SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

SIMULIZI: Mkufu wa Malkia wa Goshen

shunieeeee
Nimewamiss [emoji7] [emoji7]
Shunie love..najua ushawahi experience arosto ya kusubiri hizi mambo, pls mumy fanya mambo kipnzi..


naomba ratiba kamili shuniee ili niwe nakuja kwa wakati bibie maana kila nikishtuka naingia humu nakuta hollaaaaa

Shunie bhana utatutoa roho

Shunie Shunie arostooo, umetuacha na arostoooo!!!!!!

Shunieeeeeeee ingekuwa kuitwa ni hela basi mi ningekuita mpaka bhasi

Shunie leo umeamua kutususa?

Jaman arosto mbaya

Niko mpakani mwa Goshen nasubiri mpambano wa usiku. Shunie leta mambo mrembo
 
MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 015
Simulizi za series


Siku na jua lake liliangaza. Karim aliamka mapema sana siku hii akajiandaa kwa kutafuta nguo zake nadhifu na kumfungulia farasi wake mpendwa, mkubwa na mwekundu.

Lakini pia akawataka vijakazi wake wawili wapate nao kujiandaa kwa ajili ya safari. Safari hii ilikuwa ni ndefu, ya kwenda kwa Sultan, hivyo basi akapakia maji na hata chakula vya kutoshea njiani.

Walitembea kwa masaa kede huko njiani wakipumzika na kulowanisha tena makoo yao makavu, na kujaza matumbo yao kisha safari ikadumu. Hawakukoma mpaka pale walipotia timu kwenye hekalu la Sultani Mansoor. Hapo walipekuliwa na walinzi kisha wakaruhusiwa kuzama.

Sultan hakuwepo mazingira ya nyumbani kwa muda huo, alikuwa ametoka kwenda ziwani – mahali ambapo hupenda sana kwenda kupumzisha akili yake pindi anapokuwa amechoka. Akiwa huko hupenda kuvua viatu vyake kuacha miguu yake mipana ibarizi na kuchezea maji baridi ya ziwa.

Vijakazi ndani ya hekalu la Sultan walimhudumia Karim pamoja na vijakazi wake. Mganga huyo maarufu akadumu kwa lisaa limoja mbele kabla ya Sultan na mke wake mkubwa kuwasili makaoni mwao, sehemu maridadi inayomeremeta kwa usafi na samani ghali. Karim na vijakaziwe walisimama kumlaki kiongozi huyo. Baada ya kusalimiana na kuketi, hakuna lililokawia zaidi ya maongezi kiini.

Japokuwa mke wa Sultan alikuwa amejitenga, macho na masikio yake yalikuwa pamoja na maongezi hayo. “Ndege yupo wapi?” Aliuliza Sultan akijaribu kuangaza. Karim alishusha pumzi akanyoosha mkono wake.
“Sijaja naye, Sultan. Nimekuja kwanza kuteta nawe.” Uso wa Sultan ulibadilika kwenda kwenye shari. Hakungoja Karim aendelee kusema, akamkatiza.

“Sitaki maneno tena Karim, nimeshayasikia vya kutosha. Nilidhani kijakazi wako amekufikishia vema ujumbe wangu, ila naona kumbe hukuupata.”

“Niliupata, Sultan.”

“Sasa kipi hakijaeleweka?”

“Nimeelewa kila jambo, Sultan. Lakini nasikitika kusema hilo jambo halitawezekana. Huyo ndege …” Sultan alipiga makofi mara mbili, mara wakajiri wanaume watatu waliobebelea majambia marefu yanayometa.

Walikuwa wamevalia kanzu rangi ya krimu na kofia nyekundu, balaghasia. Nyuso zao zilikuwa kazi. Walimtazama Sultan, Sultan akawaelekezea kwa Karim na vijakaziwe.

“Sultan! Mbona …” Karim alinyanyuliwa mkebe mkebe. Alimuomba Sultan aachiwe kwani amesilimu. Walinzi wakamuacha akaketi chini. Alimtazama kijakazi wake mmoja na kumpatia ishara, kijakazi akasimama na kwenda nje. Wakati akimngojea arejee, alitazamana na mke mkubwa wa Sultan, ndugu yake. Hawakusema jambo.

Kijakazi alirejea akiwa amebebelea mkoba wa ngozi, akampatia Karim. Karim alitazama ndani ya mkoba huo kabla hajaanza kutoa kitu kimoja baada ya kimoja. Mayai matatu makubwa yenye rangi nyeupe ya kufifia, manyoya kadhaa, vibuyu viwili virefu rangi nyeusi pamoja na kioo saizi ya kati.

Alipotoa hayo aliingiza tena mkono wake ndani ya mkoba ila mara hii hakutoka na kitu. “Ni hivi hapa Sultan,” alisema Karim akikabidhi mkoba, juuye ukiwa umebebelea vitu vile alivyovitoa. Sultan alivipokea na kuomba kusaidiwa namna ya kumwamuru na kumuongoza ndege tumishi, Karim akafanya hilo zoezi.
Lakini kuna kitu bado alikuwa nacho mkononi, amekificha katika namna ya kutoonekana. Aliuweka mkono wake huo nyuma nyuma, akarudi kuketi wakati Sultan akiendelea kufaidi maono yake kupitia macho ya bundi. Alipomtazama mke mkubwa wa Sultan alimuona anamtazama. Na macho yake ni dhahiri shayiri yalikuwa naye kwa muda mrefu. Akapata shaka.

Kwa muda wote alitulia. Sultan alipomaliza kutazama kioo, akiwa amefurahi, akampongeza sana Karim kwa kazi yake na kumtaka akae zaidi hekaluni kwani amemtendea mema.

“Nashukuru sana, Sultan,” alisema Karim. “Nimefurahishwa pia lakini nasikitika kusema sitaweza kukaa hapa zaidi ya kesho, kule nyumbani kuna kazi lukuki za kufanya.”

“Kwani huna vijakazi wa kutosha?” aliuliza Sultan. “Sema kama hawakidhi nikuongezee."
“Hapana, wanatosha,” akadakia Karim. “Kuna baadhi ya kazi hakuna mtu anaweza fanya isipokuwa mimi binafsi.”

Walipiga domo hapo kwa muda wa lisaa, Sultan akaaga anaenda kupumzika yeye pamoja na mkewe. Karim na vijakaziwe waliachwa hapo sebuleni, lakini vijakazi wakijaa tayari kuwahudumia.

Baadaye majira ya jioni, Karim alikuwa ameketi peke yake kwenye uwanja wa hekalu. Alikuwa anawaza juu ya mambo kadhaa. Baada ya muda aliupeleka mkono wake ndani ya mfuko wa kanzu aliyoivaa, akatoa kidude fulani mithili ya kijiti kidogo cheusi kifupi chenye michoro kadhaa maridadi.

Alikitazama kidude hicho akatabasamu. “Nilikuona,” sauti ya kike iliita pembeni yake, akashtuka na kuficha kitu hicho. Alitazama sauti ilipotokea, akamkuta mke mkubwa wa Sultan. Akashusha pumzi.

“Kumbe wewe!” Mke wa Sultan alitabasamu. Alikuwa yu mwenyewe. Aliketi pembeni ya Karim.

“Ni kitu gani kile ulificha?” Aliuliza. Karim alitazama kando na kando, akajibu:
“Sijaficha kitu.” Mke wa Sultan akatabasamu.

“Sawa, nitaenda kujadiliana na Sultan kama wewe hautaki.” Karim akatahamaki.

“Tafadhali usifanye hivyo, ni kitu cha siri sana.”

“Kitu gani hicho?” Karim akameza mate kwanza. “Najua wewe ni damu yangu, huwezi ukanisaliti.” Mke wa Sultan akatikisa kichwa.
.
.
.
.
.
.
.
*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***
.
.
.
.
*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***
.
.
.
.
.

Bado jua halikuwa limezama.

Rhoda, baada ya kumaliza kazi zake za kukokotoa mahesabu ya chakula, alikuwa amesimama kwenye dirisha la chumba kidogo kilichopo kwenye sakafu ya juu pa mahala pake pa kazi. akiwepo kwenye kaghorofa hako, alipata kutazama madhari kiasi ya tawala ya Goshen, lakini akili yake haikuwepo pale, macho yake yalisema.

Alikuwa anamuwaza Phares, ndio. Akili yake tokea jana inasumbuka kuchambua maneno aliyopewa na Phares kumhusu malkia Vedas. kwa namna kubwa sana anahofia aidha Phares anajua lengo na dhamira yake iliyopo kichwani juu ya malkia, ila kivipi? Na yeye je, Phares, yupo upande gani?

“Anaweza akanisaidia?” alijiuliza. “Hilo ni wazo la kijinga kabisa,” akajipinga.

“Inawezekana akawa ananichunguza. Inawezekana akawa ananivutia kwenye mdomo wa mamba.” Kichwa chake kilikosa majibu na nafsi yake ilijawa na kiu kubwa, lakini pia na uoga ndani yake. Kuna muda alijikuta anatetemeka kabisa.

Baada ya kufikiria kwa kina, aliamua jambo. Alikwapua koti lake alilokuwa amelitundika kando, akalivaa na kushuka chini. Aliaga wafanyakazi wake akaondoka. Alikwea farasi akaelekea upande ilipo kasri ya malkia. Muda mfupi tu akawa karibu na eneo hilo. Hakuingia ndani, lah! Aliangaza macho yake akamwita mlinzi mmojawapo.

Aliongea naye kwa sauti ya chini kisha akampatia kiasi fulani cha fedha, mlinzi akaondoka, ila Rhoda akabakia. Mara hii alisogea mbali kidogo na kasri, akajifichaficha.

Dakika tano mbele yake, ndani ya kasri, anatoka mlinzi mwingine mrefu mwenye mwili mpana. Kichwani amevaa kofia ngumu na uso wake umejawa na ndevu nyingi. Anatazama huku na kule, anamuona Rhoda. Taratibu anasogea.

“Nina kazi nataka kukupa,” Rhoda alisema baada tu ya kujuliana hali. Mwanaume yule mlinzi alikuwa anamtazama kwa umakini akimskiza.

“Najua hautoniangusha na nakuahidi kukupa pesa nzuri sana.” Rhoda kabla ya kuendelea, alitazama kwanza usalama. “Kuna taarifa nataka toka kwa malkia na yule bwana ‘ake. Nataka kujua vyote wanavyovifanya, kujadili na kupanga. Najua wewe huwa unaongozana nao mara kadhaa, unaweza kuifanya?”

“Ndio,” alisema mwanaume yule jabali kwa sauti yake nzito. Hakuonekana kama mtu wa kufikiria mara mbili. Rhoda alitoa kiasi fulani cha pesa akamkabidhi.

“Kadiri utakavyokuwa unaniletea habari, nitapandisha pesa.” Mwanaume yule alitabasamu pasipo kusema jambo, akaondoka kurudi kasrini. Rhoda alimsindikiza na macho yake mpaka anatokomea, kisha akakwea farasi wake na kuondoka.
Wakati anaondoka, akiwa mbali, Phares aliyekuwa kwenye ghorofa ya juu alimwona mwanamke huyo aliyekuwa anapepea juu ya farasi. Bahati nzuri hakujua ni wapi ametokea, ila alijikuta anapata shaka na haja ya kujua.
.
.

Alitazama mpaka Rhoda anaishia ndipo akafunga pazia la dirisha.
.
.
.
.
.
.
.
*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***
.
.
.
.
.*** MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN! ***
.
.
.
.
.
.

Phares alielekea sebuleni alipoketi na kukunja miguu yake kutengeza nne. Baada ya muda mfupi kijakazi akafika kumuuliza hitaji lake, akaagiza kahawa nyeusi.
.
.
Mwanaume huyu alikuwa amevaa koti la bluu lenye fito za rangi ya dhahabu mikononi. Suruali yake pia, iliyomkaa vema, ilikuwa ni ya rangi ya bluu na chini kwenye enka ilijazwa pia michirizi ya rangi ya dhahabu. Chini kabisa kulikuwa kuna kiatu cheusi cha ngozi kilichofungwa barabara! Alinawiri na ni wazi alikuwa na mtoko.
.
.
Baada ya kahawa kuletwa, alikunywa mafundo mawili tu akashindwa kuendelea. Alimkabidhi kijakazi kikombe cha kahawa akishukuru.
.
. “Tokea nimekunywa kahawa ya yule mwanamke, bado haijatoka kabisa gegoni,” alijisema akirejelea kahawa ya mgahawa wa Rhoda. .
.
Alinyanyuka upesi akajinyoosha mwili.
“Labda nahitaji kwenda tena kuionja.” Alitazama jua kwa kupitia dirishani akaliona karibia kuzama.
.
.
“Bahati mbaya muda haupo upande wangu,” alilaani kisha akasonya. Alielekea bandani kumtwaa farasi wake kisha akiongozana na walinzi watatu, akatoka ndani ya eneo la kasri kuelekea mpakani.
.
.
Alimwacha malkia Vedas akiwa amelala hoi bin taaban baada ya kupeana raha za kitandani. Hakumuaga, ingawa alijua wazi hilo jambo litakuja kuzua ugomvi hapo mbeleni, hakujali. Kuna mambo aliona hayana haja kumshirikisha ya malkia. Kuna mambo aliamini anaweza kuyakabili yeye mwenyewe pasipo kusumbuka na mwanamke huyo.

Baada ya mwendo wa robo saa, sasa giza likiwa limeingia, Phares alifika kwenye kambi ya wanajeshi iliyowekwa mpakani kwa ajili ya kujilinda dhidi ya uvamizi wa jeshi la Jayit.
.
.
Alipokelewa na kupelekwa moja kwa moja kwenye hema la viongozi wakuu. Huko aliketi akamiminiwa mvinyo kwenye bilauri. Taratibu akawa anakunywa huku wakibadilishana maneno. .
.
“Taarifa yenu ilinishtua. Ni nini haswa kinachoendelea?” aliuliza Phares.
.
.
“Ni mambo ya kutisha,” akajibu mkuu wa jeshi. “Tulishindwa kuvumilia ndio maana tukaamua kumshirikisha malkia. Mbona hujaja naye?”
.
.
“Amechoka, anahitaji kupumzika,” alijibu Phares. “Nipo hapa kwa ajili ya kumuwakilisha. Mnaweza kunambia yaliyotokea?”
.
.
“Nadhani ingekuwa bora ukajionea mwenyewe,” alisema mkuu wa jeshi kisha akasimama akimtaka Phares aongoze safari kwenda nje.
.
.
Wakiongozana na walinzi watano, mkuu wa jeshi, makamu wake na Phares waliongozana mpaka mbele kidogo ya mpaka wao, wakasimama hapo. Japokuwa ilikuwa ni usiku, mwanga hafifu uliokuwepo ulitosha kuonyesha nyayo lukuki za watu juu ya ardhi. .
.
“Hatujajua watu hawa ni wakina nani na walikuja hapa muda gani. Muda wote tumekuwa lindo, hatukuona watu wa aina yeyote!” Mkuu wa jeshi aliweka kituo akamtazama Phares. Uso wa mkuu huyo ulikuwa una hofu. .
.
“Jana wakati wa usiku, kuna baadhi ya wanajeshi walidai wamewaona vivuli vya watu vikikatiza. Mbaya zaidi ni kwamba mpaka sasa kuna wanajeshi takribani nane ambao haijulikani wapi walipo. Mara yao ya mwisho walikuwa lindo kandokando na mpaka. Tumetafuta kote pasipo kufanikiwa. Kitu pekee tulichokiona ni kile …”

Mkuu wa jeshi alinyooshea kidole upande wake wa kulia. Mwanga wa viginga vya moto ulipomulika huko, yakaonekana masalia ya damu. Phares alisogea eneo hilo akatazama vema. .
.
“Hatujajua ni damu ya nani,” alisema mkuu wa jeshi. “Ila tunadhani inaweza kuwa ya wanajeshi wetu, na wameuawa na hawa wenye hizi nyayo.” .
.
Baada ya maelezo hayo, walirejea ndani ya mpaka mpaka hemani. Waliketi wakajaziwa mvinyo kwenye bilauri.
.
. “Inabidi hatua zichukuliwe haraka. Leo usiku wa manane tunaweza kuvamiwa,” alisema Phares kwa kujiamini, makamu mkuu wa jeshi akapaliwa. Alikohoa mara tatu kabla hali haijawa shwari.
.
.
Phares alikunywa fundo moja la mvinyo. Kichwa chake kilikuwa kazini kusaka mawazo na namna ya kufanya, ila kabla hajatia tena neno, kelele kali ya yowe ilisikika nje, wakashtuka. Mara sauti ikaita mlangoni mwa hema.
.
. “Mkuu, kuna kitu unapaswa kuona!” Haraka mkuu wa jeshi, makamu wake na Phares wakatoka ndani. Nje walimkuta mwanajeshi mmoja akihangaika huku akishikiliwa na wenzake wawili. Mwanajeshi huyo aliyekuwa ameshikiliwa alisema kwa papara:
.
.
“Sijachanganyikiwa! Ni kweli nimeona, mkuu!”
.
.
“Umeona nini?” Phares aliwahi kuuliza.
.
.
“Nimemuona Malkia!” akajibu mwanajeshi yule.
.
. “Nimemuona Malkia Sandarus! Kwa macho yangu nimemwona akitembea!”
.
. “Amerukwa na akili!” mkuu wa jeshi alisema kwa mapuuzo, ila Phares hakuchukulia jambo hili masikhara. Aliamrisha mwanajeshi huyo aachiwe huru kisha akamuuliza:
.
.
“Umemuona wapi?”
.
.
“Kule!” mwanajeshi akanyooshea kidole upande wake wa mashariki.
.
.
“Unaweza ukanipeleka?”
.
.
“Ndio!”
.
.
.
.
.
.
~ Ina mana Mwili wa Malkia uendeshwao na ramli za bibi wa Tanashe umeshawasili Goshen?? ~ .
.
Nini Karim amemficha Sultan?? Sultan atagundua?? .
.
~ Goshen imejiandaa kuwapokea "wageni wao wa usiku" toka kwa Jayit wakiwa chini ya jenerali mpya bwana Rayden??
.
. ~ Nini hatma ya Zura aliye ulimwengu wa chini?? .
.
~ Rhoda na Phares, nani atamzidi mwenziwe kete??
.
.

LAKO JICHO!
 
MKUFU WA MALKIA WA GOSHEN -- 016
Simulizi za series


Haraka Phares akiongozana mbele kabisa na mwanaume yule mshahidi, walielekea kule kuliponasibiwa kuonekana kwa Malkia. Hii ilikuwa ajabu na kila mtu alitaka ashuhudie muujiza huu, hivyo wengi wakaenda.
.
.
Walifika huko wakahaha. Walizivunja shingo zao kwa kutafuta, walizungusha macho yao kwa kusaka, patupu! Hakukuwepo yeyote.
.
.
“Una uhakika ni hapa?” Phares alimuuliza mshahidi.
.
.
Wengine walikuwa tayari wameanza kupuuza, na hata kujutia juhudi zao kwenda eneo lile.
.
.
“Ndiyo ni hapa!” Alisisitiza mshahidi. “Nilikuja kukojoa nikamwona.”
.
.
Mkuu wa jeshi alisonya. Aliamuru mshahidi atiwe pingu na kufungiwa ndani kabla hajaleta madhara mengine, amri ikatimizwa. Watu waliondoka toka eneo hilo la tukio akiachwa Phares pekee.
.
.
Mwanaume huyo aliendelea kutazama huku na kule, bado hakuamini kama mwanaume yule ni mwehu kwa kuona tukio alilolisema. Alijongea huku na kule akiangaza. Mara akaona nyayo za mtu kwenye mchanga mzito wa tope. Alizitazama vema nyayo hizo akagundua ni za mguu wa kike.
.
.
Alipata maswali juu ya nyayo hizo, ila muda wa kutafuta majibu hakuwa nao, akaondoka kurejea kule hemani kwa ajili ya kuandaa mipango kabambe ya kujilinda. Hili swala aliliweka kama kiporo.
.
.
Hemani mipangoni, kwanza, akaagiza watu wote wanaoishi karibu na mpaka wakae ndani kwa muda wote huo wa usiku, asionekane yeyote akiwa anazurura. Vilabu vyote vya pombe vifungwe mapema, na atakayekaidi ataadhibiwa vikali. Agizo likatekelezwa ndani ya muda mfupi tu.

Baada ya hapo mitaro mirefu ilichimbwa kwa awamu mbili, ya kwanza karibia na mpaka, ikikaribiana kabisa na mashimo ya awali, ya pili ikiwa hatua kadhaa mbele. Jeshi lilijigawa makundi tatu katika idadi ifuatayo:
.
.
la kwanza lililokaribu na mpaka lilikuwa na wanajeshi wengi, la pili lililotenganisha na la kwanza kwa mfereji mrefu, lilikuwa na wachache ukilinganisha na la kwanza, la tatu pia vile vile likifuata mtindo huo wa kupunguza idadi.
.
.
Mbali na hapo, wanajeshi watatu walikuwa mbele ya mpaka. Hawa walikuwa mahususi kwa ajili ya kutambua hatari upesi na kutoa taarifa. Njia hii ilionekana yenye ufanisi zaidi ukilinganisha na mtu mmoja kukaa mtini kutazama, japokuwa ilikuwa ndiyo yenye hatari zaidi.
.
.
Kwenye mifereji mirefu iliyochimbwa, ilisakafiwa na majani makavu. Majani haya yakaloweshwa na mafuta ya taa. Yaliwekwa juu katika mfumo wa kwamba, kama wewe ni mgeni basi hauwezi ukatambua hilo.
.
.
Mipango yote hiyo ilifanyika ndani ya dakika kumi tu! Phares aliasisi na kusimamia kila jambo. Wanajeshi wakaelimishwa namna ya kujipanga na kupambana. Baada ya hapo kukawa kimya kila mtu akiketi mahala pake alipotakiwa kuwepo kwa mujibu wa mpango, kisha kukawa kimya cha kifo.
.
.
Ndani ya nyumba ndogo ambayo haipo mbali sana na mpaka, takribani kama nusu maili, mwanaume aliyekuwa amevalia shati chakavu lenye kifungo kimoja, suruali kuukuu inayoishia kwenye enka ya miguu, alikuwapo sebuleni akinywa pombe iliyotunzwa ndani ya chupa ya hovyo.

Nywele zake zilikuwa vurugu. Aliketi kwenye kiti kana kwamba mgonjwa mahututi asubiriaye kumuona tabibu kwa hali zote. Ila kwa namna alivyokuwa anapeleka chupa mdomoni na kugida, ndipo ingekuacha mdomo wazi kwa kujiuliza anatolea wapi nguvu hiyo?
.
.
Mwanaume huyo, asiyeeleweka ni aliyekula chumvi nyingi au lah, alinyanyuka toka kochini baada ya kuhakikisha amemaliza kinywaji chote kilichomo ndani ya chupa. Alipindua mdomo wa chupa akaungalizia chini, hakukuwa na kitu. Alilaani. Alijivuta kuelekea jikoni, akiwa njiani macho yake yakamtaarifu kuna mtu amekatiza dirishani.
.
.
Nani! Alishtuka na moyo wake. Taarifa ilitolewa muda si mrefu kwamba haitakiwi yeyote kuwapo nje ya nyumba kwa usiku mzima, sasa huyo aliyekatiza ni nani? Ni adui? Au ni mwananchi ambaye hana habari?
.
.
Haraka mwanaume huyo, mlevi, alikimbilia upande wa pili wa nyumba yake, dirishani akatupa macho njiani. Mara akamuona yule aliyekuwa anakatiza. Alikuwa ni mwanamke ndani ya nguo kuukuu. Hakumtambua mwanamke huyo ni nani, lakini alitamani kumfahamu. Akili yake ya kilevi ilimtuma apaze sauti kuita, akafanya hivyo.
.
.
Sauti ya mwanamke iliyotoka jikoni, inaweza kuwa ya mkewe, ikamkaripia mlevi huyo dhidi ya kupiga kelele. Asikome mwanaume huyo akaendelea kuita. Mara mwanamke akageuka. Hakuwa mbali sana na nyumba lakini mwanga wa muda huo ulikuwa hafifu kuonekana vema.
.
.
“Hairuhusiwi kuzurura nje we mwanamke! Nenda kwako upesi!”
.
.
Mwanamke huyo alisimama, kama mwanasesere, akamtazama mlevi huyo pasipo kusema jambo. Mlevi alitwaa ginga la moto lililokuwa linaning’inia ukutani mwake, akaonyeshea kule alipo mwanamke yule. Hapo ndo akamwona.

Malkia Sandarus!
.
.
Haraka mlevi alikimbilia jikoni kumwambia mke wake alichokiona. Ni kama vile pombe iliyeyuka kichwani. Macho yalikuwa yamemtoka, uso ukibebelea kitendawili. Mke wake alimpuuza, hakumwamini. Mlevi aliendelea kumsumbua mkewe mpaka pale alipokubali kwenda naye kutazama. Mke alirusha macho nje ya dirisha, hakumuona mtu. Alisonya akalaani akiondoka kwenda jikoni.
.
.
Mlevi alibaki akitazama pale dirishani kama vile mtu asiyeamini. Alifikicha macho yake, akatikisa kichwa. Alitazama na kutazama, hakuona mtu. Mwishowe aliamua kurudi kwenye kiti chake.
.
.
“Naomba chupa nyingineee!” alipiga kelele.
.
.
“Hiyo uliyokunywa inakupa mawenge, unataka nyingine!” mkewe akafoka. “Embu nenda kalale huko!”
.
.
“Nimemuona kweli! Naapa!”
.
.
“Kalalee!” Mke alifoka tena.
.
.
Katika kambi ya jeshi huko mpakani, kilikuwa ni kimya kirefu sasa baada ya kila kitu kusukwa na kupangwa vema. Mpaka muda huo walikuwa tayari wamedumu kwenye ulimwengu wa ububu kwa takribani robo saa na huku hakuna lolote lililotukia. Ukimya huo ukahamisha mawazo ya Phares.
.
.
Aliwaza kumhusu Vedas huko kasrini. Nafsi yake ilimsuta kwanini hakumuaga mwanamke huyo. Lakini kilichomshangaza na kumpa maswali zaidi, ni kwanini mwanamke huyo hajaja kumuulizia mpaka muda huo?
.
.
Ameshindwa hata kutuma watu kuja kumtazama kama yupo hapo kambini? Au amechoka ukaidi wake ameamua amwache? Hakupata jibu.
.
.
Alichojua ni kwamba amekosea, na aliona sehemu pekee ya kurekebisha makosa yake ni kushinda vita. Atarudi nyumbani akiwa na tabasamu pana, atapanua mikono yake amkumbatie malkia.

Alidumu fikirani kwa ziada ya dakika kumi, mambo yakaanza kuwika. Sauti kali ya filimbi iliita kuwashtua. Filimbi hiyo ilikuwa ni kiashiria cha ujio wa adui. Haraka kila mtu alipasha mwili wake moto tayari kwa ajili ya pambano.
.
.
“Wanakujaa!” Sauti ilisikika kwanguvu. “Hawaonekanii!” Taarifa nyingine ikaja upesi. Vishindo vya watu lukuki wanaokuja vilisumbua masikio ya kila mmoja, lakini hakuna aliyefanikiwa kuona wageni hao. “Shikilia mpangooo!” alipaza Phares. Mstari wa kwanza wa wanajeshi ukakaa tenge kwa ajili ya kuwakabili maadui.
.

Jeshi la Jayit, lililokuwa linaonekana kwa uhafifu, lilikuja kwa kasi mno, vishindo vyao vilieleza. Wakiwa hawana hili wala lile, lukuki waliparamia na kuzama ndani ya mfereji mrefu wa kwanza. Haraka moto ulitupiwa humo, kufumba na kufumbua likatokea tanuru kubwa! Viumbe wote waliozamia humo waliteketezwa kama makaratasi wakipiga yowe kali.
.
.

Kwa wanajeshi kadhaa, wa Jayit, waliofanikiwa kuvuka mfereji huo wa kwanza nao hawakufika mbali wakadhibitiwa kwa urahisi. Moto uliokuwa unawaka kwa pupa nyuma yao ulitoa mwanga mkali ambao uliwaonyesha vizuri wanajeshi hao mbele ya macho ya wanajeshi wa Goshen, waliotumia wingi na silaha zao kuwamaliza.
.
.
Baada ya kumalizika kwa zoezi hilo, kundi lote la kwanza la wanajeshi wa Goshen likalala chini ghafla. Wanajeshi wote wa Jayit waliovuka mfereji wa kwanza, pasipo matarajio, wakaanza kupokea mvua ya mishale ya moto. Hata wale ambao walikuwa bado hawajavuka, nao waliteketezwa kwa mishale hiyo iliyoshushwa kwa fujo.
Wakati mapambano yakiendelea, kundi la pili liliungana na la kwanza kuwaongezea nguvu, mfereji wa pili ukawashwa moto. Sasa mapambano yakawa yanatukia katikati ya mifereji miwili yenye kuwaka moto, na huku kundi moja tu la jeshi la Goshen, lile la tatu, likiwa ndio limebaki pasipo kuguswa. Kundi hilo kazi yao ilikuwa ni kuwadungua wanajeshi wa Jayit kwa ncha za mishale.
.
.
Kutokana na kuwekwa katikati ya moto, wanajeshi wa Jayit walishindwa kurudi walipotokea, wala kuingia ndani ya Goshen. Kushambuliwa kwa kushtukizwa kuliwapukutisha wapambanaji wao wengi, na hali ya kuwekwa hadharani na mwanga wa moto, kulirahisisha kazi kwa wana Goshen, ikawa kama wanapambana na wanadamu wenzao.
.
.
Vita ilidumu kwa muda wa dakika arobaini na tano tu, ushindi mnono ukaenda kwa Goshen. Ni wapambanji wanne tu wa Jayit ndio waliobaki hai wakikimbia kuokoa nafsi zao, ikiwemo kamanda wao mkuu mpya, bwana Raiden. Salama ya wanaume hao ilikuwa ni kutoingia kwenye uwanja wa vita, wao walibakia kando wakitazama.
.
.
“Waacheni wakaupeleke ujumbe,” alisema Phares akiwakataza wanajeshi kuwafukuzia maadui hao. Walifurahia ushindi, Phares akiteka nyoyo za wapambanaji kwa michoro na mipango yake thabiti iliyozaa matunda. Walimnanyua kama mtoto wakamrusha juu juu kama kitenesi.
.
.
Hakukaa tena hapo, Phares akaaga anataka kurudi kasrini baada ya kazi yake kuisha. Akisindikizwa na wanaume watatu wenye silaha, akaondoka zake akitumia farasi wenye nguvu waliokuwa wanakimbia kama upepo.
Hakudumu sana njiani akawasili kasrini. Alikuwa na tabasamu pana usoni, na pia mwenye nguvu na hamu ya kueleza yale aliyotoka kukumbana nayo alikotoka, haswa ushindi. Haraka alishuka toka kwenye mgongo wa farasi akakimbilia ndani. Lakini kuna kitu hakikuwa sawa, na pengine furaha yake aliyokuwa nayo ilimfanya asichambue mazingira vema.
.
.
Mbele ya uzio mkubwa wa kasri walikuwapo walinzi kama kawaida, wakisimama kwa ukakamavu huku wakishikilia silaha zao, hata ndani ya uzio vilevile hali ilikuwa vivyo hivyo, wanaume waliobebelea silaha wakisimama kwa ukakamavu. Lakini baada ya kupita ngazi ya kwanza kwenda chumba cha juu cha malkia, hakuonekana tena mlinzi yeyote. Hii haikuwa kawaida.
.
.
Phares alinyoosha miguu yake mpaka mlangoni mwa chumba cha malkia alipoubetua kitasa na kuzama ndani. Alikaribishwa na vitu vilivyokuwa shaghalabaghala, mathalani meza ilivyovunjika na bilauri kadhaa za maua zikiwa chini. Hapo ndipo moyo wake ukalipuka kwa hofu, bup!
.
.
Haraka alikimbia akarusha macho yake kitandani, huko akauona mwili wa malkia Vedas ukiwa umelala, na vitu zaidi vilivyovunjika na kuwa hovyo. Aliuendea mwili wa malkia akiita, lakini hakukuwa na jibu. Alisogea karibu zaidi, sasa kwa hofu, akagundua jambo chungu alilogoma kuamini kwa hapo awali. Malkia alikuwa amekufa!
.
.
Majeraha kadhaa yalikuwa usoni mwa marehemu; pua na mdomo wake vilikuwa vinachuruza damu, nywele zake zilikuwa hovyo na gauni lake alilolivaa lilikuwa limechanwa kifuani. Lakini zaidi ya yote, hakuwa na mkufu!
Phares aliushika mwili wa Vedas, akagundua bado ni wa moto. Hii ilimaanisha ameuawa muda si mrefu. Haraka alitoka ndani ya chumba akawaita walinzi na kuwapasha habari. Alikuja kugundua walinzi wa karibu wa malkia walikuwa wamejeruhiwa vibaya, na hata wengine kufa, na kufungiwa ndani ya stoo.
.
.
Haraka alitoa agizo la mipaka yote kufungwa, doria na msako kufanyika mpaka muuaji apatikane.
.
.
Wamkamate mtu yeyote yule watakayemuhisi, yeyote yule atakayekuwa anafanana na Malkia Sandarus!
.
.
.
.
.
.
.
.
***
.
.
.
.
.
.
.
Ni furaha iliyoje kwa vikongwe wa Tanashe! Macho yao sasa yalikuwa yanaona kitu walichokuwa wanakitafuta kwa muda mrefu, na si kingine hiko bali ni mkufu.
.
.
Kwa kupitia kioo chao cha kilozi, waliona vyote vilivyojiri. Furaha yao ilikuwa kubwa zaidi kwasababu sasa walikuwa wamelipiza kisasi kwa mwanamke aliyewafanyia mchezo mchafu wa kuwasaliti, bibie Vedas, basi vinywa vyao vyenye upungufu mkubwa wa meno vikawa wazi muda wote kwa tabasamu na macheko. Kazi pekee sasa iliyokuwa imebakia mikononi mwao, ikawa ni kuuingiza mwili wa Malkia ndani ya himaya ya wachawi, Tanashe.
.
.
Kazi hii haikuwa nyepesi kama mtu anavyoweza kudhani. Tamu ni kwamba vikongwe hawa wa Tanashe walitambua hilo jambo na hawakutaka kumwaga supu ingali wamebakiza fundo moja.
.
.
Ramli zao zilisogeza miguu na mikono ya Malkia upesi. Hawakutaka kuharibu umakini wao kwa fanikio la fataki. Malkia akiwa amebakiza kama nusu kilomita kuingia ndani ya Tanashe, ghafla anakutana na wanajeshi watatu, wanamuamuru asimame papo hapo.
Wanajeshi hawa walikuwa juu ya migongo ya farasi wakiwa wameshikilia viginga vya moto. Kwenye mapaja yao walikuwa wamebebelea mifuko ya jambia ndefu. Macho yao yaliyokuwa na shaka yalimtazama mwanamke waliyemsimamisha, ambaye alikuwa ameinamisha chini uso wake.
.
.
“Wewe nani na unaelekea wapi?” aliuliza mwanajeshi mmoja kwa sauti ya ukali. Kimya, hakukuwa na majibu.
.
.

Wanajeshi wakachomoa jambia zao. “Wewe!” alifoka mwanajeshi mwingine akipiga bega la mwili wa Malkia kwa bapa la jambia.
.
.
“Hujasikia ulichoulizwa? – wewe nani, unatoka wapi na unaelekea wapi?” Hakukuwa na majibu.
.
.
Wanajeshi walitazamana kwa nyuso za mashaka. Mmoja alijivika ujasiri akashuka chini, akatumia ncha ya jambia lake kunyanyua uso wa mwanamke waliyemsimamisha. Uso uliposimama, wakamuona Malkia Sandarus. Ajabu! Ndio, hawakuwa wanafananisha.
.
.
Kabla wanajeshi wale hawajatoka kwenye taharuki, mwanaume aliyekuwa karibu alinyanyuliwa mithili ya mtoto. Alirushwa kwanguvu kuwakumba wenzake aliowadondosha chini kama matofali. Kabla wanaume hao hawajajikusanya, tayari mwili wa Malkia ulikuwa umetwaa jambia la mmojawao, na katika kasi ya ajabu, ukawamaliza wanajeshi wale kana kwamba wadudu.
.
.
Farasi mmoja alichukuliwa, mwili wa Malkia ukajiweka juuye na kisha kuondoka kwa kasi kumalizia safari ya Tanashe. Farasi aliachwa mpakani, Malkia akazama ndani ya himaya.
.
.
Alitembea kwa muda mdogo tu kabla ya kukomea mbele ya mlango wa nyumba ya vikongwe. Alipokelewa kwa shangwe kubwa, na baada tu ya mkufu kutwaliwa na vikongwe wale, alipoteza nguvu na kuanguka chini kama mzigo, vikongwe wakambebelea na kumuingiza ndani.

“Hana kazi tena, tumuue!” alisema kikongwe mmoja. Ilikuwa ni vigumu kuwatofautisha maana kila mmoja alikuwa na jicho moja, wakivalia mashuka meusi.
.
.
“Hapana!” akawaka mwingine. “Usiwe mpumbavu asiye na akili. Unajua kabisa mkufu huu huendana na damu ya huyu kiumbe. Tukimmaliza ni vipi tutapata utawala wa mkufu?” Kweli.
.
.
Damu ya Malkia ilikuwa inahitajika, ama basi kiungo chake kwa ajili ya kukamilisha ibada. Ila vikongwe hawa hawakuona haja ya kuharakisha hivyo. Walitoka kufanya kazi kubwa kwa muda wote huo na wakaona haja ya wao kupumzika kisha kumalizia zoezi lao kesho yake usiku. Waliona linapendeza hili, wakakubaliana.
.
.
Muda ukiwa unaendelea kuyoyoma, huko mbali ya jengo kubwa la kuogofya la vikongwe hawa, anakatiza fisi mkubwa. Fisi huyu alikuwa anaperuzi na kuzurura huku na kule. Lakini ghafla, akiwa kazini, anakutana na nyayo juu ya ardhi. Ananusa nyayo hizo, anasikia ladha ya binadamu. Anafuatilia nyayo hizo taratibu, zinamuelekeza mpaka kwenye jengo la walozi vikongwe.
.
.
Fisi huyo alisimama, umbali wa kama hatua thelathini, akarusha macho yake kutazama jengo la vikongwe. Alitazama hapo kwa muda pasipo kuona kitu, ila kabla hajaondoka, anapata fursa ya kuuona mwili wa Malkia kwa kupitia dirishani. Si kwamba alikuwa amesogea karibu, la hasha! Aliliona hilo wakati vikongwe wakiupeleka mwili huo chumbani.
.
.
Fisi alijikuta akibweka kidogo kwa bumbuwazi, kisha haraka akaondoka toka eneo hilo kwa mbio kali.
.
.
.
.
.
.
.
.
FISI HUYU NI NANI, NA ANAELEKEA WAPI? JE NI WA BWANA FAKI? - BWANA MWENYE JESHI LA FISI NDANI YA TANASHE? UNAMKUMBUKA FAKI?
.
.
.
NI NINI PHARES ATAFANYA BAADA YA KIFO CHA VEDAS? NI NINI RHODA NAYE ATAFANYA? HIMAYA YA GOSHEN ITAKUWAJE BAADA YA MKUFU KUKWAPULIWA?
.
.
.
.
.
MKUFU UKIWAPO TANASHE, KUNA SHIDA YEYOTE ITAJIRI? NA JE MKAIDI JAYIT ATAKUBALI KUSHINDWA NA GOSHEN?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom