifanye jambo lolote la kijinga.”
.
.
Mzee huyo akaenda zake asigeuke tena. Brian akabakia akisimama, akitazama huku na kule, na hatimaye akaenda zake. Alipitia kwa rafiki yake fulani kisha ndiyo akaenda nyumbani. Ilikuwa ni majira ya jioni ya saa moja sasa. Akamkuta mamaye akiandaa chakula cha usiku.
.
.
Akaketi sebuleni na kulaza kichwa chake kwenye kiti akitafakari siku yake nzima. Alitamani kumshirikisha mama yake lakini alihofia. Alishamkataza kuhangaika na mambo hayo, basi akawa anahangaika mwenyewe akipanga na kupangua vipande vya ‘pazo’.
.
.
“Amekuambia chochote?” sauti ya mama yake ikamshtua.
.
.
“Nani?” akauliza.
.
.
“Kwani umetoka wapi? Si kwa Brewster?”
.
.
“Umejuaje kama nimetoka huko?” Brian akauliza akiketi vema kitini kumtazama mama yake aliyekuwa amesimama hatua kadhaa toka kwake.
.
.
“Amekuja hapa kunambia.”
.
.
“Nani? Brewster?”
.
.
“Ndio. Amekuja hapa akaniambia ulienda kumwona.”
.
.
“Saa ngapi?”
.
.
“Si muda mrefu tangu uondoke. Vipi amekuambia kitu?”
.
.
Kabla Brian hajajibu, alikabwa na mawazo. Brewster amewezaje kufika hapo muda mfupi baada ya yeye kuondoka. Amefanya hilo kwa kasi gani? Mama yake alimshtua kwa kurejea kumuuliza, “Amekuambia nini?”
.
.
“Hajaniambia kitu … hamna kitu alichoniambia,” alimalizia akitikisa kichwa. “Wewe amekuambia nini?” akauliza.
.
.
Mama akaketi na kumtazama Brian, akasema, “Amenisisitizia uache kuyafuatilia hayo mambo.”
.
.
Brian akasonya na kunyanyuka. “Kuna siku utaniambia mambo mengine zaidi ya hilo?” akaenda zake chumbani na kubamiza mlango.
.
.
.
**
.
.
.
“Karibu,” alisema Mrs Garett akiufungua mlango kumkaribisha Padri Alfonso. Padri huyo alikuwa amevalia shati jeusi alilolichomekea vema, shingoni lilikuwa na doa jeupe. Mkono wake wa kuume alikuwa amebebelea Biblia ya zamani.
.
.
“Ahsante,” akasema kwa tabasamu, akazama ndani na kuketi kwenye kiti. Naye Mrs Garett akaketi akimwita Olivia ambaye alimwagiza alete chai kwa ajili ya mgeni.
.
.
Padri akautazama uso wa Mrs Garett uliokuwa umeharibika kwa majeraha, akamuuliza mwanamke huyo, “Ni mume wako?”
.
.
Mrs Garett akatikisa kichwa pasipo kutia neno. Macho yake yalikuwa mekundu, mdomo wake ulikuwa umevimba na upande wa juu wa shavu lake la kushoto kulikuwa kumevilia damu.
.
.
“Pole sana.”
.
.
“Nashukuru, usijali,” Mrs Garett akasema akijitahidi kutabasamu.
.
.
“Yupo wapi sasa?”
.
.
“Ameondoka. Alisema anasafiri hivyo atarejea kesho asubuhi.”
.
.
Padri akatikisa kichwa. Baada ya muda mfupi mlango ukagongwa, akaingia mwanadada aliyekuwa amevalia sare ya mtawa wa kike rangi nyeusi na nyeupe. Mwanamke huyo mrefu mwembamba alikuwa amebebelea chupa mkononi mwake na sanamu ya msalaba yenye ukubwa wa wastani.
.
.
“Anaitwa dada Magdalena. Tutakuwa naye kwa ajili ya sala,” alisema Padri. Mrs Garett akaagiza chai kwa ajili ya dada huyo.
.
.
“Karibu sana, dada.”
.
.
“Ahsante, nimekaribia.”
.
.
“Nimefurahi sana kuja kunitembelea, natumai tatizo langu litakoma.”
.
.
“Kwa uweza wa Mungu, litawezekana,” akasema Padri Alfonso. “Natumai tukitoka hapa, roho hiyo haitarudi tena kwenye makazi haya. Itakuwa mwanzo na mwisho!”
.
.
Basi baada ya maongezi hayo mafupi, mazingira yakaanza kuandaliwa kwa ajili ya sala. Olivia alikuja sebuleni, taa zikazimwa na mishumaa ikawasha na ile sanamu ya msalaba ikasimamishwa mezani.
.
.
Dada Magdalena akachovya mkono kwenye maji yaliyokuwa ndani ya chupa na kukung’utia kwenye kila kona ya sebule akiteta maneno kadha wa kadha ya sala. Baada ya hapo akaungana na Padri Alfonso kuanza kusali, Mrs Garett pamoja na Olivia wakifuatisha yale yaliyokuwa yanatamkwa.
.
.
Wakasali kwa takribani nusu saa. Wakiwa wanaendelea kufanya vivyo, Olivia akafungua macho yake na kuangaza. Akatupa macho yake huku na kule kana kwamba mtu anayehisi kitu.
.
.
Mbali na sauti ya sala, kuna sauti nyingine alikuwa anaisikia kwa mbali sikioni mwake ikinong’oneza. Sauti ya mtoto wa kike. Sauti ikimwita jina lake.
.
.
“Oliiviaaaa … Oliiviaaaa … njoo kwangu. Oliviaaaa … Oliviaaaa …. Njoo kwa …”
.
.
Mara akamwona binti mdogo mlangoni! Binti huyo alikuwa ameshikilia mdoli mkono wake wa kuume. Alikuwa anamtazama Olivia kwa macho makali na kinywa chake amekiachama.
.
.
Akaanza kupiga hatua kumsogelea Olivia. Hatua zake zilikuwa nzito kinyume kabisa na mwili wake. Kila alipokanyaga chini ilisikika tih! Tih! Tih!
.
.
Olivia akajawa na woga mkubwa, akapiga kelele kali sana na kumshtua kila mtu!
.
.
.
**
.
.
.
LAKO JICHO.
Ahsante mkuuDuuh simulizi inasisimua hasaaa.brovo kwa steve