SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

Mtasoma story asubuhi kasema shunnie me secretary wake leo laptop anaitumia kwa forex mumuwie radh
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 47*

*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Chupa hii ilikuwa pana nyeusi. Ndani yake kulikuwa na mwanga hafifu wa kijani. Akaiteka kwa mikono yake na kuiangaza vema.

Kwa mbali akagundua chupa hii ilikuwa inatoa mlio wa mapigo ya moyo!

ENDELEA

Akashangazwa sana na hilo. Asiamini akaiweka chupa hiyo sikioni aisikie vema. Tih! - tih! - tih! Chupa ilikuwa inalia. Akatamani kuifungua, lakini akasita!

Ni nini hiki? Vipi nikikifungua itaniathiri? Akajiuliza kifuani. Akakitazama tena kitu hicho, na mara akasikia mlango unagongwa! Haraka akaificha chupa hiyo mgongoni.

"Samahani ewe kipenzi cha mfalme," alisema kijakazi. "Nahitaji kufanya usafi!"

"Saa hii?" Tattiana akatahamaki.

"Ndio. Huwa nakifanyia usafi majira haya baada ya kwengine.'

Tattiana akafikiria kidogo kisha akasema:

"Hapana! Acha tu, kwa sasa nina matumizi nacho!"

Kijakazi akaenda zake. Tattiana akaketi kitandani na kufungua ile chupa. Moshi mkubwa rangi ya kijani ukatoka humo. Haraka Tattiana akaifunga.

Lakini moshi huo uliotoka ukasambaa humo chumbani na kuenea. Akashangaa mbona umeongezeka kiasi hicho? Katika namna ya kushangaza akaona moshi ukijikusanya na mara ukajiumba kiumbe mkubwa wa kiume mwenye ndevu zilizojivingirita kutengeneza namba moja.

Kichwani hakuwa na nywele. Mikononi alikuwa ana bangili na sikio lake moja alikuwa ametoga hereni ya duara.

Tattiana akaogopa sana. Akajikunyata kwa hofu akisogelea konani mwa kitanda. Mwili wake ukatetemeka na akatamani kupiga yowe.

"Nefil njhami khatu habab?" Akauliza yule kiumbe. Tattiana akamtikisia kichwa akimwambia hamwelewi. Lakini kile kiumbe kikarudia tena swali lake mara mbili. Kimya. Mara akapotea.

Akamwacha Tattiana kwenye maswali kedekede. Akaitazama ile chupa kwa mshangao na kwa kutaka kujua zaidi, akaifungua tena!

Moshi ukazagaa na yule kiumbe akatokea kwa mara nyingine. Akamuuliza swali lile lile:

"Nefil njhami khatu habab?"

Tattiana hakuwa anaelewa. Akamuuliza yule kiumbe yeye ni nani na ametokea wapi? Hakujibu. Akabaki kurudia swali lake mpaka akapotea.

Tattiana akarejesha chupa kabatini kuificha alafu akaenda nje akiendelea kuiwaza. Hata baadae akataka kumuuliza mfalme lakini akaogopa.

Akajiuliza vipi kama chupa hiyo itakuwa ya kwake, inamhusu? Vipi kama kiumbe kile akawa anakimiliki yeye? Hakutaka kuwa msumbufu ama kumfanya mtu aanze kumtilia macho kila anachofanya. Akaona kheri anyamaze.

Atafuatilia zaidi.

**

Usiku ...

Matarumbeta matatu yakalia kwa kuigana sauti. Mfalme alikuwa amesimama nje ya kasri yake akiambatana na viongozi kadhaa. Walikuwa wamesimama hapo wakiwapokea wazee waliowatuma kwenda kwa Venim.

Baada ya mfupi, wakagundua ni mzee Harid pekee ndiye alirejea. Wakamkarimu na kumkaribisha ndani asifahamu kabisa kama mambo yameharibika. Akaeleza yaliyotokea huko.

Venim yupo tayari kuwasaidia, ila kwa malipo. Anamhitaji huyo mwanamke aliyevaliwa na mlozi, ambaye ni Rhoda. Na kama haitoshi anahitaji kiasi fulani cha dhahabu ambacho atampelekea.

Hiyo ya dhahabu akiwa ameliongezea yeye mwenyewe apate 'cha juu'.

"Anamtaka Rhoda?" Mfalme akauliza kana kwamba hakusikia. Hili swala lilimuwia vigumu kidogo kuliridhia.

"Ndio, anamhitaji mwanamke huyo," Venim akasisitizia. "Bila shaka hatuwezi kuiteketeza Goshen nzima kwasababu ya mwanamke na vipande kadhaa vya dhahabu. Si ndio?"

"Kabisa," mfalme akaitikia. "Hatuna budi kufanya kila lililo mikononi mwetu kuikomboa Goshen."

Mzee Harid akamtazama Tattiana na kutabasamu. Tattiana akamkazia macho akimtazama kwa uso mgumu. Moyoni mwake alikuwa anaungua na hasira dhidi ya mzee huyo.

Alipomuona akamkumbuka Roboth na namna alivyokufa kinyama. Akatamani kumrukia mzee huyo na kumraruararua.

"Unaendelaje binti yangu?" Harid akauliza. Tattiana akamtazama pasipo kumjibu. Kinywani mwake alikuwa akisaga meno.

Akataka kunyanyuka, lakini mfalme akamzuia kwa kumdaka mkono kisha akatazamana na wanajeshi wake waliokuwa eneoni na kuwapa ishara kwa kichwa. Mara wanajeshi wakamsonga mzee Harid na kumweka chini ya ulinzi.

"Mfalme, nini hiki?" Harid akatahamaki.

"Hiko ndicho unachostahili!" Mfalme akamjibu. "Hicho ndicho wanachostahili wauaji na wafanyabiashara haramu!"

Harid akazidi kutahamaki. Akakabwa na kigugumizi.

"Muuaji? Mimi? Biashara gani? Mbona hakuna ninachoelewa hapa? ... kujitolea kwangu kumekuwa kosa!
"
"Nyamaza!" Mfalme akamkaripia. "Unavyozidi kuongea upuuzi wako ndivyo na ukubwa wa adhabu yako itakavyokuwa! Kila kitu kipo bayana. Hakuna cha kuficha tena Harid! Damu ulizozimwaga zitakuwinda."

Mfalme akaongea kwa hisia sana. Akapiga meza na kutangaza:

"Kuanzia leo cheo chako cha uzee wa himaya umevuliwa. Utakuwa mfungwa mpaka kifo chako!"

Harid akalia kwa sauti kuu.

"Nisamehe mfalme! Nimekosa sana. Nami ni mzee mno niache nifie nyumbani kwangu mikononi mwa watoto wangu!"

"Watoto gani?" Mfalme akauliza. "Hao unaowaagiza wakaue watu? Hawapo, wanatafutwa himaya nzima. Na watakapopatikana watafungwa wakamalizie ujana wao wote gerezani!" Mfalme alifoka.

Mzee Harid akamwaga machozi. Akamwomba mfalme ampatie angalau nafasi ya kwenda kutembelea nyumba yake kabla hajapelekwa huko wanapotaka kumpeleka.

Mfalme akakataa. Harid akamwomba zaidi. Tattiana akamsihi mfalme amkubalie mzee huyo ombi lake la mwisho. Mfalme akakubali.

Harid akachukuliwa chini ya ulinzi mkali, akapelekwa mpaka nyumbani kwake. Huko akapekua nyumba yake nzima, mpaka kule mafichoni ajuapo yeye na wanaye tu, hakuona senti hata moja!

Fedha zote alizozihangaikia hazikuwapo! Hakubakiziwa hata tone.

Akaishiwa nguvu.

"Oragon ..." akaita kwa uchungu. "Ottoman!" Akayarudia majina hayo ya wanawe mpaka wanajeshi walipokuja kumzoa na kumtupia ndani ya toroli la farasi.

Akamimina machozi njia nzima. Hata haikujulikana alikuwa anatakia nini hizo pesa na wakati anaenda gerezani.

Akawekwa kwenye chumba chake cha pekee, komeo zikakaba mlango.

"Hayo ndiyo maisha yako mapya!"

**

"Kwanini lakini uliamua kufanya hivyo?" Tattiana alilalamika akishikilia nondo za lupango. Macho yake mekundu yalikuwa yanamtazama mzee Harid aliyekuwa ameketi chini kimya.

Yalikuwa ni majira ya asubuhi.

"Roboth alikutendea nini baya ukammaliza kinyama vile?" Tattiana aliongea kwa sauti ya kilio. "Alikutendea nini?" Akafoka. "Alikutendea nini?" Akarudia tena.

Harid akamtazama kwa jicho la hasira.

"Nyamaza!" Akapaza sauti yake. "Ewe mwanamke mpumbavu usiye na macho wala akili."

Akanyanyuka na kusogea.

"Unadhani ungekuwa meza moja na mfalme, ukalala naye kitanda kimoja, ukaishi naye nyumba moja pasipo mimi? Nani ameroga hiko kichwa chako ewe ng'ombe uliyepelekwa mtoni usijue kunywa?" Harid akalalama. "Kwanini umekuwa wa kushupaza na kutoona wema?"

"Wema gani? - kumuua Roboth?" Tattiana akalia.

Harid akamtazama kwa msisitizo na kumwambia kwa sauti ya chini:

"Nilikupokonya moja ili ubaki na moja la maana, sema ahsante angalau. Lililobakia mkononi mwako ni la thamani mno. Hauoni namna mfalme akupendavyo? U mpofu wa aina gani wewe?"

Tattiana akataka kunena, Harid akamkatiza.

"Najua moyo wa mfalme upo mikononi mwako. Nenda kamshawishi kwa sauti yako tamu karibu na sikio aniachie huru."

"Sahau kuhusu hilo!" Tattiana akamwambia akitikisa kichwa. "Halitawezekana angani wala ardhini."

Harid akatabasamu.

"Nadhani umesahau baba yako anahusika kwenye hili. Sasa chaguo ni lako. Ukamwambie mfalme anitoe ama niropoke kila kitu kwenye masikio yake."

Tattiana akakaukiwa maneno mdomoni.

**

Akajilaza kitandani akiwaza na kuwazua.

Alikuwa ana mafundo moyoni na mawazo mengi kichwani. Alihisi kuchanganyikiwa. Hakupata hata usingizi.

Akaketi kitako na kushika tama. Akawaza siku yake nzima kuanzia kwa yule kiumbe aliyemwambia maneno ya ajabu asiyoyaelewa mpaka kwa Harid aliyempa vitisho. Akaona ni mzigo mkubwa. Kichwa chake hakiwezi peke yake.

Akamgusa mfalme na kumtikisa.

"Mfalme, naomba niongee nawe," akanena moyoni. Kinywa kilikuwa kizito kutamka.


**
 
*MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN II -- 48
*Simulizi za series*

ILIPOISHIA

Akaketi kitako na kushika tama. Akawaza siku yake nzima kuanzia kwa yule kiumbe aliyemwambia maneno ya ajabu asiyoyaelewa mpaka kwa Harid aliyempa vitisho. Akaona ni mzigo mkubwa. Kichwa chake hakiwezi peke yake.

Akamgusa mfalme na kumtikisa.

"Mfalme, naomba niongee nawe," akanena moyoni. Kinywa kilikuwa kizito kutamka.

ENDELEA

Mfalme hakuamka kwani alikuwa kwenye usingizi mzito. Tattiana alimwamsha kwa uoga akimparasa. Hata maneno aliyokuwa anayatamka hayakutoka kinywani, yakaishia mdomoni.

Alikuwa anaogopa. Mfalme atamwelewa? Au atakuwa amemrahishia uchunguzi wake na basi atatuma wanajeshi wake wakamnyake baba yake?

Akasimama na kwenda dirishani. Akaendelea kuwaza. Akiwa hapo akasikia sauti ya kitu kama sufuria kikianguka. Akashtuka lakini hakudiriki kutoka nje ya chumba.

Hakujisikia kwenda mahali popote leo hata kule chumbani kwake. Basi akasimama hapo dirishani kwa muda mrefu mpaka aliposikia sauti ya mfalme ikimuita.

Hakujua ilikuaje akaamka.

"Mbona upo dirishani saa hii?" Mfalme akamuuliza. Akamjibu hana usingizi. Mfalme akanyanyuka na kumfuata.

"Una tatizo gani, Tattiana. Nieleze?"

"Hata nikikueleza utaelewa?" Tattiana akajiuliza moyoni. Akamtazama mfalme na mara akashindwa kujizuia kulia. Mfalme akambembeleza sana. Akamsihi amweleze kinachomsibu. Yupo radhi kumsaidia.

Basi Tattiana akafungua kinywa chake. Akamweleza mfalme kwamba baba yake naye anahusika na biashara ya Cedar.

Mfalme akatahamaki.

"Unasemaje?" Akauliza kwa hasira. Lakini uso wa huzuni wa Tattiana ukayeyusha hasira yake ngumu.

"Alifanya hivyo kwa kulipa fadhila kwa mzee Harid baada ya mzee huyo kukukutanisha na mimi. Hakuwa na namna, kwani hakuna familia isiyotaka kutoa malkia."

Akapiga magoti na kulia miguuni mwa mfalme.

"Naomba umsamehe baba yangu. Naomba utusamehe kwani tumekuingiza kwenye matatizo makubwa!"

Mfalme akakosa cha kusema. Akajaribu kuukaza moyo wake lakini akashindwa. Akamnyanyua Tattiana na kumsihi anyamaze. Amemwelewa na atalifanyia kazi.

Kesho yake asubuhi Melkizedek akaitwa kasrini na kuketi meza moja na mfalme pamoja na Tattiana. Alikuwa anaogopa mno. Hakuweza hata kumtazama mfalme usoni akatazama chini.

Mfalme akamtaka amweleze kila kitu asifiche jambo. Melkizedek akaweka bayana tangu siku ya kwanza kukutana na mzee Harid na namna alivyomwambia kumhusu binti yake.

"Nipatie msichana huyu, hakika anaweza kuyadaka macho ya mfalme akamuoa."

Lakini hakumweleza kama angehitaji fadhila hapo baadae. Bahati mfalme alipompenda mwanae, sasa ndipo alipoanza kutaka kutumia hiyo fursa.

"Sasa ni wakati wa malipo. Inabidi ufanye hivyo ili nami nikatie juhudi asiishie kwenye uchumba bali aolewe kabisa," akahadithia Melkizedek. "Na malipo yake hayakuwa fedha, ningempatia, yalikuwa kumsaidia kupitisha cedar mpakani."

Alipoeleza hayo, mfalme akakasirika sana. Kumbe Harid alitumia nafasi yake ya kutokuwa na mke kama mtaji? Hakujua mzee huyo alikuwa dhalimu kiasi hicho.

Kwasababu hii ilikuwa siku moja kabla hajaitwa na baraza la wafalme, akaona ni bora akafanya jambo. Akawaagiza watumishi wake wajiandae kwa ajili ya safari ya kwenda Maam hivi punde.

Wakamtoe mzee Harid gerezani, wamtie kambani na kumpakia kwenye toroli.

"Naweza nikaenda nawe?" Tattiana akauliza.

"Hapana," mfalme akamjibu kisha akamshika mikono. "Bakia na Goshen. Hili inabidi nikalifanye mwenyewe."

Baada ya chini ya lisaa, mfalme akaanza safari yake kwenda Maam akiwa ameongozana na kikosi chake kikubwa cha wanajeshi, viongozi kadhaa pamoja na mfungwa, mzee Harid.

Wakatumia masaa kadhaa kufika huko. Hayakuwa mengi, kama mawili ama matatu, kwani Maam haikuwa mbali sana.

Wakakutana na baraza la wazee la himaya hiyo, kwani mfalme alikuwa hoi kitandani. Wakibashiri hata leo ikipita hajafariki, basi itakuwa miujiza ya miungu yao.

Mfalme akawaomba msamaha kwa yote yaliyotokea. Akawaambia wamefanikiwa kumpata yule aliyehusika na biashara hiyo. Na wamemleta wamfanye watakavyo.

Harid akapokelewa na kuhamishiwa kwenye gereza la Maam tayari kwa ajili ya kunyongwa kesho yake mbele ya watu.

"Ina maana amehusika mtu mmoja tu na hii biashara?" Mfalme akaulizwa.

"Hapana," akajibu akitikisa kichwa. "Alikuwa akifanya pia na wanawe, bado wanatafutwa. Inaaminika watakuwa wamekimbilia himaya zingine."

Mfalme akajua sasa mambo yatakuwa yamekwisha. Lakini kinyume na hayo, baraza la Maam likamwambia alichofanya bado hakikuwa kinatosha! Uzembe wa himaya yake unapelekea mfalme wao kufa, kumtoa mtu mmoja kutawezaje kufidia hilo?

"Tayari uhusiano kati ya Maam na Goshen umepasuka," akaeleza mzee mmoja wa baraza. "Inabidi zifanyike jitihada za ziada kuurejesha upya. Sasa kesho kutwa tutamkabidhi mtoto wa kwanza wa mfalme madaraka ya baba yake. Mtoto huyo atahitaji kupata mke. Mke mzuri atakayekuwa malkia wa Maam. Ni kheri kumtafutia mke huyo huko Goshen kwa dhumuni la kuboresha uhusiano wetu tena."

Mfalme hakuwa na namna ya kulikataa hilo. Aliona ni kheri, akaahidi kulifanya. Akaaga na kabla hajaondoka akaenda kuonana na Harid gerezani.

"Najua umemhifadhi, Melkizedek kwasababu ya Tattiana," Harid akamwambia mfalme. "Nimeshiriki naye kwenye hili kwanini yeye amepewa huruma?"

"Kwasababu ulimlazimisha alifanye kama malipo," mfalme akamweleza.

Harid akatabasamu kisha akamwambia mfalme.

"Mimi ni mzee. Kifo changu hakitajalisha sana. Mbali na hivyo umri wangu mwingi umeishia kuitumikia Goshen kwa kuwa mshauri wa mambo kadha wa kadha. Najua ambacho watakuwa wamekueleza. Nina uzoefu mkubwa na hayo mambo."

Akaweka kituo wakitazamana na mfalme. Kisha akauliza:

"Je, hawajakueleza kwenda kumtafuta mke kwa ajili ya mfalme wao ajae?"

"Hayo mambo hayakuhusu!" Mfalme akamkaripia. Mzee huyo akatabasamu kisha akasema:

"Kuwa mwaminifu, Phares. Hakuna msichana mzuri ndani ya himaya nzima kushinda Tattiana. Bado haujamuoa. Mtoe kwa ajili ya Goshen."

Mfalme akampuuzia. Akageuza mgongo wake aende. Harid akapaza sauti.

"Kama wewe hautawaambia kuhusu hilo. Mimi nitawaeleza!"

Mfalme akageuka na kumtazama Harid kwa jicho batili.

**

Koh!- Koh!-Koh!

Sauti ya kikohozi iliwashtua Fluffy na Zura. Walikuwa wamejikunyata ndani ya chumba chao chenye bakuli la mchele. Wakanyanyuka upesi na kuangaza kwenye chumba kingine, hamaki wakamwona Malkia na Waheed wakiwa wamejilaza wamechoka mno na wana majeraha kadhaa.

Wakawakimbilia na kuwauliza kulikoni. Malkia akawaambia wamepitia jaribu kubwa mno. Huko porini walipokuwa walikutana na watu wote wawapendao ambao walikufa huko miaka ya nyuma, na hawakuweza kuyashinda hayo kupata ufunguo pasipo kuwaua tu.

Wakiwa hapo mara wakasikia sauti ya kiume ikilia. Wakatazama chumba cha tatu, wakamwona Seth na Alk! Seth alikuwa anamimina machozi. Macho yake yalikuwa mekundu, mwili wake umejawa na mchanga. Wakamuuliza kulikoni?

Akawaleza amemuona baba yake baada ya miaka na miaka sasa kupita. Lakini si hilo linalomliza. Bali kumwona baba yake akifa mbele ya macho yake, mikononi mwa Alk.

"Hakuwa baba yako huyo!" Malkia akamtoa hofu.

"Ndio," akajibu Seth. "Hakuwa baba yangu, alikuwa ni jini na mara tulipommaliza akatupatia funguo. Lakini amenikumbusha baba yangu!" Seth akalalama. "Ni kitambo sana sijamwona."

Fluffy akamkumbatia Seth kumpa pole. Akamfuta machozi na kumtaka waendelee na safari. Washukuru wametoka wazima kwenye kila pambano. Kamwe haikuwa rahisi.

Basi wakaunganisha funguo zao na mara mlango mkubwa ukatokea ukutani. Wakaufungua na kuendelea kutembea.

Baada ya muda kidogo, wakakutana na watu watatu. Wanawake waliopendeza haswa. Wamebana nywele zao, wananukia na wamejipara wakavutia.

Wanawake hao walikuwa wakiongea kuhadithiana jambo fulani lililoonyesha kuwavutia. Lakini hawakuonyesha kama waliwaona wakina Malkia, wakapishana nao kama kivuli, wakaendelea na safari yao wakihadithiana mpaka wanapotelea.

Dakika mbili mbele, wakawaona tena wanawake hao. Sasa walikuwa wawili na si watatu kama mwanzoni. Walikuwa wamevalia majoho ya dhahabu, nywele zao ndefu wameziachia, wejipara usoni wakavutia, wananukia mithili ya bustani. Weupe waking'aa kama mwezi.

Walikuwa wana furaha wakihadithiana jambo. Na kama wale watatu waliopita, nao wakawapita wakina Malkia kama kivuli. Wakayoyoma wakiendelea kuhadithiana kwa furaha.

Mbele tena kidogo, wakamwona mwanamke mwingine akija. Sasa hivi alikuwa yu mmoja tu. Alikuwa amevalia joho la kupendeza akitembea taratibu anatazama chini. Alionyesha yu mpweke na hana furaha.

Alipowakaribia wakina Malkia akanyanyua uso wake na kuwatazama. Wakashtuka. Kinyume na wale wanawake wengine waliopita, huyu hakuwa mzuri hata kidogo. Mdomo wake ulikuwa umechanwa mpaka sikioni. Wanja aliokuwa ameupaka kuzunguka macho yake ulikuwa umevuja kwa machozi.

Akawauliza:

"Mimi ni mzuri?"

**
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom