MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 017
Simulizi za series
Usiku ulikua na kukua, mwishowe kukakucha kukipokelewa na habari za kifo cha Malkia Vedas. Habari hii ilikuwa nzito, shughuli zote ndani ya tawala ya Goshen zilisimama kupisha msiba huo. Kila mtu alishangazwa katika namna yake, ingawa si wote walioumizwa. Malkia Vedas hakuwepo ndani ya mioyo ya watu kabisa.
.
.
Watumishi walitumwa huku na huko kusambaza taarifa za msiba wa Malkia Vedas kwenye tawala zingine za ng’ambo. Mpaka kufikia mchana, habari hizo zilikuwa zimesambaa vya kutosha, ila muitikio wake ulikuwa finyu. Hakuna tawala iliyokuwa na uhakika kama itahudhuria msiba huo.
.
.
Mahema yalitengwa na maeneo pa kupokelea wageni. Maiti ya Vedas ilifungwa katika sanda ya gharama na kutunzwa kwenye chumba mahususi cha maiti. Watu kadhaa, haswa wa ndani ya himaya walijongea maeneo ya uwanja mkuu palipokuwa panaendeshwa ratiba za msiba. Hata wao hawakuwa wengi.
.
.
Miongoni mwa hao watu alikuwapo mwanamke aliyevalia gauni refu jeusi, kofia yenye miwani ya wavu, glovu nyeusi na viatu virefu vyeusi. Japokuwa alikuwa masitikoni, alikuwa amependeza. Midomo yake ilikuwa na rangi nyekundu na macho yake yakitingwa na rangi nyepesi nyeusi. Mwanamke huyu alikuwa Rhoda.
.
.
Aliketi mahala pa juu, sehemu za watu muhimu. Alipoketi alijipepelea na kipepeo chake chenye matundu kadhaa akirusha macho yake huku na kule kama mtu anayehesabu watu. Nani alikuwa anamtafuta? Haikujulikana. Kama vile alikata tamaa, akaacha kuangaza na kupoza machoye. Ila mara akasikia sauti ya mtu inamuita. Aligeuza macho akamuona mwanakijiji.
“Unaitwa kule!” Alisema mwanakijiji huyo akinyooshea kidole upande wake wa kaskazini. Rhoda alipotazama, akakutana na Phares. Alimpa ishara ya kumuita.
.
.
Phares alikuwa amevaa suti ya kaki ya ngozi iliyokuwa imedariziwa na nyuzi za dhahabu. Nywele zake zilikuwa zimechanwa vema ziking’aa, ndevu zake pia. Alivutia kutazamwa.
.
.
Rhoda alisimama, akiwa ameshikilia gauni lake, akaondoka kumfuata mwanaume huyo. Aliketi kandokando yake pasipo kuongea kitu. Baada ya kama dakika moja ndipo wakaanza kuteta, Rhoda akiwa wa kwanza kutoa sauti yake inayolaghai masikio ya nyoka wa pangoni.
.
.
“Nimesikia ameuawa, nani kafanya hivyo?”
.
.
Phares alivuta pumzi ndefu.
.
.
Hakujibu kwa papara bali alingoja. Macho yake yalikuwa madogo na mekundu. Mahali alipokuwa ameketi palikuwa papweke, konani mwa uwanja, ila aliweza kuona kila linalotukia.
.
.
“Sijajua nani aliyefanya hilo tukio, na sijajua nini lengo lake juu ya hili.”
.
.
“Hujapata kiashiria chochote?” Rhoda aliuliza.
“Nilichokipata ndicho kinanipa mashaka,” akasema Phares kwa ufupi.
.
.
Aliendelea kutazama watu lakini fika akili yake ikiwa inadadavua. Rhoda hakuuliza tena, alikuwa anangoja jibu la swali lake.
.
.
“Aliyemuua Vedas ni Malkia Sandarus,” alisema Phares. Rhoda akashindwa kujizuia na kutabasamu.
.
.
“Phares, nini unaongea? – Malkia Sandarus aliyekufa kitambo?”
.
.
“Ndio maana nikakuambia nilichokipata kinanipa mashaka.”
.
.
“Ila inawezekanaje? Umejuaje hayo?”
.
.
“Ni kwa mujibu wa maneno ya mlinzi,” alijibu Phares, kisha akaongezea:
.
.
“Mlinzi wa malkia alipambana naye kabla hajashindwa, akajeruhiwa na kutupiwa stoo.”
“Ndio amesema ni Malkia?”
.
.
“Ndio. Adui alikuwa na mwili wa Malkia Sandarus!”
.
.
“Vi – vipi? Kuna kitu chochote amechukua?”
.
.
Rhoda alilipuka na swali. Uso wake ulibebelea shaka. Kuna namna alikuwa ameguswa. Phares alimtazama akaona shaka lake hilo usoni.
.
.
“Vipi, kuna tatizo?”
.
.
“Hapana, nilitaka tu kujua,” alipoza Rhoda. Alijitahidi kuigiza kila jambo li shwari.
.
.
“Sijaona chochote ambacho amechukua mtu huyo,” alisema Phares. Moyo wa Rhoda ukawa wa baridi kabla haujalipuliwa na muendelezo.
.
.
“Isipokuwa tu mkufu.”
.
.
“Mkufu!”
.
.
“Ndio, mkufu,” alijibu Phares. Pasi na shaka hakuona kama kuna jambo kubwa hapo. “Nimeshangazwa kwanini ameubeba mkufu huo? – kuna lolote unalolijua kuhusu huo mkufu?”
.
.
“Hapana,” alijibu Rhoda uso wake ukimsaliti. Phares alimtazama mwanamke huyo, alikuwa amepoteza amani. Uso wake ulibebwa na mafuriko ya mawazo.
.
.
“Rhoda,” aliita. “Kuna shida yoyote?”
.
.
“Hapana, Phares.”
.
.
“Hapana, Rhoda. Kuna jambo unanificha. Naomba unieleze kuhusu huo mkufu, na kama unajua kama kuna lolote linalohusiana na marehemu Malkia Sandarus na mkufu huo.”
.
.
Mdomo wa Rhoda ulikuwa mzito. Alikuwa anataka kusema lakini moyo wake ukimkataza. Ila akinyamaza, mkufu huo utageuka ndoto, wapi ataupata na anauhitaji?
.
.
Kwa namna kubwa aliona Phares ndiye pekee anayeweza kuutafuta huo mkufu na kuusogeza tena karibu, kwahiyo hakuwa na budi kupambana na moyo wake kueleza.
.
.
“Phares,” Rhoda aliita. “Mkufu ule ni mali kubwa sana. Ni nguvu, na ni madaraka.”
.
.
“Kivipi?”
Kabla Rhoda hajaendelea, sauti kubwa ya pembe la ng’ombe iliita. Phares alinyanyuka akamuaga Rhoda.
.
.
“Bila shaka nahitajika. Nitakutafuta tuongee zaidi.”
.
.
Rhoda alimshika mkono Phares. Kuna kitu alitaka kusema ila akaamua kughairi na kuishia kusema:
.
.
“Sawa, tutaongea.” Phares akaondoka. Alipoishilia, Rhoda akanyanyuka kwenda mpaka kwenye kasri kumtafuta mlinzi wa marehemu, yule aliyempatia kazi ya upelelezi.
.
.
Alimuulizia mlengwa wake, akaelekezwa na kumpata baada ya kuhonga kiasi fulani cha dinari. Mwanaume huyo alikuwa amefunga mikono yake kwa kitambaa, uso na kichwa chake pia vikiwa na majeraha.
.
.
Walisogea na Rhoda mpaka kando ya kificho.
.
.
“Nini kilitukia?”
.
.
“Ni Malkia Sandarus!” alistaajabu mlinzi. Aliongea akiugulia maumivu.
.
.
“Ni ajabu sana, sikuweza kufua dafu hata kidogo. Kila nilipojitutumua niliishia kugaragazwa kwa maumivu. Yule si Malkia kabisa!” alitikisa kichwa mlinzi.
.
.
“Si Malkia. Kuna roho ndani yake. Macho yake yalikuwa yanaogopesha. Nguvu zake hazikuwa na mithili.”
.
.
“Kuna lolote alilosema?” Rhoda aliuliza. Mlinzi akatikisa kichwa.
.
.
“Hapana, hakusema kitu. Wakati akitenda hayo yote alikuwa kimya asiyefungua kinywa.”
.
.
“Ulimuona wakati anakwapua mkufu wa malkia?”
.
.
“Hapana. Alihakikisha kwanza amemalizana na sisi kabla hajaingia chumbani. Alitu muda mchache sana kutimiza haja yake.”
.
.
“Unadhani atakuwa ameupeleka wapi ule mkufu? Una wazo lolote wapi alipotokea?” Mlinzi akatikisa kichwa na kubinua mdomo wake.
“Ila kuna taarifa zinaweza zikasaidi kujua. Kuna wanajeshi watatu wameuawa karibu na mpaka wa Tanashe. Jambo hilo linanifanya niamini mtu huyo atakuwa ameelekea huko baada ya hayo mauaji.”
.
.
“Tanashe! – himaya ya wachawi?”
.
.
“Ndio!”
.
.
“Kuna mtu yeyote anayeweza kudiriki kwenda huko?”
.
.
“Kama tu kuna sababu kubwa ya kufanya hivyo.” Haraka kichwani mwa Rhoda ikaja taswira ya Phares. Huo unaweza ukawa mlango wa kutokea, alijisemea. Ila ni wazi atahitaji nguvu kubwa ya ushawishi. Kutobakiza hata tone moja la shaka kwenye kichwa cha mwanaume huyo.
.
.
Aliaga akaondoka. Alibakiwa na kazi moja kubwa sasa, namna ya kufua na kuondoa shaka kwenye moyo wa Phares; namna ya kumpa sababu nzito mwanaume huyo.
.
.
.
.
.
.
.
*** .
.
.
.
.
.
Giza kali lililoambatana na milio ya wadudu lilikuwa linazonga macho. Si kwamba giza hili liliingia muda huu, hapana. Lilikuwa ndilo lililopo kila siku kwenye himaya hii ya Jayit, Devonship. Laiti kama wewe binadamu ungekuwamo humo basi ungelazimika kutumia kurunzi, la sivyo usingefika popote.
.
.
Basi kulikuwa kimya, wakati huko ulimwengu mwingine kukiwa ni majira ya mchana sasa. Kwenye kasri ya Jayit kulikuwa kimya zaidi. Maginga machache ya moto yaliyokuwa yanawaka, bado hayakutosha kupambana na giza hivyo basi kulikuwa na kagiza chenye ladha nyekundu kwa mbali.
.
.
Ndani ya kasri hiyo kulikuwa kana kwamba shimo. Ungeweza kusikia sauti za watu wakihema, ila usingewaona. Na pia ungeweza kuwasikia watu wakitembea, lakini pia usiwaone. Yani shughuli zinakuwa zinaendelea kama kawaida, ila katika hali ambayo macho ya mwanadamu yasingeweza kufua dafu.
Sauti ya kimiminika ilivuma, kisha ikafuata sauti ya kuamuru:
.
.
“Basi inatosha.” Sauti ya kimiminika ikakoma, ikafuatiwa na sauti ya koromeo likipokea kilichomiminwa: gulp! – gulp! – gulp! Aaaagh…
.
.
“Nimeshaamua,” sauti ya Jayit ilisema kimamlaka, ikaongezea: “Sidhani kama nahitaji tena ushauri. Tufunge mjadala kwenye hili.”
.
.
“Lakini mkuu, nadhani ingekuwa ni nafasi ya wewe kutusikiliza sasa baada ya mpango wako wa kwanza kufeli,” ilisema sauti moja kavu ya kizee.
.
.
“Laiti kama ungekuwa umetupa fursa ya kusikia tuliyosema hapo awali, haya yasingetukia.”
.
.
“Kwahiyo unanikosoa, Badili?”
.
.
“Hapana, mkuu, ila nadai nafasi ya kusikilizwa. Wote tunajenga nyumba moja, hatuna haja ya kugombea fito.”
.
.
Kulikuwa kimya usijue kama watu wapo ama wameondoka. Baada ya muda kidogo, kama dakika moja na ushenzi, kukasikika sauti ya kusafisha koo, kisha:
.
.
“Sawa, nawasikiliza. Mlikuwa mnasemaje?”
.
.
“Mkuu, adhabu ya kuwaua wanajeshi walioponea vitani, pamoja na kumining’iniza jemedari Raiden, ilikuwa kubwa sana. Tumepungukiwa sana kijeshi, tumebakiwa nao haba, bila shaka tulikuwa tunawahitaji. Ila kwakuwa ya nyuma si hoja, tutazame ya mbele.” Sauti hiyo ilikomea hapo, na mara ikapokelewa na nyingine. Hii ya sasa ilikuwa laini, ila pia ya mtu aliyekula chumvi, na mtulivu.
.
.
“Tuna haja kubwa ya kutulia kwa sasa, kama kweli tuna nia ya kuweka himaya zote hizi chini yetu.”
.
.
“Kutulia?” Sauti iliuliza.
.
.
“Ndiyo, kutulia,” sauti ya awali ikavuma.
.
.
“Endapo tukivamia kwa papara tutaendelea kuwa wahanga wa kushindwa. Habari zitavuma kote, na kila himaya sasa watakuwa wanajipanga ama kujua namna ya kutukabili.”
“Kwahiyo mnashaurije? Tunatulia namna gani?”
.
.
Sauti nyingine, ile kavu iliyokuwa inaongea hapo awali, ikaendeleza soga.
.
.
“Tumekaa tukajadili, tukashauriana na kukubaliana. Njia nzuri ya kuujua udhaifu na mipango ya kila himaya, ni kwa kupandikiza watu wetu. Mkuu, tunahitaji kupandikiza watu tunaowaamini kwenye kila himaya kubwa. Watu hawa majukumu yao yatakuwa ni kupenya kututafutia nyaraka na taarifa muhimu. Kutujuza nini kinaendelea, nini kinapangwa na kutekelezwa.”
.
.
Akadakia mwingine.
.
.
“Kwa kufanya hivyo, tutajua nini cha kufanya, namna gani ya kuingia na kushambulia. Kuna baadhi ya himaya hazihitaji nguvu, bali tu ulimi na masikio.”
.
.
“Hamuoni kwa kufanya hivyo tutangoja milele kukamilisha kazi yetu?”
.
.
“Ni bora kungoja kwa uhakika kuliko kuwahi kwa mashaka,” ilisema sauti kavu kwa namna ya kujiamini.
.
.
Hili swala lilikuwa gumu kupenya kwenye kichwa cha Jayit. Alikuwa anaamini nguvu zake za kilozi kuliko utumizi wa akili na mwili kwenye utendaji. Kwa namna alivyofanya matambiko ya kuita nguvu za babu na bibi yake, alitegemea asingekutana na nguvu zozote za kumpinga. Alitegemea awe mfalme wa himaya zote wakati wa usiku, jambo ambalo amelifanikisha kwenye himaya tatu tu. Alikuwa na njaa zaidi.
.
.
Ni kweli wapambanaji wake walikuwa hawaonekani wakati wa usiku. walikuwa ni wenye nguvu na wepesi zaidi. Ila kwa Goshen walikutana na kisiki. Hata kama Jayit angefanikiwa kushinda himaya zote, akashindwa kwa Goshen bado angeliona yu mtupu. Na bado mwenye deni kubwa la kutimiza.
Kishingo upande, alikubaliana na mawazo ya washauri wake, ila akawapa majukumu ya kutafuta watu hao ambao wao wanaona wanafaa kwa ajili ya kazi ya upandikizwaji. Watu hao wafundwe na kisha kutumwa haraka iwezekanavyo, wakianzia Goshen.
.
.
.
.
.
.
.
***
.
.
.
.
.
.
.
Siku na muda uliwadia. Ulikuwa sasa ni usiku wa ile kesho waliyokuwa wanaisema jana yake. Vioo kikubwa viliwekwa sebuleni kwenye kila kona. Marashi ya maiti na moshi wa kijani ulitawala. Mwili wa Malkia Sandarus uliwekwa juu ya meza nyembamba ndefu ukiwa umelala kana kwamba maiti ndani ya jeneza. Juu yake uliwekwa mkufu.
Vikongwe walikuwa wamevalia magauni marefu meusi, yalikuwa yamewabana. Nywele zao zilikuwa zimesimama kwa kuwa hovyo. Vifuani mwao walikuwa wamebebelea mikufu yenye vidani vya vichwa vya mijusi. Mikononi pia walikuwa wamevalia bangili za chuma zilizokuwa na alama zisizoeleweka. Wote walikuwa peku.
Mwili wa Malkia ulikuwa umevikwa joho jekundu lililomfunika mpaka miguu. Alikuwa ameogeshwa na hata nywele zake kuchanwa. Japokuwa alionekana asiye na uhai, bado uzuri wake wa asili ulikuwa unang’aa. Ni kama vile mwanamke mrembo aliyekuwa amelala juu ya mchanga wa bahari akiwa anapunga upepo kipindi cha joto.
Vikongwe wale watatu, kila mmoja wao akiwa na jicho moja, waliuzunguka mwili wa Malkia wakiimba nyimbo ya lugha ngeni. Walienenda mizunguko mitatu kabla hawajasimama na kuutazama mwili uliokuwa mbele yao, mwili wa Malkia Sandarus uliokuwa umepooza kwa kulala. Walitazamana, wakapeana ishara. Mmojawao akarudi nyuma na kurejea na kitabu kimoja kikubwa, kikuukuu.
Kitabu hiki kilikuwa kina jalada gumu mno. Mbele yake, jaladani, kilikuwa kumechora nyota kubwa yenye pembe sita. Nyota hii ilikuwa imeundwa na pembetatu mbili zilizokuwa zimeingiliana, moja ikitazama chini na nyingine juu. Mbali na nyota hiyo kulikuwa na maneno na ishara kadha wa kadha ambazo kuzing’amua kulihitaji ujuzi.
Kitabu hicho kilifunguliwa mpaka kwenye kurasa inayokaribia na mwisho. Hapo kulikuwa kuna mchoro wa mtu akiwa amelazwa kama vile ulivyofanywa mwili wa Malkia. Juu ya mchoro kulikuwa kuna kichwa cha habari, na chini yake kulikuwa kuna maelezo lukuki, ambayo yalianza kusomwa na kikongwe aliyekuwa amebebelea kitabu hicho.
Akiwa anasoma maneno hayo, taratibu hali ya hewa ikawa inabadilika. Radi na ngurumo ziliita, pepo kali nayo ikavuma. Ndani ya nyumba kukaanza kuwa giza ingali kulitundikwa maginga ya moto kadha wa kadha. Mpaka maneno yanamalizwa kusomwa, tayari kulikuwa giza totoro, radi zilikuwa zinafululiza na upepo ukichachamaa.
Kitabu kiliwekwa chini kisha ukatwaliwa mkasi mdogo. Ulikuwa una kutu na mpini wake ukiwa na rangi nyekundu. Kikongwe aliyekuwa amebebelea mkasi huo aliunyakua mkono wa mwili wa Malkia, akaweka mkasi wake kwenye kidole cha mwisho apate kukikata.
Kabla hajafanya hivyo, mara mlango wa sebule yao ukagongwa mara tatu, na sauti ikaita:
“Faki hapa mlangoni.” Haijulikani ni kwa muda gani, ila huko nje ya nyumba ya vikongwe walikuwa tayari wameshajaa fisi si chini ya mia mbili! Walikuwa wakubwa mno kimaumbo. Na nyuso zao zilionyesha hamu, kama sio utayari wa kushambulia.
.
.
.
.
.
.
.
.
LAKO JICHO.