Simulizi: Namtaka mpenzi wangu arudi

Simulizi: Namtaka mpenzi wangu arudi

SEHEMU YA 41

“Niamini! Nilikuwa na hasira sana na wewe. Yule msichana alikuja kufanya mapenzi na wewe kwa lengo la kukukomoa, alikurekodi na mwisho wa siku akanitumia video na kusema kwamba lazima akufunge, kwa kuwa nilikuwa na hasira, nikaamua kumuunga mkono, lakini mwisho wa siku nimegundua kwamba wewe ni mwanaume wa kweli, uliyekuwa moyoni mwangu, hakika nitakuwa nawe bega kwa bega kukusaidia,” alisema Linda.

Alipokuwa akiongea hayo, machozi yalikuwa yakitiririka mashavuni mwake, alijifanya kuumia mno, hakutaka kumwambia Dickson kwamba kila kitu kilichokuwa kimetokea kilikuwa ni mpango wake.
Moyo wa Dickson ukabadilika na hatimaye kuamua kwa moyo mmoja kuwa na msichana huyo kwa lengo la kufuta ile kesi ambayo ilionekana kuwa mbaya zaidi kwa upande wake.

Kitu pekee kilichokuwa kikimuumiza kichwa kilikuwa ni Nandy, hakujua ni kwa jinsi gani angemwambia msichana huyo kwamba hakutaka kuwa naye tena, alimpenda kwa moyo wake lakini aliona kabisa kwamba kungekuwa na ugumu mkubwa mno kumwambia ukweli.

Akapiga moyo konde, alichokuwa akikiangalia kilikuwa ni maisha yake tu. Mapenzi yalikuwepo, aliamini kwamba hata kama angempoteza msichana aliyekuwa akimpenda, bado mwingine angekuja mikononi mwake.

Akampigia simu Nandy na kumwambia kwamba alitaka kuzungumza naye. Hilo halikuwa tatizo, tena kwa msichana kama Nandy ambaye kila siku alikuwa akimfikiria mpenzi wake, akawa tayari kuzungumza na mwanaume huyo.

Wakapanga sehemu ya kuonana, ndani ya saa moja wakawa katika Mgahawa wa Karambezi na kuanza kuzungumza. Muda wote huo Nandy alikuwa kwenye sura ya tabasamu, kwa maisha yaliyokuwa yakiendelea na mpenzi wake huyo yalimtia hofu na kuhisi kwamba ndiyo ungekuwa mwisho wake kuwa na mwanaume huyo.

Baada ya kuonana hapo, akawa na uhakika kuwa penzi lao lilikuwa likiendelea kama kawaida na si kama vile ambavyo alikuwa amehisi.
 
SEHEMU YA 42

Alitabasamu, hakujua kile ambacho angeambiwa na mwanaume huyo mahali hapo. Wakati yeye akiwaza penzi kunoga, kichwa cha Dickson kilikuwa kikifikiria kumwambia msichana huyo kwamba walitakiwa kuachana kwani alimpata msichana mwingine ambaye alitakiwa kumuoa.

Hakujua msichana huyo angeumia vipi, hakujua msichana huyo angejisikiaje, alichokuwa akikihitaji ni kumwambia ukweli tu ili kuepusha kesi nzito iliyokuwa mbele yake.
“Nandy!” aliita Dickson huku akimwangalia msichana huyo.

“Ndiyo mpenzi! Kwanza naomba uniambie ukimya wako, tatizo nini?” aliuliza Nandy huku akimwangalia Dickson kwa jicho lililoonyesha mapenzi yote yaliyokuwa moyoni mwake.
“Ni kama nilivyokwambia...”
“Nina habari njema.”
“Ipi?”

“Nimechaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, natumaini tutakuwa wote kuanzia mwezi ujao,” alisema Nandy huku akionekana kuwa na furaha isiyo kifani, badala ya kufurahia, Dickson akahuzunika zaidi.

“Tatizo nini mpenzi? Kuna kitu gani kinaendelea?” aliuliza Nandy, aliishangaa hali aliyokuwanayo mpenzi wake huyo.
Dickson akabaki kimya, machozi yakaanza kumtoka na kutiririka mashavuni mwake. Aliumia mno, Nandy alibaki akishangaa, hakujua kilichokuwa kikiendelea kwa mpenzi wake huyo.

Alimbembeleza na kumwambia amwambie ukweli juu ya kilichokuwa kikiendelea mpaka kuwa katika hali ile lakini Dickson hakusema kitu zaidi ya kuendelea kulia tu.

Alikuwa kwenye hali hiyo kwa dakika kumi nzima, akajifuta machozi na kumwangalia Nandy tayari kwa kumwambia kile kitu alichokuwa amemuitia.
“Nandy!” alimuita msichana huyo.
“Nipo hapa mpenzi!”

“Kwanza naomba unisamehe sana, najua kuna siku utajua ukweli wa kila kitu, ila naomba unisamehe sana,” alisema Dickson, akanyamaza, akaangalia chini, aibu nzito ikautawala uso wake.
“Kuna nini? Unanitisha!”

“Nisamehe kwa kukupoteza muda wako!”
“Niambie kuna nini,” alisema Nandy, akaanza kuogopa.
“Sistahili kuwa mume wako! Sistahili Nandy,” alisema Dickson na kuanza kutokwa tena na machozi.

Moyo wa Nandy ukapiga paa, hakuamini alichokisikia, alimwangalia Dickson, alihitaji kuona kama kijana huyo alikuwa akimaanisha alichokuwa akimwambia au la.
“Unasemaje?”
 
SEHEMU YA 43

“Naomba tuachane, naomba unisamehe kwa kukupotezea muda wako. Nahitaji kuwa huru, ninahitaji kuwa na furaha maisha yangu, najua kuna siku utakuja kujua kila kitu, ila naomba tuachane Nandy, ukipata mwanaume mwingine wa kukuoa, acha akuoe, ila naomba unisahau, naomba usahau kila kitu kuhusu mimi,” alisema Dickson kwa sauti ndogo.

Nandy alichanganyikiwa, alimwangalia Dickson mara mbili-mbili, hakuamini alichokuwa akikisikia. Yeye mwenye machozi yakaanza kumtiririka, alihisi kama alikuwa ndotoni ambapo baada ya muda fulani angeamka na kujikuta akiwa kitandani.

Dickson yuleyule aliyekuwa amemwambia kwamba anampenda, Dickson yuleyule aliyemthamini na kumruhusu autoe usichana wake ndiye ambaye alikuwa mbele yake na kumwambia kwamba waachane.

Alihisi kichwa kumuuma, alihisi kitu chenye ncha kali kikiuchoma moyo wake, pale alipokuwa akaanza kutetemeka, japokuwa mgahawa huo ulikuwa ufukweni tena wakipigwa na upepo mkali wa baridi, akaanza kutiririkwa na kijasho chembamba.

“Dickson...” aliita Nandy.
“Naomba uniache Nandy! Sistahili kuwa mume wako,” alisema Dickson, hakutaka kubaki mahali hapo, akasimama na kuanza kuondoka.

Nandy akasimama pia, akaanza kumfuata Dickson huku akimuita. Kila mtu aliyekuwa hapo akabaki akishangaa, ilikuwa sehemu tulivu, kulikuwa na wapendanao ambao walikuwa wakiongea mambo yao lakini kelele za kuita za Nandy zilimshtua kila mtu mahali hapo.

“Dickson....Dickson...” aliita, Dickson akapotea machoni pake, akashindwa kusonga mbele, akahisi miguu yake ikikosa nguvu, kizunguzungu kikamuanza, hakupiga hatua zaidi, hapohapo akaanguka na kupoteza fahamu. Hakujua ni kitu gani kiliendelea baada ya hapo.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 44

Nandy alipata fahamu akiwa hospitalini, akayafumbua macho yake na kuangalia huku na kule, hakujua mahali alipokuwa lakini baada ya kuona dripu iliyokuwa ikining’inia juu yake, haikuwa ngumu kugundua kwamba alikuwa hospitalini.
Akaanza kufikiria ni kitu gani kilitokea mpaka kufika mahali hapo.

Alichokumbuka ni kwamba alikuwa na mpenzi wake, Dickson, walikuwa wakizungumza lakini mwanaume huyo alimwambia kwamba hakutaka kuwa naye tena kwa sababu alikuwa amepata mwanamke mwingine.

Hapohapo kitandani alipokuwa, akaanza kulia, hakuamini kama yeye ndiye aliyeambiwa hivyo na mwanaume huyo aliyekuwa akimpenda, mwanaume aliyemuona kuwa kila kitu kwake, mwanaume ambaye alikuwa ndoto ya maisha yake, mwanaume ambaye alipanga kuwa mume wake hapo baadaye.

Moyo wake uliuma mno, pale kitandani alipokuwa, akaanza kulia, maumivu hayakupungua, yalizidi, baada ya dakika chache, nesi mmoja akafungua mlango na kuingia ndani.

Alipomuona Nandy analia kitandani pale, akamsogelea na kuanza kumbembeleza kwa kumtaka kunyamaza. Hakunyamaza kwani kila alipokuwa akiikumbuka sura ya Dickson alizidi kulia.

“Kwa nini Dickson ameniacha? Kwa nini amepata mwanamke mwingine? Kwa nini? Kwa nini ameniacha?” aliuliza Nandy huku akilia.

Hazikupita dakika nyingi baba yake, mzee Gwamaka akaingia ndani ya chumba hicho, alipomuona binti yake, akauinamisha uso wake chini, maumivu aliyosikia moyoni mwake yalikuwa makubwa mno.

Akamsogelea na kuanza kumbembeleza, alijua kwamba binti yake alipoteza fahamu alipokuwa akizungumza na mwanaume, hakujua mwanaume huyo alikuwa nani kwani wale waliokuwa wamempigia simu na kumpa taarifa hawakumwambia kitu chochote kile zaidi ya hali aliyokuwanayo binti yake.

Nandy alipomuona baba yake, kilio kikazidi, mzee Gwamaka akasogelea kitanda kile na kukaa karibu ya binti yake huyo ambaye alibaki akilalamika kwa kutaka kujua tatizo lilikuwa nini mpaka Dickson kumuacha.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom