Sehemu ya 36.
Ilikuwa ni furaha zaidi kwao, kila mmoja alitamani kumuona mwenzake kwa mara nyingine. Gibson hakumfikiria Shadya kwa sababu kwake alikuwa msichana wa kawaida, wa ku-hit and run.
Maandalizi ya kumpokea mpenzi wake yakaanza kufanyika, wakati hayo yote yakiendelea ndipo akakumbuka kulikuwa na msichana aliyeitwa kwa jina la Shadya.
Huyu alikuwa Mpemba, mzuri wa sura lakini hakutaka kabisa kuona akimsababishia kutengana na mwanamke wa ndoto yake, aliyetaka kutengeneza naye maisha.
“Wanawake wa chuo huwa ni wa kupiga na kuacha, tunaishi hivyo kama wanachuo, kwani naye anataka mimi kuwa wake maishani ama?” alijiuliza.
“Na kama aking’ang’ania, kweli nitaamini hawa wasichana wa mwaka wa kwanza magumashi,” alijisemea na kuachia tabasamu pana.
Alikuwa tayari kugombana na msichana yeyote katika dunia hii lakini si Paula, huyo alikuwa kila kitu kwake hivyo kitu cha kwanza kabisa kilikuwa ni kulazimisha kupunguza ukaribu baina yake na Shadya.
Hiyo ndiyo ilikuwa hatua ya kwanza ya kumuacha msichana ambaye hukuwa na malengo naye. Kama kwa siku ilikuwa ni lazima mpigiane simu mara tano basi ilikuwa ni lazima ipunguzwe na kufika mpaka mara mbili, kama ulikuwa na haraka mno ya kujibu meseji yake kila inapotumwa, ilikuwa ni lazima upunguze uharaka, meseji moja ichukue hata dakika ishirini kujibiwa.
“Nitaanza na haya mambo mawili kwanza. Nikijidai nipo beneti naye huyu malaya anaweza kuniharibia,” alijisemea, alianza kumuita Shadya malaya kwa sababu tu alimkubalia kumvua nguo na kufanya naye mapenzi, mara mbili, ila kwenye hayo yote, hakuwa msichana wa kumuacha moja kwa moja, yaani pale ambapo angemtaka, angekuwa akimtafuta huku akimuomba msamaha.
*
*
Je, nini kitaendelea?