SEHEMU YA THEMANINI MBILI
Asubuhi wakiwa darasani baadhi ya wanafunzi walianzisha minong'ono kuwa Zena hajafika shule,
Licha ya Samson kusikia vile lakini hakutaka kusikiliza mambo yale alijisahaulisha kama vile hakijatokea kitu.
Lakini baada ya muda fulani kuna gari fulani liliingia shuleni pale huku baadhi ya vitu wakimtambua kuwa ni baba yake Zena. wanafunzi watukutu waliinuka kwenye viti vyao wakichungulia dirishani na kubaini mzazi yule anaingia kwenye ofisi ya walimu.
Mmmmh Zena bwana!
Yaani haishi ujanja ujanja, kwahiyo ndiyo kamleta mzazi wake kabisa , lengo ajifanye alionewa? Ila haya hatatuhusu ngoja tufuatilie yetu. alisikika mwanafunzi mmoja.
Maneno yale yalikuwa mwiba kwa Samson, pamoja na kwamba wenzake walikuwa wanabahatisha tu lakini yalibeba ujumbe mzito kwa Samson.
Alijiinamia kwenye kiti kama vile anasoma lakini, masikio na macho vyote vilikuwa Nje, na kitendo cha mzazi wa Zena kukaa ofisini muda mrefu kilimtisha zaidi Samson.
Sasa muda wote huko staff wanaongea nini? isije kuwa Zena kaenda kusimulia mambo yaliyotokea jana, si nitaumbuka mimi, Mzee Mgaya nitamweleza kitu gani?
Si ataniua yule mzee, mama je, na alivyo na mdomo si nitafungashiwa virago leo leo niende mkoani. Hii Sasa ni shida tena nzito. alijiwazia Samson.
Baada ya dakika kadhaa alimuona mwalimu wao wa darasa ambaye alikuwa mwalimu wa nidhamu pia, alikuwa anakuja darasani kwao akiwa kaongozana na yule mzee anayesemekana ni mzazi wa Zena,
Tumbo la Samson hapa lilivuruga huku haja ndogo ikitaka kulazimisha kutoka.
Wanafunzi wote waliinuka na kumsalimia mwalimu wao, Kisha yule mzazi wa Zena ,
wakakaa huku Samson akiwa makini Nini kitajiri maana kichwani alikuwa na majibu anayoyajua yeye binafsi.
Jamani huyu ni baba yetu, mzazi wetu na kwakuwa ni baba wa mwanafunzi mwenzenu Zena, sijawahi kumfahamu kabla ila nimependa maongezi yake tukiwa ofisini hakika ni mfano wa kuigwa kabisa, lakini pia Kuna tabia imeshamiri sana hapa shuleni, ni namna watu mnavyojiamulia kutokufika shule bila taarifa, tena nyie wanafunzi wa kidato cha tatu nyinyi ndiyo mnaongoza kwa utoro shule nzima, tuna utafiti wetu usio rasmi kutokana na mtiririkom wa madarasa.
wanafunzi wa kidato cha kwanza wengi wao huwa na mahudhurio mazuri pengine ni kutokana na ugeni wao, form two kwao ni mwaka wa mitihani hivyo kwa mwenye akili timamu yeye hukimbiza kitabu tu, form four kwao ni mwaka wa paper pia hivyo huwa Kuna ubize fulani kwaajili ya kuhakikisha wanapata division nzuri mengine huwa ni bahati mbaya, lakini form three, ni watu huwa mnajiona mnapaswa kurelax tuuuu kwanini, aliongea yule mwalimu huku wanafunzi wakicheka maana pengine utafiti wake haukuwa wa uhakika.
Licha ya furaha na vicheko kutawala mle darasani, lakini kwa Samson ilikuwa tofauti sana, alikuwa tu na shauku ya kutaka kujua mzazi wa Zena kafuata nini?
Jamani kwanza tambueni kuwa mwanafunzi mwenzenu anaumwa , siyo sana ila anasumbuliwa, kumbukeni kumuombea apone haraka ili aungane nanyi na masomo kama kawaida, na huyu baba yake ni mwalimu wa shule ya msingi ya (akitaja jina)na pia ni mjumbe wa kwenye bodi ya wazazi wa shule yetu hivyo popote mkimuona mumpe heshima yake. alifafanua yule mwalimu huku baba yake Zena akitabasamu.
Hapa tuna list ya watu ambao wao wakijisikia tu, basi hafiki shule. Niseme tu ule ukweli mnajiweka kwenye mazingira hatari sana. Kwani mkija kuingia kwenye kitabu chetu, Kuna uwezekano wa kushindwa kuendelea na masomo hivyo niwaase muwe makini, Tena Samson unaongoza kwa utoro, pamoja na kuwa unaishi mita chache toka hapa lakini ni mmoja wa watoro sugu. Unashindwaje kuwaambia wazazi wako waje watoe taarifa?
Ni upuuzi sana huwa unafanya. baadaye mwalimu na yule mzazi walitoka huku wakiongea mambo yao na Samson akashusha pumzi huku akimshukuru MUNGU wake maana ni kama muujiza , kwanza hakuamini kama angeweza kuchomoka kwenye ile hali.
Baada ya mwalimu kutoka wanafunzi walianza tabiri zao kuwa Zena haumwi ila kilichomuweka kwao ni aibu kwakuwa alikuwa kamchokoza Samson ile Jana yake hivyo, ameamua kuzuga anaumwa, kauli ile ilimuaminisha Kila mwanafunzi mule ndani , huku Samson pekee akiwa anajua kilichomkwamisha Zena asifike shule.
************************************
Mkorofi, mtukutu na mkurupukaji Samson alirejea nyumbani huku akiwa anajiamini kwani hakuwa na mawazo yeyote, aliingia ndani mwao na kukuta Mzee Mgaya pamoja na mwanaye Glory wakiwa wanapitia matokeo yake ya mitihani, huku wote wakikubaliana kuwa Samson apelekwe shule nyingine ambayo itamnyima uhuru wa kufanya mambo yake ya kijinga.
Huku mama Kulwa akiwa yeye hakubaliani na suala la Samson kupelekwa shule nyingine akidai ni uharibifu tu wa pesa kwani mtoto mwenye ana mwenendo mbovu Sana hapaswi kuaminiwa Wala kudhaminiwa .
Samson alijifanya kama haelewi kinachojadiliwa pale, aliendelea na mambo mengine tu Kisha akaingia ndani chumbani kwake kubadilisha nguo.
Wewe Samson hebu toka huko ndani njoo kwanza hapa, aliita Mzee Mgaya.
Kila siku nimekuwa nakuasa na kukukanya kuhusu tabia zako, ona sasa inatakiwa tupige kura ili wewe uhamie shule nyingine, mimi na dada yako tupo radhi , si kwamba tunafurahishwa na tabia zako, ila bado tunajaribu kukubeba , maana kama Mimi nilitakiwa nikate tamaa siku nyingi, lakini nilijikuta namuhurumia mdogo wangu namna jina lako lilivyouzwa kwa watu wengine wakati ni haki yako. unasahau ni wewe ulibandika matokeo yako ya mitihani kuizunguka nyumba yenu , lengo Mimi nione . Kipindi hicho unaniogopa huwezi hata kukaa karibu na Mimi, niligundua kuwa ulifanya vile tena kwa kushawishiwa na mama yako, nikapata huruma ya kuwasaidia lakini ulipofikia unakatisha tamaa mwanangu, wewe umekuwa na matatizo kwenye hii nyumba kushinda hata wanangu wa kuwazaa. Mbona si msikivu wewe mtoto? aliongea Kwa masikitiko Mzee mgaya.
Samson alipiga magoti mbele ya Mzee mgaya na wengine huku akiahidi atabadilika na kuzingatia masomo, alimgeukia mama kulwa ambaye ndiye mwenye hasira na kinyongo zaidi huku akiomba amuamini.
Samson kaka yako Jose alikuja kipindi kile akalaumu kwanini unasoma hapo, akataka afanye mpango uhamishwe lakini nilikataa , kwakuwa ndicho kipindi tulikwazana ukawa unakaa kwa Tausi.
Jose ni mwanangu hangebishana na Mimi mama yake, nilimwambia kuwa ni lazima nione mabadiliko ya tabia zako kwanza ndipo tutajua cha kufanya, lakini mwanangu ndiyo kwanza umezidisha matatizo.
Leo hii dada yako tangu afike naye anahitaji akusaidie, lakini hofu yangu ni wanangu wasije kutupa gharama zao bure, ni afadhali wafanye mambo yao tu kuliko kumsaidia mtu ambaye yeye mwenyewe hajui anataka nini.
Mama kulwa alimchana makavu Samson.
Sasa hatima ya shule yako ipo mikononi mwangu, nitahakikisha nagundua umebadilika ndipo nitaruhusu mwenye uwezo akusaidie vinginevyo haiwezekani, wanangu hawawezi kutumbukiza hela zao baharini. alipigilia msumari mama Kulwa, huku Mzee Mgaya na Glory wakitikisa vichwa vyao kumuhurumia Samson, maana alichoongea mama Kulwa kilikuwa na uhalisia.
Samson alijikuta anawaza mambo mengi sana
Hivi ishu ya Mimi na Zena ikigundulika itakuwaje?
Halafu Mzee wake anaonekana siyo choka mbaya na anaaminiwa pale school. aliwaza Samson.
Itaendelea................