Simulizi: Roho yake inadai

Simulizi: Roho yake inadai

*ROHO YAKE INADAI --- 13*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA
.
.
Basi Brian akaaga na kwenda zake. Mpaka anayoyoma Mrs Garett akawa anamtazama kwa namna ya kubanwa na maswali. Brian alimtibua kabisa akili yake na kumwacha kwenye hamu kubwa ya kutaka kujua.
.
.
Hata bado hakumweleza kijana huyo ujumbe aliopewa na mumewe, Mr Garett, ya kwamba Kecie anawinda roho zao.
.
.
Mrs Garett akajikuta anaona mate ni mazito kuyameza.
.
.
ENDELEA
.
.
Aliwasha gari na kutimka eneo la makaburini bado kichwa chake kikishindwa kabisa kuacha mawazo juu ya Brian. Alikuwa anahofia sana. Alikosa kabisa amani. Ni kivipi Kecie amwambie Brian amwokoe? Ni kwamba Kecie yupo hai au?
.
.
Mama huyu kwa muda akasahau kuhusu kifo cha mumewe. Hata kwa kiasi fulani akawa si mzingatiaji barabarani. Akiwa katika fikra zake hizo ni ghafula akamwona Kecie pembezoni mwa barabara! Haraka akaminya breki na kuangaza akiwa ametoa macho.
.
.
Breki yake kali ilisababisha nusura agongwe na gari lililokuwa nyuma. Dereva wa gari hilo alifoka kumtuhumu kwa ujinga huo. Lakini Mrs Garett hakuwa anajali. Pengine hakuwa hata anasikia kelele hizo. Alitazama kule alipomwona Kecie lakini ajabu hakuona kitu tena! Hakuwa Kecie bali mtoto fulani ambaye alikuwa anatembea ameshikwa mkono na mama yake.
.
.
Akashusha pumzi ndefu na kuendesha kujiondokea.
.
.
**
.
.
“Tushukie hapa,” alisema Dkt Hamill akizima gari. Alikuwa amevalia koti refu jeusi na kofia. Pembezoni mwake alikuwa ameketi Brian aliyekuwa anatazama huku na kule. Barabara ilikuwa pweke ikiwa imezingira na miti.
.
.
Hakukuwa sehemu ya kufurahisha hapa. Ni sehemu iliyojawa na misitu na ipo pweke. Miti yake ni mirefu na imefunga anga kujaza giza.
.
.
“Una uhakika?” akauliza Brian. Alihofia kushuka. Dkt Hamill alimtazama na kumtikisia kichwa alafu yeye akatangulia kushuka.
.
.
“Papweke na pakimya sana!” alisema Dkt Hamill akiwa anafunga vifungo kadhaa vya koti lake. Alimtazama Brian aliyekuwa anaufunga mlango wa gari, akamwambia, “Hapa palikuwa pamejawa na watu.” akamgoja Brian asogee karibu kisha akaendelea kueleza, “Kila mtu aliona ufahari kuwa karibu na Helo. Lakini habari ilipokuja kubadilika, wakamtenga. Na baada ya nyumba yake kuchomwa, watu wakahamishwa kupelekwa maeneo mengine …
.
.
Hapa pakabaki penyewe. Miti ikaota na kupazinga. Kukawa sehemu iliyosahaulika kabisa … sidhani kama kuna watu huja huku tena. Kufanya nini?”
.
.
Brian akiwa anatoatoa macho kuangaza, akauliza, “Iko wapi hiyo nyumba yake?”
.
.
Dkt Hamill akaonyeshea upande wao wa mashariki na kuanza kuufuata. Wakatembea kwa kama dakika tano, sasa wakaanza kuona mabaki ya nyumba fulani. Walipomalizia mwendo wao kwa dakika tatu, mbele yao sasa kukawa kumesimama nyumba kubwa ya ghorofa. Si nyumba, bali tuseme ghofu.
.
.
Lilikuwa bado lina makovu ya kuchomwa na kuungua. Lilikuwa limefichwafichwa na majani baadhi ya sehemu zake. Rangi yake ya kijivu, rangi ya kuungua, ilikuwa imegeuka na kuwa kijani kwasababu ya kutambaliwa na majani na matawi ya miti.
.
.
Lilikuwa ni ghofu kubwa. Na hivi halikuwa na watu na lipo misituni, lilikuwa laoghofya. Ni wazi ndani yake kutakuwa na wadudu ama wanyama ambao wangeweza kujeruhi mtu.
.
.
“Hapa ndipo alipokuwa anakaa,” akasema Dkt Hamill akitazama ghofu hili kila upande.
.
.
“Kumbe He --” kabla Brian hajamalizia, Dkt Hamill akamziba mdomo kwa kiganja chake. “Usitaje jina lake ukiwa hapa … sawa?”
.
.
Brian akatikisa kichwa kukubali. Dkt Hamill akatoa kiganja chake na kuendelea kutazama jengo lile.
.
.
“Kwanini?” Brian akauliza. “Kwanini tusitaje jina lake? Kuna shida yoyote?”
.
.
Dkt Hamill akamtazama Brian na kumwambia, “Shida ipo tena kubwa … simulizi zina kweli ndani yake kwamba ukitaja jina lake ukiwa hapa kwenye makazi yake, basi ataitikia wito wako na kujitokeza… sidhani kama ungelipenda hilo lijitokeze.”
.
.
Brian akanyamaza asitie neno. Basi wakalizunguka jengo hilo na kisha wakasimama mbele ya lango kuu la kuingilia.
.
.
“Tunaweza kuingia ndani kutazama?” akauliza Brian. Dkt Hamill akanyamaza kwa muda kidogo kabla hajasema, “Sidhani kama hilo ni wazo jema.”
.
.
“Ina maana tutaishia hapa baada ya kufunga safari yote hiyo?” Brian akatahamaki. Alikuwa ana hamu kubwa ya kuona na kutambua mapya. Basi Dkt Hamill kumtimizia haja yake, akamkumbalia, japo kishingo upande, wakaingia ndani.
.
.
Hakukuwa na kitu zaidi ya mabakimabaki tu. Majani yalikuwa yameota karibia kila sehemu pia tando za buibui zikiwa zimetalaki ndani ya eneo. Kulikuwa ni giza na pakimya sana.
.
.
“Nadhani inatosha, Brian,” akasema Dkt Hamill. “Twende sasa.” Lakini Brian hakuwa mwepesi kukubali. Ndiyo kwanza walikuwa wameishia sebuleni, kwanini wasitembelee kila eneo wakaona?
.
.
“Dkt Hamill kwanini unahofia?” Brian akauliza. “Kuna chochote ambacho hujanambia?”
.
.
“Hapana, ila sioni kama ni wazo zuri kuendelea kupekua nyumba hii,” akasema Dkt.
.
.
“Kwahiyo tulikuja kuishia nje tu?”
.
.
“Ndio. Si ulitaka kujua ilipo?”
.
.
Brian akanyamaza. Akaendelea kutazama huku na kule akitaka kujua zaidi.
.
.
“Brian, kama kuna namna ya kuepuka makubwa, basi tufanye hivyo. Hamna haja ya kuingia kwenye matatizo ya kujitakia, sawa? Mimi ni mzee sasa kuhangaikahangaika. Twende.”
.

Ila kabla Brian hajasema jambo, wakastaajabu mlango kufungwa! Wakatazamana kwa hofu. Dkt akarudia, “Twende! Twende, Brian!”
.
.
Wakaufuata mlango na kujaribu kuuvuta, haukufunguka! Wakahangaika sana pasipo mafanikio mwishowe wakaona wakatumie madirisha. Wakafuata dirisha la kwanza kabisa toka walipo, wakavunja mabaki ya fremuze na kutoka.
.
.
Ila wakati wanafanya vivyo, Dkt alijikata kidole chake cha mwisho. Kwakuwa hakukuwa na muda wa kungoja, walikuwa na haraka sana, Dkt Hamill hakujali. Muda si mrefu wakajikuta ndani ya gari na tayari ameshawasha watimke.
.
.
Baada ya mwendo wa dakika kadhaa, ndipo Brian akaona damu kwenye usukani. Dkt Hamill alikuwa anachuruza damu, na asioenakane kujali. Brian akatahamaki akimwambia,
.
.
“Unavuja damu!”
.
.
Dkt Hamill akatikisa kichwa chake asitie neno. Alionekana hayuko sawa. Sura yake alikuwa ameikunja kana kwamba anasikia maumivu na ana mawazo kwa wakati huohuo.
.
.
Brian akaona si vema akiendelea kumwongelesha. Akanyamaza lakini kila saa akiwa anamtazama Dkt na kile kidole chake kilichojeruhiwa.
.
.
**
.
.
Upepo ulipuliza kidogo na kukoma. Damu bado ilikuwapo pale dirishani na hata kwa pembeni yake. Haikuwa imekauka. Kwa mtu mwenye macho makali angeliiona na kama angeigusa basi angeliondoka na doa.
.
.
Baada ya upepo kukoma, kishindo cha miguu kilisikika kwa muda mfupi, na mara mtu mmoja ambaye hakuwa anaonekana kwa juu alijiri na kusogelea dirishani.
.
.
Mtu huyu alikuwa amevalia suruali nyeusi ngumu na chini akivalia viatu vyenye visigino vya kutesa sakafu na ncha butu. Kishindo chake kilionyesha ni mtu mzito mwenye kilo zake.
.
.
Alipofikia dirisha alisimama, akatia kidole chake kwenye matone ya damu yaliyokuwa yamedondoka kisha akapeleka kidole mdomoni kuyanyonya.
.
.
Alipofanya hivyo, matone yote ya damu yakapotea! Na dirisha lililokuwa limevunjika, likajirudi upya na kuwa kama lilivyokuwapo hapo awali.
.
.
.
**
.
.
.
“Dkt Hamill!” Brian aliita kwa hofu. Dkt alikuwa amechoka, macho yake yanarembua, mwili umekosa nguvu! Hakuweza kumudu gari. Brian akashikilia usukani na kufanya jitihada kusimamisha chombo hicho.
.
.
“Dkt Hamill!” Brian akaita. Akamtikisatikisa kichwa. “Dkt Hamill! Dkt Hamill!”
.
.
Dkt Hamill alikuwa amechoka mno. Macho yake yalikuwa mazito na mdomo ulikuwa wazi akihema kwa uzito. Brian akahofia sana. Akamtazama kidole cha Dkt Hamill, bado kilikuwa kinachuruza damu. Haraka akafanya jitihada za kumfunga kidole hicho na kisha akamhamisha kiti, akawasha gari na kutimka upesi.
.
.
Ni moja kwa moja akampeleka Dkt hospitalini. Akapokelewa na wahudumu na kuwekwa ndani kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
.
.
“Una uhakika?” Dokta akauliza.
.
.
“Ndio,” Brian akasema akitikisa kichwa. “Alijikata kidole tu, sikuona kingine zaidi ya hiko.”
.
.
Dokta akashusha pumzi na kwenda zake akimtaka Brian aendelee kungoja. Baada ya kama lisaa limoja, Dokta akamfuata Brian na kumtaka akaonane na mgonjwa kwani ameomba hivyo.
.
.
Brian aliyekuwa amepatwa na hofu, akanyanyuka na kwenda huko akisindikizwa na Daktari. Alipofika, daktari akaenda zake kuwapa faragha.
.
.
“Brian,” Dkt Hamill akaita. Sauti yake ilikuwa kavu isiyosikika vema. Brian akasonga karibu na kumtazama kwa macho ya huruma.
.
.
“Mimi sikuwa wa kuletwa hospitalini,” Dkt Hamill akasema kwa shida. Akageuza shingo yake kumtazama Brian. Akamtazama kwa sekunde kadhaa alafu ‘lips’ yake kavu ikasema, “Brian, sasa nitakuwa nimelaaniwa.”
.
.
“Na nani?” Brian akauliza kwa pupa. Dkt Hamill akakohoa kwanza kisha akatafuta hewa yake na kusema, “Nitakuwa nimelaaniwa na Helo … Brian, maisha yangu hayatakuwa sawa tena.”
.
.
.
***
 
*ROHO YAKE INADAI --- 14*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA
.
.
“Mimi sikuwa wa kuletwa hospitalini,” Dkt Hamill akasema kwa shida. Akageuza shingo yake kumtazama Brian. Akamtazama kwa sekunde kadhaa alafu ‘lips’ yake kavu ikasema, “Brian, sasa nitakuwa nimelaaniwa.”
.
.
“Na nani?” Brian akauliza kwa pupa. Dkt Hamill akakohoa kwanza kisha akatafuta hewa yake na kusema, “Nitakuwa nimelaaniwa na Helo … Brian, maisha yangu hayatakuwa sawa tena.”
.
.
ENDELEA
.
.
Brian akashangazwa na maneno hayo. Akamuuliza Dkt Hamill kwanini anasema hivyo? Je kuvunja tu dirisha ndiyo imekuwa ya kupata laana?
.
.
“Hapana, Brian!” akasema Dkt Hamill kisha akakohoa kidogo. Ilikuwa ni ngumu kuamini kama ameletwa hospitali leo. Ungeweza kudhani ni mgonjwa wa muda.
.
.
“ … Ni damu. Ni damu yangu iliyobaki kule,” akasema Dkt kisha akatulia kama mtu anayeishiwa pumzi, sasa anaitafuta. “Nilijua toka nilipokuwa nimejakata pale. Hayakuwa mazingira ya kawaida. Lakini bado tulifanya busara kuondoka mapema. Huenda mambo yangekuwa mabaya zaidi.”
.
.
“Nisamehe, Dkt Hamill,” Brian akalia. “Kama isingalikuwa mimi yote haya yasingejiri. Laiti ningekusikiliza …”
.
.
“Ssshhh! …” Dkt Hamill akamnyamazisha Brian. “Huna haja ya kulia Brian. Hakuna kosa lolote ulilolifanya kwani kama mimi nisngetaka kwenda mule ndani basi nisingelikwenda.” akamshika Brian mkono na kumminya akimtazama kwa sura inayojitahidi kuumba tabasamu.
.
.
“Brian, wewe ni kijana mwerevu lakini pia shupavu sana. Nimefurahi mno kukutana na wewe. Si vijana wengi wako kama wewe. Una kitu ndani yako. Najua unataka kuyajua mengi sana. Ila …” akakohoa. “Tazama yasije yakakugharimu.”
.
.
Aliposema hayo akatulia kwa dakika moja, alikuwa anatazama chumba alicholaziwa kana kwamba ni kipya machoni. Aliporejesha macho yake kwa Brian, akasema, “Ni bora nikafa.”
.
.
Kauli hiyo ikamshtua Brian, “Kwanini unasema hivyo, Dkt Hamill? Tafadhali usiseme hivyo!”
.
.
Dkt akatabasamu. Akamtazama Brian aliyekuwa na sura ya hofu kisha akasema, “Brian, mimi ni mzee sasa. Si kama wewe. Wewe bado damu yako yazunguka, mwili wako una joto na hata akili yako inayoendelea kukua inafanya kazi upesi.
.
.
Hutonihitaji tena mimi, Brian. Niliyokupa yanatosha. Nashukuru sana kwa kuwa na mimi japo kwa kipindi kifupi, umenipa faraja na ‘kampani’ ya rafiki.”
.
.
Hapa ndipo Brian akajifunza ya kuwa Dkt Hamill hana familia. Yu mpweke sana na amekuwa akiishi hivyo kwa miaka mingi sasa. Mke na watoto wake wote walikufa lakini hakumwambia Brian nini kiliwaua.
.
.
Kauli yake ya mwisho alimwagiza Brian aende nyumbani kwake, akamwelekeza wapi atapata ufunguo, azame ndani na kumletea nyaraka zake tatu kwenye kabati.
.
.
Brian akitumia gari la Dkt Hamill, akaelekea huko, kulikuwa ni kingoni mwa mji wa Boston. Akaukuta ufunguo alipoelekezwa, akazama ndani na kunyookea kwenye kabati.
.
.
Ilikuwa ni nyumba kubwa yenye vyumba takribani vitano ila vyote vikifungwa isipokuwa kimoja tu alimokuwa anaishi Dkt Hamill mwenyewe. Nyumba hiyo ilikuwa kubwa na kimya sana. Pia pweke. Brian alishangazwa namna gani Dkt Hamill alikuwa anaweza kuishi mwenyewe hapo.
.
.
Asipeleleze sana, akarudi kwenye gari na kuanza safari ya kurudi hospitali. Alichukua takribani dakika kumi tu kutokana na mwendo wake wa kasi. Alipofika, ajabu hakumkuta Dkt Hamill. Dokta akamwambia tayari mzee huyo amekufa, amehifadhiwa mochwari.
.
.
Akashindwa kuzuia chozi. Akajihisi kuishiwa na nguvu. Aliketi kwenye benchi kama mtoto yatima akiwa na kujiona mpumbavu kwa namna alivyofanya mzee huyo akafariki. Alijiona muuaji. Alijiona mwenye makosa.
.
.
Macho yake yakiwa yamejawa na machozi yaliyomfanya asione vema, Dokta akamjia na kumgusa bega. Akamkabidhi karatasi fulani na kumwambia, “Ni ujumbe wako alinambia nikupatie punde utakaporudi hapa.”
.
.
Kabla Dokta hajaondoka akamshika Brian begani mara mbili kumpa pole.
.
.
.
**
.
.
.
Saa moja jioni …
.
.
.
Brian alikuwa amejifungia chumbani kwake, uso wake ukiwa mwekundu, macho yake bado yanachuruza machozi. Kitandani kulikuwa kuna zile nyaraka tatu ambazo Dkt Hamill alimwambia akazichukue, pamoja pia na ujumbe aliopewa na Dokta kule hospitalini.
.
.
Alitazama nyaraka zile na ule ujumbe. Sijui alikuwa anawaza nini kichwani mwake. Kwa muda kidogo hakuwa anajua cha kufanya ilhali kila kitu kipo bayana ya kwamba yampasa atazame vilivyomo ndani.
.
.
Baada ya kutulia kidogo ndipo akachukua ule ujumbe kwenye karatasi, akaanza kuusoma. Uso wake ulikuwa umepooza. Macho yake yalikuwa yanatia huruma.
.
.
Taratibu akawa anapitisha macho kwenye ujumbe uliokuwa unasomeka kama ifuatavyo,
.
.
“Inabidi niende, Brian. Sidhani kama nitakuwa nimekuacha mpweke. Nimeenda kwenye ulimwengu wa pili. Ulimwengu ambao siujui moja wala kumi yake. Nimekamilisha maisha yangu huku duniani. Lakini nakusisitizia Brian, mimi nimekwenda. Ni hivyo tu. Endapo ukiniona tena muda wowote mahali popote, basi jua si mimi.
.
.
Kwenye hizo nyaraka tatu, tafuta muda usome kwa makini. Tafadhali usipuuze. Nakutakia kila la kheri ukatimize haja yako. Usiogope, Brian. Na usiache jitihada zako za kumwokoa Kecie. Huwezi jua utawaokoa na wakina nani pamoja naye.”
.
.
Ujumbe ulikwisha ukimwacha Brian akidondosha machozi. Kichwa kilikuwa kinamgonga na alijikuta anaumia sana moyoni. Anaumia mno. Alisaga meno yake kwanguvu akiangushia kichwa chake kitandani.
.
.
Hakukumbuka aliishia wapi kulia, usingizi ulimsomba kwa pupa sana kumpeleka kwenye ulimwengu wa kiza ila angalau wenye unafuu.
.
.
“Brian! Brian! Tih-tih!-tih!” alikuwa anaitwa na mlango unagongwa. Ni kama takribani dakika ishirini tangu alipozolewa na usingizi. Alihisi huenda anaota, ila ilikuwa ni uhalisia. Alikuwa anaitwa.
.
.

Mama yake alikuwa amesimama mlangoni akiwa ameshikilia kiuno chake kwa mkono wa kushoto, wa kulia akibondea mlango.
.
.
Mara punde mlango unafunguliwa Brian akiwa anafikicha macho yake. Alimtazama mamaye na kumuitikia kilevi.
.
.
“Uko sawa?” mama akauliza akifinyanga uso wake kwa hofu.
.
.
“Ndio … niko sawa!” Brian akaongea kivivu. Macho yake bado yalikuwa mekundu ila kwakuwa alitoka kulala, mama yake hakujali sana. Alishani ni usingizi.
.
.
“Mbona umelala pasipo kula?”
.
.
“Mama sisikii njaa.”
.
.
“Umekula wapi?”
.
.
Brian kimya. Mama akamtazama na kutaka kumuuliza tena kama yupo sawa, ila akasita. Akadaka kiuno chake kwa mikono yote alafu akamwambia, “Una mgeni wako sebuleni. Anataka kukuona hivi sasa.”
.
.
“Nani?”
.
.
“Mrs Garett. Fanya uje haraka.”
.
.
Mama aliposema hivyo akaenda zake kurudi sebuleni. Mama Kecie aliyekuwa ameongozana na Olivia walikuwa wameketi kwenye kochi la kwanza kabisa upande wa kulia wa mlango, akawaambia kuwa Brian yuaja muda si mrefu.
.
.
“Kweli hamtahitaji kitu?” mama Brian akauliza wageni huku akiwapatia tabasamu.
.
.
“Hapana,” Mrs Garett akasema akitikisa kichwa. “Tupo tu sawa, usijali.”
.
.
“Hata chai? Ni baridi jamani.”
.
.
“Sawa, tutashukuru.”
.
.
Mama Brian akaenda jikoni na kurejea na vikombe viwili vya chai, akawapatia Mrs Garett na Olivia. Taratibu wakawa wanavuta kimiminika hicho cha moto kumngoja Brian.
.
.
Punde Brian akafika sebuleni na kuwasalimu..
.
.
“Pole kwa usumbufu.,” Mrs Garett alisema akimtazama Brian. Kwa kumtazama tu mama huyu hakuwa sawa. Sauti yake ilikuwa ajabu na uso wake ulikuwa ulioganda. Hakuwa na lepe la furaha. Ungelitabiri vema hakukuwa na kitu kilichomfurahisha siku nzima ya leo.
.
.
“Usijali, Mrs Garett. Karibu.”
.
.
“Brian, nina shida sana. Nahisi maisha yangu yapo hatarini.”
.
.
Kauli hii ya upesi na iliyosikika vema ilimfanya Brian na mama yake wawe wasikivu zaidi.
.
.
“Baada ya mume wangu kufa, ni mimi ndiye yuaja. Naombeni mnisaidie.” Mrs Garett akaanza kububujikwa na machozi. “Kecie anataka kuniua kama alivyomuua baba yake. Anawinda roho yangu!”
.
.
Brian na mamaye wakatazama kwa puzo. “Kwanini Kecie akuue?” Briana akauliza. “Na kwanini alimuua baba yake?”
.
.
Mrs Garett kwa kujikaza, akasema kila kitu. Hakutaka yale ya mficha maradhi. Alikuwa anataka msaada haswa. Alipomaliza kueleza, akajikuta anatoa machozi zaidi na kupaliwa na kilio. Alikuwa anamwomba msamaha mwanaye.
.
.
Lakini kwanini alidhani Brian anaweza kumsaidia kwenye hilo?
.
.
“Ni wewe tu na sisi ndiyo hutokewa na Kecie. Lakini akija kwako hukuomba msaada. Akija kwetu hudai roho zetu,” alisema Mrs Garett akitoa macho yake mekundu. “Kama Kecie hukuskiza wewe, naomba utuombee msamaha, Brian!”
.
.
Mama Brian akamtazama mwanaye na kumuuliza, “Kecie, hukuomba umsaidie?”
.
.
“Ndio,” Brian akajibu na kuongezea, “Huniomba nimwokoe!”
.
.
“Umwokoe wapi? Kutoka kwa nani?”
.
.
Brian akamtazama mama yake na kumwambia, “Toka kwa Helo.”
.
.
“Ndiyo nani huyo?”
.
.
Kabla Brian hajajibu, akaona kitu dirishani.
.
.
.
***
 
Dah! Nilianza nayo kimasikhara hivii! Kadri niendeleavyo ndivyo mautam yanazidi kunibamba. Ahsante sana mkuu Steve Mollel.
 
*ROHO YAKE INADAI --- 15*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA
.
.
“Umwokoe wapi? Kutoka kwa nani?”
.
.
Brian akamtazama mama yake na kumwambia, “Toka kwa Helo.”
.
.
“Ndiyo nani huyo?”
.
.
Kabla Brian hajajibu, akaona kitu dirishani.
.
.
ENDELEA
.
.
Alikuwa ni mtoto akiwa amesimama na mwanaume mweusi asiyeonekana lakini wenziwe walipoangazia huko, hawakuona kitu! Kila kitu kilikuwa kimepotea katika kasi ya kufumba na kufumbua.
.
.
“Kuna nini, Brian?” Mama yake akauliza.
.
.
“Kulikuwa na mtoto akiwa amesimama pale na kando yake kuna mtu!” akasema Brian akinyooshea kidole kule dirishani. Ila hakukuwa tena na kitu! Na si kwamba watu hawakumwamini, la hasha. Ni kwamba tu hawakufanikiwa kushuhudia.
.
.
“Brian! Kecie atakuwa ananifuata mimi!” akasema Mrs Garett akijawa na woga. Aliangazaangaza huku na huko. Hakuwa na amani. Hofu aliyokuwa nayo ilikuwa ni ile iliyo kuu.
.
.
“Usijali, Mrs Garett!” Mama Brian akamfariji. “Leo utalala hapa wewe pamoja na Olivia. Nadhani msiba wa mumeo utakuwa umekuathiri.”
.
.
Mama hao wakakumbatiana. Mama Brian akaendea chai ya Brian na ya kwake wakaendelea kukaa hapo wakiteta. Lakini kila saa Mrs Garett akawa anamsisitizia Brian ya kwamba endapo Kecie akijiri basi amwambie ya kwamba anaomba msamaha. Ambakizie roho yake.
.
.
Usiku ukazidi kukua na mwishowe kabisa wakaenda kulala. Mrs Garett alienda kulala na Mama Brian huku Olivia na Brian kila mmoja akilala chumba chake.
.
.
Usiku huo wakati watu wakipambania kupata usingizi, Brian yeye akawa ndiyo anautumia huo muda kusoma zile nyaraka za Dkt Hamill. Zilikuwa ni za kuogopesha lakini hakuwa anataka kuzieka chini mpaka kumaliza. Haikuwa kazi nyepesi.
.
.
Basi na sehemu ya nyaraka hii yasomeka kama ifuatavyo …
.
.
“… Kifo kina wivu sana. Kinatutenga na wale tuwapendao. Kimeniacha na kidonda kikubwa sana kwani kichwa changu kimekuwa hakikomi kuwaza na kukumbuka matabasamu ya mke na watoto wangu. Waliniacha kipindi nawahitaji sana. Pengine waweza kuwa unanionea huruma, lakini utakapomaliza kusoma haya, labda utaniona mimi ni mkatili sana. Mtu asiyestahili huruma hata lepe.
.
.
Basi ningalikuwapo kijana nilikuwa mtanashati sana. Mwenye nguvu na kaliba ya kufanya kazi kwa bidii. Doa langu lilikuwa moja tu, nalo ni kupenda sana kujifunza na kujua. Sikuwa na jambo dogo, na niliamini kila lionekanalo kidole basi lina mwili mzima.
.
.
Kutokana na hulka yangu hiyo, nikawa napenda sana kujitenga na kujisomea. Lakini pia kuchangamana na watu kuwauliza mambo kedekede ambayo nilikuwa nataka kuyafahamu.
.
.
Baba yangu, Mr Lambert, alikuwa ni mtu mkorofi sana. Kwenye moja ya shamba lake la pamba alikuwa na watumwa weusi kumi na tano. Hakuwa anapenda kuniona nikichangamana na watumwa hao. Mara kadhaa alikuwa ananiadhibu kwa kunikuta nikiwa nakaa na kuongea nao, lakini sikuwa naskiza.
.
.
Watumwa hao walikuwa na simulizi tamu sana, haswa mwanamke mmoja mzee aliyekuwa anaita Jasmine. Yeye alikuwa akiniona anafurahi na kunikumbatia tofauti kabisa na mama yangu. Alikuwa ananipenda sana, na alikuwa anajua nini napenda pia.
.
.
Angeniweka kwenye mapaja yake na kuniambia simulizi mbalimbali, hata za kule Afrika. Lakini kwasababu ya umri wake, alikuwa ameona mengi. Alikuwa ni mkubwa kuliko hata baba yangu. Alinihadithia mambo mengi ya Boston ambayo hata baba yangu hakuwa anafahamu.
.
.
Ni yeye ndiye aliyenieleza juu ya familia ya Helo. Kipindi kile akiwa msichana , japo bado mtumwa, alikuwa anatoroka kwenda kwenye maonyesho ya bwana huyo. Japo ilikuwa hairuhusiwi kwenda, na hata huko kwenye vibanda, watu weusi walikuwa hawatakiwi, hakukoma kwenda kufurahisha nafsi yake.
.
.
Alikuwa ni jasiri. Mgongo wake ulijawa na makovu ya kupigwa, lakini hakuwa anaskiza. Alikuwa anaufuata moyo wake. Siku moja nilimuuliza, huoni kuwa mgongo wako unaisha kwa ukaidi? Basi akatabasamu na kunitazama na macho yake mekundu. Akanishika mashavu na kuniambia,
.
.
“Kuna furaha gani kwa mtumwa aliye ndani ya minyororo? … hata nikikaa hapa, bado nitaonekana mkaidi kwa maana mtumwa hupewa jina hilo tangu na uzao wake. Maisha yake ni mafupi na yanapokoma hukusanywa kama kiroba na kutupiwa shimoni.
.
.
Hamill, huoni kuna haja ya kuthubutu kutafuta tabasamu langu hata mara moja kwa miaka yote hiyo?”
.
.
Hakika alinitia moyo sana na alinifanya nifuate nikipendacho pasipo kujali nini kitanitokea. Ilimradi nina furaha, basi yatosha.
.
.
Lakini siku ile wakati Helo anachomwa moto baada ya kugundulikana kuwa ni mlozi, Jasmine alishuhudia kila kitu kwa macho yake. Alikuwa bado ni binti. Na kitu kile kilimuumiza sana. Hata alipokuja kunihadithia, japo ni miaka mingi ilipita, bado macho yake yalikuwa yanageuka kuwa mekundu. Na hakukoma kunihadithia hilo mara kwa mara.
.
.
Hatimaye tabasamu lake lilikuwa limekoma. Hakuwa na la kumfurahisha tena isipokuwa mateso ya kitumwa tu. Lakini katika hilo nilikuja kugundua kuwa Jasmine alikuwa na ratiba ya kwenda msituni mwenyewe, tena pasipo kumuaga mtu.
.
.
Mara kadhaa nilipokuwa namtafuta, hakuwa bandani wala shambani. Nilipomuuliza, hakuwa radhi kuniambia. Hivyo nikapanga kujua ni wapi huwa anaenda japo kwa siri. Niliwaza pengine atakuwa amepata kitu kingine cha kumfurahisha.
.
.
Siku hiyo wakati namfuatilia nikaenda naye mbali kuzama msituni. Hakuwa anajua kama mimi namtazama kwa mbali. Alienenda ndani kabisa mpaka kwenye ghofu fulani kubwa. Humo akazama ndani na kukaa kwa dakika kadhaa.
.
.
Sikujua alikuwa anafanya nini humo ndani. Nilitamani sana kujua. Ila kwa kuhofia kuonekana, ikabidi nikae mbali. Alipotoka nikakimbia upesi kurudi nyumbani.

Siku iliyofuata hakwenda tena kule. Nikamfuata na kumuuliza, wapi huwa anakwenda? Mbona kuna muda namtafuta, simwoni! Hakunijibu, bali akaniuliza akinitazama kwa macho ya kuumba, ‘Hamill haujui ninapokwenda?’ Nikapandisha mabega yangu juu nikisema, sijui.
.
.
Akatabasamu na kuendelea na kazi yake ya kufuma nguo. Nikadhani labda atakuwa aliniona nilivyokuwa namfuatilia, basi nikaona niwe mpole, nikamuuliza kule alikuwa ameenda kufanya nini?…”
.
.
Hapa ndipo Brian alikuwa ameishia kusoma kabla hajasikia kelele kali zilizomshtua. Alidhani pengine ni masikio yake, ila alipotulia vema akasikia sauti zingine. Hapo akaamini kuwa ni uhalisia! Kelele zote hizo usiku za nini?
.
.
Haraka akafungua mlango na kutoka nje. Akaenda chumbani kwa mama yake alipomkuta Mrs Garett akipiga makelele na mama yake akiwa anamtuliza. Akauliza nini kimejiri.
.
.
“Mrs Garett amemwona Kecie bafuni!” Mamaye akamjibu. Uso wake ulikuwa umeelemewa na usingizi, mshangao na woga.
.
.
“Yu kwapi Olivia?” Brian akauliza.
.
.
“Chumbani huko!” mama yake akajibu. Kwa haraka Brian akapata wazo la kwenda kumwona binti huyo. Alifungua mlango pasipo hata kubisha hodi, akatupa macho yake kitandani.
.
.
Olivia hakuwapo!
.
.
Akatafuta kwenye kabati, chini ya kitanda na nyuma ya mlango. Olivia hakuwapo! Haraka akarudi kule kwenye chumba cha mama na kuwaambia kuwa Olivia hayupo! Wakamtafuta nyumba nzima, kweli hakuwapo.
.
.
Wakiwa sebuleni, kwa mbali huko nje, Brian akamwona binti akiishilia na barabara! Akapayuka, “Yule kule!” haraka akafungua mlango na kumkimbilia binti huyo.
.
.
“Olivia! … Olivia!” alimwita lakini Olivia hakuitikia. Aliendelea kutembea akitazama mbele. Brian akamfikia na kumnyanyua juu, akamwita, “Olivia! Olivia!” akiwa anampigapiga makofi shavuni kumwamsha.
.
.
Macho ya Olivia yalikuwa yanatazama kule mbele alipokuwa anaenda. Kuna kitu alikuwa anaona. Akakinyooshea kidole. Lakini Brian alipotazama hakuona jambo.
.
.
“Kuna nini Olivia?”
.
.
Olivia hakuwa mtu anayejielewa. Bado macho yake yalikuwa yanaangazia kule mbele. Hakuonekana kama anasikia hata kile anachoambiwa.
.
.
Baada ya muda fulani ndipo akamtazama Brian. Macho yake yalikuwa yanatisha. Na Brian asifahamu kinachoendelea, akajikuta anadondoka chini na kupoteza fahamu!


Hewa inakuwa nzito sana. Hata harufu nayo pia inabadilika na kumfanya Brian apige chafya na kukurupuka. Hakuwa kwenye mazingira anayoyajua. Hapa chumba kilikuwa ni chembamba na kuta zake zilikuwa hafifu, kukuu.
.
.
Mwanga ulikuwa hafifu sana. Mwanga ulioshindwa kupambana na giza.

Brian akatazama kushoto na kulia. Hakumwona mtu. Alikuwa anatamani kunyanyuka, lakini mwili haukuwa na nguvu kabisa. Ni shingo tu ndiyo ilikuwa na uwezo wa kupeleka kichwa huku na kule.
.
.
Punde mlango ukafunguliwa, Brian akatazama huko. Akamwona Kecie na gauni lake. Mkononi alikuwa na mdoli. Binti huyo akamsogelea karibu na kumtazama machoni.
.
.
“Brian, naomba niokoe,” akasema kwa sauti ya upole.
.
.
“Nikuokoe na nini, Kecie?” Brian akauliza.
.
.
“Mimi ni mfungwa, Brian,” Kecie akasema. Mkono wake wa baridi ukamshika Brian. “Nipo kifungoni, nataka kutoka roho yangu iende kwa amani.”
.
.
“Nani amekufunga, Kecie?” Brian akauliza. Kecie akatazama mlangoni na kupanyooshea kidole pasipo kusema kitu. Ajabu, Brian akapata nguvu ya kunyanyuka. Akatoka kitandani na kuuendea mlango, akaufungua na kutazama nje.
.
.
Kulikuwa na korido ndefu sana. Sakafu yake haikuwa inaonekana kwani imetwaliwa na moshi. Kutani kulikuwa na fremu za picha na kwa mbali kulikuwa kunasikika sauti nzito ya mwanaume ikinena na hata kucheka.
.
.
**
 
*ROHO YAKE INADAI --- 16*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA
.
.
Kulikuwa na korido ndefu sana. Sakafu yake haikuwa inaonekana kwani imetwaliwa na moshi. Kutani kulikuwa na fremu za picha na kwa mbali kulikuwa kunasikika sauti nzito ya mwanaume ikinena na hata kucheka.
.
.
ENDELEA
.
.
Brian akapata shaka na walakini. Akatazama nyuma kumwangalia Kecie, Kecie akamnyooshea kidole huko huko mbele. Lakini Brian hakuwa anajua cha kufanya. Alinyanyua miguu yake kwenda mbele akiwa hafahamu anaenda kukutana na nani.
.
.
Sakafu ilikuwa ya baridi kupita kiasi. Ilimfanya atetemeke na akunjekunje vidole vyake kila alipokuwa anakanyaga. Kwenye kuta, zile picha zilizokuwa zimetundikwa, zikawa zinanyamaza na kumtazama Brian alipokuwa anapita.
.
.
Picha hizo zilikuwa ni za sherehe. Zilikuwa ni za vifijo cha kipindi kile ambapo Helo alikuwa anatumbuiza. Bado picha hizo zilikuwa hai. Watu walikuwa wanafurahia na kushangilia mazingaombwe ya Helo, lakini Brian akitazama zilikuwa zinaganda na kuwa picha kamili!
.
.
Brian akazitazama akisonga. Moyo wake ulikuwa unapiga kusema hofu iliyomtawala. Kadiri alivyokuwa anasonga kwenda mbele, ndivyo sauti ile aliyokuwa anaisikia kwa mbali ikawa inamjongea na hata kuleta maana.
.
.
Kuna muda ilikuwa ni wimbo waimba. Na kuna muda kulikuwa na sauti ya mwanaume ikifoka ama kuteta. Mwanaume huyo ni nani? Na wimbo huo - ngoja! Atakuwa ni Helo. Brian alikuwa na kikao kichwani mwake. Na huyo anayemfokea ni nani?
.
.
Hakukuwa na majibu zaidi ya yeye kusonga na kutazama kwa macho yake. Japo alikabwa na woga, hakika alitaka kujua. Alipofika kwenye mwisho wa korido, taratibu, akachomoza kichwa chake kuchungulia sebuleni.
.
.
Kwa macho yake akamwona mwanaume fulani mzito aliyekuwa amevalia kofia ndefu kichwani yenye michirizi mekundu kwenye kingo zake. Mwanaume huyo alikuwa amevalia nguo za sherehe, zinazometa na kuvutia.
.
.
Koti jeusi la kumbana, suruali iliyoshika mapaja na nyonga zake kisha kubwaga huko chini. Miguuni ana viatu vyenye visigino virefu na kuchongoka kwa mbele. Mikononi amevalia glovu nyeusi malighafi ya ngozi.
.
.
Vitu vyote hivyo ambavyo vimetajawa vilikuwa vyametameta kana kwamba nyota angani!
.
.
“Helo!” Brian akajikuta ananong’ona mwenyewe akistaajabu. Mbele ya macho yake alikuwapo mwanaume ambaye amekuwa akisikia tu simulizi zake. Mwanaume aliyewahi kutikisa Boston na Massachusetts nzima!
.
.
Bado mwanaume huyo alikuwa amevalia nguo zake alizokuwa anatumbuiza nazo, hata picha zake huko ukutani zilikuwa zamwonyesha hivyo.
.
.
Hakika alipendeza na basi ungetamani umwone akiwa anatumbuiza. Lakini endapo ungekumbuka kuwa mtu huyu ni mfu, ungepoteza hamu yote! Mtu aliyechomwa moto miaka iliyopita na hata nyumba yake kutiwa pia motoni, leo yu hai, mzima na anacheza!
.
.
Pembeni yake kulikuwa na santuri ya kale iliyokuwa inamimina muziki wa bluzi. Hakika muziki huu ulikuwa unamkonga moyo wake, alikuwa akiimba pamoja nao na muda mwingine akijikuta anapiga kelele kali za nguvu!
.
.
Lakini sura yake haikuwa inaonekana. Alikuwa amempa mgongo Brian. Kichwa chake anakitikisatikisa na mkono wake uliopo ndani ya glovu unatengeneza ala kwa vidole.
.
.
Brian atamfanya nini mtu huyu? Akatazama nyuma, akakutana uso kwa uso na Kecie. Kecie hakusema jambo, bali akaendelea kumnyooshea kidole huko mbele, yaani sebuleni. Brian alipotazama tena kule sebuleni, Helo hakuwapo! Kiti pekee kilikuwa kinachecheza.
.
.
Moyo wa Brian ukalipuka kwa woga sana. Akapepesa macho yake kule na kule, hakumwona Helo. Hakujua wapi ameenda, tena ‘hafla hivyo! Kurudisha uso kwa Kecie, hapo akamwona mwanaume mrefu akiwa amesimama! Mwanaume mzito aliyeshiba.
.
.
Uso wake haukuwa unaonekana kwa kufichwa na kivuli cha kofia. Nguo zake zilikuwa zametameta, zang’aa, kana kwamba vito vya almasi vimeshikiziwa kwenye shuka.
.
.
Alikuwa anatisha kwa urefu wake. Brian alitetemeka na akatamani kupiga kelele kwanguvu sana. Mwili ulimuisha nguvu. Mkojo ulimbana, maungio ya mwili yalipata ganzi!
.
.
Kecie alijificha nyuma ya mwili wa mwanaume huyo, naye pia akiwa na uso wa hofu kuu.
.
.
“Unafuata nini kwenye himaya ya walio wafu?” sauti nzito ikauliza.
.
.
Brian hajajibu, akazabwa kofi kali sana. Akapaa juu na kwenda kujikita ukutani na kupoteza fahamu papo hapo! Hakujua tena kilichoendelea. Alipokuja kufungua macho, hajui hata majira, akajiona yu sebuleni kwao. Kichwa kilikuwa kinamuuma sana, haswa upande wake wa kulia.
.
.
“Mama!” akaita.
.
.
“Brian!” mama yake akamjongea upesi kumtazama. “Brian, mwanangu. Unaendeleaje?”
.
.
“Kichwa kinaniuma sana …” Brian akatazama kushoto na kulia kwake, akamwona Mrs Garett na Olivia. Akaita, “… Olivia.” kabla hajaongeza neno, kichwa kikamgonga sana, akakunja uso wake kus’kizia.
.
.
“Pumzika, Brian,” mama yake akamsihi. “ulipoteza fahamu ghafla.”
.
.
“Mlikuta Olivia?” Brian akauliza.
.
.
“Ndio. Olivia alikuwa ndani. Tulistaajabu kukuona wewe ukikimbia kwenda huko nje.”
.
.
“Alikuwa ndani? Mbona sikumwona? Wote hatukumwona!”
.
.
“Sisi tulimwona, alikuwa amelala kitandani. Tulikuambia lakini hukutuelewa. Tulistaajabu unakimbilia nje. Tulipokufuata tulikukuta ukiwa umezirai, umelala barabarani!”
.
.
Brian akaduwazwa na hayo maelezo. Yule hakuwa Olivia? Mbona alimwona vivyo? Basi na ilikuwa ni njia ya Kecie kumpeleka kule kwenye ulimwengu mwingine. Ulimwengu ambao Helo aliuita wa wafu.
.
.
Hakuwa anaota. Ulimwengu huo ni wa dhati. Maumivu ya kofi zito alilozabwa, bado alikuwa anayasikia sana yakiathiri sikio lake la kulia. Akawaza, atamwokoaje Kecie kule? Na je baada ya yeye kuondoka huko, Helo atamfanya nini Kecie?
.
.
**
.
.
Saa nane mchana.
.
.
.
Hakukuwa na shule siku hiyo, wanafunzi wote pamoja na wafanyakazi wa shule walikuwa wamehudhuria msiba wa Dkt Hamill. Shule ilikuwa pweke. Makaburi ya Boston yalikuwa yamefurika watu waliovalia sare za wanafunzi.
.
.
Hakukuwa na ndugu, jamaa wala rafiki wa marehemu. Kwa heshima za wafanyakazi wenzake, shule ikiwa imesimamia kila jambo, Dkt Hamill akaagwa na kuzikwa.
.
.
Watu walipotawanyika, Brian akaenda nyumbani kwa Dkt Hamill moja kwa moja. Alikuwa ndiye mtu mwenye ufunguo wa nyumba hiyo, pamoja pia na wa gari yake.
.
.
Alipofika, akaitazama nyumba hiyo kana kwamba ni kitu anachokijua ila kilipotea kwa muda mrefu. Akaikagua sana kwa nje, kila kona, akajikuta anajawa na machozi machoni mwake. Aliingia ndani na kuendelea kupekua. Akatazama picha za Dkt Hamill na familia yake. Akapata maswali sana kichwani,.
.
.
Familia hii ilipotelea wapi? Kwanini Dkt Hamill amekufa akiwa mpweke. Hana ndugu wala rafiki? Ni maisha gani hayo aliyokuwa anaishi? Alitamani sana kujua.
.
.
Akiwa anaendelea kupekuapekua, akiwa kwenye ghorofa ya juu, kwa chini nje ya uzio, akamwona mwanaume mmoja akiwa amesimama … amesimama anamtazama!
.
.
Mwanaume huyo alikuwa amevalia koti refu jeusi. Kichwa chake amekihifadhi ndani ya kofia na mikono yake ameidumbuliza kwenye mifuko ya koti.
.
.
Brian akastaajabu kuwa mwanaume huyo amemwonaje akiwa juu huko? Na kwanini amesimama kana kwamba mnara akimtazama? Ni nani?
.
.
Alipotazama vema akagundua mwanaume huyo ni Brewster! Mwanaume kikongwe ndani ya mji wa Boston. Mzee huyo anafanya nini hapo? Brian alishangazwa na namna ambavyo Brewster amekuwa wa kumfuatilia.
.
.
Akashuka upesi toka ghorofani, akaendea geti na kutazama nje. Hakumkuta mtu! Brewster hakuwepo. Alikimbilia kaskazini mwa barabara na kusini lakini hakumwona mzee huyo. Haikujulikana wapi alielekea.
.
.
Basi Brian akaona shughuli imetiwa doa, akafunga kila kitu na kwenda zake nyumbani, akiwa na maswali juu ya Brewster.
.
.
Alipofika, kwakuwa alikuwa na njaa, akaendea jikoni na kupakua chakula. Alimkuta Olivia pekee sebuleni anatazama televisheni.
.
.
“Wapo wapi hawa?” akamuuliza akitafuna.
.
.
“Wametoka,” Olivia akamjibu kwa ufupi.
.
.
Hapa ndipo Brian akakumbukua kuwa gari halikuwapo nje.
.
.
“Wameenda wapi?”
.
.
Olivia akapandisha mabega juu pasipo kutia neno, hakuwa anamtazama Brian. Basi Brian akaendelea kula, lakini ghafla kuna kitu kikamjia kichwani. Hakujua kwanini, ila alijikuta akikumbuka tukio la ajali ya Mr Garett!
.
.
Aliyakumbuka yale maneno ya Mrs Garett kuwa bwana wake alimwambia kuwa Kecie anawinda roho yao kabla hajafariki, punde ndogo baada ya kupata ajali ya gari.
.
.
Basi Brian akajikuta anakosa amani. Hata chakula hakukimaliza, akakiweka kando.
.
.
“Wametoka muda mrefu?” Akauliza.
.
.
“Tangu asubuhi,” Olivia akajibu, bado akiwa anatazama televisheni. Ila sauti yake ilikuwa tofauti kidogo. Hili kwa kiasi likampa mashaka Brian. Akaita, “Olivia!”
.
.
Olivia akaitikia. Hakumtazama Brian. Uso wake ulikuwa umeng’ang’ania kutazama televisheni.
.
.
“Olivia, nitazame.”
.
.
Olivia akakaa kimya. Hakutikisika wala kupepesuka. Brian akarudia kumwambia akimtaka ageuke. Mara hii Olivia akajibu kwa swali, “Kwanini nigeuke?”
.
.
Sasa mara hii sauti yake ndiyo ilikuwa tofauti kabisa. Sauti nzito ya kiume! Brian akajikuta akishtuka mno.
.
.
.
***
 
*ROHO YAKE INADAI --- 17*

*Simulizi za series*


ILIPOISHIA

Olivia akakaa kimya. Hakutikisika wala kupepesuka. Brian akarudia kumwambia akimtaka ageuke. Mara hii Olivia akajibu kwa swali, “Kwanini nigeuke?”

Sasa mara hii sauti yake ndiyo ilikuwa tofauti kabisa. Sauti nzito ya kiume! Brian akajikuta akishtuka mno.

ENDELEA

Moyo wake ukaenda mbio na mwili wake ukaanza kutetemeka kwa fujo! Kufumba na kufumbua, Olivia akageuza shingo yake kumtazama Brian! Lakini namna ambavyo alikuwa amegeuza kichwa hiko ilikuwa ni ya ajabu haswa! Mwili wake bado ulikuwa unatazama upande ilipo runinga, lakini uso wake ukiwa umegeuka nyuma kabisa!

Kwa mtu ambaye ni mzima, hawezi kufanya hivi, labda tu awe amevunjika ajalini. Macho yake yalikuwa meusi ti! Mdomo wake ulikuwa mkavu kana kwamba muhogo uliotelekezwa juani.

“Nini unataka kujua, Brian?” Olivia akauliza kwa sauti yake ya ajabu. Brian akabaki akiwa ametoa macho. Anahema kana kwamba mbwa aliyetoka kukimbizwa.

“Nini unaogopa? Si umetaka nigeuke?”

“Wewe ni nani?” Brian akauliza. Alikuwa amejiminyia kochini nusura atokee upande wa pili.

“Mimi? - wataka kunijua mimi?” Olivia akauliza. Kwa haraka mwili wake ukageuka kufuata uso wake, akasimama na kumtazama Brian huku shingo yake ikiwa inakunjikakunjika hovyo kupeleka kichwa huku na kule.

“Mimi ni mwenyeji wako, Brian! Hunijui?” Olivia akauliza. Brian akiwa anatweta kwa hofu kuu, akatikisa kichwa chake upesi. Paji lake la uso lilikuwa linatiririsha jasho.

“Sikujui!” akasema. “Sikujui wewe ni nani!”

Olivia akaangua kicheko na mara akakunja tena sura yake kwa hasira. Akamtazama Brian kiupande. “Mimi ni mwenyeji wako!” akamwambia kwa sauti yake ya mashine. Macho yake yaliyokoza uweusi yakiwa yametoka nje mithili ya balbu!

“Ulikuja kwenye himaya yangu kun’tembelea … Je nataka kumtorosha mwanangu?”

“Mimi hata simju-!” Brian hakumalizia kauli yake, akasombwa yeye pamoja na kiti. Ilikuwa ni nguvu ya ajabu. Alibamiziwa ukutani pasipo hata kuguswa, akaja kujikuta akiwa chini anagugumia na maumivu.

“Kamwe!” Akasema Olivia akipeperusha kidole chake kushoto na kulia. “Kamwe … kamwe … usije kuthubutu!”

Aliposema hayo akakunja ngumi ya mkono wake wa kuume, Brian akaanza kukabwa na mkono asiouona. Akadaka shingo yake akijitahidi kuhema. Mishipa ya shingo imemshupaa. Olivia akaendelea kuiminya ngumi yake. Brian akaendelea kuteseka maradufu, sasa hewa akiwa hapati! Jasho jingi lamchuruza. Macho yamemtoka nje! Alikuwa anaelekea kufa.

Uso wake ulibadili rangi kuwa mwekundu, na kila mshipa uliokuwapo kichwani ukasimama dede! Kwa sekunde tatu tu za mbele, kijana huyu alikuwa anaiacha dunia.

Kheri, huko nje sauti za watu zikajongea. Walikuwa ni watu wawili wanaongea na huku wakiwa mwendoni kufuata makazi ya wakina Brian. Hapa ghafla, Olivia akanyong’onyea na kudondoka chini akiwa hana fahamu! Hiyo ikawa ahueni ya Brian ya maisha yake yaliyokuwa yamebakia kwenye nyuzi nyembamba!

Punde mlango ukafunguliwa, akaingia Mama yake Brian pamoja na Mrs Garett.

“Mungu wangu!” Wakahamaki. Brian alikuwa ameegemea ukuta, yu hoi, na kwake pumzi ikiwa ni bidhaa yenye thamani kubwa akihangaika kuitafuta. Hata nguvu hakuwa nayo. Jasho limemvaa uso wake gubigubi. Anakohoa kwa pupa.

Olivia alikuwa hayupo hata kwenye ulimwengu huu.

“Brian, nini kimetokea?” Mama Brian akauliza akimkimbilia mwanaye upesi kumtazama. Mrs Garett naye akamsongea Olivia na kumpekua. “Amezirai!” akasema kwa mshangao. Baada ya muda kidogo, wakawa wamemweka Olivia juu ya kiti, na Brian naye amepumzishwa papo.

Nyuso za wanawake hawa zilikuwa na taharuki na hofu juu. Walikuwa na kiu kikubwa cha kufahamu nini kilichojiri.

Baada ya muda wa takribani dakika sita, Brian, akiwa ametulia na kurudi kwenye hali yake mbali na maumivu aliyokuwa anayahisi kwa mbali shingoni, akaelezea namna ambavyo mambo yalitokea. Habari hizo zikawashtua sana Mrs Garett na mama yake.

“Namna gani nitamwokoa mwanangu lakini?” akalia Mrs Garett. A;lijikuta anatamani hata kumwona huyo ‘mwanaume’ ambaye amemshikilia mtoto wake huko eneo ambako palikuwa panaitwa ulimwengu wa walio wafu.

Lakini Brian akamwonya. “Sidhani kama unataka kufika huko.” wakati Brian akisema haya, alikuwa ni mtulivu sana. Anajua anachokiongelea. Anajua kilichopo kule.

“Si mahali salama hata kidogo. Panatisha, na kuna uwezekano hafifu wa kurudi hai.”

Mrs Garett akakabwa na kilio cha gubi. Mama yake Brian akajitahidi kumpooza na kumtuliza. Punde kidogo Olivia akaamka. Hakuwa anajielewa. Aliambazaambaza macho yake huku na kule na kukutana macho kwa macho na Brian! Bado Brian alikuwa na hofu juu ya binti huyo.

“Olivia!” Mrs Garett akamkumbatia mwanawe. Akambusu kwenye paji la uso na kumuuliza wapi alipokuwa. Nini anachokumbuka. Hamna kitu! Olivia hakuwa anakumbuka chochote kile zaidi ya mara ya mwisho kusinzia baada ya kutazama runinga kwa muda mrefu.


**

Saa tatu usiku …


Walikuwa sebuleni wanakula chakula cha usiku. Walikuwa wamekawia kula leo maana chakula kiliandaliwa kwa kuchelewa. Kulikuwa ni kimya mbali na sauti ya vijiko vikigonga sahani na midomo ikitafuna.

Brian alikuwa anamtaza Olivia mara kwa mara. Macho yake hayakukaa muda pasipo kuangukia kwa mtoto huyo. Bado alikuwa na hofu naye. Alidhani pengine aweza badilika kuwa kama alivyokuwa muda ule, lakini haikuwa hivyo mpaka wanaelekea kumaliza kula.

“Brian,” mama akaita. Yeye alikuwa ashamaliza kula. “Vipi msiba? Kila kitu kilienda sawa?”

Brian akatikisa kichwa pasipo kutia neno. Akaendelea kula.

“Tulitoka leo, kwenda nje kabisa ya mji. Ni kwasababu ya haya mambo yanayotokea, ila bahati haikuwa kwetu, hatukufanikisha!” mama alizungumza. Maongezi haya yakamvutia Brian, akamtazama mamaye na kumpa miamko yote impasayo mtu aliye makini.

“ … Tulienda kumtafuta mtaalamu wa mambo ya majini, ila hakuwapo. Inaonyesha ni mtu wa ratiba nyingi. Tungempata pengine angesaidia.”

Mama alipomaliza kusema hayo, Brian akaendelea kula. Hakuona kipya. Alikuwa anatafuna lakini asihisi ladha ya chakula. Mawazo yake hayakuwapo hapo kabisa. Mama akamtazama na kisha akasafisha koo lake, Brian akampatia macho.

“ … kwahiyo tukaona itakuwa kheri endapo tungetafuta namna nyingine, hivyo tukaenda kanisani kumwona padri aje kutusaidia kwa maombi.”

“Padri Alfonso?” Olivia akauliza kwa macho yalojawa woga. Mrs Garett akamtazama na kumtikisia kichwa kuafiki. Olivia akakunja uso wake na kulalama. “Simtaki padri Alfonso!” akarudia tena, “Simtaki padri Alfonso!” alafu akaangua kilio.

“Usijali, Olivia,” akasema Mrs Garett. “Kila kitu kitakuwa sawa!” akambeba binti huyo na kumweka mapajani mwake akimbembeleza. Brian hakutia neno, akaishia kutazama tu. Na alipomaliza kula, akaenda zake chumbani.

Alipojilaza, akatazama zile nyaraka tatu alizoachiwa na Dkt Hamill. Akainyaka ile ambayo alishaanza kuisoma. Akatafuta eneo alipoishia na kuendelea kuipitia taratibu …

“ … Jasmine kabla hajanieleza kule alienda kufuata nini, akatikisa kwanza kichwa chake,” Dkt Hamill aliendelea kuhadithia kwenye nyaraka. “ … alifuma mafundo matatu alafu akaniambia kama unataka kujua basi kesho tuongozane kwenda huko. Nilihofia. Japo nilikuwa nataka kujua nini kipo kule, bado nilikuwa na hofu kifuani mwangu. Basi hapo akawa amenikata hamu, na pasipo kuaga nikajiendea.

Kesho yake nikamfuatilia, hakwenda kule msituni. Wala keshokutwa, wala mtondogoo. Ila siku iliyofuata, majira ya jioni, akapotea nyumbani. Nilimtafuta kila kona pasipo mafanikio basi nikajua ya kuwa atakuwa ameenda kule msituni.

Nikaelekea huko. Na basi kama ilivyokuwa siku ile, alipotoka nikakimbia zangu kurudi nyumbani bado nikiwa sijui ni nini mtumwa huyo anafanya mule ndani. Siku hiyo, kwenye majira ya saa mbili usiku, Jasmine akaniita. Ilikuwa ni rahisi kwa maana nilikuwa nimejiketia nje.

Akaniambia, “Hamill, twende kule bandani kuna jambo nataka kukwambia!” Nikaongozana naye kwenda huko. Akaniketisha barazani na kuniuliza, “Unapenda mazingaombwe? Unafurahi kuyaona?”

“Ndio, napenda!” nikamjibu.

“Basi kesho twende kule msituni! Twende ukaone mazingaombwe ya kufurahisha!”

“Lakini mimi naogopa kwenda msituni!” nikamwambia nikimtazama kwa hofu. Akacheka. Akanidaka mkono na kunitazama machoni. “Hamna haja ya kuogopa, upo na mimi! Usijali, nyumbani hawatajua. Kwani mimi niendapo kuna yeyote ajuaye?”

Nikalala siku hiyo nikiwa na mawazo lakini pia hamu. Nilikuwa napenda sana kwenda kuyashuhudia mazingaombwe. Nilijiuliza kumbe Jasmine huenda kwenye lile ghofu kutazama mazingaombwe! Ni nani anayafanya mule?

Wasaa ulipowadia, nakumbuka ilikuwa ni kwenye majira ya jioni ya mapema, Jasmine akauteka mkono wangu na kutokomea nami msituni. Hakuna mtu aliyetuona. Hata watumwa wengine hawakuwa wanajua. Tukatembea upesi sana.

Njiani Jasmine akinieleza namna nitakavyofurahia mazingaombwe ninayoenda kuyaona!


**
 
crime story fikirishi sana mkuu.......napenda sana kusoma mitiririko ya namna hii....
NEXT.......
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom