Simulizi: Namtaka mpenzi wangu arudi

Simulizi: Namtaka mpenzi wangu arudi

SEHEMU YA 45

Mzee Gwamaka aliposikia hilo, akazidi kuumia, hakutaka kabisa kumuona mwanaye akiingia kwenye uhusiano wa kimapenzi kwa kuwa aliamini kwamba kuna siku angeumia sana, alitamani binti huyo aendelee kukaa peke yake lakini baada ya Dickson kutokea na kumuonyeshea uaminifu mkubwa, akamruhusu kuwa karibu na binti yake.

Mvulana huyohuyo aliyemwamini ndiye aliyekuja kumuumiza binti yake na kumliza kitandani hapo. Hakuamini, alijilaumu na wakati mwingine kujiona akiwa amefanya kosa kubwa mno.
Hakutaka kubaki na maumivu, alipotoka hospitalini hapo breki ya kwanza ilikuwa ni nyumbani kwa wazazi wa Dickson, alipofika, akaanza kuwaambia kilichokuwa kimetokea.

“Haiwezekani! Dickson hawezi kumuacha Nandy,” alisema mama yake huku akimwangalia mzee Gwamaka.
“Amemuacha, na hata alipopoteza fahamu, hakutaka kujali, akaondoka zake. Kwa nini kijana wenu amefanya hivi?” aliuliza mzee Gwamaka huku akionekana kuwa na hasira mno.

Wazazi wa Dickson hawakutana kubaki nyumbani walichokuwa ni kwenda mpaka hospitalini kwenda kujua ukweli kama kile alichokizungumza mzee Gwamaka kilikuwa kweli au la.

Walipofika huko na kuonana na Nandy, akawahadithia kilichokuwa kimetokea, hawakuamini, walimfahamu Dickson, alikuwa na mapenzi ya dhati kwa Nandy kiasi kwamba kwao lilionekana kuwa jambo lisilowezekana hata kidogo kwa mtoto wao kumuacha Nandy.

Wazazi wake hawakutaka kusubiri, walichokifanya ni kumpigia simu kijana wao kwa lengo la kutaka kumsikia akizungumza hayo kwa mdomo wake. Walipompigia simu, aliwaambia kama alivyomwambia Nandy kwamba hakutaka kuwa naye kwani alipata msichana mwingine ambaye alipanga kumuoa.
“Una akili Dickson?” aliuliza baba yake kwa hasira swali ambalo hakupanga kuliuliza hata siku moja.

“Moyo baba! Siwezi kumuoa msichana ambaye moyo wangu haupo kwake, naomba mniache, kama ambavyo hakukuwa na mtu aliyekuchagulia mama, na mimi naomba msinichagulie,” alisema Dickson na kukata simu.

Walichanganyikiwa, kile walichoambiwa na Dickson hakikuwaingia akilini kabisa. Hawakutaka kubaki hospitalini hapo, wakaondoka kurudi nyumbani kwao.
 
SEHEMU YA 46

Njiani, walikuwa wakizungumza mambo mengi kuhusu kijana wao. Alibadilika ghafla, hakukuwa na mtu ambaye aliamini kama angeweza kuchukua uamuzi kama huo ambao ulionekana kuwa wa ghafla sana.

Kwao ilikuwa ni aibu nzito, wakati mwingine walijiona kama takataka kwa mzee Gwamaka ambaye alimwamini kijana wao kwa asilimia mia moja kwamba angeweza kumuoa Nandy.

Wakati wao wakifikiria kuhusu uhusiano huo, Dickson alikuwa bize na Linda, muda wote alikuwa na msichana huyo ambaye alionekana kuwa na furaha tele.
Walikuwa wakiyafurahia mapenzi, kwa Dickson moyo wake ulikuwa tofauti kabisa, alifanya kile alichokitaka msichana huyo kwa kuwa aliogopa kupelekwa polisi kwa kosa la kumbaka Amina chumbani.

“Nataka tukale fungate nchini Ufaransa, kuna hoteli moja nzuri sana inaitwa La Petit, kama tukienda kule, natumaini itapendeza sana,” alisema Linda huku akimwangalia Dickson.

Kwa kumwangalia tu lisingekuwa jambo jepesi kugundua kwamba tabasamu lile alilokuwa akilionyesha usoni mwake lilikuwa tofauti kabisa na moyo wake. Alimchukia msichana huyo kwa nguvu zote lakini hakuwa na jinsi.

Baada ya kukaa kwa kipindi cha wiki moja, Linda akalilia kwenda kutambulishwa kwa wazazi wa Dickson kwa kuwa alikuwa na malengo naye.
Dickson akawa na hofu, hakujua wazazi wake wangempokeaje kwani walimpenda Nandy kuliko msichana mwingine yeyote yule.

Kabla ya kwenda huko akawapigia simu wazazi wake na kuwaambia kwamba alikuwa njiani kwenda kuwatambulisha mchumba wake ambaye angefunga naye pingu za maisha.

Japokuwa wazazi hao walikuwa na hasira lakini katika suala kama hilo wakaituliza mioyo yao na kukubaliana na mtoto wao kwa uamuzi aliokuwa ameuchukua.
“Una uhakika huyo ni msichana wako wa dhati?” aliuliza baba yake, alitaka kufahamu kabisa kama kijana wake aliamua kwa moyo mmoja au alilazimishwa.

“Nimeamua baba! Huyu ni mwanamke wangu wa ndoa!”
“Una uhakika?”
“Ndiyo!”
“Na anakupenda?”
“Ndiyo baba!”
“Na wewe unampenda?”
“Kupita maelezo!”
“Sawa.”
 
SEHEMU YA 47

Wakaelekea nyumbani kwao na walipofika huko, akaonana na wazazi wake huku akiwa na Linda na kuanza kuzungumza naye. Aliwaambia kwamba huyo ndiye alikuwa mchumba wake ambaye alitaka kufunga naye ndoa.
Hakuishia hapo, aliwahadithia maisha yao tangu zamani, jinsi walivyokuwa wamesoma wote, kupendana na hata msichana huyo alipoondoka kwenda Ulaya kusoma.

Hilo likawafanya wazazi wake kuhisi kwamba kweli Dickson alikuwa akimpenda msichana huyo, walichokifanya ni kukubaliana naye na kutoa baraka zote kama wazazi japokuwa mioyo yao haikumkubali Linda hata kidogo na walihisi kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea ambacho Dickson hakutaka kuwaambia.

“Na mmepanga kuoana?” aliuliza mama yake.
“Ndiyo mama! Tunatarajia kufunga ndoa baada ya miezi miwili,” alisema Dickson maneno yaliyowashtua.
“Miezi miwili?”
“Ndiyo!”
“Mbona haraka sana?”

“Kwa sababu tumeamua, tumeishi sana maisha ya ujana, wasije wakatokea akina Nandy wengine,” alisema Dickson.
“Sawa. Haina shida. Tunawatakia maandalizi mema,” alisema baba yake.

*** Nandy alikuwa na maumivu makali moyoni mwake, hakuamini kile kilichotokea kwamba mpenzi wake, Dickson alikuwa amemuacha na kumchukua mwanamke mwingine.

Kila siku alikuwa mtu wa kulia tu, hakuamini kama kweli yeye ndiye aliyekuwa akipitia maisha hayo. Wakati mwingine alipiga magoti na kumuomba Mungu msamaha, alihisi kwamba hayo ndiyo yalikuwa matokeo yake ya kuchanganya mambo ya kidunia na kiroho.

Hakuwa na furaha, hata alipokuwa akienda kanisani na kuimba mbele ya kanisa, alionekana kabisa kutokuwa na furaha hata kidogo.
Hali yake ikazua maswali mengi, wengi wakataka kufahamu sababu ya msichana huyo kubadilika ghafla lakini hakukuwa na mtu yeyote yule aliyegundua kitu chochote kile.

Kilichotokea kilikuwa siri yake na baba yake. Japokuwa aliumizwa na Dickson lakini moyo wake haukuwahi kumchukia kijana huyo, alimpenda, yeye ndiye aliyemuonyesha jinsi dunia ya mapenzi yalivyo, ndiye mwanaume aliyemvua nguo yake na kufanya mapenzi kwa mara ya kwanza.
 
SEHEMU YA 48

Aliyakumbuka maisha yaliyopita aliyoishi na Dickson, moyo wake uliumia mno na wakati mwingine alijiahidi kuwachukia wanaume, kuyachukia mapenzi lakini kitu cha ajabu kabisa alishindwa kabisa kumchukia Dickson.

Siku zikaendelea kukatika, moyo wake uliamini kwamba mwanaume huyo angerudi tena kwake na kuanza kuyapanga mambo yao kwa mara nyingine lakini hilo lilishindikana.
Alitamani kuifuata namba ya mwanaume huyo katika simu yake, alijaribu kufanya hivyo lakini alishindwa kabisa, kila alipotaka kuifuata, kwanza aliiandika pembeni, alipoifuta baadaye akaisevu tena.

Yalikuwa ni maisha ya mateso makubwa, mapenzi yalimuendesha kupita kawaida. Siku zilizidi kukatika. Kwa kumuonyeshea Linda kwamba alikuwa akimpenda, Dickson akawa anaweza status za mapenzi kwenye Mtandao wa WhatsApp, akawa anaweka picha nyingi akiwa na msichana huyo kitu ambacho kilimuumiza sana Nandy.

Mwili wake ukadhoofika, alikonda kutokana na mawazo aliyokuwanayo. Wengi walimjadili na kuhisi kwamba alikuwa mgonjwa lakini zaidi ya kukonda hakuwahi kwenda hospitalini.

Kila siku kazi yake ikawa ni kumuomba Mungu tu, alimwambia kwamba alitamani kuyabadilisha maisha yake, kitu cha kwanza alichohitaji Mungu akifanye kilikuwa ni kuubadilisha moyo wake, amuondoe Dickson moyoni mwake na kuliweka neno lake, mistari mingi ya Biblia ambayo aliamini kwamba ingembadilisha lakini hilo lilishindikana.
Baada ya kumalizika mwezi mmoja, akatumiwa ujumbe na Dickson kwamba alitarajiwa kufunga ndoa na Linda hivyo alitakiwa kuhudhuria harusi hiyo ambayo ingefungwa katika Kanisa la Mtakatifu Yehova lililokuwa Mwenge, jijini Dar.

Ulikuwa ni ujumbe wenye kuuma sana, siku hiyo alilia zaidi ya alivyolia siku alipoachwa na mwanaume huyo. Akajifungia chumbani, alihitajika kwenda kanisani kwa ajili ya mazoezi ya kwaya lakini akashindwa kabisa kutokana na maumivu aliyokuwanayo kipindi hicho.

Kwake, hayo yote yalionekana kuwa majaribu makubwa. Hata alipoanza kwenda chuo, hakuona raha ya kusoma kwa kuwa alikuwa akimuona sana Dickson huko kitu kilichomfanya kuumia mno.
“Mungu! Siwezi kuishi! Nimeshindwa, nimeshindwa Mungu! Maumivu yamenizidi,” alisema Nandy.
 
SEHEMU YA 49

Hakuona sababu ya kuendelea kuishi tena, kama kuumia, aliumia kupita kawaida, alichokuwa amekifikiria kilikuwa ni kujimaliza tu.
Kichwa chake kikafikiria sehemu ambayo angeweza kujimaliza vizuri, kilichokuja kichwani mwake kilikuwa ni kwenda katika Ghorofa la LAPF lililokuwa Makumbusho, apande mpaka juu kabisa na kujirusha.

Alipopata wazo hilo, hakutaka kubaki chuoni, akatoka, akachukua bodaboda na kumwambia dereva ampelekea Makumbusho.
Safari ikaanza, njiani alikuwa akimuomba Mungu msamaha kwa uamuzi aliokuwa ameuchukua, hakutaka kuendelea kuishi huku akiwa na maumivu moyoni mwake, ili awe na furaha, amani ilikuwa ni lazima kujimaliza.

Pikipiki ilikuwa ikiendeshwa kwa mwendo wa kasi. Ilipofika Mwenge, dereva akakata kushoto na kuchukua Barabara ya Ally Hassan Mwinyi na kuanza kuitafuta Bamaga.
Wakati dereva akiwa kwenye mwendo wa kasi, kwa mbele yake akaiona gari ikija kwa mwendo wa kasi. Hakuogopa, alikaa upande wake akiwa anaendesha kwa mwendo wa kasi pia.

Wakati gari lile la upande mwingine lilipokuwa limekaribia, dereva wa gari hilo akayumba, akahama njia na kwenda katika upande ule uliokuwa pikipiki ile, hapohapo wakakutana uso kwa uso.

Ulisikika mzinga mkubwa, gari likabondeka kwa mbele, pikipiki ikarushwa, dereva na Nandy wakarushwa, na kwa sababu Nandy hakuwa amevaa helmenti, akafikia kichwa kwenye lami, damu zikaanza kumtoka, kama jinsi alivyokuwa amefikia, akatulia hivyohivyo juu ya lami, hakutingishika hata kidogo.
“Mungu wangu!” alisema jamaa mmoja huku wakiwakimbilia watu hao.

Dereva alivunjika miguu na kiuno huku Nandy kwa kumwangalia harakaharaka, alikuwa amevunjika shingo na alionekana kuumia sana kichwani na mgongoni akiwa amechunika kutoka na mwili wake kuburuzika kwenye lami kabla ya kufikia pembeni kidogo ya mtaro na kutulia hapo.
“Jamani huyu mwanamke naye vipi? Mzima?” aliuliza jamaa mmoja.

“Huyu amekufa! Jamani simamisheni gari tuupeleke mwili huu hospitali,” alisema mwanaume mwingine aliyekuwa amemsogelea Nandy pale alipokuwa.

JE, nini kitaendelea?
Je, huo ndiyo mwisho wa Nandy?
Je, Dickson atamuoa Linda?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom