Sehemu ya 43.
“Shadya! Maisha yananichanganya sana. Unajua unapokosa pesa wakati mwingine mpaka mapenzi huyafikirii kabisa,” alisema Gibson maneno yaliyouchoma moyo wa Shadya vilivyo, lakini akatoa tabasamu kama aliridhika na maneno hayo.
“Oh! Pole kwa ubize mpenzi! Naomba uniambie kitu kimoja,” alisema Shadya.
“Kitu gani?”
“Kuhusu msimamo wako!”
“Upi?”
“Juu yangu! Ni kwamba tunaendelea kuwa wapenzi ama basi?” aliuliza msichana huyo.
Hakutaka kujishtukia kuuliza swali hilo, kama mwanamke ilikuwa ni lazima aujue msimamo wake, kama angeona aibu kuuliza maswali hayo ilimaanisha hakuwa siriazi na maisha yake.
Ni kweli alimpenda mno Gibson lakini muda huo ulikuwa ni wakati wa kujua ukweli wake, kama kweli alihitaji kuendelea kuwa naye ama la!”
Shadya unajua na...”
“Gibson! Usirukeruke! Ninahitaji kuujua msimamo wako! Wewe ni mwanaume, niambie ukweli, sihitaji kupoteza muda kwa mwanaume ambaye sina nafasi kwake, sipendi kuumizwa, sipendi kulia, ninahitaji nijue msimamo wako!” alisema Shadya, kwa jinsi alivyokuwa akizungumza, ni kama mwanaume aliyekuwa akimwambia mwanamke.
“Naomba muda nijifikirie!”
“Gibson! Hilo ni jibu tosha kwamba sina nafasi kwako, huwezi ukahitaji muda wa kujifikiria juu yangu na wakati unajua mimi ni mpenzi wako. Mapenzi yameshuka, nashukuru kuna mambo nimejifunza kwako,” alisema Shadya huku akionekana kutia huruma.
Ghafla meseji ikaingia kwake. Ilikuwa ni ya Alex.
“Namba yangu huyo,” ujumbe ulisomeka, akausoma, hapohapo akaujibu.
“Nashukuru! Naomba nikuulize swali, nijibu haraka sana.
Kama mwanaume ameniumiza, nikiwa naongea naye, natakiwa nifanye nini ili naye achanganyikiwe?” aliandika, baada ya sekunde kama thelathini ukajibiwa.
“Kill him with your smile!” (muue kwa tabasamu lako) uliandika ujumbe kutoka kwa Alex.
“Sawa!” akaujibu.
“Tena muonyeshe kama hujaumia, yaani kuwa poa, hata kama unalia moyoni.”
“Nimekuelewa!”
Muda wote huo Gibson alikuwa kimya, alimwangalia Shadya ambaye alionekana kuwa bize kidogo na simu yake, alipouinua uso wake, ulitawaliwa na tabasamu pana.