SEHEMU YA SITINI NA TATU
Hebu kwanza kung'uta hiyo miguu ndipo uingie ndani, halafu mbona umechafuka hivyo ulienda kanisani wewe kweli, usijekuwa umecheza na akili zetu, halafu saa hizi ni saa kumi na moja kwani ulikuwa wapi muda wote huo? aliuliza mama Kulwa.
Nilipotoka kanisani niliungana na wanafunzi wenzangu tukaenda kujisomea, alijitetea Samson.
Sawa, sina uhakika na maelezo yako , isipokuwa naomba ujitahidi kuheshimu wengine na kujiheshimu wewe mwenyewe, jana uliomba ruhusa vizuri sana kwamba unaenda kanisani, lakini kitendo cha kurudi muda usiostahili tayari unajivunjia uaminifu, chakula kipo nadhani japo kitakuwa kimepoa ule halafu ukae hapahapa sawa.usifanye kama siku ile mara unatoka. alisema mama Kulwa huku Sam akiitia kwa kutikisa kichwa.
Mimi naenda kwa yule dada yako Cathy, kuna mambo naenda kuongea naye narudi siyo muda na njoo ufunge geti. aliongea mama Kulwa huku akilitoa nje gari lake.
Samson moyo ulipiga paaah!!!
Kitendo cha mama Kulwa kwenda kwa Cathy Samson alikosa raha, aliona kama Kuna mambo yanaenda kukaa hadharani, muda si mrefu alikosa amani kiasi japo siyo sana kwani alikuwa nusu kuamini kama kweli Cathy mtu mzima anaweza kusema vitu vile, lakini upande mwingine akili iliona Cathy huwa hana aibu anaweza kusema tu. alijitahidi kujisahaulisha ili awaze mambo mengine ila kila akikumbuka moyo ulimuenda mbio.
Halafuu leo hapa kumepooza sana Rahma naye sijui yuko wapi, mbona si kawaida kwenda sehemu peke yake, au katumwa? lakini muda wote niliofika hapa awe hajarudi bado?
Samson alikosa majibu ya maswali aliyojiuliza, akachukua ndoo ya maji ili akaoge maana Kuna kijiharufu kibaya alikuwa anakisikia, alimaliza kujisafisha na kujifuta vizuri Kisha akaliendea poti la Chakula akawa anakula nyama tu kwa tamaa zake maana hakuwa na hamu ya kula tena, si alikula kwa Cathy?
Akatoka nje na kuanza kufua nguo zile alizosimangwa kwamba mbona zimechafuka sana, wakati kigiza kikiingia mama Kulwa alirudi , Samson alikuwa makini sana kuona mama kaja na ujumbe gani kutoka kwa Cathy? lakini alishangaa kuona mama yake akiwa Hana maswali yeyote yupo kawaida tu, akajua hakuna kitu maana mama Kulwa akisikia jambo huwa hachelewi lazima akuulize tu muda huohuo.
Mama Da Rahma yuko wapi,
aliuliza Samson.
Mchana alikuja Tausi hapa akaomba kuondoka naye nadhani atarudi kesho, alijibu Mama Kulwa.
Mzee Mgaya alirudi akiwa amelewa kiasi fulani kwani alionesha hali ya uchangamfu sana huku akileta vichekesho fulani pale sebuleni.
Ila mume wangu leo nina masikitiko kidogo juu ya yule mwanangu Cathy, nasema nasikitika kwasababu,
Baada ya kurudi huyu Samson nikaona ngoja nimuache niende kwa Cathy, maana kuna vitu nilitaka tukajadiliane naye, nimefika nimegonga geti vizuri yule mwanamke mwenzake kanifungulia akaniambia kuwa anaenda kumwita Mimi nikimsubiri barazani kwake, cha ajabu yule dada wa kazi akaniambia kuwa kasema asiamshwe,
Ikabidi nimwambie kuwa amwambie ninayemuita ni mimi, lakini bado aligoma kuja. masikini mimi ikabidi nitoke kwa aibu nikarudi hapa.
Najiuliza mambo mengi sana kwani kapatwa na nini au kafanyaje?
Cathy Nina historia yake kubwa tu kuhusu yeye, yapo mengi nimemfanyia Mimi ni mama yake, kwanini anifanyie hivi. alilalamika mama Kulwa.
Unajua mke wangu Mimi sioni hoja yako ya msingi, sanasana unajiaibisha tu,
Ulitakiwa ujiulize, alikuwa na nani?alikuwa akifanya nini?
Utakimbilia lawama bure mke wangu,
ingekuwa mmekutana barabarani, au sehemu tu ya wazi halafu akaonesha ujeuri huo. ungekuwa na hoja za msingi, lakini pale ni kwake, alikuwa chumbani kwake, vyumba vyetu vina mengi yanayofanyika hakuna shahidi zaidi ya hizi Kuta.
Mke wangu utakuwa unazeeka vibaya. aliongea Mzee Mgaya akitaka mkewe ajiongeze kuliko kukimbilia kulaumu.
*************************************
Siku ya jumatatu Samson alienda shule huku akiwa na amani sana,
Maisha yalikuwa yanaenda vizuri huku kelele pale nyumbani zikiwa zimepungua,
Akiwa darasani siku hiyo alikuwa makini sana, yaani hakuwa na kale kauvivu ambako huwa anako siku zote, badala yake Kila mwalimu aliyeingia kufundisha somo lake, Samson alikuwa makini.
Mwalimu mkuu aliingia huku akiwa kakasirika baada ya kuona wanafunzi wakipiga makelele,
Hebu nyamazeni huko, hapa ni darasani au kilabu cha pombe za kienyeji, eeh yaani watu hamna hata chembe ya aibu, kwanini mnakuwa mnalazimisha kuchapwa, kwanini?
aliongea huku akiwa analinganisha fimbo alizoshika mkononi ipi itafaa kuchapa darasa zima.
Wapo waliojitetea kuwa walikuwa kimya wakijisomea lakini wapo pia waliosema kuwa wapo tayari kuwataja waliokuwa wakipiga kelele, lakini baada ya muda alitupa fimbo zake chini huku akiwasema kuwa kama wazazi na walezi wao wapo tayari kupoteza ada na muda kwaajili yao ni vyema wajikite kuwa na nidhamu shuleni pale.
Baada ya kusema yale, alimuita Samson amfuate ofisini kwake,
Walifika huku akimuashiria aketi, huku akifunua funua mafaili yake Kisha akainua uso na kuanza kuzungumza na Samson.
Samson unakaribia kuingia kidato cha tatu, na nadhani bado miezi miwili ili kufikia kufanya mitihani yenu, Sasa nasikitika kusema Kuna uongozi kutoka mkoani, namaanisha kuna maofisa walikuja hapa kukagua uhalali wa wanafunzi ambao wanasoma hapa, huku wale ambao si halali, wakitakiwa kusimamishwa kwa muda hili zoezi limefanyika siku nyingi sana , na nasikitika kusema kuwa wewe ni mmoja wa wanafunzi ambao watasimama hadi zitakapokuja taarifa zako sahihi basi utaendelea na masomo yako kama kawaida, aliweka kituo mwalimu mkuu.
Samson tumbo lilimkoroga huku, miguu ikimuisha nguvu lakini alijitahidi akauliza,
Kwani mwalimu Mzee Mgaya na wewe si mlimalizana na Kila kitu kikakaa sawa, Sasa Kuna Nini tena mwalimu wangu, maana kipindi chote hicho imeshindikana Hadi nisimamishwe kipindi hiki? aliuliza Samson.
Sikia Samson, Mimi mwenyewe ni muajiriwa, nina wakubwa zangu , ni kweli nilimsaidia baba yako ili uendelee na masomo lakini taarifa zako hazikukamilika na Kuna sehemu mlitakiwa mgonge mihuri hamkufanya hivyo, na kibaya zaidi maofisa Elimu ngazi ya Mkoa ndiyo wameamua haya, siyo Mimi,
Mimi kwanza napenda sana maendeleo yako hapa shuleni wewe ni kipenzi cha walimu hapa shuleni lakini hatuna namna, haya utamfikishia Mzee wako, ningeandika barua lakini sioni sababu za kufanya hivyo. alimaliza kuongea mwalimu mkuu huku akimwambia Samson abebe vitu vyake na asionekane shuleni pale hadi watakapokamilisha taratibu zao.
Samson machozi yalitiririka kuanzia shuleni pale hadi nyumbani, huku baada ya kufunguliwa geti na kuwaona wazazi wake akizidisha kilio, hakika alikamatwa na kukamatika.
Ni lini milango ya mafanikio itafunguka, endelea kuifuatilia simulizi hii.
Itaendelea.........................