MISS TANZANIA
SEHEMU YA 22
MTUNZI : PATRICK.CK
CONTACT: 0764294499
ILIPOISHIA SEHEMU ILIYOPITA
“Kwa penzi zito nililonalo kwako ambalo haliwezi kulinganishwa na kitu chochote,kwa kuwa wewe ndiye mwanaume pekee niliyekukabidhi moyo wangu uutunze hadi mwisho wa maisha yangu,ninakuahidi kwamba sintarudi nyuma.Niko tayari kukabiliana na lolote lile ambalo linaweza kuwa kikwazo cha sisi kutimiza ndoto yetu ya kuwa pamoja.”
Happy akasema huku macho yake yakilengwa na machozi
“Nimekuelewa mpenzi wangu.naomba sasa ulale tutaonana kesho.Nitakupigia simu kesho asubuhi na mapema kukupa busu la asubuhi” Patrick akasema
“nashukuru sana malaika wangu .Sasa ninaweza kulala baada ya kuisikia sauti yako.Ah kabla sijasahu naomba uniimbie ule wimbo uliopenda kuniimbia kila siku kule Arusha” Happy akasema
“Wimbo upi? Patrick akauliza
“Ule wa Diamond Platinum..Lala salama”
Patrick akacheka na kuanza kumuimbia Happy wimbo ule mzuri luiomfanya Happy ahisi kama vile yuko na Patrick karibu yake..
ENDELEA………………
Mlio wa simu ulimstua Patrick toka usingizini.Kitu cha kwanza alichokiangalia ni saa yake ya ukutani ambayo ilimuonyesha kwamba ilipata saa tisa na dakika nane za usiku.Akafikicha macho na kunyoosha mkono akaichukua simu yake iliyokuwa juu ya droo ya kitanda akatazama ni nani aliyempigia simu usiku ule mkubwa .Ilikuwa ni namba ya simu ya Vero.Patrick akakunja uso
“tayari ameshafika.Sijui anataka kuniambia kitu gani.Ngoja nipokee nimsikilize”
“Hallo “ akaita Patrick baada ya kubonyeza sehemu ya kupokelea
“Hallo my love.Unaendeleaje? Vero akauliza
“Naendelea vizuri Vero.Umeshatua?
“Nimeshatua niko kitandani hapa” akasema Vero kwa sauti laini
“Pole na safari” akasema Patrick
“Nimekwishapoa mpenzi wangu.Pole sana kwa kutojisikia vizuri.Nilitegemea kukuona uwanja wa ndege lakini nikamkuta Andrew na Vick peke yao nikaambiwa kwamba umeshindwa kufika kunipokea kwa sababu hukuwa unajisikia vizuri.Vipi maendeleo yako kwa sasa? Vero akauliza
“Naendelea vizuri Vero.” Patrick akajibu.
“nashukuru kama unaendelea vizuri.safari yangu ilikuwa nzuri.Dada na shemeji wanakupa salamu nyingi na wanakutakia uponaji wa haraka.Wameahidi watakuwepo siku ya harusi yetu.”
“Ahsante sana” Patick akajibu kwa ufupi
“Darling are you ok? Vero akauliza
“I’m ok Vero.Kwani vipi? Patrick akajibu
“Ninaona sauti yako haiko kawaida.Naona kama bado hauko sawa.Nini kinakusumbua mpenzi wangu? Nilitaka nije moja kwa moja kwako ili niwe nawe usiku huu lakini Andrew akanikataza akaniambia nikuache upumzike.Baby najisikia vibaya sana kuwa mbali nawe hasa katika kipindi hiki ambacho haujisikii vyema” akasema Vero
Patrick akavuta pumzi akafikir kidogo na kusema
“Usjali Vero.Mimi ninaendelea vizuri .Usihofu kitu”
“najua unaniambia hivyo ili kunitoa wasi wasi .Ngoja nikuache ulale upumzike.Nilitaka kukufahamisha kwamba tayari nimesharudi .Nitakuja kukuona kesho asubuhi kabla sijafanya kitu chochote kile.Sintakuwa na amani ya moyo bila kukuona.Niliondoka bila kukuona na siku zote nimekuwa roho juu juu nikikuwaza wewe mpenzi wangu.Patrick nakupenda sana na sintaweza kuishi bila kuwa nawe.Usiku mwema mpenzi.I love you”Vero akasema
“Bye baby” akajibu Patrick na kuitupa simu pembeni.
“Laiti angejua ninavyomchukia asingethubutu hata kunipigia simu.Angeniogopa kama ziraeli.” Akawaza Patrick wakati akijifunika vizuri
“vero ni mwanamke mzuri,ana roho nzuri ya ukarimu, ni mrembo,msomi na ana kila sifa ya kuwa mke.Sikutegemea kama kuna siku itanitokea nikamchukia kama ilivyonitokea sasa.Kitendo cha kunitenganisha na mtu niliyeyatoa maisha yangu kwake kimeniuma sana.Maumivu niliyoyapata wakati ule sitaki kuyakumbuka.Niliumia sana.Niliteseka kupita kiasi kwa kuamini kwamba ni kweli Happy amenisaliti.Ilinichukua muda mrefu maumivu yale kunitoka moyoni mwangu .Happy naye aliteseka kiasi kikubwa sana baada ya kusikia kwamba mtu pekee ambaye alikuwa akimpenda amefariki dunia.Mateso na maumivu aliyotusababishia Vero ni makubwa sana na kwa hili sidhani kama nitamsamehe.Dunia nzima haitanielewa ni kwa nini nimechukua maamuzi haya lakini sintajali mtu yeyote.Maamuzi niliyoyachukua hakuna mtu anayeweza kuyabadili.Lazima niachane na Vero na kuendelea na mtu ninayempenda maishani.Happy ndiye mwaname pekee mabaye nimepangiwa niwe naye katika maisha yangu na si huyu mlaghai Vero.” Patrick akawaza akiwa amejilaza pale kitandani.Akasikia hasira nyingi akaamka na kwenda kuchukua glasi ya maji akanywa na kurudi tena kitandani.
*********************
Kengele ya mlangoni ndiyo iliyomstua Patrick toka usingizini.Akaangalia saa ya ukutani ilioyesha ni saa tatu za asubuhi.Akajinyoosha na kwa uchovu akatoka mle chumbani na kuelekea mlangoni.Akafungua mlango mdogo wa geti na kukutana na sura yenye tabasamu pana sana ya Vero ambaye alimrukia na kumpa mabusu mengi
“Ouh my love nimefurahi sana kukuona tena mpenzi wangu” akasema Vero kwa furaha huku akimkumbatia Patrick kwa nguvu.
“karibu sana Vero” Patrick akasema .Akalifungua geti na Vero akaingiza gari lake. Na kisha akatoa begi kubwa na kulivuta kuelekea ndani.
“Darling hizi zote ni zawadi nilizokuletea toka uingereza.” Akasema Vero na kumfanya Patrick atabasamu
“nashukuru sana Vero” Patrick akajibu na kwenda kukaa pembeni ya Vero.Wakatazamana kwa sekunde kadhaa.
“Unajisikiaje leo mpenzi wangu? Vero akauliza akiwa ameiweka mikono yake shingoni kwa Patrick
“Najisikia vizuri sana leo.Unajua wewe ndiye dawa yangu.Umekuja na nimepona kabisa” akasema Patrick na kumfanya vero atabasamu na kumkumbatia kwa nguvu.
“Nimekwambia hivyo kukupa moyo tu lakini siku ya leo haitaisha kabla hujalia machozi ya damu” akawaza Patrick.
Wakiwa bado wamekumbatiana ,simu ya Patrick ikaita.Akaichukua na kutazama mpigaji.Alikuwa ni mama yake.
“mama shikamoo”
“marahaba mwanangu hujambo?
“sijambo mama”
“Unaendeleaje? ” akauliza mama Patrick kwa sauti ya upole isivyo kawaida yake.
“mama ninaendelea vizuri sana”
“sasa mwanangu mbona jana hukwenda kumpokea mwenzio? Kwa nini unamfanyia hivyo mwenzako?
“mama nilishindwa kwenda kule uwanjani kwa sababu sikuwa najisikia vyema na ndiyo maana nikamuomba Andrew aende akampokee Vero badala yangu”
“yaani kwenda kumpokea mwenzako hapo uwanjani hujisikii vizuri .mbona kwenye dharura zako husemei kwamba hujisikii vizuri? Mama Patrick akauliza huku sauti ikianza kubadilika na kuwa ile ya ukali iliyozoeleka.
“mama si kwamba nilifanya makusudi kutokwenda kumpokea Vero.Nilikuwa naumwa na ndiyo maana nikamuomba Andrew aende badala yangu.” Patrick akajibu
“Sawa baba nimeshakuelwa manake ukiendelea utaanza kuzungumza vingereza vyako halafu tukashindwa kuelewana.Usichelewe leo kwenye kikao .Tayari kila mtu nimeshampa taarifa na nimewasisitiza kwamba wasikose.”
“haya mama tutaonana mida hiyo.Msalimu baba” Patrick akasema na kukata simu
Wakati Patrick akiongea na mama yake vero alikuwa ameingia bafuni.Aliposikia tayari Patrick amemaliza kuzungumza na simu akatoka mle bafuni akiwa amejifunga taulo na kumfuata Patick pale kitandani akaanza kumtoa zile nguo za kulalia ambazo bado Patrick alikuwa amezivaa.
“Ratiba ya leo itakuwa kama ifuatavyo.Kitu cha kwanza tunatakiwa tukaoge pamoja halafu tupate stafstahi halafu tutajifungia chumbani kwetu siku nzima ya leo” akasema vero akilivua shati la Patrick na kuliweka pembeni.
“Ulimtaarifu mama kwamba sikufika kukupokea uwanja wa ndege? Patrick akauliza
“Nilimpigia simu usiku kumtaarifu kwamba nimeshatua kwa sababu aliniomba nikishafika salama nimfahamishe.Aliniuliza kama ulikuwepo uwanjani nikamwambia kwamba hukuweza kufika kutokana na kutokujisikia vizuri.Samahani kama nilikosea kwa hilo” Akasema Vero huku akimshika Patrick mkono na kumuongza kuelekea bafuni.
“Patrick nilipokuwa safari nilikuwa nikiweweseka kila usiku nikilitaja jina lako mpaka watu wakashangaa umenipa kitu gani cha kunifanya nikupende kiasi kikubwa namna hii.Naomba nikiri kwamba sintaweza kuishi bila kuwa nawe.Wewe ndiye pumzi yangu,wewe ndiye maisha yangu,wewe ndiye kila kitu kwangu.Bila wewe siwezi kitu.” Akasema Vero huku akiutembeza mkono wake taratibu katika kifua cha Patrick wakiwa katika jakuzi.Patrick akamuangalia Vero kwa sekunde kadhaa akataka kusema kitu lakini Vero akamuwahi na kumuwekea kidole mdomoni.
“shhhhhhhh…..Don’t say anything” akasema vero na kutoa kidola kile na taratibu akakisogeza kichwa chake karibu na kuigusanisha midomo na kutoa busu moja zito ,halafu akatoa ulimi na kuilamba midomo ya Patrick.Wakari akifanya hivyo alikuwa akilisugua sikio la kushoto kwa mkono wake wa kulia kwa ufundi mkubwa.Sehemu hii ndiyo ambayo huwa inayaamsha mashetani ya Patrick.Kama Vero alivyokuwa amekusudia Patrick akaanza kuhema mfululizo huku akitoa mguno Fulani kwa raha aliyokuwa akiisikia.Akashindwa kuvumilia na kumvuta Vero karibu zaidi.Wakati wakiendelea kunyonyana ndimi simu ya Patrick ikaanza kuita kule chumbani.Mlango wa bafuni haukuwa umefungwa hivyo aliweza kuisikia simu yake vizuri ikiita
“Vero ngoja kwanza nikapokee simu.Anaweza akawa ni mtu muhimu ananipigia”
“No Patrick.No phone calls at this time.Its only me and you” akasema Vero huku akiendelea na mautundu juu ya mwili wa Patrick.
“Anaweza akawa ni Happy ndiye anapiga.Nisipoipokea simu yake atajiuliza maswali mengi “ akawaza Patrick.
Simu ile ikaita na kukata.Ikaita na kukata tena .Ikaanza kuita kwa mara ya tatu.Patrick akamsukuma Vero pembeni akainuka na kukimbia huku akichuruzika maji kuelekea chumbani .Kabla hajaifikia simu ikakatika.Akachuka na kutazama mpigaji alikuwa ni Happy.Akaishikilia simu ile kwa dakika nzima akijiuliza kama ampigie Happy ama la.
“Nitampigia baadae.Siwezi kumpigia wakati Vero yupo.Hii inaweza ikaharibu kila kitu.Nataka nikamalize mambo yote mbele ya wazee” akawaza Patrick na kuiweka simu yake mezani akarudi bafuni.
“Nani aliyekusumbua namna hiyo kwa kukupigia simu wakati kama huu na kuharibu starehe zetu? Akauliza Vero
“Foregt about it…Kuna jamaa mmoja nilikuwa na miadi ya kuonana naye leo jioni lakini sintaweza kuonana naye kutokana na kikao tutakachokihudhuria ”
“Kikao !! “ Vero akauliza kwa mshangao
“Ina maana hauna taarifa kwamba kikao cha mwisho kinakaa leo ? Saa tisa za alasiri itatubidi tuelekee sote katika kikaohiki.Taarifa zimekwisha sambazwa kwa kila mhusika awepo katika sherehe hii”
“Ouh basi hiyo ni habari nzuri .Hakuna shaka tutahudhuria ili tuweze kuona mpaka sasa maandalizi ya harusi yamefikia wapi.” Akaseam Vero huku akimshika mkono Patrick na kuimvutia katika jakuzi ili waendelee kuoga.
“Vero No! Siwezi kufanya hivyo tena.Sina hamu tena.Tumalizie kuoga tukapate kifungua kinywa.”
Vero akamuangalai Patrick kwa jicho kali lakini hakuwa na la kufanya.wakamaliza kuoga na kuelekea chumbani .
***************************
Mlango wa chumba cha Happy ukagongwa na kumfanya astuke toka usingizini.Akajiinua kitandani na kutembea taratibu huku akifikicha macho na kwenda kuufungua.Alikuwa ni mdogo wake Margreth.
“Wow ! Margreth “ Happy akasema huku akitabasamu
“Ouh Happy…” Magreth akaruka ruka kwa furaha na kumkumbatia dada yake.
“habari za Arusha? Yaani Happy unarudi hutaki hata kunijulisha kama umesharudi” akasema Margreth
“Samahani kwa hilo mdogo wangu.Nilirudi jana jioni na mama akanieleza kwamba umepata kazi katika kampuni ya mtandao wa simu na umeingia zamu ya usiku.Sikutaka kukusumbua kwa sababu nilifahamu lazima tutaonana asubuhi..Kwanza hongera kwa kupata kazi nzuri “ Happy akamwambia mdogo wake.
“nashukuru Happy.Niko upande wa huduma kwa wateja.kazi yangu ni kupokea simu za wateja,kupokea malalamiko ya wateja na kuyawasilisha sehemu husika.Nipe habari za Arusha..naona mambo yalikwenda vizuri kiasi kwamba ukasahau hata kunitaarifu kinachoendelea”
“Margeth ,kwanza kabisa napenda nikushukuru sana kwa kazi kubwa uliyoifanya ya kuniunganisha tena na Patrick.Sikutegema kama ningeweza kumuona tena Patrick maishani mwangu .Mara tu nilipofika katika hoteli ile ya Kobe Village nilikuta tayari Patrick amekwisha fika muda mrefu akinisubiri.Nilipomtia machoni sikuamini kama kweli ni yeye.Nilishindwa kujizuia nikaanza kulia.Nililia sana kwa sababu tayari nilikwisha poteza matumaini ya kuonana naye tena.Kwangu mimi ilikuwa ni kama muujiza mkubwa .Kwa ufupi kwa siku hizi chache nilizokaa na Patrick Arusha nilihisi kama niko peponi kwa raha ya ajabu niliyokuwa nayo.”
Margreth akamtazama dada yake huku akitabasamu na kisha akasema
“Ulimuuliza ni kwa nini aliamua kutangaza amekufa kumbe sivyo?
“Ndiyo nilimuuliza kuhusu jambo hilo na akashangaa sana kwani hakuwahi kufanya jambo kama hilo.Yeye pia aliniuliza ni kwani nini niliamua kumuacha gerezani na kuolewa na mzungu ambaye nilizaa naye mtoto mmoja.Nilistuka sana baada ya kusikia kitu kama hiki.Nilimuuliza alipata wapi taarifa kama hizo.Nilimuonyesha barua niliyotumiwa ikinieleza kwamba amefariki dunia.Akaisoma barua ile na kwa bahati nzuri akafanikiwa kuutambua mwandiko wa mtu aliyetuma ile barua.Kwa mujibu wa maelezo yake ni kwamba baada ya kuhamishwa gereza alikutana na dada mmoja aitwaye Vero ambaye alifika hapo gerezani kumsalimu mjomba wake aliyekuwa mkuu wa gereza jipya alilohamishiwa Patrick.Kwa kuwa kila siku Patrick alipangiwa kwenda kufanya shughuli za usafi nyumbani kwa mkuu wa gereza alijikuta akizoeana na Verona wakawa marafki.Muda wa Vero kuwepo pale ulipokwisha ilimlazimu kurejea jijini Dar es salaam na hivyo Patrick akamuomba amtumie kama kiungo baina yangu na yeye.Vero akakubali lakini kumbe alikuwana lake moyoni.Akatunga uongo ule kwa kunitaarifu kwamba Patrick amefariki dunia na halafu akamweleza Patrick kwamba mimi nimemsaliti kwa kuamua kuolewa na mzungu na kumuacha yeye akiozea gerezani.Margreth niliumia sana baada ya kusikia hivyo. Siwezi kuelezea ni maumivu gani aliyoyapata Patrick baada ya kusikia eti nimemsaliti na kuolewa na mwanaume mwingine.Patrick alifungwa gerezani kwa sababu ya upendo wake kwangu.Alifungwa baada ya kuua bila kukusudia kwa kuniokoa mimi nisidhalilishwe na wale wahuni sasa iweje leo niamue kumtelekeza gerezani na kuolewa na mwanaume mwingine? Ni jambo ambalo haliingii akilini lakini Vero alilifanya likaonekana ni kweli “ Happy akasema na kumtazama mdogo wake.
“Pole sana Happy.Kumbe hivyo ndivyo mambo yalivyokuwa !! “ Margreth akashangaa.
“Siamini kama dunia hii kuna watu wenye ukatili wa namna hii.Jambo alilolifanya huyu Vero ni baya sana ambalo lingeweza kusababiosha hata mmoja wenu akajitoa uhai.Hebu niambie Vero alifanya ubaya huu kwa sababu ya nini? manake hata mimi nimesikia uchungu sana kwa ukatili huu alioufanya Vero.” Margerth akauliza
“ sababu kubwa ni kwamba alimpenda Patrick na akautumia umbali uliokuwepo baina yetu kututenganisha.Kweli alifanikiwa alichokuwa akikihitaji.Amefanikiwa kuwa na Patrick na kikubwa ni kwamba mwezi ujao wanafunga ndoa.” Happy akasema na kumfanya Margerth astuke.
“Ama kweli siku hizi binadamu ni wakatili kuliko hata wanyama.Kumbe uongo wote huu mkubwa ni kwa ajili ya kumpata Patrick ! loh ! “ margerth akasikitika sana.
“lakini siku zote kitu alichokipanga Mungu binadamu hawezi kukipangua.” Happy akasema
“kwa nini unasema hivyo Happy? Margreth akauliza
“Si unaona mambo yalivyojitokeza. Nimekutana na Patrick katika mazingira ambayo sikutegemea.Uongo wa Vero umegundulika muda mfupi kabla ya ndoa yake.Hii ina maana kwamba Mungu hakupendezwa na kitu alichokifanya Vero.Baada ya kuonana na Patrick kwa mara nyingine tena imenibidi nikubaliane na ukweli kwamba sina uwezo wa kumtoa Patrick moyoni mwangu.Yeye ndiye mwanaume pekee anayestahili nafasi katika moyo huu”
“Happy unamaanisha nini unaposema hivyo? Margreth akauliza. Happy akamshika bega na kumtazama machoni kwa makini.
“Nimeamua kuachana na Mike.”
“What !! Margreth akastuka
“Toka moyoni mwangu nimeamua kuachana na Mike na kuendelea na Patrick.”
“Happy sidhani kama inawezekana.Mike tayari amekwisha kuvisha pete ya uchumba.Itawezekana vipi umwambie kwamba umekusudia kuachana naye? Kingine kinacholifanya suala hili kuwa gumu zaidi ni kama ulivyosema kwamba Patrick na Vero wako katika maandalizi ya mwisho ya kufunga ndoa.Unadhani itawezekana vipi kuwatenganisha ?
Happy akatabasamu na kusema
“Itawezekana Margreth.Baada ya kugundua kilichotokea tulijadili suala hii kwa undani na kufikia uamuzi mmoja kwamba hakuna kitu cha kuweza kututenganisha,tukaamua kwa kauli moja kwamba tunaachana na wapenzi wetu wa sasa na kuurudisha uhusiano wetu wa awali.Nitamueleza Mike na nina imani atanielewa.Patrick naye atafanya hivyo hivyo na ataachana na Vero.” Happy akasema na kuichukua simu yake akazitafuta namba za Patrick na kupiga .
“Unampigia nani simu? Margreth akauliza
“Ninampigia Patrick.nataka kufahamu maendeleo yake” akajibu Happy
Simu ikaita na kukata,ikaita tena mara ya pili bila kupokelewa,hakukata tamaa akapiga tena mara ya tatu lakini bado simu haikupokelewa.
“Hapokei simu nadhani atakuwa yuko mbali na simu yake” akasema Happy
“Happy mimi sina tatizo na maamuzi yoyote utakayoyachukua .Najua unahitaji kuwa na furaha maishani na kama Patick ndiye mtu pekee ambaye unaamini atakupa furaha ya maisha ,sina kipingamizi na hilo.lakini ninachokihofia ni kwamba katika maamuzi haya mliyoyachukua watu wengi wataumia.Nina wasi wasi mkuwa na hilo.Mwezi mmoja umebaki Patrick na Vero wafunge ndoa kwa maana hiyo maandalizi yatakuwa yameshafanyika ya kutosha.Kitendo cha Patrick kutangaza kuivunja ndoa kati yake na Vero kitawaumia watu wengi na wengi watakuchukia kwa kuamini kwamba wewe ndiye chanzo cha haya yote.Sitaki uingie katika mtafaruku mwingine dada yangu.Sipendi kukuona ukiw akatika mateso na maumivu.Umekwisha lia kiasi cha kutosha dada yangu” Akasema Margreth.
“Margreth nakubaliana nawe kwamba suala hili ni gumu na litawaumiza watu wengi sana lakini tayari tumeshafanya maamuzi na hakuna kurudi nyuma .Niko tayari kukabiliana na chochote kile .Mambo mengi yatajitokeza lakini nitakabiliana nayo” akasema Happy kwa kujiamini
“Nitakutana na Mike baadae na nitaitumia nafasi hiyo kumweleza ukweli na nina imani atanielewa na kuniacha huru ili niweze kuwa na mtu ninayempenda kuliko wote katika maisha yangu” Happy akasema na Margreth akamtazama dada yake kwa huruma